December 06, 2017

“NYASA INAWEZA KUJENGA KIWANDA CHA MATUNDA. HOTELI NAZO ZINATUDAI MAHITAJI MENGI WANYASA”

NA MARKUS MPANGALA

MAELFU ya vijana waliotokea Wilaya ya Nyasa mkoa wa Ruvuma wamesoma elimu ya Sekondari  katika shule ya Lundo iliyopo Kata ya Lipingo wilayani humo. Hata hivyo sio vijana wote wamepata elimu ya sekondari ndani ya Wilaya ya Nyasa au shule hiyo pekee, lakini idadi kubwa wamesoma hapo. Katika kipindi cha miaka 2000 kumekuwa na ongezeko la shule za sekondari, ambapo nyingi sasa hivi ni za Kata tofauti na awali. 

Miongoni mwao ni ALPHONCE KWENDE ambaye ni mwanazuoni wa masuala ya Kilimo hapa nchini.  Yeye ni mzaliwa wa kijiji cha Chinula, tukiwa tumehitimu pamoja shuleni.  Amejikita katika fani ya Kilimo na anaitazama wilaya Nyasa ikiwa na uwezo wa kujenga Kiwanda pamoja na watu kubadilika kuwa na mawazo ya kibiashara kupitia kilimo. 
SOMA MAHOJIANO KAMILI…..

SWALI:  Habari za mchana mtumishi. Hebu tueleze baada ya  elimu ya Sekondari  Lundo ulichaguwa kwenda shule gani?
ALPHONCE KWENDE: Yes, nilijiunga na Kibiti High School, iliyopo mkoani Pwani kusoma masomo ya kidato cha tano na sita.
Mwanazuoni KWENDE akiwa kwenye shughuli za Kilimo.

SWALI: Umewahi kujiunga na Chuo chochote baada ya kuhitimua ‘High School’?
KWENDE: Sikujiunga na Chuo Kikuu kingine zaidi ya SUA. Hiki ni Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, kipo mkoani Morogoro. Hapo ndipo nilihitimu Shahada yangu ya Kilimo kwa ujumla wake.

SWALI: Aaah! Ndiyo maana kilimo kimekushika sana? Nadhani ni msingi wa Lundo katika somo hilo. Nililipenda sana ila likafutwa. 
KWENDE: Ni kweli kabisa. Kabisa, Lundo walitengeneza msingi mzuri sana kwenye somo la Kilimo, ndiyo matunda yake niliyonayo sasa. Nilimalizana na elimua ye sekondari ya juu  High School, mwaka 2004. Kisha mwaka 2009 nilifanikiwa kuhitimu shahada yangu ya Kilimo pale SUA.

SWALI: Tutajie mambo muhimu ambayo unadhani yanaweza kuipaisha Wilaya ya Nyasa kiuchumi, Afya na Mengine.

KWENDE: Kujibu hilo inatakiwa akili iwe imetulia kidogo. Mimi ningependa sana kuzungumzia sekta yangu ya Kilimo na Ufugaji. Ujio wa Wilaya ya Nyasa unaibua hitaji kubwa sana la kuanza kufanya kilimo chenye tija na cha kibiashara maana mpaka sasa bado wilaya ya Nyasa inategemea Muhogo kama zao kwa chakula na biashara. Ingawaje jitihada zinaendelea kufanyika kuendeleza uzalishaji wa zao hilo ili lilete kipato cha kutosha kwa wakulima hao. Ujio wa Wilaya mpya unakuja na ujenzi wa Mahoteli ambako hakuna uzalishaji wa kutosha mpaka sasa wa mazao ya bustani ya uhakika kukidhi hitaji hilo hivyo kutakuwa na uhitaji wa mboga hizo na matunda kama Mananasi,Parachichi,Matango,Matikiti maji na kadhalika.
Mojawapo ya Hoteli iliyopo wilaya ya Nyasa.
SWALI: Bwana Kwende hapa unatudhihirishia kuwa fursa hii inawahitaji waliosomea fani ya Horticulture (kilimo cha mboga mboga na matunda), kwamba wanahitajika sana Nyasa?

KWENDE; Bila shaka, nimetaja matunda, kwahiyo kama nguvu ikitumika kuangalia fursa hiyo basi Nyasa wataendelea kuboresha maisha yao kwa kuanza kuzalisha mazao mengine kuliko Mihogo  tuliyozoea kulima. Sasa ngoja nikuambie hii fursa ya Hoteli zinazojengwa Nyasa. Mahoteli hayo yanaibua uhitaji mkubwa wa nyama za Mbuzi,Kuku,Ng’ombe na kadhalika, pamoja na uzalishaji wa mayai. Ukiangalia sekta hii ya kilimo bado ina nafasi kubwa ya kuinua maisha ya wanyasa kwa ujumla, ukiangalia tumejaliwa na mabonde mazuri yenye rutuba, uhakika wa maji pia ni mkubwa, kwani mito mingi sana. 
Hoteli zitachochea ongezeko la ufugaji wa Ng'ombe
Kwa ujumla wake kilimo kwa Wilaya ya Nyasa ni fursa kubwa sana ili kuboresha maisha yetu.  Yapo mambo mengi, hapa nimeweka dokezo tu. Mimi ni mmoja kati ya watu wenye mipango ya kurudi na kuwekeza kwenye mabonde hayo na kutoa elimu namna ya kufanya kilimo chenye tija kwenye wilaya yangu. Hayo ni kwa ufupi ila yapo mengi.
  
SWALI; hebu nyongeza kidogo ili wenzetu waweze kufaidi mawazo yako mwanazuoni.
KWENDE: Hebu tazama usafarishaji. Bado kuna fursa ya usafiri wa Meli tunaweza kuzalisha na kusafirisha na kupeleka mikoa ya karibu ya mwambao wa Ziwa lakini pia katika nchi ya jirani. Kwa mfano, Malawi na Msumbiji. 

SWALI:. Hebu tueleze nini nafasi ya ufugaji katika wilaya yetu?

KWENDE: Kuna fursa pia hapo. Fursa ya ufugaji wa samaki, ziwa Nyasa siyo tena chanzo cha kutegemewa kulingana na sheria zinazopitishwa kuzuia baadhi ya aina ya uvuvi hivyo upatikanaji wa samaki kama sehemu ya kipato nao upo mashakani, hali ya hewa ya ziwa na mabadiliko ya kila mara. Hapo mwanzoni nimesema Wanyasa wanatumiaje fursa ya Mahotel yanayojengwa? Unagufa na kwenda kuwauzia nyama au samaki vyote vipo. 

SWALI; Asante sana kwa mawazo mazuri. Unaweza kutuambia changamoto ya jamii ya Kinyasa katika masuala hayo?
KWENDE:  Lazima wanyasa hasa waishio wilayani kwetu Nyasa waanze kubadilika kuacha kuangalia mambo kama walivyozoea na kuona ujio wa Wilaya imekuja kuwaondoa ukaa Vilabuni na vijiweni visivyo na Tija. Kila mmoja ana eneo nyumbani kwake, liwe la ukoo au familia lazima aone anaweza kufanya nini sasa katika eneo hilo. 

SWALI; Maeneo ya Ngindo,Mkali na Hongi kuna watu walikuwa wakilima ulezi milimani huko. Watamudu hilo tena sasa?
KWENDE: Kuna Ulezi wa Milimani. Kuna Mpunga wa Milimani. Name nataka kuanzisha vitunguu vya msimu wa Mvua kama wanavyofanya mkoani Singida na Arusha, wao wanalima msimu wa Mvua tu. 

SWALI: Vipi kiwanda cha Sukari pale Lwika kiliishia wapi?
KWENDE: Yaani hata sijui kilipoteaje kile kiwanda. Ni fursa nayo ingawa hatuna mabonde makubwa sana ya kuzalisha Miwa maana mabonde yaliyopo ndiyo tunazalisha Mpunga na wameanza kilimo cha Umwagiliaji. Hayo ni fursa. 
Shughuli za Kilimo katika Bonde la Mto Lwika.
SWALI: Ukiacha Lwika, hakuna maeneo mengine yanayolima Miwa kiasi kikubwa?
KWENDE:  Kwa Nyasa hakuna kabisa. Bado sana.

SWALI: Haya, kuna matunda pale Kijiji cha Mango. Je, yanatosheleza kuwa na kiwanda kidogo cha Juisi?
KWENDE: Yeees, Machungwa,Mananasi, inawezekana kabisa. Kuna maeneo mengi ya mazao hayo Lundo, Nkali, Hongi,Nkalachi kwa juu kule ni ardhi nzuri sana na kubwa kuzalisha Mananasi, Machungwa, maeneo ya Mango huko na kadhalika.


SWALI: Wewe ni mtaalamu sasa, tunafanyaje ili hilo l;itekelezwe?
KWENDE: Kama nilivyosema haya mambo tunatakiwa kukaa chini na kuainisha hayo yote na kuweka mpango wa mkkakati na kazi kimaandishi, kama sapto inapatikana vinginevyoi itakuwa ni juhudi za mtu au vikundi. Tunayo rasilimali watu kama akina Hoops Kamanga na wengine tukikaa pamoja tunaweza kutengeneza kitu.

SWALI: Ninarudia kutoa shukrani tena kwa kushiriki kipengere hiki cha “KURUDI NYUMBANI” ndani ya blogu hii ya “KARIBUNI NYASA” kwa manufaa ya Wanyasa wote bila ubaguzi.
KWENDE:  Asante sana, japo nilikabiliwa na kikao lakini nimeona nishiriki, maana sikushangaa sana. Ilikuwa muhimu kuongea na wenzetu kuwapatia dokezo kuhusu Nyasa.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako