December 01, 2017

WAZIRI MKUU ATAMBUE NYASA IMEJAA UTAJIRI

Na MARKUS MPANGALA
 
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akifunga mkutano wa tisa wa Bunge la 11 Novemba 17 mwaka huu alibainisha jambo muhimu linalohusu ubora wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambayo inajumuisha mikoa ya Ruvuma, Mbeya, Lindi na Mtwara.
Makala haya yalichapishwa katika safu yangu ya MAWAZONI ndani ya gazeti la RAI linalotoka kila alhamis
Waziri mkuu katika hotuba yake alimwagiza Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangala kuanzisha Mamlaka ya Fukwe za Bahari na Maziwa ili kutangaza utalii na kuendeleza fukwe ambazo hazina shughuli.
 
Agizo la Majaliwa linaakisi mpango wa serikali wa kuendeleza utalii Nyanda za Juu Kusini kwani kuna vivutio vingi lakini pamekuwapo idadi ndogo ya watalii wanaotembelea ukanda huo, ukilinganisha na Kaskazini.

 
Aidha, Waziri Mkuu alisema serikali imepokea dola za Marekani milioni 150 kupitia mradi wa Resilient Natural Resources Tourism and Growth kwaajili ya kutekeleza kuanzia mwaka fedha wa 2017/2018. Lengo la mradi huo ni kuongeza mchango wa sekta ya utalii. Taarifa ya Waziri Mkuu ilinisisimua sana. Nakiri nimezaliwa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma. Wilaya ambayo imejaa utajiri ambao kwa hakika haujauvunwa na haujatumika ipasavyo. 

Aidha, nakubali kuwa wilaya hii imejaa vivutio vya utalii kiasi kwamba hata wageni wamekuwa wakishangaa kwanini hatushughulikii miundombinu. Mwaka 2003 nikiwa kidato cha tano nilikutana na wageni wanne kutoka Ujerumani wakiwa katika ufukwe wa nyumbani kwetu kijiji cha Lundu. Wageni hao walikuwa na binti yao ambaye alikuwa mwanafunzi na alivutiwa mno na mazingira ya fukwe hizo na kusisitiza kuwa maeneo hayo yalipaswa kuthaminiwa na kutangaza vivutio vyake duniani. 
Katika maongezi yangu na binti yule alichoniambia mwaka 2003 ni kwamba alishangazwa na kwanini hapakuwa na huduma za ziada kama hoteli, barabara nzuri, usafirishaji na huduma za afya wakati mazingira yalikuwa ya fukwe yalikuwa bora zaidi.


Mazungumzo yangu na binti yule yalinichochea kuanzisha mtandao wa blogu (www.lundunyasa.blogspot.com) mwaka 2007 yaani miaka minne baadaye kwa lengo la kupasha habari za mwambao wa Ziwa Nyasa. Malengo yalikuwa kuhakikisha maeneo ya utalii na utamaduni wa wakazi wa wilaya ya Nyasa yanajulikana na kuwafikia wengi. 

Jitihada hizo zilimvutia Profesa Joseph Mbele wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Olaf, kilichopo Northfield, Minnesota nchini Marekani ambaye ni mzaliwa wa kijiji cha Litembo wilayani Mbinga. Profesa Mbele alinishawishi kuongeza nguvu za kutambulisha utalii maeneo ya Nyasa. Juhudi hizi sasa zimewavutia wengi ambapo tumeona kaka yangu Albano Midelo akibeba jahazi hili na kulifikisha kiwango kingine. Tunaendelea kushirikiana. 

Aidha, Parokia ya Lundu ina urafiki na Jimbo la Kanisa Katoliki la Wurzburg la Ujerumani ambalo mara kadhaa limekuwa likielekeza watalii kutembelea kijiji chetu. Urafiki huu umechochea mkururo wa watu kutoka Ujerumani kutembelea nyumbani kwetu Lundu. 

Wageni wanaogelea, wanaburudishwa na maji safi, fukwe nzuri zisizo na uchafu wala kuhitaji gharama kubwa za kuendesha.  Nimeshuhudia hayo si mara moja au mbili bali zaidi ya hapo. Nimeshuhudia watalii walioingia kijiji chetu kupitia Kanisa Katoliki hususani Shirika la Benedictine Fathers la Peramiho. Baadhi yao nawakumbuka majina na wengine walikuwa marafiki wa ndugu zangu hapo hapo kijijini akiwamo baba yangu mzazi.

Miaka ya nyuma nilishuhudia wazamiaji wengi wakivuna samaki katika Kijiji cha Lundu. Wengi wa samaki waliochukuliwa tuliwaita kwa jina la kienyeji, ‘Kanchungu”. Ni aina ya samaki ambao wanapendeza mno, wana rangi ya manjano na nyeupe kwa mbali, wengine wana rangi za bluu,nyeusi na kadhalika.

Samaki wa mapambo wanapatikana zaidi Ziwa Nyasa na Ziwa Tanganyika.  Samaki mmoja anauzwa  dola 19 na kuendelea katika soko la dunia. Ukiingia kwenye mtandao wa www.liveaquaria.com au watendaji wa serikali yetu waamue kutafuta kupitia ‘Google African Cichlids’ wataona maajabu ya wilaya Nyasa yalivyohifadhiwa. 

Hao ni Samaki tu, na kumbuka hawa samaki tunasafirisha baada ya miaka ijayo wanunuzi wanaweza kuzalisha wa kwao kisha wakaacha kununua tena kwetu au kwenda Ziwa Nyasa ili kuvuna samaki zaidi hivyo nayo bei itashuka sana.

Kuna jingine limeibuka hapa hapa nchini. Samaki wa mapambo tunaowaona mitaani  hapa Tanzania  wengi wao wanatoka Malaysia na kwingineko wote wamehasiwa huwezi kuwazalisha na wakifa inakulazimu ununue mwingine.
Sisi tunalo Ziwa Nyasa lenye samaki wa mapambo wengi mno lakini hatuna barabara nzuri za kutufikisha maeneo husika, hatuna mawasiliano mazuri ya simu, hatuna huduma nzuri za afya, hatuna mazingira mazuri ya kukuza uchumi. 

Kwahiyo wakati mamlaka ya Fukwe za Bahari na Maziwa inaanza kazi itambue, njia mojawapo ya kuleta ufanisi ni kuikumbusha Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi inatimiza wajibu wake wa kujenga barabara ya Mbinga kwenda Mbamba Bay kama ilivyotangazwa Bungeni mwezi Julai na waziri Profesa Mbarawa. Pia barabara ya Songea kwenda Lituhi kama njia mojawapo ya kuvutia watalii kwenda Folkland. 

SALAMU KUTOKA ISRAEL KUHUSU UTALII NYASA
Katika mfululizo wa makala hizi nitaonyesha mazingira na hali halisi ya utajiri wa Wilaya ya Nyasa unavyokosha wengi. Mwezi mmoja uliopita nilipata salamu hizi kutoka kwa rafiki yangu Ilan Shtrikman mkazi wa mji wa Tiberias nchini Israel. Ilan aliniandikia baruapepe, baada ya kusoma taarifa za uzinduzi wa Meli mpya za Mizigo ya Mv. Njombe na Mv. Ruvuma katika Wilaya ya Nyasa nilizoandika kwenye blogu yangu. 

“Salama Mr. Markus Mpangala. Jina Langu Ilan, natoka Israel ila najua kidogo Kiswahili. Nipo kwenye YouTube, nimepata e-mail yako kutoka blogger. Nimeshawahi kutembelea Tanzania. Ningependa tena kusafiri kwenu, hatimaye kutembelea Lupingu. Nataka kuuliza, kuna Meli siku hizi kutoka Mbamba Bay ama kutoka Kyela kwenda Lupingu? Najua kwamba kuna meli mbili mpya Njombe na Ruvuma lakini yanabeba abiria ama mizigo tu? (zamani nimeshawahi kusafiri na Mv Iringa na Mv Songea),”

Ilan anaendelea kusema, “Nashukuru sana kunijibu e-mail yangu na maswali yangu! Na mimi najibu maswali yako pia: Nimetembelea kwenu hasa Lupingu mara nne masika 2011-2014. Nimefika pia hadi Liuli na Mbamba Bay na NkhataBay upande wa Malawi pia sikuwa na shughuli ila kufurahi na Mazingira tu. Lupingu nilikuwa najenga hema Ziwani na kula ugali wa muhogo na dagaa kwa wakazi wa Lupingu. Ila mara kwa mara Uhamiaji walikuwa wananiuliza mahojiano kuhusu nia yangu ya Safari. Hakuamini kwamba sipati faida, na tarafa hakupenda jinsi ninakaa hemani. Tangu 2014 sikusafiri tena kwenu ila mwaka jana nilienda Kigoma. Januari, Februari na Machi wakati wa baridi kwetu napenda kwenda Afrika"

“Niliwahi kuwa Mwanafunzi Germany zamani na kule nimeanza mahusiano yangu na Lugha na Utamaduni Swahili kupitia majirani yangu waliotoka Kenya. Sio rahisi kusafiri kwenu, -Jua kali sana, kwa ajili ya ngozi nyeupe kama ninayo mimi. Hali ya vyombo vya safari sio nzuri, kuna uhalifu, hasa dhidi ya watalii, ila ningependa hata hivyo kurudi tena kwenu. Nimesoma kidogo kuhusu wewe, kwamba unapenda Sport, Siasa na kuogelea pia na mimi napenda pia kuogelea hasa chini ya maji kwasabau Ziwa Nyasa maji masafi sana.”

ITAENDELEA….

2 comments:

Maoni yako