Na
MARKUS MPANGALA
SEHEMU ya kwanza ya makala haya
katika safu hii tulichagiza kuwa agizo lililotolewa na Waziri mkuu katika
hotuba yake akimwagiza Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangala kuanzisha
Mamlaka ya Fukwe za Bahari na Maziwa ili kutangaza utalii na kuendeleza fukwe
ambazo hazina shughuli kwa madhumuni ya kukuza utalii Kanda ya Kusini na
mengineyo. Endelea kusoma….
Madhali linalozungumzwa ni
kuhakikisha fukwe zinakuwa na tija ni muhimu pia kuikumbusha mamlaka husika
kuwa wilaya ya Nyasa inao utajiri mkubwa sana wenye tija kupitia sekta ya
utalii ambayo kihistoria maeneo mengi bado ni mbegu bora n zenye kuvutia.
Si hilo, wilaya hiyo inao uwezo
wa kuwa na viwanda vya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali lakini kwa sharti moja
muhimu; iwapo changamoto zinazoikabili Halmashauri zitattuliwa kwani zitakuwa
chachu ya kukuza mapato ya ndani. Hatuimwagii sifa hizo za bure bali yapo mambo
ya kuyaangalia kwa kina. Leo ninatoa mifano mingine ambayo kwa namna moja au
nyingine itawafumbua macho wasomaji na watu mbalimbali wanaofuatilia mfululizo
huu.
FUKWE
Sifa kubwa ya Ziwa Nyasa ni
kuwa fukwe bora na zisizo na uchafu wowote. Kama tulivyoona wiki iliyopita sifa
zilizotajwa na rafiki yangu Ilan kutoka Israel, ndivyo ukweli ulivyo. Katika Kijiji cha Mtupale
kilichopo Kata ya Chiwanda kuna fukwe za mawe ambazo ni kivutio adimu cha
utalii. Ukitembelea mwambao mwa ziwa Nyasa kuna maeneo mengi yenye fukwe za
mchanga unaovutia, lakini katika mwambao mwa Kata ya Chiwanda kuna fukwe za
mawe ambazo bado wawekezaji hawajafungua milango ya Utalii kanda ya Kusini.
Ufukwe wa Mchanga katika forodha ya Chivanga iliyopo kijijiji cha Lundu |
Ikumbukwe Kijiji hicho
kinapakana na kingine cha Chiwindi ambacho ndicho cha mwisho kabla ya kuingia
mpaka kati ya Tanzania na Msumbiji. Eneo hili linao ubora wa hali ya juu. Zipo fukwe zingine zenye
kuwavutia watu ni Ndengere, Ngindo, Lundo, Lipingo, Mkali,
Hongi,Liuli,Kihagara,Mkili, Lundu,Mbaha, na Ndumbi kwa kuzitaja chache ni
sehemu ambazo zinahitaji nguvu kidogo sana za uwekezaji kabla ya kuleta tija
kwa wawekezaji. Ikumbukwe kijiji cha Ndumbi ndicho chenye bandari ambayo Makaa
ya Mawe yanayochimbwa na Kampuni ya TanCoal. Ni mahali ambapo unaweza kutumia
darubini kuitazama nchi jirani ya Malawi kwa ufasaha.
Fukwe za miji iliyozoeleka
kupokea wageni kutoka ng’ambo ni Mbamba Bay, Kilosa, Liuli, Lundu na ufukwe
bora kabisa wa Mhalo (Mhalo Beach) ni miongoni mwa maajabu yaliyopo katika
wilaya ya Nyasa. Baadhi ya fukwe hususani zilizopo Mbamba Bay kuna hoteli za
uhakika ambazo zinawapa nafasi watalii kuishi kwa utulivu. Mji wa Liuli umemuwa
mkongwe kwa kupokea watalii, nao umekuwa na hoteli zenye uhakika.
HIFADHI
ZA ASILI
Mosi, Miongoni mwa mambo ambayo
yanaipatia sifa Wilaya ya Nyasa ni hifadhi za asili. Mkoa wa Ruvuma umepata hifadhi ya wanyamapori
ya pili ya asili inayoitwa ‘Mbamba Bay Hill’ ambayo ipo mjini Mbamba Bay makao
makuu ya wilaya ya Nyasa.
Hifadhi hiyo ni ya kipekee hapa
Tanzania ya kwanza ya asili iliyopo mjini inaitwa Luhira iliyopo kilometa saba
toka mjini Songea mkoani Ruvuma iliyoanzishwa mwaka 1974. Hivyo basi mkoa wa
Ruvuma umepata hifadhi ya pili ya asili mjini.
Kwa mujibu wa Afisa Maliasili
na Utalii wa Mkoa wa Ruvuma, Afrikanus Chale anasema mchakato wa kuendeleza
Mbamba Hill unaendelea vizuri na kwamba ya tayari bajeti ilipitishwa. Eneo la hifadhi hiyo limeshapimwa na lina
ukubwa wa ekari 420, ndani ya hifadhi hiyo kuna wanyama kama Nyani, Nyoka,
Pimbi, Chui na ndege wa aina mbalimbali.
Aidha, bajeti ya kujenga uzio
kuzunguka Mbamba Bay Hill imepitishwa na kwamba ujenzi unatarajia kuanza wakati
wowote fedha zitakapoletwa na kwamba mara baada ya ujenzi wa uzio kukamilika
wanyamapori wa aina mbalimbali wanatarajia kuongezwa, kwa mfano, Swala,
Fisimaji, mbuzi Mawe, Digidigi, Mbawala na kwamba wanyama watakaongezwa ni wale
ambao wanaweza kuishi katika mazingira ya hifadhi hiyo ambayo imeungana na ziwa
Nyasa.
Ufukwe wa Mawe |
Hifadhi nyingine itakuwa ni
kisiwa cha Mbamba Bay maarufu kwa jina la Kisiwa cha Zambia, kina ukubwa wa
ekari 27. Kisiwa hicho kimependekezwa kuwa hifadhi ya wanyamapori, kimejaliwa
kuwa na uoto unaovutia wa misitu ya miombo ambao ni maarufu duniani ambapo mawe
yanayozunguka katika kisiwa hicho ni mazalia ya samaki wa mapambano aina zaidi
ya 400 wanaopatikana katika ziwa Nyasa pekee.
Kutokana na udogo wa kisiwa cha
Mbamba Bay Afisa Maliasili na Utalii wa Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe
anashauri katika kisiwa hicho kusijengwe makazi ya kudumu kwa ajili ya
wafanyakazi wa kuhudumia watalii ili kuendelea kutunza uoto wa asili uliopo
hivi sasa.
Hifadhi ninyingine ni msitu wa
asili wa Chiwindi yenye ukubwa wa ekari
3000 ambao upo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji. Nyingine ni hifadhi ya misitu ya asili ya
tarafa ya Ruhekei yenye ukubwa wa zaidi ya ekari 2000 ambayo iliyoanzishwa
mwaka 1938 na serikali ya Kikoloni.
Kisiwa cha Lundo ni miongoni
mwa visiwa vilivyopo katika Ziwa Nyasa, kikiwemo cha Lundo kilichopo kata ya
Lipingo na Tarafa ya Ruhekei wilayani Nyasa. Kisiwa hicho kina jumla ya ekari
20 kimepewa jina la Lundo kwa sababu watu wa kwanza waliovuka kisiwa hicho
kwenda ng’ambo ya pili walifikia kijiji cha Lundo.
Taarifa za Maliasili ya mkoa wa
Ruvuma inaonyesha kuwa kisiwa hicho tangu zamani kilikuwa na manufaa makubwa
kwa wananchi wa vijiji vya Lundo, Ngindo na Chinula kwa sababu wakati wa vita
ya Majimaji vilivyotokea kati ya mwaka 1905 hadi 1907 watu walikuwa
wanakimbilia katika kisiwa hicho ambacho kina maeneo ya maficho.
Baada ya vita ya Majimaji
kuanzia mwaka 1908 kisiwa hiki kilitumika na wakoloni wa kijerumani kuwahifadhi
watu waliopata ulemavu kutokana na ugonjwa wa ukoma ambao baada ya uhuru
walihamishiwa katika makazi ya Ngehe wilayani Nyasa. Serikali imependekeza
visiwa vya Lundo na Mbamba Bay kuwa hifadhi za wanyamapori.
Visiwa hivyo vitakuwa ni
hifadhi ya pekee ya wanyamapori pamoja na samaki wa mapambo wanaozaliana katika
visiwa hivyo ndani ya ziwa Nyasa. Ndiyo kusema vitavutia watalii kufika kusini
na kutekeleza Sera ya nchi ya kufungua biashara ya utalii Kusini. Usikose sehemu ya tatu ambayo nitakupa
simulizi za kushangaza kuhusu wilaya ya Nyasa. Tuwe sote.
ITAENDELEA….
No comments:
Post a Comment
Maoni yako