Nipo kijijini kwetu Lundu kwa
muda wa mwezi mmoja sasa. Naendelea kukusanya taarifa mbalimbali zinazofaa
kuchapishwa hapa barazani “Karibuni Nyasa”. Kama tunavyoona habari mbalimbali za utalii,
basi ndivyo utakavyosikia habari usizowahi kuzijua kutoka mwambao wa Ziwa
Nyasa. Mazingira yanayovutia mno, yenye kuhitaji kutembelewa.
Kuna picha mbili; ya kwanza
nikiwa katika Mto Chipapa, uliopo mtaa wa Likwambe hapa hapa kijijini Lundu. Ni
mto ambao miaka 1990 ulikuwa ukitiririsha maji yake mwaka mzima kwa ufasaha. Lakini
sasa mambo yamebadiliika, hakuna uwezekano huo. Kwahiyo mto huo unangojea msimu
wa masika kama hivi sasa uweze kuwa na maji ya kutiririsha hadi Ziwa Nyasa.
Safari yangu katika eneo hilo
lilikuwa kufuatilia uchomaji wa Mkaa, ambao haujawahi kufanyika hapa kwetu
Lundu. Nyaka hizi maisha yamebadilika, watu wanahitaji zaidi mkaa, majiko ya
mkaa na unga wa sembe kwaajili ya chakula. Utegemezi wa unga wa Muhogo
umepungua.
Picha ya pili nikiwa na wanafunzi
wa Shule ya Msingi Lundu. Wanafunzi wanaoonyesha uchu wa kutafuta maarifa
ingawa mazingira yamekuwa yakiwabana kidogo. Kwa hayo machache nawatakieni
maandalizi mema ya Noeli na mwaka mpya.
Kizito Mpangala
Lundu, Nyasa
12 desemba, 2017.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako