February 19, 2018

FEROUZ, BABA YAKO YUPO KIJIJI CHA MATIMBWA, BAGAMOYO

Na. HONORIUS MPANGALA
MAISHA kama yalivyo na tafsiri pana kwa binadamu tunaoishi katika hii dunia,inatufanya tusiwe na maana halisi.Ujana kwa jinsi zote mbili yaani ya kike na ile ya kiume una changamoto nyingi.  

Waswahili husema ujinga wa ujanani ndio umaskini wa uzeeni. Katika umri huo yatupasa kujiandalia kila aina ya mazingira ili tuweze kuwa na uwepesi katika kutimiza majukumu yetu uzeeni. Unamjua msanii wa bongo fleva aliyesifika kwa kutoa wimbo ambao ulikuwa na ujumbe mzito wa Starehe. Anaitwa Ferouz Mrisho kama watanzania wanavyomfahamu. Kabla ya hapo alikuwa kundi la Daz Nundaz pamoja na Daz Baba.

Inadaiwa aliyekuwa rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa alipata kumpa zawadi ya gari kwa kazi yake nzuri aliyeshirikiana na mbunge wa sasa wa jimbo la Mikumi Joseph Haule maarufu kama Prof. Jay.
Sasa katika vitu ambavyo hawavifahamu kutoka kwa Msanii Ferouz ni kwamba, hamjui baba yake na hajawahi kumwona. Aliwahi fanya na mahojiano na moja vituo vya redio na akakiri kulelewa na mzazi mmoja ambaye ni mama na akisema baba yake yuko Bagamoyo ila hamfahamu.

Nilipoanza na neno maisha kuwa na tafsiri pana ni kutokana na kile nilichofahamu kupitia yale niliyosikia kutoka kwa Baba yake Ferouz. Nimemfahamu. Nimepafahamu nyumbani kwake. Nimeongea nae katika mazungumzo ya kirafiki sana. Anaitwa Mzee Shomary Omary Makwaruzo maarufu kama Tito. Yuko kijiji cha Matimbwa wilayani Bagamoyo.

Haikuwa rahisi kulijua hilo kwani nilimshangaa kwa umri wake Mzee wa makamo lakini simu yake huita kwa wimbo wa Kamanda ulioimbwa na kundi la Daz Nundaz, hoja ilianzia kwenye wimbo. Katika hali ya kuzungumzia Maisha ya msanii huyo ndipo Mzee Tito aliposema maneno haya. “Baba yake Ferouz anaishi kijijini, hakujitokeza wakati mtoto huyo kazaliwa. Alikuwa anafanya kazi uwanja wa ndege, zamani alikutana na mama yake Ferouz. Mkimwona hamtoweza kuamini,” alisema Mzee Tito. 

Wakati anatuambia haya mimi na rafiki yangu Mathayo tukabaki kuwa kawaida kwasababu ni vitu ambavyo havishangazi sana kwani wako wachezaji au wasanii waliotelekezwa na wazazi wao hasa baba na kuacha malezi kwa mama.

Tukiwa katika shamba lake akinichumia Nazi ili niweze kula madafu ndipo anapotuambia tena. “Baba yake Ferouz ni Mimi”. Kila mmoja akili ikaenda haraka kwa Ferouz na kurejea kwake na kuona anachokisema kina uhalisia ndani yake.

Mzee Tito kama anavyojulikana kijijini hapo alikiri wazi alipokuwa kijana, alikuwa ‘msela’ mno. Ananiambia alifanya kazi uwanja wa ndege baadaye akaenda kupata kazi katika kiwanda cha kiwanda cha kutengeza Bia cha kampuni ya TBL.

Moja ya sababu kubwa anayoisema kutokuwa karibu na Ferouz ni kwamba anafahamu kama mtoto wake huyo hamjui. Hii ni kutokana na mazingira yake aliyokuwa amejiweka tangu awali wakati msanii huyo akiwa mchanga kwa mama yake. Hakumhudumia tangu angali mdogo. Ni kama anayoongea haya akiwa katika hali fulani ya kujisikia aibu lakini kutokana na ucheshi wake na alivyokuwa mtu wa kupenda masihara unaweza kuona ni jambo la kawaida.

Tukiwa njiani kurejea nyumbani kwake tukitoka shamba la Minazi akatuambia anatamani sana siku moja Ferouz amjue kama yeye ni baba yake. Ghafla simu yake ikaita tena, kabla hajapokea kijana mmoja wa makamo akamwambia.
“Nakuona umeweka wimbo wa mwanao wa kuitia simu.”  Jibu lake lilituacha hoi. Alimjibu kuwa na wewe uzae mwanao awe msanii tuweke nyimbo zake katika simu.

Tulipofika nyumbani kazi niliyokuwa nayo ni kuendelea kuchokoza maswali kuhusu maisha yake. Lengo nijue huo usela anaosema je kuna chochote akichonufaika nacho?

Baadaye akaniambia ana nyumbani zaidi ya mbili katika mji wa Mlandizi na zote amezipangisha. Na hapo kijijini anamiliki nyumba ya kulala wageni inayoitwa ‘Baraka Guest House’ ukitokea Mlandizi iko upande wa kulia kabla ya kufika Matimbwa Magengeni au kama unatokea Bagamoyo mjini iko upande wa kushoto baada ya kupitia magengeni.
Baba yake Ferouz mwenye jakati (wa pili nyuma yangu)
 Hoja yake ya msingi ikabaki pale pale baada ya kumuuliza kuwa kwanini mwanao hakujui. Alisema, “Natamani sana Ferouz anijue ila sijajua ni namna gani tutafahamiana licha ya kwamba mimi namfahamu kupitia kazi zake za kimuziki. Akasisitiza hakuna ninachokihitaji kutoka kwake kwasababu kama maisha nilikwishayatafuta ila kinachobaki ni kufahamiana tu na kutambuana.”
Watanzania mwambieni Ferouz baba yake yupo. Ni mzima wa afya, mcheshi mjanja sana. Anapenda kuongea na watu wa rika yoyote bila kukwaruzana nao. Ile hoja yake ya kusema alikuwa msela sana nyakati za ujana, ukikaa naye kwa muda mfupi utakubariana naye.

Wako watu maarufu ambao wamekutana na haya kama ilivyotokea kwa Ferouz. Na baadaye watu wakayamaliza na maisha yakaendelea. Hatuwezi kuingilia maamuzi ya mtu na kuhoji vitu vingi ambavyo haviwezi kusaidia pale watu wanapohitaji suruhu ya yale yaliyokwisha kutokea.

Yaliwahi kumkuta mchezaji wa Manchster United, Paul Pogba, pale baba yake alipoitelekeza familia. Mahangaiko ya dunia pamoja na changamoto ndogondogo zikaifanya familia itumie njia ya soka kuweza kujinasua na maisha magumu yaliyokuwa nanhata hivyo Baba yao waliweza kuungana naye na kuendeleza familia. 

Kuna wakati wanaume hujikuta wakifanya maamuzi ambayo kwa imani yao kuwa watakuwa wanafanya hivyo ili kuepusha shari la kimahusiano baina ya baba na mama. Lakini ukweli wanakosea kwani malezi ya mtoto ni muhimu kwa kuyapata kutoka pande zote mbili kama inavyohitajika. 

Mzee Tito licha ya yeye kusema alikuwa msela ujanani lakini amekuwa ni mtu ambaye aliwekeza kupitia majengo. Hivyo anaposema yeye lengo lake ni Ferouz amfahamu tu anasema hayo akimaanisha kwani hana cha zaidi cha kuhitaji toka kwake zaidi ya utambuzi wa kimahusiano kati ya baba na mtoto.
Ferouz ukifika kijiji cha Matimbwa hata mtoto mdogo ukimuuliza nyumbani kwa Mzee Tito wapi atakufikisha. Ni maarufu hata jamii inajua kama baba yako ni huyo ambaye siku zote umekuwa ukisema simjui ila unasikia anaishi Bagamoyo.

0628994409

No comments:

Post a Comment

Maoni yako