March 01, 2018

USHAURI KWA RAIS: NAKUOMBA KUBALI TUENDELEE KUCHANGISHANA

NA.HONORIUS MPANGALA
KWANZA kabisa nianze na kukusalimia shikamoo mheshimiwa Rais wangu, Dk. John Pombe Magufuli. Najua hii kazi ni ngumu kama usemavyo wewe mwenyewe lakini sina budi kukuombea uione nyepesi ili uweze kupata nguvu ya kututumikia vyema kama yalivyokuwa malengo yako siku unaenda kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo.

Mheshimiwa nikiwa safarini kuelekea makao makuu ya nchi yetu Dodoma, katika gari nilipata tafakuri  ambayo ilinifanya nitoe kitabu changu cha kuandika kumbukumbu na kuhifadhi mawazo yangu ambayo nimeona nikuandikie. 

Hoja yangu kubwa ambayo ilikuwa ikizunguka katika kichwa changu ni ile niliyokumbuka kauli yako ya kupiga marufuku wananchi kuchangishwa mchango wowote katika shule za serikali.


Hii ilikuwa baada ya kukaa na waziri wa elimu, sayansi na teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako pamoja na Waziri wa Ofisi ya Rais Tamisemi,  Selemani Jaffo. Siku zote kauli ya rais ni kauli ya serikali. Hivyo hata kilichotamkwa binafsi nilikipata kwa sura ya kauli ya serikali.

Rais wangu, tangu zamani katika makuzi ya watanzania nyakati hizo wakiitwa watanganyika walikuwa watu waliokuwa wanafuata misingi ya kijamaa. Misingi ambayo rais mwenzako wa awamu ya kwanza mheshimiwa Mwalimu Nyerere aliifuata Azimio la Arusha lililofanyika mnamo mwaka 1967 lilikuwa na kauli mbiu ya “Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.”

Katika hali ya kawaida mheshimiwa rais kila mtanzania anaweza kutambua maana ya ujamaa na kujitegemea vyema kabisa. Kama inavyofahamika ujamaa ni hali ya kuwa pamoja kwa kujaliana na kuthaminia kwa kiwango kinacholingana kwa kila binadamu lakini pia,kujitegemea ni hali ya mtu kuweza kumudu kujitafutia riziki kwa kutumia maarifa yake na kuishi. Yawezekana nikawa sio mtaalamu wa kutoa maana ya siasa lakini kwa mazingira ya azimio la Arusha ilihitaji siasa itakayokuwa ikifanyika ilenge ujamaa na kujitegemea.

Kama ilivyo kumbukumbu ya malengo ya azimio lenyewe ambavyo ni vinne ni watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora lakini pia ilikuwa kupambana na ujinga, umaskini, magonjwa na dhuluma miongoni mwa raia. Katika kupambana na ujinga elimu ilitolewa bure kwa watu wote katika ngazi zote. 
 Sasa mheshimiwa rais kama wananchi wako wanataka kukusaidia kujitatulia changamoto kwa uwezo wao  wakilienzi azimio la Arusha katika kipindi hiki ambacho elimu ni bure pia kwanini ukataze? Natambua michango inayotolewa bila hiyari ya mwananchi inakuwa kama kero, lakini wakati mwingine yawezekana kuna muhtasari ambao unaonyesha maridhiano na makubaliano yaliyowekwa na wananchi juu ya mchango fulani.

Mheshimiwa rais hivi umekataza hata kile ambacho kiliazimiwa katika mkutano wa wazazi wa shule kuwa wamchangie Mwalimu Shaabani Malunde aliyehitimu  Chuo Kikuu ili awafundishe masomo ya Fizikia na Kemia wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Nyakitonto, iliyopo Kata ya Nyakitonto wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma? 

Je, wale wanafunzi waliokosa mwalimu wa Fizikia, Commerce, Book Keeping na Bailojia katika Shule ya Sekondari ya Monica Mbega iliyopo Kata ya Mbaha, wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma nao wasichangishane kama muhtasari wa makubaliano ya mkutano wa wazazi kuamua kumtafuta mwalimu wa kufundisha watoto wao kama walivyokubaliana na bodi ya shule?

Vipi wale wanafunzi ambao wazazi wao kupitia mkutano mkuu wa wazazi waliowaonea huruma watoto wao kwa kupoteza idadi ya vipindi vya mchana kwa kukaa darasani wakiwa wanasinzia kwa njaa kutokana na kutoenda kula chakula mchana kwao ni mbali au walioenda na wakapoteza vipindi viwili kila siku. 

Wazazi hao katika ajenda ya mengineyo wakasema tunachanga mahindi Sado tatu kwa kila mwanafunzi ili wote wale chakula shuleni nao hutaki wachangishane na wabaki wakishinda bila kula au kupoteza vipindi ilihali ni makubaliano ya mkutano mkuu wa wazazi na wakauandikia muhtasari?

Kama itatokea wakasema wanachangishana kujenga madarasa kutokana na watoto wao kusomea chini ya mti wa mkorosho kama ilivyo kwa shule ya msingi Mchonda iliyopo wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi utawakayalia na kusema serikali italifanyia kazi na masika ndio hii watoto wakinyeshewa mvua?. 

Kwa mtazamo wangu nilifikiria ungewaachia wale wanaofanya hayo kwa lengo kujisaidia wenyewe na watoto wao na ukapiga marufuku ile michango iliyo ya holela isiyo na kikao chochote wala muhtasari wowote ulioandikwa kama makubaliano ya mkutano wa wazazi. Nasema haya kwasababu hili jambo la elimu bure ni zuri lakini kuna changamoto ambazo shule inakutana nazo.

Moja ya vitu ambavyo vimenishangaza mheshimiwa rais ni kile kilichotokea katika Kata ya Ruaha wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro. Kuna shule imekuwa ikifanya vizuri sana katika matokeo ya darasa la saba. Baada ya wazazi kuvutiwa na hali hiyo wengi wakawa wanaenda kuwaandikisha shule watoto wao hapo.

Kwa uwingi wa watoto ilifikia hatua shule hiyo iwe na upungufu wa matundu ya choo. Wazazi kwa kuona umuhimu wa suala la afya ya watoto wao wakachangishana na kutafuta mkandarasi wa kujenga choo. Mheshimiwa baada ya tamko lako wazazi waliitwa na kurejeshewa michango yao ila sasa kilichopo watoto wengine wanakimbia kwenda kujisaidia nyumbani kwao kutokana na uwepo wa foleni katika vyoo vya shule.

Mheshimiwa kama tungekuwa na mawasiliano yenye afya kati ya jamii na viongozi wa serikali za mitaa hakika naamini malalamiko ya michango yasingekuwepo ila ni kutokana na uwepo wa kulalamikiwa kwa watendaji wadogo katika serikali. Nasema hili kwasababu malalamiko ya jamii juu ya watendaji yako kila eneo achilia mbali hili la wakuu wa shule za msingi na sekondari.

Katika Kata ya Tungi  mtaa wa Tubuyu Manispaa ya Morogoro wazazi na  waliamua kushirikiana kujenga vyumba vya madarasa lakini baada ya tamko lako limesababisha hata mtendaji wa eneo hilo kusimamisha ujenzi huo na kusema hana taarifa ya ujenzi huo hivyo upungufu huo utaendelea katika kata hiyo.

Mheshimwa rais inatakiwa ufanye ziara bila kutoa taarifa kwa kiongozi wako yoyote katika shule kama ya Msingi Mpopoma Kata ya Mbaha wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma ukatazame kilichopo pale kuhusiana na mazingira ya kujifunzia na kufundishia. 

Pia unaweza kufanya hivyo kwenye shule ya msingi Shishiyu Kata ya Mwatumbe wilaya ya Maswa halafu upate majibu ya watendaji wako labda wanakuambia kila kitu kuhusu ellimu bure kiko sawa. Labda nikuambie tu mheshimiwa rais hili jambo linaonekana kuwa kisiasa zaidi kuliko kufikia malengo yaliyokusudiwa ya dhana ya elimu bure. 

Darasa la kwanza shule ya msingi Murubanga Kata ya Nyakitonto wilaya ya Kasulu wanafunzi 241 wanaojazana chumba kimoja chenye idadi ya madawati 27 unaweza kujiuliza wanakaaje hao wanafunzi lakini pia jiulize wanafundishwaje na mwalimu mmoja? 

Natambua ulikuwa mwalimu lakini kuhusu changamoto za kuhudumia hawa watoto wadogo wa madarasa kama la kwanza na la pili muulize mama yetu Janeth Mgufuli atakueleza ukweli ulivyo.

Ni kama kila kitu mmejitwisha serikali kukitekeleza japo yako maeneo wako wananchi wenye mitazamo tofauti wakaamua kuchangishana ili kutatua matatizo yao. Mheshimiwa rais ziko jamii zinaweza kukusaidia yale yaliyo ndani ya uwezo wao wakafanya jambo ambalo litakuwa msaada kwa serikali yako.

Labda nikushike sikio ile tabia ya udanganyifu juu ya utekelezaji wa miradi bado ipo na mifano iko mingi sana ambayo ukibaini unaweza kusema hakuna faida ya kurasimisha madaraka.

 Mheshimiwa rais sitaki kuuliza kuhusu ahadi zako wakati wa kampeni ya milioni 50 kila kijijii, lakini naomba tu katika Shule zote ungewaambia kama mchango umeridhiwa katika mkutano mkuu ambao mtendaji wa kijiji anakuwa kama mjumbe na pia ni msimamizi wa shughuli za maendeleo akimwakilisha mkurugenzi ni vyema ungeiacha tu. 

Nasema ungeiacha kwasababu licha ya  kuhudumiwa na serikali lakini shule ni mali ya jamii. Maendeleo ya shule ya sekondari Nelson Mandela Kata ya Mkambarani wilayani Morogoro yanahitaji juhudi za wananchi wa eneo husika au ndani ya Kata ndio maana zikaitwa jina la ‘Shule za Kata’. 

Kile ambacho wanakijiji wa Kijiji cha Kazikazi wilaya ya Uyui mkoani Tabora na kijiji cha Mpurukasese wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma watakiamua kwa maendeleo ya shule zao nilifikiri kingekuwa kinaachwa kwasababu hadi wanafikia hatua ya kutatua kero zao wenyewe maana yake wameona uchelewaji wa serikali katika eneo lao.

Ziko jamii zilizofikia hatua ya kuwaajiri walimu kwa kuwapa ‘fedha za sabuni’ ambazo ni kujitoa kwao kwa shule zao na uchungu wao kwa watoto wao hao ungewaacha wakachangishana tu mheshimiwa maana wapo ambao wameingia kidato cha pili lakini hata kujua nini maana fizikia hawajui  na ni shule ya Kata.
Mheshimiwa mwananchi wako naishia hapa, na nikutake radhi kama kosa lolote ambalo utalipata kupitia kalamu yangu. Uhalisia wa maisha kijijini ndiyo yamenisukuma kukuandikia kutokana na uhalisia wa maisha yetu ulivyo.

Baruapepe; mpangalahonorius@gmail.com/ 0753 44 92 54

No comments:

Post a Comment

Maoni yako