WIKI iliyopita tulijadili juu ya matatizo ya filamu zetu katika uteuzi wa
majina na matumizi ya lugha. Jambo la pili tuliona namna filamu hizo
zilivyotongolewa kutoka kwa filamu za nje. Tulitaja filamu
mbalimbali, na sasa tuendelea zaidi ya tulipokomea. Kwa mfano filamu za ‘Deception’,
imechezwa na marehemu Steven Kanumba na Rose Ndauka.
Lakini jina la
filamu kama hiyo lilishawahi kutolewa na waigizaji Michelle Williams, Hugh
Jackman, na Owen Macgregory. Kwenye hadithi ya filamu ya Bongo tunaambiwa mke
anatoka nje ya ndoa yake na kupata bwana wa pembeni, lakini wakiwa kwenye
matembezi yao mwanamke anauwa.
Upelelezi
unafanyika kisha muuaji ni mume halali wa mke. Lipo funzo kwenye filamu ya
Kanumba na Ndauka, lakini itoshe kusema kwenye Deception ya Owen Macgregory na
wenzake, tunaambiwa kulikuwa na danguro wanaliita The List, ambalo lilianzishwa
na marafiki wawili.
Baadaye mwanamke
mmoja anatoweka na kiasi kikubwa cha pesa. Hata hivyo ni mpango ambao
unagundulika vilevile ambavyo muuaji anayetajwa na filamu ya Kanumba na Ndauka.
Filamu nyingine ni ‘The Bestman’.
Kwenye filamu hii
tunakutana na masuala ya ndoa na mapenzi kati ya Robin na Lance, pamoja na
Jordan. Mapenzi yanayosimuliwa kwenye filamu hii hakuna tofauti na The Bestman
ilitotolewa hapa Bongo ikiwa na maudhui yaleyale ya ‘bestman’ wa harusi
anampindua bwana harusi na kumchukua bibi harusi.
Mwishowe filamu
hiyo inaonyesha kuwa mauaji yanatokea, vivyo hivyo kwa filamu yetu ya Bongo,
ambapo Gabriel (Mlela) anarejea kutoka masomoni nje ya nchi kwa ajili ya kuwa
Best Man, siku mbili kabla ya ndoa hiyo ya rafiki yake Morris (Hemed) na Noreen
(Mariam) lakini siri iliyofichwa na Gabriel & Noreen kwa muda mrefu
inafichuka.
Ni kisa kilekile
kichosanifiwa kwa kusema Gabriel alikuwa masomoni ughaibuni, lakini filamu
yenyewe fani na maudhui yake haykuna tofauti na The Bestman ya akina Lance na
Jordan. Kuna filamu
nyingine ya What Is It ambayo iliingia sokoni hapa Bongo muda mrefu kidogo. Lakini
maudhui ya filamu hii yanashabihiana na visa alivyotengeneza Crispin Glover.
Tofauti yenyewe ni
kwamba Glover ameongeza suala la visa vya kishetani, lakini mikasa inayotokea
inalingana nay ale yaliyoko kwenye filamu ya Bongo. Pengine watetezi watasema
ni mgongano wa mawazo.
Lakini kuna jambo
la kujiuliza zaidi kwamba huu mgongano wa mawazo unatokea kila siku hadi fani
na maudhui yake yakilingana kwa kila jambo? Ni vema wasanii wetu waamke na
kufahamu kuwa wapo wanaofuatilia filamu kila siku, ndani na nje ili kujua
ulimwengu huo ukoje na kipi kinaingia sokoni.
Tukikumbusha
uteuzi wa majina ya filamu ni vema kuangalia matumizi sahihi ya lugha.
Haiwezekani filamu ikapewa jina ambalo linaleta utata. Lazima wasanii wetu
waangalie mfano bora uliopo kwenye filamu ya Ulimi ya Jackline Wolper Masawe.
Kwanza ni jina la
filamu kujenga udadisi kulikoni ‘Ulimi’, kisha humfanya mteja awe na shauku
zaidi hasa anapoona kitu kilichozoeleka lakini anapaswa kujihadhari nacho.
Hakuna filamu
inayoweza kupigiwa kelele iwapo itazingaitia ujuzi au utunzi ambao una fani na
maudhui tofauti na nyinginezo za ughaibuni. Lakini kwa wasanii wenyewe
wanatakiwa kutazama filamu nyingi ili kuepuka migongano huku hadhira ikiwaona
kama hawana jambo jipya.
Hakuna njia
nyingine hapo zaidi ya kuzingatia matumizi ya lugha, maana ya maneno, kuacha
kutongoa filamu za nje, kuwa wabunifu zaidi, kutengeneza fani na maudhui
yanayorandana na mandhari yetu. Haya yatawafanya wasanii wawe bora zaidi kwa
kazi zao ili kuepusha utata huo.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako