Wiki iliyopita
niliandika makala iliyokuwa na kichwa, “Imani yako inasadifu fedha zako”. Kama
ilivyo ada nimepokea mirejesho mingi kwa baruapepe, simu za miito na jumbefupi.
Wasomaji wamekuwa na mitazamo tofauti tofauti wengine wakiipongeza makala ile
na wengine wakionesha dukuduku.
Pia wapo wachache wamepinga kabisa uthubutu wangu wa
kuchambua fedha katika sura ambayo wanadai nahamasisha watu kutafuta fedha.
Hawa ni wale ambao wanaamini “fedha si nzuri kwa sababu inaharibu tabia za
watu”
Nilivutiwa sana na
mchango wa msomaji mmoja kutoka Arusha aliyeniandikia baruapepe ifuatayo, “Bw.
Sanga nakupongeza sana kwa makala zako. Unaandika ujasiriamali na mambo ya
kujitambua in unique style kiasi kwamba kila ninaposoma makala zako napata
ladha na impact kubwa mno. Kwenye makala yako ya leo umeeleza vizuri mno kuhusu
imani za fedha”
“Loo! Makala hii
imenisaidia na kuniokoa mno kwa sababu nimekuwa na kawaida ya kushiriki
gossiping kuhusu wenye fedha. Mfano hili la kuamini kuwa kuna makabila
yanafanikiwa kwa sababu ya wizi ama ushirikina nimekuwa ninaamini pasipo kujua
kuwa ninaathiriwa na imani hizo”.
Na Albert Sanga, Iringa |
“Hata hivyo Bw. Sanga
ninaomba unisaidie nawezaje kuzalisha fedha za kunitosha? Kwa sababu mimi ni
mwajiriwa lakini kadiri siku zinavyoenda ninaona majukumu yanaongezeka na
mshahara naona hautatui mahitaji yangu vizuri, maisha ni magumu, nikitafiti
naona biashara karibia zote zimeshafanyika, Je, nitafanya kitu gani ama namna
gani ili niweze kuzalisha fedha? Narudia tena kukupongeza na ninaamini
utanisaidia katika hili” Mwisho wa kunukuu.
Katika makala haya leo
ninajibu swali la msomaji huyu aliyeniuliza, “Nawezaje kuzalisha fedha za
kunitosha?” Hata hivyo kabla sijaeleza namna gani mtu unaweza kuzalisha fedha
za kukutosha, ninapenda kueleza kidogo kuhusu dukuduku walilokuwa nalo baadhi
ya wasomaji kuwa fedha siyo nzuri kwa sababu zinaharibu tabia za watu.
Kimsingi fedha imebeba
chembechembe nyingi za kisaikolojia zenye uwezo mkubwa wa kuamsha tabia za mtu
hata zile ambazo hazijapata kuonekana. Mtu mchoyo akipata fedha uchoyo wake
unaongezeka na unakuwa dhahiri. Mtu mwema na mtoaji akipata fedha wema wake
huongezeka na ataonekana akitoa zaidi na zaidi.
Kwa jinsi hii tunaona
kuwa kimsingi fedha haibadilishi wala kutengeneza tabia ya mtu isipokuwa fedha
hudhihirisha tabia na hulka aliyonayo mtu ambayo alishakuwa nayo hata kabla
hajaipata fedha. Fedha naweza kuifananisha na mfumo wa mashine za sauti “Amplifier”.
Kwenye “Amplifier”
ukitoa sauti yako kama ni sauti mbaya ubaya huo utakuzwa na kama sauti yako ni
nzuri basi uzuri wa sauti yako utakuzwa vile vile. Kwa kuwa fedha zina mfumo wa
kukuza tabia, ni vema sana mtu akatumia muda na rasirimali maarifa kujenga
tabia na hulka zake ili fedha inapokuja isilete mushkeli.
Na ninapotaja habari ya
mtu kuwa na fedha isidhaniwe kuwa ninagusia fedha nyingi sana, la hasha! Watu
tunatofautiana sana linapokuja suala la mitazamo na hulka zetu katika fedha.
Wapo watu ambao akiwa na elfu kumi tu mfukoni lazima ujue kwa maana ataleta
vurugu na maujiko kibao.
Mtu mwingine akiwa na
hiyo shilingi elfu kumi mfukoni haoni kama ana fedha, isipokuwa anaweza hata
kukueleza kuwa “sina fedha kabisa”. Kwa mwingine milioni moja sio fedha wakati
kwa mwingine milioni moja ni utajiri!
Kinachofanya mtu mmoja
aone kuwa elfu kumi ni fedha na mwingine aone kama si fedha inatokana na
mtazamo wanaokuwa nao watu hawa katika fedha. Mtazamo huu hauanzi pale mtu
anapoishika hiyo elfu kumi, isipokuwa ni kuwa mtazamo wao ulishajengeka mapema
kabla hata ya kushika hiyo fedha.
Baada ya kusema hayo
sasa nigeukie upande mwingine kulijibu swali la msomaji Yule, “Je, nawezaje
kuzalisha fedha?”. Kwa wale wenye kumbukumbu bila shaka wangali wanaikumbuka
makala niliyopata kuiandika wiki chache zilizopita iliyokuwa na kichwa,
“Tumeamua kuichuuza thamani ya fedha yetu”.
Katika makala hiyo
nilieleza kwa kina dhana na maana ya fedha, lakini pia nilisema fedha sio
mafanikio zikisimama peke yake; isipokuwa fedha ni matokeo ya mtu kufanikiwa.
Fedha inatakiwa kumjia mtu baada ya kuzalisha thamani fulani katika uchumi.
Hapa tunaangalia maeneo kadhaa zinakopatikana fedha.
Kunapotokea mdororo wa
uchumi, mara nyingi mitaani huwa tunasema fedha zimepotea,! fedha hazionekani,! Kitu cha kujiuliza ni
“Je, fedha zinapopotea ama kutoonekana zinakuwa zimepotelea wapi?” Ukweli ni
kuwa fedha zote zilizopo duniani zinazunguka miongoni mwa watu. Idadi ya fedha
huwa haipungui, ila kinachopungua ama kuongezeka ni thamani ya fedha.
Ukiwa na fedha leo na
kesho ukawa huna basi ujue fedha zipo kwa watu. Kwa maana hii ukitaka kupata
fedha ni lazima uzitafute kutoka kwa watu. Fedha zinapatikana kutoka kwa watu. Je,
unazipataje fedha kutoka kwa watu?
Watu katika maisha ya
kila siku wanakabiliwa na changamoto na matatizo mbalimbali. Unapochukua wasaa
wa kutatua changamoto na matatizo yao ni lazima utapokea ujira wa utatuzi wako.
Hii ina maana kuwa wakati wote ikiwa unahitaji fedha ni lazima uwe ni mtu
unaetazama matatizo na changamoto kama fursa za kukusaidia kupata fedha.
Tunaposikia kuwa
Tanzania inakabiliwa na tatizo kubwa la ajira; kuna makundi mawili ya watu
yanayolitazama hili kwa mitazamo tofauti. Mosi wapo wale wanaosimama upande wa
kulalamika na wakitazamia kuhurumiwa. Ni vema wasomaji mkafahamu siri hii: kihisia,
fedha ni kama ina masikio, haitaki malalamiko haitaki manung’uniko!
Ukizoea kulalamika na
kunung’unika ovyo unaifukuza fedha! Lakini ukichunguza upande wa hawa
walalamishi na wanung’unikaji sana; utagundua kuwa wengi wao huamini kuwa
kushindwa kwao ikiwemo kiuchumi(kifedha) ni matokeo ya uzembe ama
kutokuwajibika kwa wengine.
Kundi la pili ni wale
wanaofikiri namna ya kuikabili na kuitatua changamoto hii. Ndani ya kundi hili
la pili ndimo wanakopatikana wale wanaoamua kujiajiri lakini ninaowakusudia
zaidi hapa ni wale wanaowasaidia wengine kujiajiri. Hawa ni kundi la watu
wanaoamua kufanikiwa katikati ya matatizo na changamoto.
Ndio maana ukichunguza
kwa umakini utabaini kuwa, watu wanaofanikiwa katika jamii zetu katika maeneo
mbalimbali (ikiwemo kifedha) huwa wako “bize” na mambo yao, hawana muda wa
kulalamika wala kunung’unika ovyo. Wanaofanikiwa mara zote huwa hawawanyooshei
vidole watu wengine kutokana na kushindwa kwao. Wanaofanikiwa huamini kuwa
wanawajibika kwa sehemu kubwa katika mafanikio yao.
Kwa kuwasaidia wengine
kuweza kujiajiri kundi hili hufanikiwa kujipatia fedha. Unapotatua changamoto
ama tatizo lolote kiubunifu ni lazima unufaike. Tunatakiwa tufahamu kuwa
matajiri wote duniani wameupata utajiri wao kwa kutatua changamoto na matatizo
waliyoyabaini miongoni mwa watu. Fedha zinapatikana kwenye matatizo na
changamoto
Tunapoangalia kuwa
fedha zinapatikana kwa kutatua changamoto na matatizo tunajiuliza, Je,
unawezaje kutatua hayo matatizo na changamoto? Jibu lipo hivi: Ili kutatua
tatizo ama changamoto ni lazima ubuni bidhaa na huduma zinazojibu matatizo na
changamoto hizo. Watu walipoonekana wanatembea peku na kuhatarisha afya zako,
alitokea mtu akabuni viatu.
Mpaka leo tunawalipa
wanaotengeneza viatu. Baada ya kuona watu wanahitaji kusafiri kwa haraka na kwa
ufanisi, walitokea waliogundua ndege na hadi leo tunawalipa watu mbalimbali
wanaofanikisha usafiri huo kila tunapotaka kusafiri. Kila bidhaa unayonunua ama
huduma unayolipia unatakiwa kutambua kuwa ni matokeo ya ubunifu wa
wajasiriamali uliochagizwa na changamoto na matatizo waliyaona miongoni mwa
watu.
Wapo wajasiriamali
mbalimbali ambao wamechangamkia fursa zilizotokana na ukosefu wa ajira na sasa
wameanzisha makampuni yanayotoa huduma za kiushauri na kimafunzo kuwawezesha
watu kujiajiri. Hivyo tunaona kuwa eneo jingine ambako fedha zinakaa ni katika
bidhaa na huduma
Njia rahisi ya
kubuni bidhaa na huduma zitakazowavutia
wengine kukuletea fedha ni kutumia karama na vipaji vyako. Kama wewe ni
mwimbaji, ukiimba nyimbo nzuri moja kwa moja utauza nakala na utatumbuiza
katika matamasha. Kama wewe ni daktari mwenye uwezo na kipaji kikubwa cha
kutibu kwa ustadi, ni lazima watu watakuja kupata huduma na kukuletea fedha. Ndani
ya karama na vipaji ndiko zinakopatikana fedha.
Kitu ambacho tunatakiwa
kuepukana nacho ni mawazo ya kupata fedha za mkato-mkato. Shida ya fedha za
mkato-mkato kama ufisadi, wizi, utapeli, udokozi na uhujumu; sio ile hatari ya
kukamatwa na kufungwa jela; isipokuwa zipo hatari kubwa zaidi ya hapo ambazo
ndizo ambazo mimi daima huzitambulisha.
Ukifanya ufisadi kazini
na ukajipatia fedha kasha ukajenga majumba na kuanzisha miradi lukuki, hata
usipokamatwa usidhani upo salama! Kuna kitu kinaitwa hukumu ya moyoni
“Spiritual Condemnation” ambacho kinaweza kukutesa sana. “Spiritual
Condemnation” ni hatia anayokuwa nayo mtu kwa ndani kutokana na njia alizotumia
kupata fedha zake.
Hili la madhara ya
kutafuta fedha na mafanikio kwa njia
zisizohalali linahitaji makala ya peke yake. Hata hivyo kitu cha kufahamu na
kuamini ni kuwa inawezekana kupata fedha na utajiri kwa njia halali; huna
sababu kupita njia za mikato zitakazokutesa unapofanikiwa. Nihitimishe kwa kusema kuwa inawezekana na
tena ni rahisi kuzaisha fedha ikiwa tutajizoesha kuyafuatilia na kuzingatia
maeneo niliyoyataja ambako fedha zinapatikana!
Ni haki ya kila
mtanzania kuwa na fedha za kutosha
No comments:
Post a Comment
Maoni yako