Mheshimiwa
Mwenyekiti wa Kamati,
Mnano tarehe 13
Septemba, 2017 nilipata wito wa kufika mbele ya Kamati yako kutoa ushahidi wa
masuala mbalimbali. Nilipata wito husika saa nane na dakika 40 mchana,
nikitakiwa kufika mbele ya kamati yako, hapa Dodoma saa saba mchana siku hiyo
hiyo.
Nililetewa wito
huo na RCO Mkoa wa Kigoma nikiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani la
Manispaa ya Kigoma Ujiji. Sikuweza kufika, isingewezekana katika mazingira hayo
niwe na uwezo wa kusafiri kutoka Kogoma na kufika mbele ya kamati yako hapa
Dodoma. Kwanza muda ulishapita, lakini hata taratibu za kiusafiri pamoja na
umbali kati ya Kigoma na Dodoma hazikuwezesha Jambo hilo.
Siku iliyofuata
nilipata ajali, ambapo nyumba yangu iliwaka moto wakati nikiwa njiani kwenda
Nairobi kumuona mbunge mwenzetu mgonjwa, ndugu Tundu Lissu. Jana tarehe
Septemba 20, 2017 nikiwa natokea Kigoma ili kuja kwenye Kamati nilikamatwa na
Polisi ili kufikishwa mbele ya Kamati yako.
Leo nimefika
mbele yenu na nitajibu wito wenu kama ifuatavyo:
A: Kwamba maoni
yangu kwenye mtandao wa Twitter kuwa "Bunge siku hizi ni Idara ya Tawi la
Utawala" yanadhalilisha Mhimili Wa Bunge.
Maneno hayo ni
ya kwangu na nimeyatoa kama raia wa Tanzania. Ninaamini kwa dhati kuwa Bunge la
Kumi na Moja limekuwa likifanya kazi kwa kuingiliwa na Serikali chini ya ndugu
Rais John Pombe Magufuli.
Maneno na
vitendo vya Rais yanaashiria kuwa Bunge halina Uhuru wake, na mimi kama Mbunge
nina wajibu wa kuonyesha kutopendezwa kwangu na hali hiyo. Nina mifano kumi
(10) kuthibitisha maelezo yangu hayo kama ifuatavyo:
1. Kuzuiwa kwa
"Bunge Live" kwa kisingizio cha kupunguza gharama za uendeshaji wa
mhimili wa Bunge, wakati Mikutano yote ya mhimili wa Serikali, hasa ya Rais
ikirushwa live (mubashara) ni dalili ya wazi ya kufifisha sauti ya Bunge na
kupandisha sauti ya serikali. Hata vituo binafsi ambavyo vilipanga kurusha
bunge Live bila malipo (na hivyo kutokuwa na gharama) vilizuiwa, lakini
vinarusha Live mikutano ya Rais.
2. Kitendo cha
Uongozi wa Bunge kurudisha serikalini shilingi Bilioni 6 bila ridhaa ya wabunge
kwa kisingizio kwamba zimebaki kutokana na kubana matumizi. Hii ni dalili ya
wazi ya Bunge "kujipendekeza" kwa serikali. Wakati Uongozi wa Bunge
ukirejesha kiwango hicho cha Fedha, kuna taarifa kwamba kamati nyingi za Bunge
zinashindwa kutekeleza wajibu wake kwa sababu ya ukata.
3. Maelekezo ya
mhimili wa Serikali kwa mhimili wa Bunge, kupitia maagizo ya Rais Magufuli kwa
Spika Ndugai kuwa "Awashughulikie wabunge" (kwa kuwafukuza bungeni)
aliowaita "waropokaji" ili waje wazungumze nje ya Bunge na yeye Rais
(Serikali) apate nafasi ya kuwashughulikia. Kauli hii ya Rais aliyoitoa wakati
akipokea Ripoti ya Prof. Osoro kuhusu Mikataba ya Madini, Juni 12, 2017
inaonyesha picha iliyo dhahiri kuwa Bunge linapokea Maelekezo kutoka Serikalini
ya kuwadhibiti wabunge hasa wanaoiwajibisha serikali. Na hatuwahi kuliona Bunge
likiyakana maelekezo hayo ya Rais kwa Spika.
4. Kitendo cha
Bunge kuhariri hotuba za kambi ya upinzani kwa kushinikiza kuondolewa kwa
vipengele vinavyoikosoa Serikali. Mathalani, Wakati wa Bunge la Bajeti, hotuba
ya Msemaji wa Kambi ya upinzani wa Wizara ya Mambo ya Ndani, ndugu Godbless
Lema, iliamriwa kuondolewa maneno yanayohusu kashfa ya Mkataba wa Lugumi,
kumhusisha Rais na kuuzwa kwa nyumba za Serikali, Mauaji ya wanasiasa, pamoja
na Bunge kulinda wahalifu.
5. Kauli ya
Rais Magufuli ya Novemba 4, 2016 akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari
kuwa "mzizi wa mhimili wa serikali ni mrefu zaidi kuliko mihimili
mingine" mara baada ya kuulizwa juu ya matumizi ya Serikali Nje ya Bajeti
iliyoidhinishwa na bunge, unaonyesha dhahiri fikra ya Rais na Serikali yake juu
ya ukuu wa mhimili wa Serikali dhidi ya Bunge.
6. Kitendo cha
Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Tanzanite na Almasi kusomwa nje ya Bunge na
kuwasilishwa kwa Waziri Mkuu na Rais bila kuwasilishwa na kujadiliwa Bungeni
ili kuwekewa azimio la Bunge. Kitendo hiki kinaifanya Kamati hiyo kuonekana
kuwa ya Serikali badala ya Kamati ya Bunge.
7. Kauli ya
Rais kuwa Spika alimpigia simu kumuuliza juu wajumbe wa kuwaweka kwenye Kamati
za Bunge za Tanzanite na Almasi inaonyesha dhahiri kuwa Spika anafanya kazi kwa
maelekezo ya Rais. Na Bunge na Spika hawajawahi kuikana kauli hii ya Rais.
8. Kwa mara ya
kwanza kwenye Historia ya Nchi yetu tumeshuhudia Mbunge akishambuliwa kwa risasi
wakati Mkutano wa Bunge ukiwa unaendelea. Haijapata kutokea katika historia ya
Bunge letu, Wabunge kukamatwa hovyo mbele ya mageti ya Bunge na kusafirishwa
usiku usiku bila hata Spika kujulishwa kama taratibu za Mabunge ya Jumuiya ya
Madola zinavyotaka. Kitendo cha 'Watu Wasiojulikana' kummiminia risasi zaidi ya
thelathini Mbunge wa Singida Mashariki, ndugu Tundu Lissu, wakati akitokea
Bungeni, tena kwenye makazi yake, ambayo Kwa mujibu wa sheria ni sehemu ya
Bunge, ni dharau ya hali ya juu kwa Mhimili huu. Ni tukio linalolenga kuliziba
mdomo Bunge. Makala yangu ya Nani alitaka kumwua Tundu Lissu (kwa lugha ya
Kiingereza) naiambatanisha katika maelezo yangu haya.
9. Kitendo cha
Serikali kutowasilisha 'Taarifa za Utendaji wa Robo Mwaka' kwenye Kamati ya Bunge
ya Bajeti kama inavyotakiwa kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti ya mwaka 2014 ni
dharau kubwa kwa Mhimili wa Bunge. Ni dharau zaidi kwamba Serikali ilileta
Muswada wa sheria kuondoa kifungu kinacholazimisha Waziri wa Fedha kutoa
Taarifa hizo, na Bunge kupitisha kuwa Sheria, hivyo kuondoa kabisa Uwajibikaji
wa kibajeti wa Serikali ndani ya Bunge, hivyo kudunisha hadhi ya bunge.
10. Bajeti ya
Bunge kutowekwa kwenye Mfuko wa Bunge kwa mujibu wa sheria, na Spika kutakiwa
kuomba vibali vya safari za Wabunge kwa Mkuu wa Tawi la Utendaji (Serikali) ni
maelezo tosha kuwa Bunge ni Tawi la Utendaji na sio Mhimili unaojitegemea.
Mheshimiwa
Mwenyekiti
Ninayo mifano
mingine mingi tu ya kuonyesha kama ushahidi wa jambo hili, kwa sasa hiyo 10
naomba itoshe.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Kwa mujibu wa
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nchi yetu ina mihimili mikuu mitatu
ya dola ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama. Katiba na Sheria mbalimbali za
nchi zimewekwa kuhakikisha kila mhimili unafanya kazi kwa uhuru bila kuingiliwa
na mhimili mwingine.
Kikatiba, mbali na wajibu wake wa kutunga sheria, Bunge lina wajibu wa kuisimamia serikali. Kwa lugha nyingine, katika utekelezaji wa majukumu yake, Bunge ni "Kiranja" wa kuibana na kuisimamia Serikali.
Kikatiba, mbali na wajibu wake wa kutunga sheria, Bunge lina wajibu wa kuisimamia serikali. Kwa lugha nyingine, katika utekelezaji wa majukumu yake, Bunge ni "Kiranja" wa kuibana na kuisimamia Serikali.
Tangu kuingia
madarakani kwa serikali ya awamu ya tano, kumekuwepo na kauli na matendo ya
viongozi wa serikali na Bunge yanayoashiria uelekeo wa serikali kuminya na
kuingilia uhuru wa Bunge. Baadhi ya vitendo hivi vimefanywa hata na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa kutambua wajibu wangu katika kulinda
heshima, uhuru, hadhi, haki, ufanisi na madaraka ya Bunge katika kutekeleza
majukumu yake, mara kadhaa nimekumbusha na ilipobidi kuonya ndani na nje ya
Bunge dhidi ya vitendo hivi.
Maoni yangu
yaliyonifanya niitwe hapa, pamoja na Mifano kumi (10) niliyoitoa hapo juu
vinaonyesha wazi nia yangu njema ya kuonya na kutaka kulindwa kwa hadhi,
heshima, haki na madaraka ya Bunge letu tukufu. Naamini bunge lilipaswa
kunipongeza ni kunishajiisha kwa kazi hiyo, na si kinyume chake ninapotuhumiwa
na kuletwa mbele ya Kamati yako kuwa nimelidhalilisha bunge pamoja na spika wa
bunge. Jambo hili litavunja morali ya wabunge kutetea hadhi ya bunge letu.
Mheshimiwa
Mwenyekiti (Mzee George Huruma Mkuchika)
Wewe ni
miongoni mwa wazee ninaowaheshimu sana hapa nchini, nilivyo sasa kwa kiasi
kikubwa ni sehemu ya malezi yako kwangu hapa bungeni, umeshiriki kunifinyanga
niwe mbunge imara kwa busara na hekima zako, pamoja na kunipa ujasiri wa
kuisimamia kutokana na uzoefu wako. Nakutambua kama muumini wa Siasa ya Ujamaa
na Kujitegemea, iliyotangazwa kupitia Azimio la Arusha. Napenda ninukuu sehemu
ya Azimio la Arusha kuhusu Uhuru wa mawazo. Azimio linasema "kwamba TANU
inaamini: kila Raia wa Tanzania ana haki ya Uhuru wa Mawazo..."
Napenda
kusisitiza kuwa kama Mtanzania ninao Uhuru wa Mawazo na Maoni, hiyo ni kwa
mujibu wa Katiba yetu, Ibara ya 18. Kitendo cha mimi kuitwa mbele ya Kamati
yako kwa maoni yangu haya, naamini ni mwendelezo wa kufinywa kwa haki na uhuru
wa mawazo na maoni ya raia.
Mimi kama
mtanzania ninaruhusiwa kuwa na maoni yangu, na pia nina haki ya kutoa maoni
yangu hayo. Kunituhumu kwa maoni yangu binafsi kuwa yanavunja heshima, hadhi,
haki na mamlaka ya bunge, na kuwa maoni yangu hayo ni kulidhalilisha Bunge na
Spika si sahihi kabisa, ni uonevu dhidi yangu, ni ukiukwaji wa Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni kinyume na Haki za Binadamu, hasa kwa kuwa
mifano hiyo 10 niliyoitoa imeonyesha usahihi wa maoni yangu hayo.
Maoni yangu
yalilenga kulinda hadhi, haki, heshima na madaraka ya bunge letu tukufu. Ni
maoni yaliyolenga kulinda heshima ya spika, ili azitumie nguvu alizonazo kwa
mujibu wa Katiba na Kanuni za Bunge kulinda heshima na hadhi ya Bunge
isiporomoke, ni maoni yaliyolenga kuonyesha imani niliyokuwa nayo juu yake
(Spika), ni maoni yaliyolenga kulizindua Bunge juu ya hali ya kukosa
mshawasha/msisimko ambao Watanzania wameuzoea.
Tafsiri kuwa
maneno yangu kuwa Spika hajafikia viwango vya Maspika waliotangulia kabla yake
kuwa ni kumdharau si sahihi. Maoni yangu hayakulenga kuonyesha dharau, bali
yalilenga kutaka Bunge liyalinde yale mambo mazuri yaliyosimikwa na Maspika hao
wa nyuma katika kuisimamia Serikali.
Jambo hili (la
kutaka kuendelezwa na kulindwa kwa mambo mazuri ya maspika wa nyuma
yaliyoimarisha hadhi ya Bunge) ni ahadi ya Spika wetu, ndugu Ndugai, wakati wa
kikao maalum cha Bunge cha msiba wa Spika wa Bunge la 9, ndugu Samuel John
Sitta. Hivyo ni dhahiri, mimi kukumbushia ahadi hiyo ya Spika mwenyewe haiwezi
kwa namna yoyote ile kuwa ni kudhalilisha Bunge na kumdhalilisha Spika, bali
kitendo cha kuitwa hapa mbele ya kamati yako kwa maoni yangu binafsi nje ya
bunge, maoni yaliyolenga tu kukumbushia ahadi husika, hakika kinalidhalilisha
Bunge na Spika wa Bunge
Kuona mawazo
huru haya yangu kuwa ni kudhalilisha Bunge si sawa. Ni kinyume kabisa na
misingi ya TANU iliyoasisi Utaifa wetu, ni kinyume na Utanzania wetu. Wananchi
wangapi wataletwa mbele ya Kamati yako kuhojiwa kwa kutoa maoni yao juu ya
hadhi ya mhimili wa Bunge?
Imani yangu ni
kuwa, Hadhi, Heshima, Haki na Madaraka ya Bunge haitotokana na kuhoji wanaotoa
maoni juu ya mwenendo wa bunge, kutumia maguvu ya Jeshi la Polisi, wala vitisho
vya Kiongozi wa Mhimili wetu huu dhidi ya wabunge, bali ni mwenendo wake wa
kuisimamia Serikali mbele ya umma ndio utakaojenga hadhi, heshima, haki na
madaraka ya Bunge kwa wananchi.
Mheshimiwa
Mwenyekiti
Iwapo Bunge
litaendelea kuwa 'paraded ' Ikulu kila wakati na kupewa maelekezo na wakati
mwengine kusimangwa na Serikali, kupitia Rais, umma utaona sio Bunge lao bali
ni Tawi tu la Serikali, na kamati yako itakuwa na kazi ya kuita maelefu ya
Watanzania.
Nawashukuru
sana kwa kunisikiliza.
Naomba
Kuwasilisha.
Kabwe Zuberi
Ruyagwa Zitto
Mbunge, Kigoma Mjini - ACT Wazalendo
Dodoma
Septemba 21, 2017
Mbunge, Kigoma Mjini - ACT Wazalendo
Dodoma
Septemba 21, 2017
No comments:
Post a Comment
Maoni yako