September 18, 2017

SHAIRI; JOHO

NA KIZITO MPANGALA

Joho tuloahidiwa,
Na yeyote kuvaliwa,
Atakayechaguliwa,
Afrika nakwambia.

Joho lenye kupendeza,
Halitaki makengeza,
Kilivaa tapendeza,
Kwa makini sikiliza.

Demokrasia twasema,
Nayo katiba ni mama,
Na sote tunasimama,
Maneno haya shahada.



Katiba ndiyo ni mama,
Wanaipiga mtama,
Na joho wanatunyima,
Tulia fikiria.

Rangi yake siijui,
Pengine ni baibui,
Joho halibagui,
Ndivyo wananyosema.

Joho limekuwa chafu,
Linazo nyingi harufu,
Za uchoyo maeadufu,
Zote zinaonekana.

Tena tuliambizana,
Kwa awamu tutavaa,
Wananchi kuamua,
Ni nani wa kulivaa.

Awamu tena ikaja,
Joho tukalitaka,
Alohutimu akana,
Joho chini kuliweka.

Akenda kwa Profesa,
Aiongeze miaka,
Zaidi joho kuvaa,
Na hataki kulivua.

Yalikuwepo Gambia,
Mamia walikataa,
Joho kulipoteza,
Alohitimu kanywea.

Ubishi aliuleta,
Majirani wakateta,
Kuyaondoa matata,
Joho wakalichukua.

Pikiniki ya Uganda,
Shughuli kwa Profesa,
Miaka ya shahada,
Ataka kuiongeza.

Miaka ya shahada,
Iachwe kuhesabika,
Yenyewe itasema,
Nani joho kulivaa.

Awali alitwambia,
Miaka ya shahada,
Ikifika joho vua,
Kwa awamu livaliwe.

Anayepinga apigwe,
Nalo joho anyimwe,
Gerezani apelekwe,
Kamwe joho asionje.

Joho hili livaliwe,
Tena liamuliwe,
Na wananchi wenyewe,
Kwa kuwa ni joho lao.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako