November 23, 2017

FREDDY MACHA ALIVYOLIZUNGUMZIA JUKWAA LA KISWAHILI SOCIETY

NA MARKUS MPANGALA 
SWALI: Naam, shikamoo Mzee Macha?
FREDDY MACHA; Marahaba. Habari zako bwana! uko wapi wewe siku hizi? Maana tangu tuliposalimiana pale Soma Café,Mikocheni na baadaye Nyumba ya Sanaa, Dar es Salaam wakati wa warsha nilizoendesha huko.
SWALI; Nipo hapa Bongo naendelea vema tu. Ni kweli, kitambo hatujawasiliana, pia nilifaidika sana na warsha zako hata hivyo si neno, tutaongea kidogo leo.
Freddy Macha
 FREDDY MACHA; Asante. Nadhani leo unalo la kuongea zaidi. Karibu.
SWALI; Ni kweli, nahitaji mengi kutoka kwako mzee wangu. Kiu yangu ni huu mradi wa Kiswahili Society, kwani umeeleza mahala fulani nikasoma nami nimevutiwa ili niwaarifu wasomaji. Je mradi huu ulianza lini na wapi?
FREDDY MACHA; Umeanzishwa na wanafunzi na Wahadhiri wa Kiswahili pale chuo cha lugha cha SOAS (School of Oriental and African Studies) hapa London,Uingereza.
SWALI: Nini dhumuni la kuanzishwa kwa Kiswahili Society?
FREDDY MACHA; Kuunganisha Wazungumzaji wa Kiswahili duniani lakini hasa hapa Uingereza.
SWALI: Nashukuru sana. Ndugu Macha, wewe ni Mwanamuziki,Mwanafasihi,na Mwandishi mkongwe. Katika fani hizi kuna mambo mengi umejifunza kutoka bara letu la Afrika,Latin Amerika,Marekani na sasa Ulaya. Unadhani jamii za watu wa Ulaya hususani Uingereza zinaweza kuhamasika kukiendeleza Kiswahili? 


FREDDY MACHA: Sio jamii, bali watu. Lugha zote duniani zinakuuzwa na watu wake. Mathalan Wabrazili wanapenda kukitangaza Kireno(lugha yao) kupitia muziki. Muziki wao (Samba) unapendwa duniani na Watunzi wanachangia kuitangaza lugha yao kwa ala hiyo. Hapa Uingereza kuna wapenzi wengi wa lugha ya Kiswahili.
Macha na Asharose Migiro
Wanafunzi wa vyuo kama SOAS, kuna watu weusi waliozaliwa nje ya Afrika hasa kutoka visiwa vya Karibean ambao wanaipenda Bongo kutokana na sifa zake za amani, na weusi wengine wa Afrika Magharibi ambao wanaonyesha mapenzi kwa KIswahili. Rais wa Kiswahili Society kwa 2010-2011 ni Jason Taffs. Halafu wapo watoto wa Waswahili waliohamia huku(Uingereza). Lakini jamii haiwezi kuiendeleza lugha hiyo. Jamii inahamasika kuendeleza lugha pale panapotokea maslahi ya kibiashara. Kwa mfano ukiacha masuala ya sanaa (muziki, vitabu, sinema) watalii wanaweza kuwa wanapenda kujifunza maneno machache wanapokuja kutembelea mbuga zetu. 


SWALI: Bila shaka kila unachoshiriki kukuza mradi huu kinatoa taswira chanya. Je, ni kwa kiasi gani mradi huu unaweza kuwakusanya pamoja wananchi wa Uingereza wanaofurahia Kiswahili?
FREDDY MACHA; Wananchi wa Uingereza wanaokifurahia Kiswahili ni wachache sana. Nguzo kuu ya kuundeleza mradi ni Waswahili wenyewe. Wale wanaoishi huku(Uingereza).
SWALI: Mara nyingi umekuwa ukihamasisha suala la kuboresha lugha ywa kujisomea vitabu. Je jukwaa hili la Kiswahili Society umeandaa mbinu gani kuhamasisha usomaji wa vitabu?
FREDDY MACHA: Ninaifanya kazi hiyo kwa kuongea na kila mtu ninayokutana naye, kutukuza kazi hiyo katika maonyesho yangu ya muziki na fasihi, katika pia kufanya semina Bongo mwaka jana na inshallah siku za mbeleni.
SWALI: Jukwaa la Kiswahili Society linaonekana kuwaunganisha wazungumzaji wa Kiswahili kama ilivyo kwa mradi wa iRafiki au Sekenge. Je nini mipango ya mradi huu kwa miaka mitano ijayo au ni mipango gani aidha mifupi au mirefu kwa jukwaa hili?
FREDDY MACHA: Mradi huu ni changamoto tu ya kuendeleza Kiswahili, ila si kiini. Kiini cha kuendeleza Kiswahili kitakuwa kwa wazungumzaji asilia wenyewe.
SWALI: Jukwaa hili limejiandaaje kukutana na changamoto ya uelewa mdogo wa wazungumzaji wa Kiswahili ambao umekuwa ukirejesha nyuma uboreshaji wa lugha ya Kiswahili?
FREDDY MACHA: Kupitia tovuti yake, na kupitia mitandaoni, ambapo vijana wengi hupata habari siku hizi.
SWALI; …Kama unavyosema kwamba Bongo siku hizi Kiswahili kimekuwa kibovu sana. Wewe unadhani tatizo hilo linasabishwa na nini?
FREDDY MACHA; …Kwanza kabisa Watanzania wanakosa msimamo wa kimtazamo. Si kama miaka 30-40 iliyopita. Elimu ilikazaniwa kutukuza nchi na jamii. Leo elimu na maisha yanaendeshwa na soko huria ambalo linakazania pesa. Kutafuta pesa si tatizo lakini wengi wanakosa uongozi wa kimawazo. Kwa mfano nchi nyingi za kibepari zilizoko nchi zinazoendelea kama India, Brazil n.k zina fahari ya lugha na utamaduni wao. Sisi tunaanza kuikosa fahari hiyo tukidhani kupiga chenga lugha mama (za kikabila na Kiswahili) ni maendeleo. Kutokujijua huku kunadidimizwa zaidi na udhaifu wa kuijua pia lugha ya Kiingereza. Kiwango chetu cha kuongea na kuandika ni cha chini sana ukilinganisha na miaka ile ya Ujamaa. Tatizo basi kimsingi linasababishwa na kuchanganyikiwa kutokana na uongozi mzuri wa ala za kitamaduni, elimu na sanaa ambazo kazi yake ni kuendeleza lugha na isimu katika jamii. 

SWALI: Naam ni somo zuri na refu sana hili. Je maendeleo ya lugha ya Kiswahili yanakuridhisha?
FREDDY MACHA; Hapana. Vitabu havipo vingi. Watanzania hatusomi. VItabu vinalengwa zaidi mashuleni badala ya kulenga pia kwa wananchi wa kawaida. Upeo wa fani zinazojenga lugha kama sinema, waigizaji, waandishi wa habari ni haba kwa kuwa hatusomi fasihi, na maduka ya vitabu ni machache kuliko mabaa kama alivyosema zamani marehemu Profesa Chachage S. Chachage.
SWALI; Unadhani Kiswahili kinaweza kuongoza lugha zingine barani afrika?
FREDDY MACHA: Suala la kuongoza au kutoongoza si muhimu. Muhimu ni kuijenga lugha na mambo mengine yatafuata. Lugha kubwa duniani zimekuzwa kutokana na kupendwa kutokana na fani kadhaa kama utamaduni (sanaa, muziki, fasihi, n.k) na pia biashara. Kispanyola mathalani kimeendelezwa pia na fani ya muziki na sinema. 

SWALI: Tukiacha suala hilo, tuangalie hili la umahiri wa Jenerali Ulimwengu. Umekuwa ukisema huyu ni gwiji wa lugha, nami nakuunga mkono. Lakini unaweza kuwaeleza Wasomaji nini siri ya Jenerali Ulimwengu kuwa mwandishi mahiri wa matumizi fasaha ya lugha ya Kiswahili? 

FREDDY MACHA: Jenerali Ulimwengu alichanua wakati wa kipindi kile cha Vijana wa TANU kuwa na msimamo pale Mlimani, wakiazimia kufuata maadili ya Mwalimu Nyerere ambaye alitaka ukombozi wa jamii, nchi na dunia. Sasa kutokana na kufunuka mawazo vile wakawa wanajisomea na kujadiliana kwa umoja. Kizazi hicho chote kimejenga Waalimu wazuri sana ambao wengine wameshafariki. Kawaida mtu huimarika kutokana na jamii, mazingira na hali inayomjenga au anayokuwepo. Mtu mwenye akili na bidii kama Jenerali Ulimwengu aliimarika na azma ya vijana wa TANU miaka ile ya 1967-1971 wakati wa vuguvugu la kuiendeleza nchi yetu. Kijana akishaivika vile ni vigumu kutetereka. Hata kama angetetereka, keshajua wajibu wake, anaijua nafasi yake katika historia ya jamii yake ni nini. Ukiyasoma maandishi yake toka enzi zile hadi leo utamwona ni mtu anayejua anakotoka na anakokwenda. 

SWALI; Pia umeeleza Jenerali Ulimwengu ndiye aliwapa mwanga wa matumizi mazuri ya lugha Kiingereza pamoja na huyu Philip Ochieng. Je wewe unawazungumzia kipi zaidi kutokana na umahiri wao?
FREDDY MACHA; Miye huvutiwa sana na ndoa ya fani na maudhui. Kama sanaa imepambwa vizuri na ujumbe ukapikwa vyema huninionyesha ukomavu. Hawa jamaa walikuwa wakitumia lugha nzuri ya Kiingereza kuchambua masuala ya jamii na kutoogopa kusema ukweli.
SWALI; Je unadhani Kiswahili hakijitoshelezi kama inavyosemwa na baadhi ya watu?
FREDDY MACHA:…Kiswahili ni lugha iliyoshakomaa. Wanachokosea watu hawa ni kutosoma. Ukitazama fasihi zinazoandikwa na Waandishi mahiri mfano Said Ahmed(Asali Chungu, 1976), Mohamed S. Mohammed (Kiu, 1970) ama karibuni zaidi Adam Shafi (Kuli, Vuta Nikuvute) utaona matumizi mazuri ya Kiswahili. Wanaelezea kila kitu kwa lugha fasaha, msamiati tosha na kuheshimu lugha inayojitosheleza bila kuazima maneno ya nje. Hao wanaosema lugha haijitoshelezi, hawaijua kwa kuwa hawafahamu mahali pa kuitazama. Kutosoma fasihi ni makosa sana. Wenzetu wa lugha nyingine kama Kifaransa, Kiingereza, nk wanaheshimu na kutukuza sana fasihi zao. Usomaji na mapenzi ya fasihi ndiyo hujenga msamiati, nahau na isimu. 

SWALI: Je inafaa kwa lugha ya Kiswahili kutumika katika taasisi za elimu ya juu?
FREDDY MACHA: Looh! Sana tena sana. Mbona nchi kama Japani, Estonia, nk zimejitahidi kufanya hivyo katika kipindi kifupi kuliko mataifa ya Uingereza nk?
SWALI: Nini mtazamo wako katika suala zima la matumizi ya Kiswahili. Je unaridhisha na kwanini?
FREDDY MACHA: Matumizi ya Kiswahili yameanza kudidimizwa na wazungumzaji kutoiheshimu na kuihusudu lugha kama ipasavyo. Huo ndiyo msingi. Makosa haya si sababu ya wazungumzaji bali ya vyombo husika. Katika vyombo vya habari mathalani, Redio za kitaifa na BBC Kiswahili au Idhaa ya KIswahili Ujerumani vinajitahidi; ila vijana wengi wanapoongea huongea kwa lafudhi ya Kiingereza. Wanablogu na waandishi wengine bado wanaandika kwa lugha za mseto kuliko Kiswahili fasaha. Ukisoma maoni ya wasomaji wa mablogu utaona udhaifu ulivyoenea. Hii ni mifano michache. Matumizi ya Kiswahili hayaridhishi kwa kuwa vyombo husika kama nilivyosema awali havikazanii ufahari wa lugha hii kama ilivyokuwa zamani, enzi za Mwalimu Nyerere. 

SWALI; asante sana kwa mchango huo. Bila shaka wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili wanaweza kujifunza jambo.
FREDDY MACHA; Nashukuru kunihitaji, nadhani wengi wataelewa japo pole pole tutafika. 

MUHIMU: Mahojiano haya yalifanyika Oktoba mwaka 2010.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako