November 23, 2017

ABDI BANDA AMETUONYESHA MAANA YA “SOKA LA KULIPWA”

Abdi Banda
NA HONORIUS MPANGALA
KATIKA pambano la kirafiki kati ya Tanzania na Benin pale mjini Porto Novo nilimshangaa Abdi Banda. Kama tumjuavyo Banda ni kiraka katika kucheza soka anauwezo wa kucheza nafasi za ulinzi kama mlinzi wa kushoto, beki ya kati na kiungo wa ulinzi kwa usahihi mkubwa. 

Sasa alichokuwa akikifanya pale Benin alikuwa anatuonyesha utulivu wa akili yake katika maeneo hayo mawili yaani kumudu hulka yake na kuwa mzuri katika kucheza soka lenyewe. Banda alikuwa mtu aliyewatuliza wachezaji wenzake waliokuwa wamepatwa na hasira kwa maamuzi ya mwamuzi wa mchezo ule. Kwa penati iliyotolewa na mwamuzi ambayo mpira ulionekana wazi kuguswa na mchezaji wa Benin lakini pigo likawa kuelekea katika goli la Tanzania. 

Wakiwa katika hali ya tafrani wachezaji wa Tanzania, alikuwa 'mlokole' Banda aliyefanya kazi ya kuwarudisha wenzake wasimsonge mwamuzi. Haikuwa Simon Msuva nyota wa Klabu ya Difaa el Jadida ya Morocco wala sio nahodha Himid Mao walipaniki kwa maamuzi yale. Juhudi za Banda zilifanya wenzake watulie na kuchukulia tukio lile kama sehemu ya mchezo. 

Michezo kumi aliyocheza Banda pale Afrika ya kusini na malezi ya ndani ya miezi mitano chini Kocha Kgoloko Thobejane akisaidiwa na MacDonald Makhubedu kumemfanya kukua na kukomaa kisoka kwa kiasi kikubwa. Katika hali ya kuzidi kujiweka katika hali kutazamwa zaidi ni jambo bora kwa Banda kuwa katika hali ile kwani amepata mwangaza kuwa maisha ya soka yako katika mtiririko ambao mchezaji mwenyewe anatakiwa kujitengenezea picha nzuri kwa vilabu vingine. 

Pesa imebadili na kumfanya atambue kuwa maisha yake katika soka ndicho kitu anachotakiwa kukifanya kwa maisha yake yote akiwa na nguvu. Banda amekuwa mzuri katika 'marking' na hata upigaji wa pasi kwa usahihi hata wakati mwingine kukokota mpira kutoka eneo la ulinzi na kusogeza timu hadi sehemu ya pili ya uwanja kwa viungo. 

Na wakati mwingine amekuwa mpigaji mzuri sana mipira mirefu na kutokana na nguvu zake za miguu mipira hufika eneo analotaka kufikisha. Mara baada ya kufanikiwa kusajiliwa na klabu yake nikiandika makala juu yake niliyoeleza,kamera za Super sport hazitamwacha salama kama ataendeleza yale matukio aliyokuwa akiyafanya alipokuwa akicheza hapa Tanzania. Naweza kusema ujumbe ulifika na nimemwona Banda anayeogopa kamera kwa kufanya matukio yasiyo ya kiuana michezo ambayo tulizoea kuona akiyafanya Mara kadhaa hapa Tanzania.


Amekuwa chaguo kwa kocha Salum Mayanga na hata Kgoloko Thobejane amekuwa akimpa nafasi ya kuanza mbele ya walinzi wenzake ambao katika nafasi hiyo yuko Banda pekee anayetoka nje ya Afrika Kusini. Ni kuimarika na ukomavu Wa hali ya juu ambayo anatuonyesha na kujitofautisha Kwa wale wanaocheza soka la nyumbani.
Abdi Banda
Saidi Juma Makapu, George Kavila na Nadir Haroub 'Cannavaro' wanaweza kushangaa kuwa yule 'mbabe' wao amekuwa mwokovu. Kwani hao katika nyakati tofauti walikutana na vichwa toka Kwa Banda na naamini ni jambo ambalo leo hii hataki kulikumbuka.

Waswahili wansema aheli uanze vibaya lakini umalize vizuri hiki ndicho kilichopo kwa Banda. Kwasasa hali imekuwa sawa kwake na kuwafanya kutambua kumbe akili hubadilika na ndio maana wako watu wanaoitwa wanasaikolojia ambao hutibu akili za watu Kwa mazungumzo tu. Katika pacha ambayo wapenda soka la Nyumbani walikuwa wakiiwazia sana na kuona kama vile inaweza kuifanya hali isiwe sawa, ni hii ya Banda na Kelvin Yondani. 

Mashaka ya wadau ni kutokana na kuwafahamu hulka zao kwani walikuwa watu ambao sio watu Wa kustahimili mihemko na mwisho wa siku huweza kufanya jambo la kughalimu. Lakini imekuwa tofauti sana sasa maana Utulivu Wa Banda jumlisha na ukorofi wa Yondani kwa washambuliaji watukutu kunaifanya ngome ya Taifa Stars kuwa salama na ni pacha ambayo inaweza kufanya vizuri zaidi ya hivyo ilivyoonekana. 

Kama ataamua kubadilika Yondani anaweza kucheza zaidi na zaidi kwani hata Raphael Marquez ameonekana akiwa na jezi ya Mexico katika michuoano ya kombe la mabara pale Urusi,hii ni kutokana na kujitunza kwake na kufuata misingi sahihi ya soka.

Ulokole wa Banda unapowashangaza wengi Tanzania,wenye utambuzi ndio wanaopata funzo na kutambua umuhimu Wa kutoka na kucheza nje ya nchi. 

0628994409

No comments:

Post a Comment

Maoni yako