January 26, 2018

UCHAMBUZI WA KITABU: SAFARI YA YERUSALEM KUTAFUTA AMANI

NA MARKUS MPANGALA
BOUTROS Boutros Ghali aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kati ya mwaka 1992 hadi 1996 amefariki dunia Februari 16 mwaka 2016 akiwa na miaka 93.

Leo tunachambua kitabu chake cha “Egypt's Road to Jerusalem:: A Diplomat's Story of the Struggle for Peace in the Middle East” kilichozindualiwa rasmi Mei 20, 1997. Kitabu hicho kina jumla ya kurasa 366, kimechapishwa na Random House(1997) na kikiwa katika lugha ya kiingereza. Boutrous amekipatia namba ISBN-10: 0679452451.

Boutros Ghali anatuelezea miaka minne ya uzoefu wake katika utawala wa aliyekuwa Rais wa Misri, Anwar as-Sadat. Anatuonyesha namna alivyochaguliwa kwenye uwaziri wa mambo ya nje mwaka 1977 na kifo cha rais Sadaat mwaka 1981. 

Katika kitabu hiki Boutros Ghala anadhihirisha umahiri alioonyesha katika masuala ya diplomasia wakati wa kusaka amani ya mashariki ya kati. Ikumbukwe eneo la mashariki ya kati limekuwa kwenye migogoro ya muda mrefu kiasi kwamba ufumbuzi umekuwa mgumu. 

Ni eneo ambalo mwandishi wa kitabu hicho anatukumbusha hatua kwa hatua walizokuwa wakichukua katika kuhakikisha amani inarejea mashariki ya kati. Anatuonyesha namna ambavyo Misri na Israel zilivyokuwa zikifanya juhudi za kumaliza uhasama wao. 


Ghali anaelezea matukio yote muhimu ya majadiliano ya mikataba ya amani, kuanzia safari ya kwenda Jerusalem akiwa na Rais Sadat, kisha Camp David kusaini mkataba wa amani na ule kati ya Misri na Israel. 

Kumbukizi anayotuletea Ghali ni namna ambavyo Rais Sadat alivyochoshwa na migogoro ya nchi za mashariki ya kati. Anatuonyesha kuchoshwa na migogoro baina ya nchi za kirabua dhidi ya Israel, pia kati ya Misri dhidi ya Israel. Kitabu hiki kinatukumbusha mazingira halisi yalivyokuwa wkati huo Sadat akisaka amani kwa kwenda huku na huko na kusisitiza kuwa Palestina walitakiwa kutatua matatizo yao si kuendekeza mapigano yasiyo na kikomo. 

Boutros anaelezea kukubaliana na mikakati ya Rais Sadat kupata ufumbuzi na ushirikiano na nchi zilizokuwa hazifungamani na upande  wowote hususani za Afrika.

Misri imetoa sadaka kubwa mno ya uhai wa watu kuliko fedha za nchi za kiarabu na Palestina. Muda wa Misri kujifikiria wenyewe ulishawadia, hapakuwa na namna ya kurudi nyuma. Niliamini mikakati ya Rais Sadat ni sahihi kwa maslahi ya Misri,” anaeleza.

Boutros anatukumbusha namna Rais Sadat alivyochukuliwa kama msaliti wan chi jirani zake za kiarabu kwa kukaa meza moja na Marekani, Israel kupata suluhisho la kudumu la amani.

Anaelezea hatua kwa hatua hadi kufikia makubaliano ya Camp David. Kitabu cha ‘Egypt's Road to Jerusalem’ kinaweza kuwa cha kwanza kuchanganua kinaga ubaga na kwa uwazi kuhusiana na harakati za kusaini makubaliano ya amani miongoni mwa mataifa ya kiarabu na Israel pamoja na Marekani ikiwemo pia jumuiya ya kimataifa. 

Ni Sadat ndiye alifanikiwa kwa kiasi kikubw akurejesha mahusiano baina ya nchi za Kiarabu na Israel chini ya ushauri wa Marekani. Jambo hilo liliiwezesha Misri kuishi kwa amani na utulivu na jirani zake.

Boutros Ghali anatukumbusha namna Rais Sadat alivyotakiwa kukabiliana na Ezer Weizman, ambaye alikuwa rais wa saba wa Israel(1993-1998). Awali Weizman alikuwa kamanda wa Kikosi cha Anga cha Jeshi la Israel na waziri wa ulinzi kabla ya kuwa Rais wa nchi hiyo. 

Rais Weizman alikuwa miongoni mwa viongozi watata mno kuwahi kutokea duniani. Ni aina ya kiongozi ambaye amepitia hatua zote za kijeshi kama ilivyo ada kwa watawala wa Israel. Boutros anatuonyesha kuwa kuthubutu kwa Rais Sadat kukaa mezani na Weizman lilikuwa jambo la aina yake. Ulikuwa ujasiri ambao viongozi walipaswa kuuga. Ni maono hayo ndiyo yalimvutia zaidi Boutros kuhusudu uongozi wa Sadat. 

Kitabu hiki tunaonyesha namna urafiki wa viongozi wenye harufu ya heshima, maslahi mapana na utaifa, kwa mfano namna amavyo  Jimmy Carter alivyokuwa karibu na mtawala mtata Moshe Dayan(ambaye anaonekana kwenye kava la kitabu hicho pichani akiwa ameziba jicho moja). 

Aidha, anatwambia jinsi watawala wa Isarel na Misri walivyoweza kuwa karibu ziadi kuliko vipindi vyote wakati wa majadiliano ya Camp David. 

Kulikuwa na mambo ya kushtukiza kidogo tulipokuwa camp David, ambapo wajumbe wa Misri na Israel walishuhudia picha za pamoja za viongozi mbalimbali wakifanya mazoezi pamoja wakiwa wamevaa mapajama yao. Wakashiriki michezo, kuendesha baiskeli na kukatisha misitu mbalimbali ikiwa ni ishara ya diplomasia ya hali ya juu. Ilikuwa unashuhudia diplomasia kutoka lwa Rais Tito (Josip Broz Tito wa Yugoslavia) na Fidel Castro (rais wa zamani wa Cuba) hadi kwa rais mshairi Leopold Senghor (Rais wa zamani wa Senegal) na aliyekuja kuwa dikteta Idi Amin (Rais wa zamani wa Uganda),

Kitabu hiki kinakupa sura halisi ya mikakati na malengo ya Misri ya kupatikana amani mashariki ya kati. Namna ambavyo Misri ilivyoweza kuweka wazi uwiano wa diplomasia na uaminifu wake kusaidia wananchi wa Palestina, uamuzi wa kujitenga kutoka muungano na Syria, Jordan na Saudi Arabia ili kufungua njia ya upatikanaji wa amani.
MWISHO

No comments:

Post a Comment

Maoni yako