January 26, 2018

NDOTO YA UPADRE ILIYOYEYUKA

Na. Honorius Mpangala
AKIWA amezaliwa katika kijiji cha Lundu wilaya ya Nyasa. Wazazi wake Daudi na Mama yake Neema wakambatiza jina la Markus ambalo lilitolewa na Padre Markus Komba alipohudumu parokia ya Lundu. Aliamini  labda siku za usoni angekuja kuwa kama yeye.
 
Alianza shule ya msingi Lundu na baadae kuhamia Kiwanjani iliyoko Mbinga Mjini akiwa darasa la sita. Maisha ya kijijini yalimfanya kujishughulisha na Masuala mbalimbali ya wakazi wa mwambao mwa ziwa Nyasa hasa ikiwa uvuvi. Alikuwa akipenda kuroposha samaki siku za mapumziko ya wiki hasa kwa siku ya jumamosi tu maana jumapili ilikuwa lazima kwenda kanisani. 


Michezo pendwa wakati huo kwa vijana wengi ilikuwa kupigana kwa kutumia maembe mabichi wenyewe wakiita ' Ngondo ya mapula' yaani vita ya maembe mabichi ba chandimu. Alikuwa mtumiaji mzuri wa mikono yote yaani wa kuume na wa kushoto katika shughuli zake lakini mkwala wa baba yake juu ya matumizi ya mkono wa kushoto ukafanya aache kuutumia kwa hofu ya adhabu.


Katika maisha yake soka ilikuwa mchezo pendwa kwake kiasi cha kupenda nafasi za ulinzi na kiungo. Lakini ndoto ya kucheza zaidi zilikoma baada ya kuumia goti alipokuwa ameenda kuchunga mbuzi eneo moja maarufu kwa kuchungia mifugo na kukiwa na maneno ya kucheza 'Kuluhaha' . Nilikuwa mtoa huduma ya kwanza kwani alipoumia tulikuwa wawili tu. 

Alipohamia Shule ya Kiwanjani ndiko alikutana na maswahiba kama January Ndunguru, Geofrey Njovu, Emmanuel Mbalale, Bonifasi, Thomas Kapinga na Willy Mapunda. 

Mbinga ilimpa ujanja wa mjini. Akamaliza darasa la saba vyema katika shule ya msingi Kiwanjani. Baada ya kuhitimu darasa la saba akafanikiwa kufanya usahili wa kujiunga na seminari ya Likonde na kufaulu vyema hatua ya awali.
Wakiwa wanasubilia mchujo wa mwisho kabla ya kwenda kujiunga wale wanafunzi wote waliofaulu walitakiwa kuhudhuria kanisani kila jumapili bila kukosa na mahudhurio yalinukuliwa na Mkurugenzi wa miito Padre Mapunda.


Kutokana na kutohudhuria kanisani kwa jumla ya jumapili mbili mfululizo, panga likampitia. Alipoenda jumapili ya tatu akashangaa baada ya misa jina lake kutosomwa katika mahudhurio, akaambiwa umefutwa kwasababu huluhudhuria kanisani Jumapili mbili na hakukuwa na taarifa yoyote dhidi yake.

Ndoto za kufuata nyayo za aliyempa jina zikawa zimefutika na kujiandaa kwa maisha yasiyo ya kiseminari. Akajiunga na shule ya sekondari ya Lundo. Nataka niwatofautishie kati ya Kijiji cha Lundo ambapo zamani iliwekwa kambi ya wakimbizi wa Msumbiji na kijiji cha Lundu ambako ndiko anazaliwa Markus. Utofauti uko katika herufi ya mwisho yaani U na O.

Akiwa Lundo Sekondari alikuwa mchezaji mzuri wa Mpira wa wavu na kwani tayari soka halikumfaa tena kwasababu kuumia goti. Maisha ya shule yana raha zake hasa ukiwa unaenda likizo mjini au umetokea mjini. Lundo walidhani ametokea Mbinga ambako ni mjini hivyo hata 'kampani' nayo inakuwa ya watu wa mjini mjini. 

A.k.a ilikuwa ni mtindo ambao wanafunzi wengi walipendezwa nao basi Markus akajikuta anakuwa maarufu kwa jina la Doggy faza badala ya lile la kupewa na wazazi wake. Rafiki yake mkuu aliyekuwa mtoto wa Padre Mkate wa dhehebu la Anglikana, Michael Mkate yeye alijulikana kwa jina la Koplo.

Alikuwa mpenda kidedea kweli kweli katika kushangilia timu yao ya Shule kwa mchezo wa soka maana alijua naye akiingia kwenye 'court' ya Volleyball atashangiliwa. Mpenzi mkubwa wa muziki wa Hiphop ndo maana hata wanafunzi wenzake walijua ukitaka 'kuchaniwa mistari' nenda kwa Markus waliyemwita Doggy faza.

Kwa kipindi chote cha maisha ya shule ilikuwa akienda likizo hasa nyakati za masika shughuli za shamba zilimhusu kwasababu ya familia kuwa wakulima wazuri. 

UANAHABARI
Sasa akiwa shambani alikuwa mtoa simulizi mbalimbali. Mara akawa anapenda kuwaiga watangazaji wa vituo mbalimbali vya radio hasa Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani (DW) hasa Ramadhan Ali na Martin Mule.

Ilifika wakati shambani uliweza kusikia sauti za watangazaji wa Sauti ya Amerika (VOA) kama Mwamoyo Hamza, na Abdulshakur Abood ambao alikuwa akiwaiga katika kutangaza. Moja ya watu ambao hawakupenda tabia ile alikuwa ni mama yake kwani aliona kama anapiga kelele shambani.

Unaweza kusema kuvutiwa na watu hao wa DW ndiko kulikomfanya atamani kuwa mwanahabari kama ilivyo sasa. Alipomaliza kidato cha nne fikra za mama ilikuwa ni kumpeleka kusomea Ualimu. Jambo ambalo alilikataa na kusimamia msimamo wake kwenda kidato cha tano katika sekondari ya Meta ya jijini Mbeya.

Mbeya kama ilivyokuwa kwa wasomi wengi wa zamani walipenda watoto wao wasome shule za mikoa ya Iringa na Mbeya ambako iliaminika kuwa na jiografia nzuri kwa mwanafunzi. 

Jina la Makaveli lilitamalaki katika midomo ya wanafunzi wa Meta kwasababu tu ya kupenda muziki wa Tupac Shakur.  Baada ya kuhitimu Meta alirejea kijijini na kuungana na wanakijiji wengine katika shughuli za kimaendeleo. Alishiriki kazi za kufyatua tofali na kuchoma. Hili zoezi la ufyatuaji wa tofali lilikuwa kama mradi maana ilikuwa kila likizo ya kasomo Mzee Mpangala alikuwa analeta kazi mradi iliyohusu ufyatuaji au tofali ambazo zilifyatuliwa na watoto wake. 

MBELE YA ABATE LAMBERT
Mwaka 2005 akiwa ameshahitimu kidato cha sita na kupata daraja la pili, alikuwa mjini Songea na Padre Chiwangu alimtuma mtu wa kumshawishi kwenda Seminari Kuu ya Peramiho. Lakini alikataa. Padre Chiwangu alimchukua tena na kwenda naye hadi Peramiho kwa matembezi. Akamfikisha kwa Abate Lambert wa Shirika la Wabenediktine katika salamu za kawaida. Licha ya vishawishi hivyo bado hakukubali kwenda Seminari Kuu Peramiho.
Amesoma uandishi wa habari, elimu na sayansi ya jamii, Teknolojia ya habari, Usanifu pamoja masuala ya masoko katika mitandao ya kijamii.

MICHEZO
Katika unazi wa soka ilikuwa kawaida kwake kutembea umbali wa kilometa kumi kufuata mechi za ligi ya mabingwa ulaya. Mwaka 2003 yeye na wadogo zake waliifuata mechi ya robo fainali kati ya Manchester United dhidi ya Real Madrid  iliyomalizika kwa ushindi wa bao 4-3 na tukio la kukumbukwa ni hat trick ya Ronaldo de Lima.

 Nilikuwepo moja ya watu waliopata wakati mgumu ni Mimi kwani nilitambiwa sana juu ya uwezo wa Real Madrid na kuonekana nimechagua kuishabikia klabu mbovu. Katika kujitanua kwa Masuala ya habari Markus ndiye  mwanzilishi na msimamizi mkuu wa blogu ya Lundunyasa.blogspot.com, Ukurasa wa Nishani Media.Co.Ltd na Mzururaji katiia mtandao wa Facebook.
Kazi hizo katika blogu na kurasa za Nishani na Mzuruaji hushirikiana na wadogo zake Honorius Mpangala na Kizito Mpangala pia Samweli Chitanya katika kuandika makala na kuhabarisha mambo mbalimbali yanayohusu Jamii,utalii,utamaduni  siasa na michezo.

VITABU
Jamaa ni mpenda kusoma vitabu tangu angali kijana mdogo. Ngoja nikusimulie katika maktaba ya baba yake kulikuwa na vitabu viwili ambavyo Mzee Mpangala hakupenda hata kuazimisha. Alikuwa cha “Historia ya vilabu vya Simba na Yanga” na kingine ni “Kuzama kwa Idd Amini” .


Kitabu cha kuzama kwa Amini kilihusu vita vya Kagera kati ya Tanziania dhidi ya Uganda. Mzee alikuwa akikitunza kwasababu ilikuwa zawadi yake toka kwa mmoja wa askari walioshiriki vita hivyo nakumbuka kwa jina moja la Magohe.
Licha ya Mzee kukificha kwa kuhofia watoto kukichukua hata sifahamu Markus aliwezaje kukichukua kitabu hicho ambacho hadi sasa Niko chini ya milki yake. Huu unaitwa “Usongo wa kutaka kujua”.

Huyu ndiye Markus Honorius ambaye wanafunzi wenzake kote alikosoma wanamjua hivyo. Ila alikuwa Ndesanjo Macha aliyemweleza achana mzigo wa majina ya kizungu na ubaki na utambulisho wa ukoo wenu. Honorius jina la babu yake aliyemzaa Baba. 

Mara nyingi watu wamekuwa wakichanganya jina lake na jina la Honorius la mdogo wake kwani kumbukumbu zao Markus Honorius ni jamaa waliyesoma nae pamoja. Huyu ndiye Markus Mpangala wengi hupenda kumtania kwa jina la Andunje wa fikra.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako