NA KIZITO MPANGALA
DUNIANI kuna ubunifu wa namna
mbalimbali unafanyika katika teknolojia ili kurahisisha shughuli mbalimbali
katika maisha yetu ya kila siku. Ubunifu wa kiteknolojia umekuwa ni lulu
mojawapo katika ulimwengu huu wa Sayansi na Teknolojia hasa katika umeme na
elektroniksi, ingawa upo ubunifu mwimgine nje ya uga huu wa umeme.
Kiti cha magurudumu manne ni
kifaa cha muhimu sana kwa wagonjwa katika hospitali mbalimbali duniani. Na ubunifu
mbalimbali hufanyika ili kuboresha utendaji wa kiti hiki. Kiti hiki kwa sasa
kina magurudumu manne ambapo makubwa mawili na madogo mawili na hutegemea nguvu
za mgonjwa kama anaweza kukisukuma yeye mwenyewe na kama hawezi basi anasukumwa
na mtu mwingine.
Tofauti na baiskeli ya
magurudumu matatu, kiti hiki kina ukubwa ambao unatosha kwa mtu mmoja tu kuketi
na anayesukuma hulazimika kuembea. Vilevile hakichukui nafasi kubwa. Hakiwezi
kutumika kama njia mojawapo ya usafiri barabarani kama ilivyo baiskeli ya
magurudumu matatu inayotumiwa na walemavu wengi duniani kote.
Kiti hiki kilianza kubuniwa
nchini China mnamo karne ya tano na baadae nchini Ugiriki mnamo karne ya sita
ambapo kilibuniwa kwa ajili ya kubebea watoto na wazee wasioweza kutembea na
kisha kuwasukuma ili kuwafikisha sehemu waliyokusidia. Nchini China awali
walikuwa wakitumia matoroli kwa ajili ya kuwabeba wazee wasioweza kutembea na
pia vilema na vilevile kubebea mizigo mizito. Michoro ya kiti cha magurudumu
mawili iliyochorwa nchini China ilionekana mwaka 525 B.K huko Ulaya.
Ulaya wakachangamka na wakaunda
viti vya namna ile kwa wingi. Lakini baadaye ubunifu huu ulipotea ghafla na
watu wakapuuzia kuutekeleza hadi kufikia mwaka 1595 kilipoonekana kiti cha
namna hiyo ambacho kilitumiwa na Mfalme Philipo wa II wa Hispania.
Aliyekitengeneza hakujulikana.
Wabunifu wengi waliona kwamba
kiti hiki kina mapungufu fulani licha ya kuwa na sehemu ya kuegemeza miguu na
sehemu ya kuegemeza mikono. Wabunifu hao walikosoa kutokuwepo kwa mfumo binafsi
wa kiti hicho kujiendesha au kuendeshwa na mtu mwenyewe aliyeketi kitini hapo
kwa sababu kama vilivyo viti vingi katika hospitali nyingi sasa, huhitajika mtu
wa ziada kusaidia kusukuma ili kumfikisha muhusika sehemu aliyokusudia kwenda.
Mwaka 1655, Stephan Farffer,
kiajana aliyekuwa na miaka 22 na fundi saa, alitengeneza kiti cha kwanza cha
magurudumu manne kinachojiendesha kwa kuongozwa na mtu aliyepanda kitini hapo.
Mfumo huo alioutumia ni kama ulivyo sasa katika baiskeli za walemavu ambazo
wanapiga pedali kwa mikono. Na mwaka
1760, viti vya aina hii ya Stephan Farffer vilikuwa vikiundwa kwa wingi kwa
ajili ya wasiojiweza.
Mwaka 1887, katika kitongoji
cha Atlantic mjini New Jersey nchini Marekani, viti hivi viliundwa kwa wingi
kwa ajili ya watalii kubebea mizingo na vingine kwa ajili ya kupumzikia tu huku
kikiserereka.
Mwaka 1933, Harry Jennings
Mdogo (Sr), na rafiki yake Herbert Everest ambaye alikuwa kilema, wote wakiwa
wahandisi wa umakanika, waliunda kiti cha kwanza ambacho ni chepesi na cha
kukunjwa, yaani unaweza kukikunja na kubeba kwa urahisi. Everest alikitumia
kiti hiki kutokana na kutoweza kutembea vizuri kwa kuwa alipata tatizo hilo
akiwa machimboni. Jannings na Everest wakaona kwamba biashara yao hii
imepokelewa vizuri na watu wengi, wakafanya maboresho zaidi.
Viti hivyo vipo vya aina
mbalimbali kwa sasa kulingana na matumizi yake lakini kubwa ni kwa wasioweza
kutembea. Hospitali nyingi duniani zina viti hivi kwa ajili ya wagonjwa
wanaopata shida za kutembea au wanaweza kutembea lakini kutokana na matibabu
hulazimika kuwa na utulivu wa mwili, hivyo hutumia viti hivi ambavyo wengi
huuta baiskeli, kwa ajili ya kufika sehemu inayokusudiwa.
Leo tunaye mwanafunzi ERASTO
CHISANU wa shahada ya uhandisi wa umeme katika chuo cha teknolojia jijini Dar
es Salaam (DIT) ambaye ametengeneza kiti cha aina hiyo kinachotumia umeme.
Erasto alipata wazo hili
kutokana na mateso aliyokuwa yakimpata bibi yake katika kutembea. Bibi yake ana
shida ya miguu, hivyo hawezi kutembea kwa ufasaha sana jambo ambalo linampa
maumivu ya miguu mara kwa mara anapotembea. Ndipo Erasto kwa utambuzi wake kuwa
ni mhandisi anayenolewa, akaandika muswada wa ubunifu wake huu na kuuwasilisha
katika idara ya kozi ya uhandisi wa umeme na kisha kuanza kazi ya kutengeneza
kiti hichi mara baada ya muswada wake kupitishwa.
Erasto alilazimika kuomba
ushauri wa kitaalamu kwa madakitari katika hospitali ya taifa ya Muhimbili
jijini Dar es Salaam. Alieleza wazo lake na madakitari wakamshauri kuhusu kimo
cha kiti hicho. Hapo Erasto akaongeza wazo kwamba kiti kitakuwa kina uwezo wa
kupanda na kushuka kinapoongozwa na mtumiaji.
Kiti hicho ambacho kukamilika
kwake kimemgharimu zaidi shilingi za Tanzania milioni mbili, kinaongozwa na
mfumo wa kielektroniki na kinaweza kupandishwa na kushushwa wakati mtumiajai
akiwa bado kitini hapo. Kama kingekuwa na lengo la kutumika hata barabarani kwa
ajili ya usafiri basi ingekuwa rahisi kwa yeyote kukitafuta na kutmia kwa
sababu kiti hicho ambacho kinatumia umeme, kina betri inayohifadhi chaji
inayoweza kutumika kwa umbali wa KILOMETA 30 na kisha kuchajiwa tena. Sasa kwa
matumizi ya kawaida tu kwa mgonjwa aliyepo nyumbani au hospitalini, chaji hiyo
inaweza kudumu kwa muda mrefu sana.
Erasto anaeleza changamoto
kubwa aliyoipata ni wanafunzi wenzake wengi kumwambia kuwa hataweza kwa sababu
jambo hilo lingemgharimu muda mwingi na hivyo angefanya vibaya katika masomo
darasani. Lakini Erasto Chisanu hakujali maelezo hayo, aliweka wazo lake mbele
na kulifanyia kazi. Mpaka sasa kiti kipo tayari, na malengo yake ni kuunda
vingi zaidi ili viweze kusaidia watu wengi wenye kuhitaji viti. Pia, mwalimu
mkuu wa chuo alichopo ametoauamuzi wa kumrudishia gharama ya fedha zote ambazo
alitumia katika kufanikisha ufundi huu. Hii ni kutokana na kukubalika na wengi
kwa kiti hicho ambacho madakitari wa hospitali ya taifa ya Muhimbili
wamempongeza kwa kazi hii na kumpa hamasa ya kuunda vingi zaidi.
© KIZITO MPANGALA (0692
555 874)
No comments:
Post a Comment
Maoni yako