January 21, 2013

WAPIGAKURA HABA, WALALAMIKAJI WAMEJAA POMONI


Na Markus Mpangala, Dar es salaam

Markus Mpangala
Wenyeji wa Latini Amerika ndio wavumbuzi wa neno “Suffragium”, ambalo walilitumia kuanzia karne ya 14. Maana ya neno hilo ni “haki ya kuchagua” au “Haki ya kuunga mkono”.

Ni ile hali ya mwananchi kuchagua viongozi, au masuala muhimu kitaifa. Tangu kuvumbuliwa kwa neno hilo ndipo dunia ilishuhudia taasisi za kisiasa zenye kujikita katika haki ya kuchagua au kuunga mkono wagombea mbalimbali katika chaguzi.

Kimsingi mkondo mkubwa wa siasa hizo ulijikita zaidi barani ulaya hususani jamii ya Warumi na Wagiriki hasa katika karne ya 17 na 18. Katika kipindi hicho wanafalsafa mbalimbali walikubali kuwa huo ulikuwa mtindo wa serikali binafsi ambapo mwananchi alikuwa na mamlaka ya kuwachagua viongozi anaowataka. 
Rais Nyerere
Wanafalsafa waliamini kuwa uchaguzi wowote unaofanywa na mwananchi (mpigakura) una lengo la kuunda serikali yake kwa mtazamo wake (Self government). Licha ya mabaidliko ya Kiliberali kuleta mfumo wa uchaguzi wa viongozi kupitia vyama vya siasa, bado muundo wa “self government’ umesalia katika serikali za kisasa duniani kote kupitia chaguzi zinazofanyikwa mara kwa mara kulingana na utaratibu wa nchi husika.
Mathalani Tanzania inafanya uchaguzi mkuu kila baada ya miaka mitano, Malawi kila  baada ya miaka minne sawa na Marekani. uchaguzi wa Rais, Wabunge wa Kongresi, Seneti, Madiwani na kadhalika wote hupitia kapu la mwananchi ambaye analazimika kuwapigia kura ili kuhalalisha mamlaka yao.

Kwahiyo, mamlaka ya mwananchi ya kupiga kura ni makubwa na ndiyo anayeamua kuwa mgombea fulani amepata kura nyingi kuliko mwenzake au wenzake(kama wanakuwa wengi). Baadhi ya nchi hurudia uchaguzi kama hakuna mgombea anayefikisha wastani wa kura zilizopangwa.
Liberia walirudia uchaguzi baada ya aliyeongoza Bi. Hellen Sirleaf kutofikisha asilimia 50, lakini duru la pili alifanikiwa kumshinda mshindani wake George Weah. Senegal pia Mack Sall alishinda uchaguzi baada ya Abdoulaye Wade kukiri kushindwa.
Kwa baadhi ya wanasiasa wapigakura ni nyenzo tu, lakini kimsingi wapigakura ni muhimu sana katika mfumo wa kidemokrasia. Hii inatokana na jinsi ushiriki wao unavyoweza kumfanya mgombea fulani kujivunia kura anazopata.

Hapa nchini Katiba yetu haizuii mgombea asiyefikisha asilimia 50 kuchukua madaraka. Kwa mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2000 haionyeshi kuwa mgombea urais wan chi yetu asipofikisha asilimia 50 basi anyimwe kutangazwa mshindi.

Bali Katiba yetu inampa nguvu yule aliyeongoza kupata kura nyingi bila kujali zimefika asilimia 50 au kidogo. Nadhani Katiba mpya inatakiwa kubainisha kwamba mshindi wa kiti cha urais anatakiwa kutangazwa tu akifikisha siyo chini ya asilimia 50.

Rais Mkapa
Tukisogea mbele kidogo tunaona kuwa katika uchaguzi wamwaka 2015 umekuwa gumzo mno kwa wananchi na mashabiki wa vyama vya siasa. Gumzo hili linatokana na hamasa mpya ambayo wananchi wameipata, na ndio maana ya haki ya kuchagua serikali waitakayo. 


Mwananchi amekuwa akiwapigia kura wagombea mbalimbali katika kiti cha urais, wabunge, madiwani na viongozi wa serikali za mitaa. Inaonekana kutoka utawala wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere tumekuwa na udhaifu mkubwa katika suala la upigaji kura.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1965, rekodi zinaonyesha kuwa waliojiandikisha kupigakura walikuwa watu 3,373,089. Katika uchaguzi huo waliopiga kura walikuwa watu 2,600,040 sawa na asilimia 77.1.

Mwalimu Nyerere alipata kura 2,410,903 sawa na asilimia 96.46, ambapo wapikura 88,600 sawa na asilimia 03.54 walimkataa, huku kura 100,537 zikiharaibika. Katika uchaguzi wa mwaka 1970, jumla wananchi waliojiandikisha kupiga kura ni 5,051,938.

Wapigakura waliompigia kura za ushindi Mwalimu Nyerere walikuwa 3,465,537 sawa na asilimia 72.2, huku kura 109,828 sawa na asilimia 03.07 zilimkataa, ambapo kura 74,388 ziliharibika.

Aidha, uchaguzi wa mwaka 1975 jumla watu waliojiandikisha kupigakura walikuwa 5,577,566, ambapo wapigakura 4,172,267 sawa na asilimia 93.25 walimpa ushindi Mwalimu Nyerere. Wapigakura 302,005 ambao sawa na asilimia 06.75 walimkataa Mwalimu Nyerere, huku kura 83,322 ziliharibika.

Katika uchaguzi wa mwaka 1980 jumla ya wananchi waliojiandikisha kupigakura walikuwa 6,696,803. Waliompigia kura Mwalimu Nyerere walikuwa 5,570, 883 sawa na asilimia 95.56, ambapo kura 295, 040 sawa na asilimia 04.44 zilimkataa, huku kura 157,019 ziliharibika.

Ukiangalia wastani wake utaona kuwa kuna kura zilikuwa zinaongezeka kwa kila uchaguzi. Mwaka 1965 waliomkataa Mwalimu Nyerere walikuwa  88,600, halafu kura 100,537 ziliharibika, kisha mwaka 1970 kura zilizomkataa zilikuwa 109,828 sawa na asilimia 03.07.

Kwa maana hiyo katika chaguzi hizo mbili Nyerere alishindwa kuwavutia wapigakura, kwani kutoka wapigakura 88,600 sawa na asilimia 03.54 waliomkataa  mwaka 1965 hadi wapigakura 109,828 ambao waliomkataa mwaka 1970 inaonyesha bado wananchi wetu hawakuwahi kuchukua uamuzi mgumu kupitia sanduku la kura.

Katika uchaguzi wa mwaka 1975 wapigakura waliomkataa Nyerere waliongezeka ambapo walikuwa 302, 005 sawa na asilimia 06.75. Lakini mwaka 1980 idadi ya waliomkataa Mwalimu Nyerere ilikuwa ndogo kuliko kwani wapigakura 259,040 walimkataa ingawaje alifanikiwa kushinda kwa wastani wa 95% ya uchaguzi huo.

Ali Hassan Mwinyi aligombea urais mwaka 1985 baada ya Mwalimu Nyerere kujiuzulu. Mwinyi alishinda kwa kura 4,778,114 sawa na asilimia 95.68 kati ya wapigakura 6,910,555 waliojiandikisha mwaka huo.

Kura zilizomkataa zilikuwa zilikuwa 215,626 sawa na asilimia 04.32, huku kura 188,259 ziliharibika. Uchaguzi wa mwaka 1990 wananchi waliojiandikisha walikuwa 7,296,553, lakini waliopiga kura walikuwa 5,198.120 sawa na asilimia 97.79%. Wapigakura 117,366 sawa na asilimia 02.21 walimkataa Ali Hassan Mwinyi.

Uchaguzi wa mwaka 1995 ulikuwa wa kwanza katika mfumo wa vyama vingi. Mgombea wa CCM, Benjamin Mkapa alishinda uchaguzi huo kwa jumla ya kura 4,026,422 sawa na asilimia 61.82 kati ya wapigakura 8,929,969 waliojiandikisha.

Wagombea wa vyama vya upinzani, Agustine Mrema (NCCR-Mageuzi) alipata kura 1,808,516 sawa na asilimia 27.77. Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) alipata kura 418,973 sawa na asilimia 6.43. John Cheyo alipata kura 258,734 sawa na asilimia 3.97. kura zilizoharibika katika uchaguzi huo zilikuwa 333,936.

Kwenye uchaguzi wa mwaka 2000 waliojiandikisha kupigakura walikuwa 10,088,484, ambapo kulikuwa na ongezeko la karibu milioni 1.2 ikilinganishwa na mwaka 1995. Benjamini Mkapa (CCM) alipata kura 5,863,201 sawa na asilimia 71.74. Profesa Lipumba (CUF) alipata kura  1,329,077 sawa na asilimia 16.26. Agustine Mrema alipata kura 637,115 sawa na asilimia 7.80. John Cheyo alipata kura 342,891 sawa na asilimia 4.20. wakati kura zilizoharibika zilikuwa 345,214.

Uchaguzi wa mwaka 2005 waliojiandikisha kupiga kura ni 16,401,694 yaani wapigakura walioongezeka ni milioni 6. Wapigakura 9,123,952 sawa na asilimia 80.28 ndio waliomchagua Jakaya Kikwete (CCM). Profesa Lipumba (CUF) alipata kura 1,327,125 sawa na asilimia 11.687. Freeman Mbowe (Chadema) alipata kura 663,756 sawa na asilimia 5.88. Augustine Mrema alipata kura 84,901 sawa na asilimia 0.75. katika uchaguzi huo, waliopiga kura walikuwa 11,875, 927 sawa na asilimia 72.4, huku kura zilizoharibika zilikuwa 310,460, kisha watu milioni 5 wakakosa kupiga kura.
Rais Mwinyi
Kwenye uchaguzi wa mwaka 2010 jumla ya wapigakura walikuwa 8,626,283 sawa na asilimia 42.8, wakati waliojiandikisha walikuwa 11,511,020 sawa na asilimia 57.2. ukiangalia hesabu za kura kwa miaka yote utagundua kuwa hakuna wakati ambao wapigakura wetu walichukua uamuzi mgumu kubadilisha uongozi wa nchi hii.

Vilevile hakuna wakati ambao hakukuwepo na kura zilizoharibika. Hii ina maana kuna wapigakura haba, lakini walalamikaji katika nchi yetu hii wamejaa pomoni. Mathalani kama tunafika mahali tunasababisha kuharibika kwa kura, mfano mwaka 1965 (kura 100,537), mwaka 1970 (kura 74,388), mwaka 1975 (83,322), mwaka 1980 (kura 157,019), mwaka 1985(kura 188,259), mwaka 1990 (kura 109,796), mwaka 1995 (kura 333,936) mwaka 2000 (kura 345,314), mwaka 2005 (kura 310,460) na mwaka 2010 zipo kura zilizoharibika.

Katika hali kama hiyo bado wapo watu wamejaa kila kona ya nchi kazi yao kubwa ni kulalamikia hali fulani ndani ya taifa hili. Mlolongo wa kura zinazoonyesha hapo inaelekea CCM imekuwa chama kinachopata kura nyingi kila chaguzi.

Na wapigakura hao ni walewale ambao miongoni mwao wanaruhusu kura 333,936 kuharibika halafu wanalalamika hali duni au hali mbovu juu ya jambo fulani ndani ya nchi yetu au wengine hawapigi kura kabisa. Sijawahi kuona wananchi wa nchi hii wakichukua uamuzi mgumu kupitia sanduku la kura tangu mwaka 1965. Hivyo tunao wapigakura haba, ila walalamikaji wamejaa pomoni.

1 comment:

  1. Kuna wimbo/muziki mmoja, zilipendwa, unasema;

    twalalamika pembeni, huku nyuma nyuma twajiweka, utamuongoza nani....
    Sikukmbuki vyema, niliwahi kuusikia,...katika mambo ya kuimarisha chama cha Mapinduzi, ..ujumbe wake unafaa sana hapa.

    ReplyDelete

Maoni yako