Albert Sanga, Iringa |
Wiki iliyopita niliandika makala iliyokuwa na kichwa
“Unahitaji gia ya uvumilivu kumudu biashara”. Kwenye makala hiyo nilieleza visa
kadhaa vilivyowahi kunitokea katika harakati zangu za kibiashara. Mamia ya
wasomaji kutoka pande zote za nchi wameonesha kuguswa mno na yaliyowahi
kunitokea.
Wengi wamenitumia ujumbe, mfupi, wameniandikia baruapepe na
kunipigia simu nyingi wakinipa pole na ushauri mbalimbali. Hata hivyo ninapenda
kuutambua mchango ya msomaji mmoja ambae alinitumia meseji kwa simu. Mchango
wake ndio msingi wa makala hii ya leo.
Msomaji huyu ni Mchungaji Ency Mwalukasa wa Dar es Salaam.
Mch. Mwalukasa anasema, “Halo kaka ALBERT! Nimefurahia sana shuhuda za mapito
katika biashara zako. Hata kwenye huduma ya MUNGU mapito ni hivyo hivyo.
Nimeguswa nikushirikishe kinga na ulinzi wa mali na fedha zetu: ni
kumtolea Mungu fungu la kumi au
zaidi.”
“Kwa kufanya hivi inaleta ulinzi na baraka. Malaki 3:8-12.
Mungu ameahidi unapotii ni lazima atende. Au asilimia Fulani ya fedha na mali
zako wape wahitaji utazidishiwa na kupokea ulinzi wa mali na fedha zako. Mtu wa
Mungu ni lazima upate mafanikio ya kudumu” Mwisho wa kunukuu.
Ninapoendelea na makala haya ninasukumwa kuweka wazi mambo
mawili ili nisilete migongano ya kifikra na kimaslahi. Mosi; ninapenda
nitangaze maslahi yangu kiimani. Mimi ni mkristo niliyezaliwa mara ya pili.
Kwa hiyo leo ninaandika ulinzi wa
biashara zetu kwa mtazamo wa tamaduni na sheria za kibiashara lakini pia kutoka
katika Biblia. Pili; si lengo langu kuhubiri katika makala haya; hivyo kama
nitarejea mafundisho ya kidini ijulikane kuwa ni nukuu tu za kutusaidia.
Kama alivyosema Mchungaji Ency Mwalukasa ni kweli kuwa
mfanyabiashara unatakiwa kutoa fungu la kumi pamoja na sadaka nyingine.
Kiimani, utoaji wa sadaka huleta ulinzi wa kiroho katika biashara zako. Ukiacha
ulinzi, utoaji wa sadaka huachilia nguvu za uweza wa Kimungu katika fahamu na
fikra za mfanyabiashara anaetoa sadaka; kiasi ambacho kunakuwa na mtiririko wa
mawazo ya kibiashara (costant flow of business ideas), unakuwa mbunifu na
unakuwa na nguvu za kuendelea mbele hata vinapotokea vikwazo kibiashara.
Mimi ni msomi wa masuala ya biashara lakini pia najivunia
uzoefu nilionao na ninaoendelea kuupata kwa kufanya biashara kwa vitendo. Hata
hivyo; kule madarasani na kwenye vitabu vya biashara kuna jambo eidha
linafichwa ama linapuuzwa. Jambo hili ni nafasi ya Mungu katika kumfanikisha
mtu kibiashara.
Watu wanapofundishwa masomo ya biashara hawaambiwi kuwa ukitaka
kuwa na mafanikio ya kweli ni lazima uanze kuimarika kiroho (spiritual
mindset). Mimi kamwe sitaacha kuitaja na kufundisha wazi nafasi ya Mungu katika
mafanikio ya watu.
Kwa sababu kama tukiwaficha watu kuhusu Mungu tutakuwa
tunajenga mafanikio yasiyo ya kudumu. Nimewahi kuandika huko nyuma kuwa, “Mtu
yeyote anayepata mafanikio ya kifedha ama mali, ikiwa hajaijenga roho yake kwa
kuwa na uhusiano mzuri na Mungu; basi mtu huyo ameuchuma msiba”
Pengine changamoto kubwa inayowakabili wafanyabiashara wengi
ni namna gani ya kutoa hizi sadaka. Mathalani, sadaka ya fungu la kumi ni
asilimia kumi ya faida unayoipata katika biashara. Sasa, utajuaje asilimia kumi
ya kumtolea Mungu ikiwa haujui unapata faida ya shilingi ngapi kwa wiki, kwa
mwezi, au kwa mwaka?
Asilimia kubwa ya wajasiriamali na wafanyabiashara nchini
wanaendesha biashara kienyeji na kwa kubahatisha. Wengi hawajui ni faida gani
anazalisha kwa wiki, mwezi au mwaka na hili linatokana na kutokuwa na utamaduni
imara wa kutunza kumbukumbu.. Jambo hili ni hatari sana linapokuja suala la
kumtolea Mungu sadaka; kwa sababu utajikuta eidha unamwibia Mungu au
unamuongezea unapotoa sadaka. Ni heri ukamzidishia Mungu kuliko kumwibia!
Binafsi nilijifunza mapema sana uhusiano uliopo kati ya
sadaka na mafanikio ya mtu kibiashara. Kitu ambacho kilinitesa kwa muda mrefu
sana ilikuwa ni namna ya kujua nimtolee Mungu kiasi gani; kwa sababu biashara
nyingi nilikuwa nazifanya kimazoea, kwa kukisia. Nilipokuwa nachanganyikiwa
zaidi ni pale inapotokea faida imerudi ‘juu kwa juu’ katika mzunguko na
ikaongezea kwenye mtaji.
Unapofika muda wa kutoa sadaka nabaki nimechanganyikiwa
maana sielewi mtaji ni kiasi gani na faida ni shilingi ngapi kwa muda gani.
Huenda hata mimi nilikuwa mmoja ya watu waliokuwa wanamwibia Mungu sadaka.
Lakini kwa sasa nimepata mwarobaini. Nilikuja kubaini kuwa biashara ili
zifanikiwe na ukitaka usigombane na Mungu wako kwa “kumdokolea” sadaka; ni vema
kuendesha biashara katika mifumo rasmi.
Ndipo nilipoamua kusajili kampuni ambapo biashara zangu zote
ninaziendesha kikampuni. Uzuri wa kufanya biashara katika mifumo rasmi ni
kwamba; unalazimika kuwa na utaratibu wa uendeshaji biashara, utunzaji wa
kimahesabu na mipango ya biashara iliyochambuliwa (business plan). Pale kwenye
kampuni huwa ninapata fedha kwa njia mbili. Mosi; ni kupitia mshahara
ninaolipwa kila mwezi. Pili ni gawio la faida inayotokana na mchanganuo wa
idadi ya hisa ninazomiliki.
Nimetaja habari ya mshahara ninaolipwa kila mwezi. Wengine
wanaweza kushangaa kidogo, inakuwaje kampuni ya kwangu halafu tena ninalipwa
mshahara? Hapa ndipo ambapo wajasiriamali wengi huwa wanateleza. Unapokuwa na
biashara hata kama iwe ndogo kiasi gani, unatakiwa uwe unajilipa mshahara
kiwango maalumu na sio kutumia faida ama fedha ya mtaji kadiri unavyojisikia.
Sasa linapokuja suala la sadaka sisumbuki. Katika ule
mshahara ninaolipwa (ama uite ninaojilipa) kila mwezi ninatenga fungu la kumi
na kumalizana na Mungu. Vile vile inapokuja suala la gawio la faida za hisa,
iwe faida itarudi kukuza mtaji ama nitaichukua; ni kwamba kabla ya chochote
ninatenga asilimia kumi na ninamalizana na Mungu. Hii nimeona inanisaidia sana
na niwe muwazi; ninauona ulinzi wa Mungu katika biashara na mipango yangu
mingi.
Ninapoeleza habari za sadaka na mafungu ya kumi mtu anaweza
kusema, Huyu Sanga mbona analeta habari za kiroho hapa? Kwa taarifa yako ulinzi
wa biashara zetu kwa njia ya sadaka unatajwa hata katika sheria na taratibu za
biashara.
Waanzilishi wa sheria na taratibu zote zinazotumika katika
biashara duniani pote ni Waingereza. Wao katika sheria hizi wanashauri na
kulazimisha kuwa biashara inapozalisha faida; ni vema ikarudisha sehemu ya
faida yake kwa jamii inayoizunguka. Faida hii ndio sadaka. Tena mjasiriamali
usisubiri mpaka uwe na mamilioni ili kutoa sadaka. Anza na hiyo faida ndogo
unayozalisha hata kama ni shilingi mia tano, toa!
Biashara yako inapowasaidia watu kuna mambo mawili
yanatokea. Mosi; biashara yako inakaa akilini na mioyoni mwa watu kwa hiyo
unaendelea kuwa na wateja waaminifu. Pili; biashara yako inakuwa inaheshimika
na jamii unayoisaidia kwa sababu wanajua kuwepo kwa biashara yako ndio kupona
kwao hivyo watailinda kwa nguvu zote.
Pamoja na juhudi zetu za utaalamu na kanuni za kuzingatia
kibiashara, mjasiriamali usisahau kuwa njia bora ya kulinda biashara zako ni
wewe pamoja na biashara yako kumtolea Mungu sadaka, kuwasaidia wahitaji na
kupeleka sehemu ya faida kuongeza thamani za maisha ya jamii inayokuzunguka.
Wajasiriamali tunahitaji ushindi
0719 127 901, stepwiseexpert@gmail.com
No comments:
Post a Comment
Maoni yako