September 27, 2017

UCHAMBUZI WA KITABU CHA THOMAS FRIEDMAN



KITABU: HOT, FLAT AND CROWDED
MWANDISHI: THOMAS L. FRIEDMAN
MCHAMBUZI: MARKUS MPANGALA

SUALA la mabadiliko ya tabia nchi ni nyeti duniani. Kutoka na unyeti huo Thomas L Friedman aliandika kitabu hiki cha “Hot,Flat and Crowded”. Kitabu hiki kilichapishwa Septemba mwaka 2008 na kampuni ya Farrar, Straus and Giroux na kikapewa nambari ISBN 978-0-374-16685-4.

Thomas L. Friedman aliandika kwa kwa namna tofauti na kitabu cha kwanza alichozungumzia dhana ya utandawazi yaani .The World Is Flat’. Akiongelea mapinduzi ya teknolojia. Ndani ya kitabu cha “Hot,Flat and Crowded” anazungumzia mabadiliko ya hali ya hewa yaani Tabia-nchi na kuibuka kwa ushindani wa nguvu za nishati ambazo huleta madhara makubwa kwa afya za wanadamu duniani.


Ushindani huu wa nguvu za nishati unasababisha kutengeneza kwa ‘layer’ za sumu ambazo zitaathiri maisha ya watu kila kona ya dunia. Friedman anatuasa kwamba utunzaji wa mazingira unahitaji jitihada za pamoja na kuzingatia mkataba wa Kyoto ili kulinda maisha ya baadaye kwa viumbe hai.

Mkataba wa Kyoto ulipendekeza kupunguzwa kwa nguvu za matumizi na uharibifu unaosababishwa na viwanda mbalimbali unapaswa kupunguzwa na kisha kuondolewa kabisa. Ili kuepusha kuelemewa na dhana hii Friedman anapendekeza kwamba ni muhimu kwa kila taifa kuunda sera za taifa zinazo husiana na mazingira.

Sera hii anaita "Geo-Greenism", ambayo siyo tu inaeleza nini kifanyike kuepusha madhara katika sayari ya dunia bali nini kifanyike kwa nchi tajiri kama Marekani na zingine ili kuondokana na janga la tabia-nchi.

Anapendekeza kuwa tunaweza kuzalisha bidhaa mbalimbali pasipo kuharibu ‘layer’ za anga ambazo zinakabiliwa na mgandamizo mkubwa unaosababisha joto kali duniani.

Anaeleza kwamba sura mpya ya dunia inakuja kulingana matukio ya sasa, akijadili dhana ya utandawazi.lakini mwangaza wa sura ya sasa unatokana na suala la Tabia-nchi. Friedman anatukumbusha matukio ya shambulizi la ndege la Septemba 11 mwaka 2001 katika jengo la kimataifa la biashara nchini Marekani, kwamba ni moja ya kubalidi tabia-nchi.

Pia anaturejesha katika janga la Katrina, na baadaye anamalizia hoja yake kwa kuangaza ongezeko la matumizi ya mtandao(ambapo kwa mujibu wake, mtandao unakusanya watu takribani bilioni 3 duniani). Watu hawa ni wahanga wa mabadiliko ya hali ya hewa ya dunia. Ili kuepusha madhara zaidi, Friedman anasema mapinduzi ya kijani hayaepukiki na matumizi ya teknolojia safi yanaweza kuifanya dunia kuwa mahali salama zaidi.

Mapinduzi makubwa katika zana za kisasa za teknolojia yanapaswa kunyumbulisha na kusogeza mbele maisha ya wanadamu. Anapendekeza kwamba tunachopaswa kubadilisha katika dunia yetu siyo taa za umeme bali viongozi ambao hawatajali suala la tabianchi.

Anasema sera maridadi ni kupata ‘Green President” na mwenye kutuletea ‘Green New Deal’, ambapo matokeo yake yatakuwa ni “Greenest Generation”. Hatuwezi kufika sehemu hizo zote itandapo hatutakuwa tayari kumhimiza kiongozi wetu(Green President) ambaye atakuwa na mipango ya mapinduzi ya kijani kwa manufaa ya wananchi wake.

Tunapaswa kuwa na vipimo vya maendeleo yetu kwa kuweka mikakati ya sera ya “Green New Deal”, ili baadaye tuwe na kizazi cha ‘Green Generation”. Ndani ya kitabu hiki cha “Hot, Flat, and Crowded” anatuondolea woga wa kubadilisha hali iliyopo sasa kwani ni muhimu na ina manufaa kwa kizazi chetu.
Upende usipenda kitabu hiki kinafunua mengi ambayo ni uozo tunaopuuza na wenye madhara makubwa sana kwa afya zetu.
Manifesto aliyoitayarisha ni kubwa na muhimu sana kwa vizazi vijavyo, na limekuwa somo kubwa kwa Wabunge wa Kongresi na wagombea urais kwa vipindi vijavyo.

Ingawaje amezungumzia Marekani, lakini hali hiyo inakwenda mbali zaidi hadi kwenye nchi zinazoendelea kiuchumi kama China,India, na Japan. Na vilevile anahamasisha viongozi wa nchi za dunia ya tatu kutilia mkazo Tabianchi. Na kwamba tusiachie siasa zinakaharibu usalama wa dunia kwasababu ya madaraka.

Tunahitaji kuona mabadiliko makubwa yanafanyika na jitihada zinaendelezwa ili kuweza kuthibiti mabadiliko haya yenye athari kwetu. Suluhisho tunahitaji mapinduzi ya kijani na matumizi ya njia salama kabisa za Kilimo kwanza na kadhalika. Tunahitaji sera maridadi kwa lengo la kuimarisha ardhi na hali ya hewa kwa kufuata mkataba wa Kyoto.

Katika mahojiano yake na Fareed Zakaria, alifafanua hivi; anaposema “Hot’ ni kwamba dunia kwa sasa imejaa joto kali linalosababishwa na viwanda na kupuuzwa kwa mkataba wa Kyoto. Hali imekuwa mbaya na itakuwa zaidi endapo itaachwa.
“Flat” anazungumzia nguvu ya zana za kisasa za teknolojia zinavyoweza kuwaunganisha watu kwa nia chanya ikiwemo kujadili madhara ya uchafuzi wa hali ya hewa.

“Crowded” ni kwamba dunia imejaa watu wengi, yaani kuzaliana kumeongezeka pamoja na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali katika masoko ya dunia ili kukuza uchumi. Nguvu ya uchumi inakuzwa zaidi na kukazaniwa huku ‘Crowded’ inaathiriwa na tabia-nchi iwe watu na bidhaa zao.

©Nishani MEDIA

No comments:

Post a Comment

Maoni yako