November 08, 2017

SASA NAMWELEWA HILARY CLINTON

NA  MARKUS MPANGALA
 
WAKATI wa kampeni za Uchaguzi nchini Marekani mwaka 2016, aliyekuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya chama cha Democrat, Hilary Clinton alisema: “Kama mgombea (wanasiasa) anakasirishwa na sentensi moja iliyoandikwa kwenye mtandao wa kijamii basi huyo hafai kupewa mkoba wa nyuklia, maana vidole vyake vitabonyeza wakati wowote,”. 
 
Tafsiri ya Kiswahili ni yangu kwa sababu ninahitaji kurahisisha kueleweka hoja yenyewe. Maneno ya Hilary Clinton yalimlenga mgombea wa chama cha Republican, Donald Trump ambaye alishinda uchaguzi huo baadaye.

Clinton aliamini kuwa kitendo cha Trump kukasirishwa na sentensi zinazoandikwa kwenye mitandao ya kijamii ikiwamo yeye mwenyewe kujibu mapigo au kuwatisha watu, ilikuwa ni ishara ya mtu ambaye hawezi kustahimili ukosoaji au kukosolewa pale anapokuwa kiongozi.

Kwamba ili uwe kiongozi unatakiwa kustahimili au kama wasemavyo wahenga lazima uwe na ngozi ngumu hata kama utapigwa mishale ya kila namna. Hii ndiyo changamoto inayotukabili vijana, viongozi wa kila ngazi na watendaji mbalimbali kwenye vyombo vya uamuzi kwa maslahi ya Watanzania. 

Mara nyingi tumesikia wanasiasa au wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi wakijiapiza kufanya jambo hili au lile. Wengine wanatajwa kuudhika kutokana na maneno kadhaa yanayozungumzwa kwenye mitandao ya kijamii.

Tunafahamu kuwa ipo sheria ya mtandao na maudhui, ambapo inalenga kudhibiti nidhamu pamoja na kukabiliana na “hatari” yoyote inayoitwa kama udhalilishaji (Cyber Bullying), matusi na hulka mbaya dhidi ya viongozi au watu wa kada mbalimbali. 

Lakini katika kipindi hiki kuna jambo limenishangaza. Nashangaa kuona wanasiasa wetu nchini wanakasirishwa na ‘status’ zinazondikwa huko Facebook, Twitter, Instagram na kwingineko. 

 

Tumejionea wanasiasa wakiwa na hasira mno. Wananuna na kutishia kuwachukulia hatua wote wanaohusika. Lakini kiwango cha kutishika ni kidogo kwani zipo dalili za dhahiri kuwa warusha maneno ya kuudhi, kebehi na dhihaka hawatakwisha na kila mara wataibuka. 

Tunapoona wanasiasa wakihangaishwa na mitandao ya kijamii maana yake ni kuwa nguvu yake ni kubwa na huo si upepo wa kupita. Kama nilivyoamini mwaka 2007 kuwa huduma ya Blog ya Kampuni ya Google haikuwa jambo la kupita na kwamba litavuka mipaka na kuingia ngazi za kiuchumi. 

Sasa hivi tunajionea namna bloga wanavyovuna fedha kupitia huduma hizo na wengine wanavuna kupitia mitandao mingine ya kijamii. Kwahiyo basi, inapofika mahali kiongozi ndani ya nchi yetu awe anachukizwa na mitandao hiyo na kudhani kuwa hasira zake zitamsaidia kutatua kwa kuwakamata kila watu itakuwa ni kuhangaika na mambo ambayo hayamtafsiri kuwa kiongozi thabiti. 

Kiongozi mahiri na thabiti hakubali kumwagiwa sifa peke yake kwamba anafanya vizuri au ametenda mambo fulani ambayo yanapaswa kumpa “ujiko” mbele ya wengine.

Ni jambo la ajabu kukutana na kiongozi ambaye anaudhika kwa kiasi kikubwa juu ya porojo zinazotolewa na wakosoaji. Lazima tukubaliane kuwa hata kama tutawashughulikia watu wenye kejeli,kebehi,dhihaka na kila aina ya dharau katu hatutamaliza. Hata kama tutatumia kila juhudi kamwe hatuwezi kuifanya nchi nzima iwe na mkondo mmoja wa mawazo. 

Kwamba watu wote wawe na mawazo sawa, wafikirie muda mmoja kwenda maliwatoni, sokoni, dukani, matembezini nakadhalika. Kwamba watu hao waimbe nyimbo za “mtukufu tu mwanasiasa au kiongozi”. 

Nchi na duniani hilo haliwezi kutokea hata mara moja. Ni lazima tukubali kuwa tunapofikia hatua ya kukasirishwa na “Status” inayoandikwa kwenye mitandao kama Facebook ni ishara mbaya na dalili ya kutawaliwa na mapokeo tofauti juu ya binadamu. 

Ni vigumu watu kukubaliana kwa kila jambo na Mheshimiwa diwani hata kama litakuwa zuri kiasi cha kuingia kwenye rekodi. Hakuna mwananchi atakayekubaliana na kila jambo kwa kuwa limesemwa na Mheshimiwa Katibu kata, katibu tawala, mkuu wa wilaya, mkoa, mbunge, waziri na Rais au Mwenyekiti na viongozi wowote kutoka vyama vya siasa. Kamwe dunia wala nchi yetu haiwezi kuwa na fikra moja kwa sekunde, saa, siku, wiki, mwezi na miaka.

Endapo sote tutafuata njia ya Trump ya kuudhika kwa kuwa bwana Fidodido amemkejeli Mheshimiwa mbunge, waziri au Rais basi tunaelekea kwenye Taifa la vifurushi vya vichekesho. 

Litakuwa jambo la ajabu pale nitakaposikia au kuona kuwa Tanzania na wananchi wake wamewekewa mipaka ya kufikiri. Kwamba mipaka hiyo iseme ni wakati wa kumsifu mbunge, waziri na wengine na hakuna nafasi ya kumhoji wala kumkosoa. Hilo litakuwa Taifa la hatari kwa kuwa bila ukosoaji hatuwezi kuishi kwa afya bora. 
Endapo kiongozi anachukizwa na kukosolewa maana yake ni kwamba alifanya makosa kuingia kwenye uongozi ambao unaruhusu ukosoaji. Ni lazima tukubaliane kuwa nchi hii inao watu wenye kufikiri,kuhoji na kutenda. 

Ni wajibu wa kila mmoja kwenye nafasi yake kutimiza majukumu anayoagizwa kwa mujibu wa sheria na taratibu. Ni lazima kiongozi atambue kuwa kuilazimisha jamii iwe inamsifu na kuimba nyimbo za kummwagia sifa pekee kana kwamba yupo kwenye pambio, ni hatari kwa afya ya nchi. 

Nchi hujengwa kwa mawazo tofauti. Misuguano ya fikra za wanazuoni, wananchi,wataalamu na wengineo. Hayo ni baadhi ya mambo yanayoweza kulifanya Taifa au taasisi yoyote kuwa sehemu nzuri ya kufanya kazi. 

Huwezi kudhibiti mkondo wa uhuru wa mawazo kisha ukategemea matokeo chanya. Kusema hivyo sina madhumuni ya kuwatetea wale wote wanaotumia vibaya uhuru wa maoni bali namna ambavyo viongozi wenyewe wanaweza kustahimili pamoja kuepukana na ukosoaji au maudhi yoyote kutoka kwa wananchi wao. 

Labda sasa namwelewa Hillary Clinton, kwamba wapo wanadamu ambao wakiudhika ni kama vile wamejeruhiwa au kutendwa jambo baya maishani lenye kuashiria uhai na kifo. Itachekesha na kusikitisha. 

Mwisho….

No comments:

Post a Comment

Maoni yako