NA KIZITO MPANGALA
JOSEPHINA Margaret Bakhita
alizaliwa mwaka 1869 mjini Darfur kitongoji cha Olgassa nchini Sudan
katika jamii ya kabila la Daju. Baba yake aliheshimiwa sana kwa kuwa alikuwa ni
kaka ya Chifu wa kabila hilo. Bakhita aliishi kwa furaha akiwa hajui mateso ya
kitumwa yanakuwaje.
Alipofikia umri wa miaka minane,
alitekwa na Waarabu wafanyabiashara ya utumwa ambao tayari walikwishamteka dada
yake miaka miwili kabla ya kumteka Bakhita mwenyewe. Alilazimishwa kutembea
mwendo wa kilometa 960 peku kutoka Darfur hadi El Obeid. Kabla ya
kufika El Obeid alikuwa ameuzwa mara mbili njiani.
Bakhita alipofikia umri wa miaka
12
alikuwa ameuzwa tena mara tatu na kisha kusafirishwa mpaka Uturuki. Huko alikumbwa
na mateso mengi na uchungu hali iliyompelekea kusahau jina lake la asili na
hivyo alilazimika kutumia jina alilopewa na Waarabu, Bakhita likimaanisha mtu
mwenye bahati. Kisha akasilimishwa.
Bakhita alinunuliwa na tajiri
wa biashara ya watumwa ambaye alikwa Mwarabu na kumtumikisha kama mfanyakazi wa
kuwahudumia binti zake wawili ambao waliishi nae vizuri. Alipokorofishana na
mtoto wa kiume wa Mwarabu huyo alipigwa na kufikia hatua ya kushindwa kutembea
kwa muda wa mwezi mmoja.
Baadae Bakhita aliuzwa kwa Jenerali mmoja wa Uturuki. Alipangiwa kuwa
mfanyakazi kuwasaidia mke wa Jenerali huyo na mama mkwe wake ambao wote wawili
walikuwa wakatili kwa watumwa. Bakhita alipigwa viboko mara kwa mara na katika
kumbukumbu yake alisema “miaka yote
mitatu niliyoishi kwenye nyumba ya Jenerali yule, hakuna siku iliyopita bila
mwili wangu kuambulia maumivu ya viboko. Jeraha fulani likikaribia kupona basi
linazaliwa jeraha jingine”
Bakhita alichanjwa mwilini ili
kuwekwa alama ya kitumwa kama walivyokuwa watumwa wengine huko Darfur. Bakhita
hakurumiwa alipokuwa akilia mara baada ya kuona dishi lenye ua jeupe, wembe, na
chumvi likisogezwa karibu yake ili achanjwe. Jumla ya chale 114
zilichanjwa katika tumbo lake, kwenye matiti na mkono wa kulia. Bakhita alisema
“niliumia sana nilipochanjwa tumboni
kuwekwa alama kama watumwa wengine”
Mwaka 1882, mji
wa El Obeid ulikuwa hatarini kushambuliwa na Dola la Mahdi, hivyo Jenerali wa
Uturuki aliwarudisha watumwa nchini Sudan na kuwauza isipokuwa watumwa 10
alibaki nao na kwenda kuwauza mjini Khartoum. Bakhita alikuwa miongoni mwa
watumwa 10
waliouzwa mjini Khartoum.
Huko Khatoum Bakhita
alinunuliwa na balozi mdogo wa Italia, Callisto Legnani, ambaye hakutumia ukali
alipokuwa akimpangia shughuli ya kufanya.
Miaka miwili baadae, wakati
balozi huyo mdogo alipopaswa kurudi nchini Italia, Bakhita alimwomba waende
wote huko Italia na mwishoni mwa mwaka 1884 walikuwa wameondoka mjini
Khartoum pamoja na rafiki ya balozi huyo, Augusto Michieli. Walisafiri mwendo
wa kilometa 650 kwa
ngamia na kufika bandari ya Sawakin kaskazini-mashariki mwa Sudan.
Mwaka 1885 mwezi
Machi, Bakhita na mwenyeji wake, balozi Callisto Legnani pamoja na Agusto
Michieli waliondoka katika bandari ya Sawakin kuelekea nchini Italia na bandari
ya Genoa mwezi April. Walipokelewa na mke wa Agusto Michieli, Bi Turina
Michieli. Hapo balozi Callisto akamkabidhi Bakhita kwa Agusto.
Bakhita aliambatana na wenyeji
wake hadi mjini Mirano kilometa 25 kutoka mjini Venice nchini
Italia. Aliishi katika familia ya Agusto kwa muda wa miaka mitatu akiwa mlezi
wa mtoto wa Agusto. Baadae, Bakhita alirudishwa Sudan na alikaa kwa muda wa
miezi tisa kisha akarudi tena Italia.
Agusto Michieli alikuwa
akimiliki hoteli kubwa mjini Sawakin, akaamua kuuza mali zake zote zilizokuwa
Italia na kuhamia Sudan na familia yake. Mkewe alihitaji kuonana na naye hivyo
akaamua kwenda Sudan kabla ya kuuza vitu vyote huko Italia. Kwa ushauri
aliopewa na mshauri wao wa biashara, Illuminato Cecchini, Bakhita na mtoto wao,
Alice, walipata hifadhi katika nyumba ya watawa wa Canossia kwa kuwa sehemu
kubwa ya nyumba yao iliuzwa, na Bakhita angekosa sehemu ya kuihsi na mtoto huyo
wakati Turina Agusto angesafiri.
Turina Agusto aliporejea Italia
kuwachukua Bakhita na mtoto wao ili wakaishi Sudan, Bakhita alikataa. Kwa muda
wa siku tatu alishawishiwa arejee Sudan, lakini Bakhita alikataa. Mahakama kuu
ya Italia ilisema “kwa kuwa Waingereza
wameifanya Sudan kuwa uwanja wa kitumwa kabla Bakhita hajazaliwa, Sudan
itamwendeleza kuwa mtumwa. Na kwa kuwa sheria za Italia hazitambui utumwa, basi
kuanzia sasa Bakhita siyo mtumwa katika ardhi ya Italia” Akawa rasmi
mwananchi wa Italia. Basi kwa mara ya kwanza Bakhita alikuwa huru kwa uhakika.
Bakhita alichagua kubaki
utawani nchini Italia, na mwaka 1890 alibatizwa na kuitwa JOSEPHINA MARGARET
FORTUNATA. Jina Fortunata ni mbadala
wa jina Bakhita ambapo yote yana
maana sawa, isipokuwa Fortunata ni
kwa lugha ya Kilatini. Hivyo, ili kutochanganya na imani ya dini ya Kiislamu,
wakuu wa shirika hilo la utawa waliondoa jina Bakhita na kuweka jina Fortunata.
Mwaka 1893,
Bakhita (Fortunata) alianza mafunzo ya utawa (Unovisi) na mwaka 1896
alifunga nadhiri na kuwa mtawa rasmi. Mwaka 1902 akapangiwa kituo cha Schio
mkoa wa Vincenza. Mwaka 1937 alihamishiwa katika misheni ya Vimercate mjini
Milan. Alifanya kazi mbalimbali katika maisha yake ya utawa na alizoeleka kwa
jina la Madre Moretta (Kiitaliano)
likimaanisha Mama Mweusi (Kiswahili).
Kitabu cha kwanza kuhusu
Bakhita kiliandikwa mwaka 1931 na Ida Zanolini. Kitabu hiki kilimfanya Bakhita
ajulikane na wengi kote nchini Italia. Na wakati wa vita kuu vya pili vya
dunia, wakazi wa Schio walitegemea ulinzi wake na walimheshimu kama mtumishi wa
Mungu. Bakhita alisali, na mabomu yote yaliyorushwa katika kijiji cha Schio
hayakuua mtu yeyote.
Saa za mwisho kabla ya kufariki,
Bakhita alisumbuliwa na maumivu ya mwili na alikuwa akilia na kusema “minyororo inanibana mno, ilegezeni kidogo”
Alipozinduka alisema “nina furaha sana. Bibi
yetu… Bibi yetu!” kisha akafariki. Ilikuwa ni mwaka 1947, na
mwili wake ulihifadhiwa kwa siku tatu ambapo watu wengi walifika kuomboleza.
Mabaki ya Bakhita (Fortunata)
yalifukuliwa mwaka 1969 na kuhifadhiwa utawani Canossia. Mwaka 1992
alitangazwa kuwa mwenye heri na Papa Yohane Paulo II. Kisha 01/10/2000
alitangazwa kuwa Mtakatifu.
0692 555 874
No comments:
Post a Comment
Maoni yako