NA HONORIUS MPANGALA
TANZANIA ni miongoni mwa nchi
zinazotajwa kuwa na amani na hii ni kutokana na muingiliano wa mambo
manne. Yako makundi yaliyojikita katika
masuala ya dini, siasa, ushabiki wa soka na mwisho hali ya kuoleana.
Kupitia makundi hayo manne
kunapelekea jamii ya watanzania kuishi pamoja. Makundi hayo hukutanisha watu
tofauti kutokana na ufuasi wake. Haitakuwa ajabu unapomuona Waziri wa Mambo ya
Ndani na kada wa CCM Mwigulu Nchemba akikaa jukwaa moja na kiongozi wa upinzani
Freeman Mbowe na kuipa hamasa klabu wanayoipenda ya Yanga. Pia haitashangaza
kwa kiongozi mkuu wa chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe kukaa pamoja na Waziri
Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa na kuipa hamasa klabu yao pendwa ya Simba. Hayo
yote hufanyika bila kujali itikadi za kisiasa walizonazo.
Katika masuala ya kiimani ni
jambo la kawaida Watanzania wenye upinzani wa kisoka kuabudu kanisa moja au pia
kuswali katika msikiti mmoja na mambo yakafanyika bila shida yoyote. Hivyo hivyo hata katika masuala
ya kuoleana, Watanzania huweza kuoa nje ya kabila lake kutokana na kutokuwepo
kwa ukabila. Mchezo wa soka umekuwa na watu muhimu sana ambao huufanya mchezo
huo kufurahiwa na wapenzi wengi.
Waamuzi wamekuwa ndio msingi wa
kupatikana kwa matokeo bora katika mchezo husika. Tanzania ina waamuzi
waliobobea vilivyo katika kutafsiri sheria kumi na saba za soka pamoja na
vipengele vinavyoweza kufanya mwamuzi akawa huru katika kutafsiri sheria na
vipengele vyake.
Licha ya ubora wa waamuzi hawa,
ipo changamoto ambayo inawakabili hasa wanapopata wasaa wa kuchezesha mechi za
wakongwe Simba na Yanga. Kutokana na
klabu hizi kuwa kubwa na zenye ushawishi mkubwa katika soka la Tanzania,
inawapa wakati mgumu waamuzi wanaochezesha mechi zao, kutokana na timu hizo
kuhitaji zaidi mafanikio.
Kuna wakati mwamuzi maarufu
nchini, Israel Mujuni Nkongo aliwahi kupigwa na wachezaji wa Yanga, licha ya
kuwa ana beji wa Fifa. Kupigwa kule kulitokana na tafsiri iliyoonekana
kujengeka kuwa ni ya kuwaumiza Yanga.
Pia imewahi kutokea mara nyingi
kwa waamuzi kama Martin Saanya kukutana na rungu la Shirikisho la soka nchini
(TFF) ikiwa ni adhabu ya kuchezesha vibaya dhidi ya timu hizo vigogo.
Hata hivyo yuko mwamuzi wa
kupigiwa mfano, kutokana na kufanya vizuri katika mechi za vigogo hawa. Huyu ni
Mfaume Nassoro kutoka Zanzibar, ambaye ndiye aliyechezesha mechi ya Simba dhidi
ya Yanga, katika michuano ya Kombe la Mapinduzi na kuisha kwa Simba kuibuka
washindi. Ni mmoja ya waamuzi ambao walisifiwa sana na wadau wa soka.
Katika msimu wa ligi
uliomalizika wa 2016/17 waamuzi watatu waliingia katika kuwania tuzo ya waamuzi
bora. Hao ni Herry Sasii alieweza kuwazidi wenzake Hans Mabena toka Tanga na
Shomary Lawi kutoka Kigoma. Katika taswira ya Mchezo wenyewe jinsi ulivyo
unaweza kusema vijana hao wa tatu kuingia katika orodha hiyo ilitokana na jitihada
zao katika kazi yao.
Mwamuzi kama Mabena ilikuwa
anachezesha kwa mara ya kwanza katika Ligi Kuu Tanzania na kufikia hatua katika
orodha ya waamuzi watatu bora. Mchezo wake wa kwanza ilikuwa kati ya Ndanda
dhidi ya Yanga na matokeo kuwa sare tasa.
Moja ya maamuzi ambayo
yalipelekea wapenzi wa soka washangazwe nayo ni kitendo cha mwamuzi huyo kutoa
adhabu ya pigo lisilo la moja kwa moja kuelekea goli la Ndanda kwa sababu ya
mlinda mlango kuushikilia mpira mikononi zaidi ya sekunde kumi. Alikuwa katika uamuzi
wa haki kwani kipa hutakiwi kuushikilia mpira muda mrefu, ndiyo maana hutakiwa
kuuburuza chini ikiwa ni ishara ya kuanzisha upya.
Shomary Lawi ni moja ya waamuzi
bora kabisa na mechi ambayo hadi leo anaiona ni ya kumbukumbu kwake, ilikuwa
kati Mbao FC dhidi ya Simba, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Katika mechi hiyo, awali Mbao
waliongoza goli mbili lakini kipindi cha pili Simba walirejesha kuanzia dakika
ya 83 na kupata ushindi mbele ya Mbao FC.
Lakini mechi za Simba na Yanga
zimekuwa ni zenye kuwapa kihoro waamuzi wengi na kuingia katika migogoro
kutokana na wadau wa soka kuwa na mitazamo tofauti hasa matokeo yasipokuwa
upande wao.
Maneno yanayotolewa na wadau wa
timu hizo hufanya waamuzi hao wenye weledi kuwa wapole, huku wakisikiliza hoja
za wadau wa soka. Ni majuzi tu katika Mchezo wa Yanga dhidi ya Simba umefanya
wadau kufanya uchambuzi kuhusu pande tatu, yaani vilabu mashabiki na hata
mwitikio wa mashaniki katika mchezo huo.
Uchambuzi dhidi ya mwamuzi
Herry Sasii umefanya nikumbuke mechi zake za kirafiki za kimataifa
alizochezesha na kuamua vyema. Nilishangazwa na yale malalamiko ya wapenda soka
juu yake. Kila mmoja alimzungumzia kwa jinsi avyoweza kuchambua maamuzi yake.
Kama Shirikisho letu la soka
halitakuwa makini basi tutashuhudia mengi toka kwa klabu hizi kubwa dhidi ya
waamuzi. Ziko kanuni katika ligi ya Uingereza ambazo huzibana klabu
kutowazungumiza waamuzi. Ukibainika unawatolea malamiko katika mahojiano yoyote
unakumbana na adhabu. Vipengele hivyo katika kanuni vimewafanya makocha kama
Jose Mourinho kuwa na staha katika mahojiano yao.
Shirikisho na Bodi ya Ligi wana
kila sababu ya kuweka ngao ambao ambayo itawalinda waamuzi kwa kufuatilia
mikutano ya wanahabari inayofanywa na klabu. Kama upo utaratibu wa kufikisha
malalamiko ufuatwe na sio vinginevyo kwani hii huwatengenezea chuki wapenzi wa
soka dhidi ya waamuzi na kuweza kuhatarisha hata maisha yao.
Waamuzi wenyewe wanatambua kuwa
jukumu la kuzichezesha Simba na Yanga ni gumu na ambalo linagusa maslahi ya
viongozi wa nyanja mbalimbali nchini. Mazingira ya kutengeneza presha ya
kimaamuzi yatawafanya washindwe kutumia vyema kanuni na sheria kwa sababu ya
kuwepo kwa mashinikizo ambayo hulenga kuwaondoa katika uhalisia wa kimaamuzi.
Usimamizi wa misingi bora ya
ligi yetu utafanya kila mmoja aheshimu kanuni na utaratibu uliowekwa. Kama
itatokea ukiukwaji basi wahusika watapaswa kufanya mwamuzi yatakayo kuwa na
tija kwa maendeleo ya soka letu.
0628994409
No comments:
Post a Comment
Maoni yako