November 08, 2017

UCHAMBUZI WA TAMTHILIYA YA BLACK MAMBA

KITABU: BLACK MAMBA
MWANDISHI: JOHN RUGANDA
MCHAMBUZI: KIZITO MPANGALA.

Black Mamba ni tamthiliya iliyoandikwa na John Ruganda kutoka nchini Uganda. Namba za usajili ni 978-9966-46-378-X na kuchapiswa na East African Educational Publishers. Kina jumla ya kurasa 70 tu. Wahusika wa tamthilya hii ni Profesa Coarx (kitivo cha sosholojia), Berewa mfanyakazi wa Profesa Coarx, Namudd mke wa Berewa, Odiambo mwanafunzi wa shahada ya kwanza ya Sosholojia, Catherine Smith mkufunzi mpya kitivo cha Sosholojia, Ofisa wa Polisi na msaidizi wake. Na mhisika msaidizi ni Namatta ambaye ni kahaba. 


Tamthilya hii ina maonyesho yaliyogawanyika katika sehemu tatu ambayo ni;

Sehemu ya kwanza
Berewa anamuita mkewe kutoka kijijini aje mjini kwa malengo maalumu ili wapate fedha za kujikimu. Pamoja na kufanya kazi nyumbani kwa Profesa Coarx, Berewa alikabiliwa na ukata. Baada ya Namuddu kufika mjini, Berewa anamweleza kuwa profesa Coarx anaishi bila mke kwa kuwa hakufika na mke wake kituo kipya cha kazi. Berewa alifanya hivyo baada ya kuona wanawake waliokuwa wanakuja kwa zamu kulala nyumbani kwa profesa huibuka na fedha baada ya kukamilisha shughuli wanayojia. Berewa akaamua kumtengeneza mkewe na kumkabidhi kwa profesa. Usiku wa kwanza wa profesa na Namuddu ulimpatia Namuddu fedha zilizokuwa ni mara mbili ya ujira wa Berewa kwa mwezi. Namuddu anamkabidhi mume wake fedha hizo na kumuambia akamnunulie magauni ili afanane na Namatta. Namatta ni mwanamke aliyekuwa na fedha nyingi kwa biashara ya kujiuza. Mabishao yanatokea baina ya Berewa na Namuddu kuhusu fedha ambapo Berewa alitaka wazipeleke benki. Mara mlango unagongwa na Odiambo anaingia kuleta kazi yake aliyoachiwa na profesa aeleze jinsi ya kukomesha ukahaba nchini kwao. Odiambo anaazna mazungumzo na Berewa kuhusu suala hilo. Berewa alikuwa anamfanyia profesa madili na hapa anamtetea baada ya Odiambo kuuliza kuhusu aina ya wanawake waokuja nyumbani kwa profesa. Berewa anamtetea profesa Coarx kwa nguvu. Odiambo anamweleza Berewa jinsi serikali ilivyojipanga kukabiliana na suala hilo la ukahaba. Njia mojawapo ni kuwachunguza watumishi wa umma na wakibainika wanapelekwa jela mwaka mmoja.

Sehemu ya pili


Profesa Coarx amerudi kutoka kazini, anaingia anakuta picha ya Namuddu iko chini, anaiokota na kuiweka mfukoni mwa koti lake. Namuddu anaingia akitokea mlango wa nyuma na anamuuliza profesa  kama ameiona picha yake, profesa anakataa. Namuddu anamkumbusha profesa ahadi alizompa kumpleleka klabu usiku lakini profesa anakataa na kumuambia anamngoja mwanafunzi wake (wa kike) anakuja kulala hapo. Namuddu anamkosoa kuwa profesa ni mwalimu wa wanafunzi inakuwaje awatafune tena wanafunzi wake? Namuddu anasema “haswaa! Uwanatamani wanafunzi wako. Unawashauri mambo mbalimbali ya maisha, unasahihisha mitihani yao na kazi wanazoleta lakini hutosheki unataka kuwatafuna ili kuwaongezea alama kwenye mitihani. Inaonekana hutaki tena mapenzi na mimi” Uk. 47. Profesa hajali maneno hayo. Mara mlango unagongwa, profesa anamwambia Nammudu aende chumbani. Mara Catherine Smith anaingia na baadae Odiambo naye, wakawa watatu wakijadiliana kuhusu ukahaba hasa kazi aliyoiandika Odiambo. Wakiwa katika majadiliano profesa alimwelekeza Odiambo jinsi ya kujiweka katika hali ya uanafunzi wa chuo kikuu anamwambia awe mdadisi wa mambo. Ghafla Namuddu anaingia na kupiga kelele huku amevaa shimizi, anasema “nyokaaa, nyokaaa, nisaidie, Black Mambaaa” Uk. 50. Anafika sebuleni Odiambo na  Catherine Smith wanashangaa. Profesa anamkemea Namuddu na kwenda chumbai kuua nyoka! Namuddu anasema “unanifokea nini? Hivi unafuga nyoka wewe mwenyewe unadhani hawatakung’ata wewe mfugani siku moja? Uk. 50. Catherine Smith na Odiambo wanaamua kuondoka na kupata jibu kwamba profesa ni mshenzi. Anakemea ukhaba lakini yeye mwenyewe yumo humo! Mara profesa anaingia na kuwazuia wasitoke huku akilazimisha kicheko cha kimakanika!


Sehemu ya tatu

Berewa na Namuddu wanajibizana kuhusu kitendo cha Namuddu kuingia chumba cha mapumziko kulikokuwa na wageni. Namuddu hajali hilo na anaweka matumaini ya kubaki na profesa maisha yake yote kwa kuwa aliahaidiwa. Namuddu anatoa kitita kingine cha fedha na kumuonyesha Berewa. Berewa anaghadhibika zaidi na kudai apewe fedha hizo. Namuddu anamlaumu Berewa kwa kumkosea heshima kwa kumwambia alale na profesa ili wapate fedha. Berewa anamkaripia Namuddu. Profesa anaingia. Namuddu anamfuata na kumkubusha ahadi alizompa lakini profesa anakataa kwa kuwa amemuaibisha mbele ya wageni wake. Afisa wa polisi anaingia na msaidizi wake na kutaka kumkamata profesa Coarx na Namuddu. Profesa anajitetea. Berewa anaitwa kutoa ushahidi. Berewa anaeleza kila kitu kuhusu uhusiano wake na Namuddu. Afisa wa polisi ametosheka na maelezo anawaacha huru anaondoka na msaidizi wake. Profesa yupo mshangaoni anamuuliza Berewa, “hivi Berewa kumbe namuddu ni mke wako kweli? Berewa anacheka na kusema, “profesa, mwenye njaa ana mbinu nyingi akiamua kufanya!”  Uk. 70.  

Dhamira 

Uzinzi ni kitu ambacho kimejadiliwa na wengi. Zipo sababu nyingi, lakini sababau kuu mbili kwa nini mtu anakuwa kahaba. Sababau ya kwanza inahusika na maadili ya ngono. Mfumo wetu wa maadili ya ngono unahimiza ukahaba. Tunaishi kwenye jamii ambayo inaamini kwamba ngono na mwenzi wako ni yenye maana na pia ngono na kahaba haina maana. Vitendo vya kijinsia kama vile ngono inayoambatana na vitendo visivyokubalika na jamii vinaweza kuwachochea wanaume wanaotaka vitendo hivyo kwenda kuvitafuta kwa makahaba na hivyo kuhamasisha ukahaba. Wanawake wanamini kwamba wanaume wanaojihusisha na vitendo vya kulala na makahaba nao ni waasherati pia. Wanawake pia wanasema, jamii inawafundisha wavulana kuwaongoza wasichana, hutazamia hivyo hata wanapokuwa watu wazima. Kwa upande mwingine jamii huwafundisha wasichana kuwa wajinga kwa wavulana na hutegemewa kuendelea hivyo hadi wanapokuwa watu wazima. Wazo kuu ni kwamba ukahaba huungwa mkono na urithi wa kiume. Hii ni kwa sababu kwamba ukahaba/uasherati huunga mkono na kuhamasisha wazo kwamba wanawake wote wanaweza kununuliwa au ni duni kuliko wanaume. 

Nadharia ya kijamii ya kisaikolojia inasema kwamba kuna sababu huwafanya wanawake kuingia kwenye ukahaba. Sababu mojawapo ni ile ya kuona wanawake wanaweza kufanya maisha kuwa rahisi kwao au kupata fedha kwa urahisi. Pia ukosefu wa ajira, shinikizo la rika, au mvuto mwingine nje.  

Je, serikali itangaze kodi kubwa kwa makahaba ili washindwe kulipa na hatimaye kuachana na biashara hiyo? Je, ikiwa kutakuwepo na watakaoweza kumudu kulipa kodi hiyo waruhusiwe kuendelea na biashara hii? Je, serikali na madhehebu mbalimbali wawalazimishe vijana kuoa au kuolewa na watulie majumbani mwao? Ni maswali ya kutafakari.

Umasikini unazikumba jamii nyingi duniani. Kitendo cha Berewa kumwambia mke wake alale na bosi wake ili wapate fedha siyo njia halali ya kujikwamua na kuondokana na umasikini. Mwandishi ananuia kusema kuwa zipo njia zenye nidhamu za kujikwamua lakini siyo kudhalilishana kama Berewa alivyofanaya.
Mtazamo wa mwandishi ni wa kiyakinifu. Mwandishi anaona kwamba ikiwa watu watajiheshimu kwa kuanza na nidhamu binafsi basi masuala yenye kudhalilisha utu yataweza kutokomea.

© KIZITO MPANGALA
   0692 555 874

No comments:

Post a Comment

Maoni yako