NA KIZITO MPANGALA
MIAKA 72 tangu jengo hili la
kiroho liliponengwa halijaleta usumbufu kiujenzi. Msingi wake ni imara. Ni
mwaka 2005 pekee jengo hili liliathiriwa na kimbunga (chinangunga) ambapo ni
paa pekee liliharibiwa na ni sehemu ndogo sana iliyoathiriwa. Ilikarabatiwa kwa
muda mfupi na kukamilika. Boriti zake kwenye paa hata watu 10 boriti moja
hawawezi kunyanyua. Huu ni uhandisi wa Wajerumani.
Tazama upande wa juu kuna
msitari mweusi umenyooka ukutani hapo. Hii siyo rangi kusema kwamba imepakwa.
Hayo ni matofali yaliyoiva na kuzidi viwango vya ubora, na ni ngumu kwa
matofali haya kuvunjika kirahisi. Hivyo msitari huo hapo juu ni urembo tu
kiujenzi.
Kuni ambazo ni bora sana
kuchomea matofali ni Miyombo. Miti hii ipo katika vinasaba vilivyopo kwenye
makundi mawili. Kuna Myombo ambao mara nyingi huzalisha aina fulani ya kamba
(mighoyi) ambazo zina matumizi makubwa sana katika jamii ya watu wa Nyasa. Aina
ya pili ni Myombo unaoitwa "Mpangala", mti huu pia ni dawa nzuri sana
endapo utasumbuliwa na tumbo hasa kwa wanaoharisha. Mimi ninatumia sana dawa
hii pamoja na Mwarobaini.
Kwa hiyo, aina hizi mbili za
miyombo ni miti inayoweza kukua na kufikia ukubwa wa muembe. Hizi ni kuni nzuri
za kuchomea matofali kwa sehemu zile ambazo matofali hupatikana kwa kuchimba
udongo, kuchanganya na maji, kufyatua, kusubiri yakauke, kisha kuyapanga kwa
utaalamu ambao hata kijana mwenye digrii ya uhandisi wa ujenzi hawezi kupanga
kama hajakulia mazingira ya upatikanaji wa matofali kwa mchakato huu niliousema
mpaka kwenye chochea kuni na kisha kuwasha moto.
Hivyo, ukuta wa jengo hilo
(kanisa) pichani ni ukuta imara sana. Hata vioo vya madirishani unavyoviona
vimekuwepo hapo kwa muda wa miaka 72 sasa. Hakika kutunza mali kuna faida sana.
Jengo linatunzwa tena hakuna mlinzi hapo lakini mlinzi ni imani za waingiao
humu kushibisha roho zao.
Sehemu ya kijani hapa chini ni
aina fulani ya nyasi ambazo zilipandwa na wahandisi wakoloni wastaarabu kutoka
Ujerumani. Ni nyasi ambazo hazipotezi rangi yake kwa mwaka mzima, hata nyakati
za jua kali zinakuwa na kiasi fulani cha ukijani wake.
Hapa ndiyo kijijini Lundu,
Wilaya ya Nyasa, Mkoani Ruvuma
No comments:
Post a Comment
Maoni yako