February 17, 2018

SOLOMON MINTUS NORTHUP: MTUMWA ALIYEMPIGA MNYAPARA WAKE NA KUANDIKA KITABU KUELEZA MAISHA YAKE YA UTUMWA MIAKA 12.

Na KIZITO MPANGALA
Solomon Northup alizaliwa mwaka 1807 katika mji wa Essex (sasa ni New York), Marekani. Alizaliwa kwa wazazi walioachiliwa huru katika mashamba ya pamba, Louisiana. Baba yake alipokuwa mtumwa asiye huru katika mashamba ya pamba ya tajiri Henry Northup aliaminika katika kazi hiyo. Baada ya kuachiliwa huru aliamua kutumia jina la mnyapara wake, Henry Northup kama jina la pili katika kizazi chake kilichofuata. 

Hapo alimwongezea Solomon Mintus jina la NORTHUP na kuwa SOLOMON MINTUS NORTHUP. Mzee Mintus aliachiliwa huru kwa sababu alimuoa mwanamke chotara katika mji wa Minerva mjini Essex ambaye alikuwa na asili ya Afrika na Ulaya, hivyo weupe ulimzidi na kwa weupe huo alitendewa kama mtu wa kutoka Ulaya. Ndipo Solomon Mintus Northup alipozaliwa akiwa mtumwa huru pamoja na mdogo wake Joseph Mintus Northup kadiri ya sheria ya “Partus sequitur ventrem” ambayo ilirithiwa na koloni la Uingereza nchini Marekani kutoka katika Dola la Warumi (Roman Empire). Sheria hiyo humaanisha “yeyote aliyefika sehemu fulani anapaswa kufuata utaratibu (kanuni au sheria) unaofuatwa katika eneo hilo” ni kama vile kusema “ukiwa katika ardhi ya Warumi ishi kama Mrumi”

Solomon Mintus Northup alikuwa akimwelezea mama yake kuwa ni robo ya Mwafika na robo-tatu ya Mzungu anayeishi Amerika. Baba yake alifanikiwa kumiliki ardhi baada ya kuwa huru. Alijiwekea utaratibu wa kuwekea akiba ya fedha na kupata mahitaji ya lazima kwa familia yake. Pia aliwasomesha watoto wake wawili, Solomon na Joseph. 


Pia aliruhusiwa kupiga kura. Lakini kuanzia mwaka 1821 sheria mpya ilianza kutumika na ilisema kwamba mtu yeyote mweusi yaani mwenye asili ya Afrika hatakiwi kumiliki ardhi, hivyo baba yake alinyang’anywa ardhi yote na ikagawiwa kwa wazungu. Solomon alifanya kazi kwa bidii katika mashamba ya familia yao kabla ya kunyang’anywa.

Solomon Mintus Northup alikuwa mtaalamu wa kupiga kinubi na alijishughulisha na muziki. Mwaka 1841 alipata ofa ya kusafiri kama mwanamuziki mjini Washington D.C. ambako utumwa ulikuwepo kwa kiasi kikubwa. Ofa hiyo alipewa na vijana wawili waliojitambulisha kwake kama wanamuziki na kufanikiwa kuondoka naye huku wakimuahidi kumlipa mshahara mkubwa katika kazi ya muziki na pia kumuongezea fedha atakapohitaji kurudi mjini Louisiana.

Katika safari hiyo kama mwanamuziki huko Washington D.C., Solomon alitekwa na kuuzwa kama mtumwa na kupelekwa katika mji wa Louisiana ambako alitumikishwa katika mashamba ya pamba ya William Ford kwa muda wa miaka 12. Solomon alifanya kazi ya utmwa na alibahatika kuonana na mzungu mmoja wa Kanada ambaye alikuwa akifanya kazi yeye mwenyewe katika mashamba yake. Hapo wakawa marafiki. Mzungu huyo alikuwa akimpasha Solomon habari mbalimbali kutoka New York ambapo habari kuu ya mara kwa mara ilikuwa ni tamko la mahakama ya New York kuwaachilia huru wale wote waliotekwa mjini New York kisha kuuzwa kama watumwa. Familia yake ilimuorodhesha na mwaka 1853 alipata uhuru.
Mtu aliyemteka Solomon alikamatwa na kupelekwa gerezani. Muda mfupi baadaye alitolewa kwa kwa utetezi wa uongozi wa wilaya ya Columbia ambapo Solomon Mintus Northup alizuiliwa kujieleza kuhusu utumwani alikokuwapo. Lakini mjini New York watekaji wenzake walitozwa faini na kesi yao ilikuwepo mahakamani kwa muda wa miaka miwili na baadae ilitupiliwa mbali.
Mwaka 1842 William Ford alimuuza Solomon kwa fundi seremara John Tibaut kwa thamani ya kiasi cha dola 400 ili kufidia deni lake. Akiwa chini ya fundi huyo, Solomon aliteseka zaidi hasa kwa kupigwa mijeredi (viboko) alipokuwa akitumia misumari ambayo mkubwa wake hakuipenda. Lakini katika hali isiyo ya kawaida kwa watumwa, Solomon alikuwa akimmrudishia mangumi mkubwa wake na kumpiga vibaya. John Tibaut alipozidiwa kwa kupigwa na Solomon aliwaita watumwa wake wawili ili wamnyonge Solomon lakini William Ford aliwakataza ambapo alimkuta Solomon amening’izwa mtini kwa kamba na alimfungua.
Solomon alijiokoa na kifo kutoka mikononi John Tibaut alipomtupia shoka  ili amuue, lakini Solomon alilidaka shoka hilo na kumpiga Tibaut mwenyewe huyo mpaka alipopoteza fahamu. Solomon baada ya kumpiga mkubwa wake, alikimbilia vichani na kumuacha Tibaut akiugulia kipigo kwa siku nne mfululizo. Tibaut alimfanya Solomon kuwa mtukutu kwa kumrudishia kipigo mara kwa mara.
Kutokana na ugomvi uliokuwepo kati ya Solomon Northup na mkubwa wake, John Tibaut, rafiki zake Tibaut walimshauri amuuze Solomon ili kuepusha aibu ya kupigwa na mtumwa. Tibaut alimuuza Solomon kwa mkulima wa miwa, Edwin Epps. Edwin Epps alikuwa na kanuni ya kuwachapa mijeredi (viboko) watumwa wake kama wanazembea kazi. Pia, alijiwekea utaratibu wa kuwabaka watumwa wa kike kila alipohitaji.
Mwaka 1928, Solomon alimuoa Anne Hampton, mwanamke chotara kama mama yake. Walipata watoto watatu. Walimiliki shamba katika mji wa Hebron na walikuwa wakiuza sehemu ya mazao yaliyopatikana ili kupata fedha za matumizi ya familia.

Solomon Northup baada ya kuwa huru, mwaka mmoja baadye alichapisha kitabu chake ambacho alisimulia maisha yake akiwa utumwani kwa muda wa miaka 12. Kitabu hicho alikiita “TWELVE YEARS A SLAVE”. Alijishughulisha na utoaji semina sehemu mbalimbali kuhusu utumwa na madhara yake na kisha kuhimiza ukomeshwaji wa utumwa. Alitoa semina hizo akihusianisha na uzoefu wake katika maisha ya utumwa.
Mwaka 1834, Solomon na mkewe waliuza shamba lao na kuhamia katika mji wa Saratoga ambako mkewe alikuwa anafanya kazi ya upishi katika mgahawa mmoja maarufu. Na Solomon alikuwa akipita katika migahawa mbalimbali kupiga kinubi chake ambapo watu walikuwa wakimpa fedha ili awapigie kinubi hicho.
Mwaka 1984, kumbukumbu ya maisha yake ya utumwa kwa muda huo wa miaka 12 ilitengenezwa kama mlolongo wa filamu katika shirika la umma la utangazaji nchini Marekani, PBS. Filamu hiyo kwa ujumla iliitwa Solomon Norhtup’s Odyssey. Na mwaka 2013 filamu mpya na iliyovutia wengi duniani ilitengezwa kutoka katika hadithi ya maisha yake ya utumwa aliyoiandika katika kitabu chake. Filamu hiyo ilibeba jina la kitabu chake yaani TWELVE YEARS A SLAVE ambapo katika filamu hiyo neno twelve limeandikwa katika namba na kuwa 12 YEARS A SLAVE”

© Kizito Mpangala
     0692 555 874

No comments:

Post a Comment

Maoni yako