February 14, 2018

TAULO ZA KIKE

NA MAUNDU MWINGIZI
LEO nimekumbuka moja kati ya matukio yaliyopata kuniumiza sana hapo zamani. Nakumbuka nilikuwa darasa la sita, Shule ya Mazoezi Mwenge, mkoani Tabora.

Siku hiyo, nikiwa nimeketi dawati la mbele kabisa darasani, lilizuka kama zogo maeneo ya katikati ya darasa; wanafunzi wakawa wamesimama; wengine wakicheka, wengine wakionekana kufadhaika. Kusogea eneo la tukio, nikamwona binti mmoja (jina ninalihifadhi) akiwa ameketi juu ya dawati ilhali wenziye wakiwa wima wamemzunguka.


Nikiwa sijatanabahi juu ya kilichotokea, baadhi ya wasichana wakamwinua mwenzao, kisha wakamfunga sweta kiunoni ili limsitiri sehemu ya nyuma. Aliposimama, ndipo nikaona kilichotokea. Damu ilienea kwenye sketi yake huku nyingine ikibaki kwenye dawati. Wenziye kadhaa wakaungana naye kumsindikiza nje ili kumpa nguvu. Lakini mambo ya kitoto, bila kujua hofu na fadhaa vilivyomuathiri kisaikolojia mwenzetu, baadhi (hususan wavulana) wakawa wakishangilia na kumcheka.

Siku kadhaa zilipita bila msichana yule kurudi shuleni. Baadaye tulikuja kujulishwa kuwa, aligoma kurudi kwa aibu na fadhaa. Alipoteza kabisa hali ya kujiamini, akawa anawataka wazazi wake wamuhamishe shule.

Kimsingi, wanapokuwa katika hali kama hii, watoto wa kike hudhalilika na kufadhaika mno. Na hata wanapowahi kujitambua, bado wanakosa namna bora, yenye heshima na staha katika kujistiri. Inafikia pahala, mtoto wa kike anashindwa kusaidia kazi nyumba na anakosa kwenda shuleni kwa kushindwa kumudu gharama za taulo za kike (pedi) ili kudhibiti hali hiyo na kuwa huru. Kama taifa tunashiriki kumfelisha mtoto wa kike kwa kujua ama kutokujua.

Leo ninapoikumbuka kadhia hiyo, niliyoishuhudia nikiwa mdogo shuleni, nabaki nikistaajabu kusikia ati kuna wanaojiita viongozi, halafu wanazuia na kukwamisha hoja ya kuitaka serikali itoe ruzuku ili wanafunzi wa kike wagawiwe taulo hizo bure mashuleni au walau kwa bei ya chini. Leo hii, imefikia mahala huko vijijini, kwa uhaba wa taulo za kike, mtu akibahatika kuipata anatamani aivae hata mwezi mzima bila kuivua.

Tazama maajabu sasa, kondomu zinapatikana kwa bei chee na wakati mwingine kugawiwa bure kabisa, kwa sababu zinapewa ruzuku na serikali ilhali kufanya au kutokufanya ngono ni uamuzi wa mtu. Lakini linapokuja suala la taulo za kike ambapo, hakuna msichana anayeweza kuamua kutopata hedhi, unasikia watu wanaamua kuzuia hoja ya kutolewa ruzuku. Aibu gani hii - ujinga gani huu.
Mmnfyuuuuuuuuu


Maundu Mwingizi (MwanaBalagha),
Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako