January 22, 2013

EMMANUEL NDEMBEKA, WAKILI MWENYE MAJUKUMU MENGI KWA WAKAZI WA WILAYA YA NYASA


Na Mwandishi Wetu, Mbamba Bay
Mwaka 2012 utakuwa wa kukumbukwa sana kwa wakazi wa Mbamba Baya na vitongoji vyake vinavyounda pia wilaya ya Nyasa. Moja ya tukio la kuelekea mwisho wa mwaka wa 2012 ni baadhi ya vijana kutoka wilaya ya Nyasa kutunukiwa nishani za uwakili kutokana na taaluma zao za sheria. Miongoni mwa vijana hao ni dada yetu mpendwa Beatrice Mpangala. Yeye ni wakili kwa sasa na analo jukumu kubwa la kusimamia haki ya wananchi wa jamhuri ya muungano wa Tanzania. 
Emanuel Ndembeka alipoapishwa kuwa wakili
Mbali ya huyo, kijana mwingine Emmanuel G. Ndembeka alitunukiwa uwakili kama ilivyo kwa dada Beatrice Mpangala. Emmanuel G. Ndembeka kijana mzaliwa wa Mbamba Bay, alianza elimu yake ya sekondari akiwa Lundo Sekondari kabla ya kuhamia Kigonsera sekondari maarufu kama Caigo Boys. 
Kigonsera sekondari ndio aliyosoma aliyekuwa rais wa awamu ya tatu katika jamhuri ya muungano wa Tanzania, Benjamin William Mkapa, mzaliwa wa Lupaso mkoani Mtwara. Emmanuel G. Ndembeka anakuwa mtetezi wa jamii yetu kutokana na taaluma yake. 
Umuhimu wake katika jamii ya watanzania ni mkubwa. Mosi, wana jamii wa wilaya ya Nyasa wanajivunia kuzalisha kijana mwenye taaluma ambayo itawasaidia kwa kiwango kikubwa katika kuelewa haki za kumiliki ardhi. 
Kama tujuavyo kwa wakazi wa wilaya ya Nyasa wengi wao wanamiliki ardhi kwa mtindo wa kiutamaduni yaani kurithi ardhi kutoka kwa wazazi hadi kizazi kingine. Matokeo ya jambo hili ni baadhi ya wakazi wasiokuwa na uelewa juu ya haki za kuhifadhi ardhi zao wanaziuza kwa bei ya chini sana kiasi ambacho husababisha matatizo kifamilia. Emmanuel G. Ndembeka anafahamu hili, na kutokana na uelewa wake na namna ya kuelimisha jamii ya wanyasa juu ya kuhifadhi ardhi bila shaka atakuwa mstari wa mbele kuwalinda na kutoa elimu mbadala ili kuzuia uuzaji radhi holela. 
Wakazi wa nyasa wanajivunia kijana ambaye amekulia mazingira yao na anayaelewa kwa kina zaidi. Kwa niaba ya wasomaji wote na wenyeji wa Nyasa, mtandao huu wa Lundunyasa(Lundunyasa Network) unamtakia kila la heri katika mafanikio zaidi. Pia tumkumbushe anauanza mwaka 2013 akiwa na nishani ya wakili mwenye elimu inayotosha kabisa. Mwenyezi Mungu amjaze hekima, upendo na amani zaidi. WAKILI EMANUEL NDEMBEKA, TUNAKUTEGEMEA SANA.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako