Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAKAZI wa Dar es Salaam wenye asili ya wilayani Handeni,
mkoani Tanga, pamoja na maswahiba zao, wamepanga kukutana Ijumaa ya Februari 8,
katika Viwanja vya Leaders Club, kuanzia saa 10 za jioni ili kutafuta namna ya
kusaidia watu wasiojiweza wilayani humo.
Kikao hicho ni cha kwanza kufanywa na watu wa asili ya
Handeni, katika jiji hili ambalo wananchi wengine kutoka mikoa na wilaya
mbalimbali wamekuwa wakikutana na kujadili hali ya maisha inayowakabili.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, mmoja wa wajumbe
wanaoandaa kikao hicho, kilichopewa jina la ‘Handeni Kwetu’, Kambi Mbwana,
alisema kwamba kukutana kwa wadau hao ni sehemu maalum ya kutafuta namna pia ya
kusaidiana na viongozi wao kwa ajili ya maendeleo yao.
Alisema kwamba Wilaya ya Handeni imekuwa ikikabiliwa na
matatizo ya kila aina, ikiwamo njaa na shida ya maji, hivyo kwa wananchi hao
kukutana pamoja, wanaweza kupata ufumbuzi katika baadhi ya mambo.
“Wakati Handeni ikiendelea kutajwa kama wilaya zisizokuwa na
maendeleo kwa miaka 51 ya Uhuru, sisi tunakutana na kutoa kauli moja yenye tija
kwa watu wote.
“Bila kuangalia nafasi zetu, vipato vyetu au heshima katika
jamii, naamini moyo tu wa kukaa na kuzungumza au kuimba wimbo mmoja wa
maendeleo, naamini mambo yatakuwa mazuri, hasa pale kitakapofanyika
kilichojadiliwa na wote,” alisema.
Handeni, inayoongozwa na Muhingo Rweyemamu kama Mkuu wa
Wilaya na Mbunge wake Abdallah Kigoda, imetajwa kukumbwa na baa la njaa na
kulazimika baadhi ya wakazi wake kulalia mboga mboga pamoja na shida ya maji,
jambo linalohitaji kujitolea kwa kila mmoja kwa nafasi yake.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako