February 01, 2013

CHOMBEZO: FIKIRIA VITU ULIVYONAVYO


Ni muhimu kujua kwamba maisha yetu yanaweza kubadilika na kuwa aidha mabaya ama mazuri kutokana na mitazamo yetu. Mitazamo ambayo inatupatia njia nyingine ama zilezile kufanikisha ama kutofanikisha malengo yetu.

Unamaliza wiki nyingine na kutafuta saa nyingine kwa mkondo uleule wenye kilio kwamba huna kitu. Kila siku unaona huna jambo linaloonyesha linakupa faraja ama burudani. Lakini hebu fikiri kwa bidii na kuyaangalia mazingira yako.

Angalia kitu gani unacho halafu jaribu kukizingatia kila dakika iendayo kwa mola wako. Jambo la maana ni kwamba jaribu kukazia fikra kwa vitu ulivyo navyo wala usihangaike kutilia mkazo kwa vitu usivyo navyo.
Kampuni ya amsuala ya habari,sanaa,budrudani,michezo na kadhalika. Chini ya mkurugenzi Kambi Mbwana.
Pengine unafikiria namna ya kumiliki vitu vingi sana, na unaamini vitu hivyo vitakupa fursa ya kupata vingine au kujisikia poa sana. Lakini angalia hakuna sababu ya kujiumiza kwasababu ya vitu usivyonavyo. Vitu kama vile nyumba nzuri, familia bora yenye upendo na mali kedekede.
Tambua hivi vyote haviwezi kukufanya wewe, bali wewe unaweza kuvifanya vitu hivi kuwa nyenzo maishani. Wahenga walipata kusema, afadhali chakula cha mboga za majani penye upendo kuliko ng’ombe dume aliyenoneshwa kwa chuki.

Jaribu kuwa na upendo wa hali ya juu kwa vitu ulivyo navyo, weka mkazo zaidi kila siku kwani hii itakusaidia kuvitafuta vile usivyo navyo. Pengine unajua familia yenu si bora, labda haina pesa, haina mali, haina elimu na hakuna uhakika wa chakula kwa siku.

Huenda mnaishi kwenye nyumba ambayo ikinyesha mvua tu inavuja. Wapo wanaolala kwenye vibanda. Labda wewe huna mavazi mazuri na ungelipenda kuwa na mavazi bora kama binadamu wengine wenye ukwasi. Natambua kuwa unachoshwa na aina yako ya maisha ya kukosa vitu muhimu ambavyo unadhani ndivyo vitakufanya ujisikie vema.

Pengine unatamani kula vyakula vya bei ghali kama na nyenye virutubisho anuai ili uende sambamba na wakati. Wapo watu wanahitaji kuwa na mwonekano mpya kila siku, na wanahitaji kujisikia bora kila dakika iendayo kwa mola.

Wapo wanaochukia nafsi zao kwa kukosa kufanya jambo fulani ama kukosa vitu fulani ambavyo vinawafanya wawe tofauti kila siku. Hebu tafakari ndugu yangu, kitu gani ukikipata kitakufanya umalize kuhitaji vitu vingine?

Kwanini unadhani kukosa kitu kile kunakufanya ushindwe kukitunza kitu hiki ulichonacho? Kwanini unakumbwa na hisia za unyonge kwakuwa umekosa kitu fulani? Nakuomba badili mtazamo huo, weka fikra zako kwenye vitu ulivyonavyo si vile usivyonavyo. Hebu fikiria, hivi unahitaji sana mavazi ya kisasa kuipendeza nafasi yako? 

Je unahitaji mapochopocho ili kuishi na kuwa na afya njema? Wapo watu ambao wakati mwingine wanajisikia kuwa wako kwenye minyonyoro ya umasikini kwa kuwa wanakosa vitu mbalimbali maishani. Wapo wengine huamua kujiingiza kwenye ulevi au matendo mabaya kwakuwa wanakosa pesa, mali, na vitu vingine.

Lakini hawazingatii vitu walivyo navyo. Lakini unapojiwekea mitazamo kwamba huna kitu fulani unajijengea mitazamo hasi ambayo itakuathiri mwili wako kila siku. Unatakiwa kutotoa nafasi kwa kufikiria vitu usivyo navyo. Unatakiwa kuweka mkazo wenye malengo yako na kwa vitu unavyomiliki.

Unaweza kudhani huna jambo au kitu unachomiliki lakini kwa hakika wewe unaweza kuwa ndiye mkombozi wa maisha yako kwa kuweka msingi kwamba hakuna kitu chochote bora bila wewe. Hakuna mtu yeyote atakayekufanya uwe bora zaidi, kuliko wewe mwenyewe. Unatakiwa kujiambia kuwa wewe ni bora kuliko kitu unachokikosa sasa na baadaye.

Ndugu yangu, nyakati zile ambazo unaona huna kitu, basi unatakiwa kujiheshimu sana matendo yako. Jiheshimu sana kwenye nyakati unazokumbwa na mitazamo mibaya juu ya kukosa vitu fulani.
Unapokosa vitu haina maana kwamba wewe si bora, bali unaweza kuheshimu suala hilo huku ukinuia kuwa bora kwa kutafuta vitu. Unaweza kujitolea katika asasi nyingi tu kwani hii inakupa fursa ya kupata mwanga mpya na matumaini mapya.
Kwani hii inakupata ridhiko na kujitambua kwamba familia yenu ina uwezo mdogo wa kifedha na kwamba huwezi kupata kila kitu. Njia nyingine mbali na kujiheshimu ni kuondoa wingu jeusi ulilonalo kwamba ukivipata vitu hivyo ni mafanikio makubwa.
Lakini unasahau kuwa kadiri unavyohitaji vitu ndivyo unavyoweza kufanikiwa kutohangaikia vitu. Kama nilivyokuasa wiki jana kwamba weka vipaumbele usiwe mtu unayeishi bila kujua unakokwenda.
Unajikuta unafanya kazi kila siku mshahara unalipa madeni kwa kuwa una hulka ya kutaka kumiliki vitu ambavyo huvimiliki na vinakuzidi uwezo. Panga njia za kuweka akiba ili uweze kujijengea uwezo zaidi. Safisha roho yako ili usiwe mtumwa wa matukio au vitu.
Maana watu wengi siku hizi ni watumwa wa vitu au matukio, pengine kuna harusi, sherehe na mambo mengine. Kama uwezo wako hauruhusu basi usitake kulingana na wale wenye uwezo mkubwa. Tafakari sana vitu ulivyo navyo na uvipatie heshima kwamba ni vitu vizuri na vinapaswa kuheshimiwa daima.

Ni wakati wa kujiangalia mwenendo wako kwani inakupa fursa nzuri ya kuukarabati ubongo wako na kujua namna ya kufanikisha kuvipenda vitu vyako. Penda kila kitu ulichonacho kwani kitakupa mwangaza zaidi wa kuyaona matumaini mapya. Matumaini haya yataanza kwa kuvitazama vitu ulivyo navyo au kazi uliyonayo ambayo inakupa wasaa wa kutafakari zaidi.
Inawezekana kuwa huoni mwelekeo kwa kuwa unapata maslahi duni, lakini kumbuka hakuna kizuri kinachokujia bila kuwepo kwa kingine. Hivyo ni wakati wako wa kujiheshimu na kutazama yale uliyonayo kuliko yale usiyonayo.

Tazama mbele zaidi wala usiumizwa na hali uliyonayo sasa, kwani saa yaja, mafanikio yako yanakuja. Nisikuchoshe msomaji, hili ndilo somo letu la leo. Mimi nakuacha hapa, naenda kuendelea kusoma riwaya nzuri na ya kusisimua iitwayo ‘Nyuso za Mwanamke.’ Je wewe umesoma vitabu vingapi mwaka huu na vimekupa maarifa. Hebu muulize mwenzio hapo! Tukutane wiki kesho.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako