• Mradi kabambe wa umeme kujengwa
• Rais Kikwete apokea ripoti ya maandalizi
• Utagharimu mabilioni ya fedha
• Utaunganisha mikoa yote kwenye Gridi ya Taifa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete leo, Jumatano, Oktoba 12, 2011, amepokea ripoti kutoka makampuni
mawili ya kimataifa kuhusu Mpango Kabambe ya mradi mkubwa wa umeme ambao
utaunganisha kwenye Gridi ya Taifa mikoa yote sita ambayo kwa sasa haiko kwenye
gridi hiyo.
Rais Kikwete amepokea ripoti hiyo kutoka makampuni ya China
National Machinery & Equipment Import & Export Corporation (CMEC) ya
China na Siemens ya Ujerumani ambayo kwa pamoja yanatarajia kujenga kituo
kikubwa cha kuzalisha umeme kutokana na gesi katika eneo la Mnazi Bay, mjini
Mtwara na pia kujenga njia ya kusafirisha umeme ya kilomita 1,100 kutoka Mtwara
hadi Singida.
Mradi huo mkubwa wa umeme wa megawati 300 utakaogharimu
karibu dola za Marekani milioni 684 na utakaozalisha umeme wa moja kwa moja na
wenye nguvu kubwa ya 300 kV (300 kV High Voltage Direct Current – HVDC)
utagharimiwa kwa pamoja na mkopo kutoka Benki ya Exim ya China na Serikali ya
Tanzania.
Umeme kutokana na mradi huo utaunganishwa kwenye gridi ya
taifa na kutoka Singida hatimaye utavutwa kupelekwa katika mikoa ya Kaskazini
Magharibi mwa Tanzania ya Kagera, Kigoma na Rukwa ambako pia utaongeza
upatikanaji wa umeme katika machimbo ya madini yaliyoko katika mikoa hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mbali na mikoa hiyo mitatu, pia
mikoa ya Lindi na Mtwara ambayo nayo haiko katika Gridi ya Taifa nayo
itaunganishwa katika Gridi hiyo kupitia umeme huo.
Kuunganishwa kwa mikoa hiyo sita katika Gridi ya Taifa
kupitia umeme wa mradi huo pamoja na Mkoa wa Ruvuma ambao utaunganishwa katika
Gridi hiyo kwa mradi unaogharimiwa na Serikali ya Sweden kutakamilisha mpango
wa Serikali ya Awamu ya Nne kuunganisha mikoa yote ya Tanzania kwenye umeme wa
Gridi ya Taifa.
Kwa sasa Mkoa wa Kagera unahudumiwa na umeme kutoka Uganda,
wakati Mikoa ya Kigoma na Rukwa inahudumiwa na umeme wa mafuta ya dizeli. Mikoa
ya Mtwara na Lindi inapata umeme wake kutoka kampuni ya Wentworth ambao
haujaunganishwa kwenye gridi ya taifa.
Kuunganisha mikoa yote ya Tanzania kwenye Gridi ya Taifa
ilikuwa moja ya ahadi kubwa zilizotolewa na Serikali ya Rais Kikwete wakati
anaingia maradakani na kwa kuuunganisha mikoa hiyo sita kwenye Gridi hiyo,
Serikali hiyo itakuwa imetimimiza ahadi hiyo.
Akipokea ripoti hiyo, Rais Kikwete ameishukuru Wizara ya
Fedha, Wizara ya Nishati na Madini pamoja na Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO) kwa juhudi zao zilizofanikisha makubaliano ya kujengwa kwa mradi huo
mkubwa wa umeme ambao utachangia kuongeza wingi wa umeme nchini katika kipindi
ambacho kwa miezi kadhaa Tanzania imekabiliwa na mgawo wa umeme kutokana na
ukame uliokausha maji kwenye mabwawa makubwa ya uzalishaji umeme nchini.
Rais Kikwete pia ameitaka Wizara ya Fedha kwa kushirikiana
na Benki ya EXIM ya China kuhakikisha kuwa fedha za kutekeleza mradi huo
zinapatikana haraka iwezekanavyo na pia ameitaka TANESCO na makampuni ya CMEC
na Siemens baada ya kupatikana kwa fedha kuanza ujenzi wa mradi huo kwa kasi na
kuukamilisha katika muda na ubora unaotarajiwa.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu
DAR ES SALAAM.
12 Oktoba, 2011
IMECHUKULIWA KUTOKA WANABIDII FORUM hii leo jumanne.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako