October 09, 2017

ZENZILE MIRIAM MAKEBA: MWANAMUZIKI ANAYEKUMBUKWA NA WENGI BARANI AFRIKA.

Na Kizito Mpangala

Zenzile Miriam Makeba alizaliwa mwaka 1932 jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini. Alizaliwa kwa wazazi wenye asili tofauti kikabila, baba yake ni Mxhosa, na mama yake ni Mswazi. Bibi yake alikuwa mkunga wa jadi na ndiye aliye fanikisha z0ezi la kumsaidia mama yake kujifungua salama. Bibi yake huyo alimuasa mama yake Miriam kwamba asione taabu na asijisikie upweka kumlea mtoto (Miriam) katika hali duni ya maisha kwani ndiye aliyemleta ulimwenguni. Alikuwa akimwambia “Uzenzile” kwa lugha ya Xhosa, likimaaniasha “Umemleta wewe mwenyewe”, hivyo akaamua kumpa mtoto huyo jina la ZENZILE MIRIAM MAKEBA.

ZENZILE MIRIAM MAKEBA
Licha ya baba yake kuwa mwalimu, lakini walikabiliwa na ukata ambapo alipotimiza siku 18 tu tangu azaliwe alilazimika kwenda kuishi gerezani na mama yake ili apate kunyonya. Aliishi gerezani na mama yake kwa muda wa miezi sita, hii ni kutokana na Makaburu walioshinikizwa na  falsafa ya Apartheid walimhukumu mama yake Miriam kifungo cha miezi sita gerezani licha ya kuwaeleza kuwa ana mtoto mchanga na hajamaliza hata mwezi tangu azaliwe. Lakini hakusikilizwa. Sababu ya kuhukumiwa kifungo hicho ni baada ya kukutwa (mama yake Miriam) akiuza pombe ya kienyeji maarufu sana nchini Afrika Kusini ambayo inaitwa umqombot. Ndugu, jamaa na marfikia walishindwa kumlipia faini kutokana na ukata wa uchumi, hivyo ilibidi akaishi gerezani.


Alipokuwa na umri mdogo, Miriam alikuwa mwanakwaya katika kanisa lao la Methodisti. Baada ya kifo cha baba yake alilazimika kufanya kazi mbalimbali ili kupata ridhiki, hapo akachukuliwa na tajiri mmoja ili akahudumu kama “house girl” katika nyumba yake, huku mama yake akipewa kazi za kufanya usafi katika nyumba za Makaburu jijini Johannesburg, na baadae wakahamia katika mkoa wa Transvaal.

Alipokuwa mkoani Transvaal, mwaka 1949 akiwa na miaka 17, Miriam alilazimishwa kuolewa na polisi aliyekuwa mafunzoni na mwaka 1950 walibahatika kupata mtoto mmoja, Bongi Makeba. Baadae Miriam aligundulika kuwa na kansa ya titi ndipo mume wake akampiga na kisha kumtelekeza moja kwa moja baada ya miaka miwili tu ya kuishi ya ndoa yao.

Zenzile Miriam Makeba akitumbuiza
Miriam Makeba alianza kuwekeza rasmi katika muziki alipokaribishwa na kujinga katika bendi ya watu wa Cuba iliyoweka makazi yake nchini Afrika Kusini, bendi hiyo iliitwa Manhattan Brothers ambapo alikuwa mwanamke peke yake katika bendi hiyo. Akiwa na bendi hiyo mwaka 1953 aliatoa wimbo wake wa kwanza kwa lugha ya Xhosa ulioitwa “Laku Tshoni Ilanga” na akatambuliwa rasmi kitaifa kama mwanamuziki.

Akiwa bado na bendi hiyo, licha ya kushirki katika bendi zingine za wenyeji, mwaka 1955 alionana na kijana mmoja mwanasheria ambaye alijitambulisha kwake kwa jina la Nelson Mandela. Nelson Mandela alijieleza kwake kuwa amemfuata ili kumpa hamasa zaidi ya kukosoa falsafa za Apartheid kupitia muziki. Kisha akamwambia si lazima aimbe kuhusu Apartheid tu, bali yapo mengine anaweza kuyaimba. Akazungumza naye maneno ya kumuongezea morali na mwisho akamwambaia “Miriam, usikate tama, utakuja kuwa mtu muhimu kwenye taifa letu hili

Mwaka 1956 alitoa wimbo mwingine ambao aliuimba kwa lugha ya Xhosa lakini baadae ukatafsiriwa kwa Kiingereza na ukaingia katika chati ya nyimbo 100 bora duniani kwenye rekodi ya Marekani iliyoitwa “US Billboard Top 100 na picha yake ikatumiwa katika ukurasa wa mbelewa jarida la Drum.

Mwaka 1959, Miriam alijizolea sifa na pongezi kemekem baada ya kuigiza kwenye filamu iliyoitwa “Come Back Afica” ambayo ilikuwa na maudhui ya yaliyokuwa yakikosoa falsafa za Apartheid nchini humo. Ni filamu ambayo ilirekodiwa kwa siri kubwa ili kuepuka pingamizi la serikali ya Makaburu kwa kuwa ilikuwa na uhalisia wa hali ya juu sana. Baadae mwongozaji wa filamu hiyo alimlipia viza Miriam na kumuambia aende nchini Italia kuhudhuria tamasha la filamu la kitaifa nchini humo. Uhodari wa Miriam katika filamu hiyo ulitambuliwa kimataifa na alipaswa kusafiri kwenda sehemu mbalimbali duniani ili kucheza mubashara jukwaani.

Miriam alipata huzuni kubwa kutokana na kifo cha mama yake ambaye aliuawa katika shambulio la mauaji ya kimbari ya Sharpeville yaani Sharpeville massacre mwaka 1960 wakati yeye akiwa uhamishoni nchini Marekani. Alipotaka kusafiri kurudi nyumbani ili kuhudhuria mazishi alifanyiwa hujuma ya kufutiwa passport yake ya kusafiria. Katika mauaji ya kimbari ya Sharpeville alipoteza ndugu zake wengine wawili.

Miriam Makeba alikwenda nchini Kenya mwaka 1962 katika harakati zake za muziki akiwa na lengo la kuishawishi serikali ya Walowezi iiache Kenya iwe huru, yaani aliongeza hamasa ya kupigania uhuru wa Kenya. Alimchangia Mh. Jomo Kenyatta fedha za matumizi katika harakati zake kama kiongozi wa kudai uhuru nchini humo.

Mwaka huo huo, Miriam Makeba alinyang’anywa uraia wa afrika Kusini na Makaburu waliokuwa wakitawala nchini humo na kupigwa marufuku ya nyimbo zake nchini humo na hata studio yke binafsi ilifungwa. Akafikia hatua ya kuwa mtu asiye na taifa (stateless person). Lakini alisaidiwa na serikali ya Algeria, Ubelgiji, Guinea, na Ghana akapata passport ya kusafiria, na aliweza kuishi katika nchi hizo tajwa. Katika maisha yake alikuwa na passport 9 za kimataifa na alipewa uraia wa heshima katika nchi 10 duniani.

Baada ya misukosuko hiyo, Miriam Makeba alialikwa na Mh. Haile Selassie nchini Ethiopia akatumbuize katika sherehe za kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika. Na katika misukosuko ya ndoa yake ya pili, alifanywa kuwa mtu wa kuangaliwa sana kutokana na ujasiri wake katika kupinga falsafa za Apartheid, hivyo Makaburu wa afrika Kusini waliwasiliana na serkali ya Marekani ambako alikuwa anaishi imchunguze kwani Makaburu walihisi kuwa Miriam ana mafunzo ya kijeshi. Hivyo, shirika la ujasusi la CIA liliweka kamera kwa kificho katika nyumba yake aliyokuwa akiishi huko Marekani. Baadae FBI nalo likajiunga katika mchakato wa kumchunguza Miriam Makeba.

Hii ni baada ya kuolewa na mwanaume mweusi wa Marekani ambaye naye aliwekewa mashaka. Miriam na mumewe waliposafiri kwenda Bahamas walizuiliwa na serikali ya Marekani wasirudi tena. Mumewe alikuwa akiitwa Stokely Carmichael. Baada ya kuzuiliwa kurudi Marekani ndipo Miriam alipotumia passport aliyoipata kutoka serikali ya Guinea na akaenda huko  na mumewe. Wakati wakiwa Guinea mumewe alilazimika kubadili jina na kuitwa Kwame Toure. Waliishi Guinea kwa zaidi ya miaka 10, wakawa watu wa karibu sana wa rais wa nchi hiyo Mh. Ahmed Sekou Toure  ambaye alisifika sana kuheshimu kazi za wasanii wa muziki kutokana na kuvutiwa na muziki wa Miriam Makeba. Tangu mwaka 1968 Makeba  hakurudi tena Marekani hadi mwaka 1987.

Mume wa Miriam Makeba, bw. Stokely Carmichael. Baadae alibadili jina na aliitwa Kwame Toure

Makeba alipokuwa Guinea alikuwa akiandika nyimbo mbalimbali na kuimba kuhusu utwala wa kibaguzi wa Marekani huku akisifu juhudi za Malcolm X, na pia alisifu juhudi za Patrice Lumumba nchini Congo kupitia muziki. Amewahi kualikwa kutumbuiza katika nchi mbalimbali barani Afrika zilipokuwa zikiachiwa madaraka na wakaloni. Amewahi kutumbuiza nchini Tanganyika (Tanzania ya sasa), Kenya, Angola, Zambia, Msumbiji, Liberia na kadhalika. Akateuliwa kuwa mhusika wa shirika la umoja wa mataifa nchini Guinea mwaka 1975.   

Binti yake, Bongi Makeba naye alikuwa mwanamuziki akiwa anaishi nchini Ubelgiji. Kwa bahati mbaya binti yake huyo lalifariki mwaka 1985 alipokuwa anajifungua ambapo mtoto alipona, hivyo Miriam alipaswa kuwalea wajukuu wake wawili, akahama nchini Guinea na kwenda kuishi Brussels Ubelgiji. Mwaka 1987 alikwenda nchini Zimbabwe kutumbuiza katika wimbo wake ulioitwa “Sangoma” ukimaanisha “mponyaji”

Mwaka 1990, rais wa Afrika Kusini Mh. Frederick de Clerk alifuta zuio la Miriam Makeba kuishi nchini Afrika Kusini, hivyo aliruhusiwa kurudi nyumbani sambamba na kuachiliwa huru Mzee Nelson Mandela kutoka gerezani. Mwezi June ikiwa ni mienzi minne baada ya kuachiliwa huru Mzee Nelson Mandela, Miriam Makeba alirudi nchini Afrika Kusini kwa kutumia passport ya Ufaransa aliyokuwa amepewa bure, hii ni baada ya kuishi umaishoni zaidi ya miaka 10.

Mwaka 1992 aliigiza katika filamu ya Sarafina ambayo inaeleza mambo ya  Afrika Kusini hasa katika matukio ya kinyama yaliyokuwa yakifanyika katika mji wa Southern West Town maarufu kama SOWETO. Na mwaka 1999 aliteuliwa kuwa balozi wa shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia kilimo na chakula, FAO.

Alifanya kazi kwa ukaribu na Mh. Graca Machel-Mandela, kisha alianzisha kituo cha Makeba Center Of Girls cha watoto yatima. Mwaka 2002 alishiriki katika filamu fupi iliyokuwa ikieleza jinsi watu weusi wa Afrika Kusini walivyokuwa wakipambana dhidi ya  Apartheid nchini humo. Filamu hiyo inaitwa Amandla. Ameandika vitabu viwili vya wasifu wake. Kitabu cha kwanza kinaitwa Makeba: My story na kitabu cha pili kinaitwa Makeba: The Miriam Makeba Story.

Mwaka 2008 aliugua ghafla kutokana na maumivu katika moyo wake alipokuwa jukwaani akitumbuiza nchini Italia. Alialikwa nchini humo katika tamasha lililoandaliwa ili kumsaidia mwandishi wa vitabu bwana Roberto Saviano ambaye alikuwa anataka kuchapisha kitabu chake kilichokuwa kikieleza maovu yanayofanywa na kikundi cha uhalifu cha Camorra. Ndipo alipofariki.

Miriam Makeba anasifiwa kwa kuchukia kuweka nakshi katika uso wake hasa make up. Alikuwa hapendi kabisa urembo wa aina hiyo na kudai anataka kuwa na mwonekano wa asili. Pia hakupenda kutia nywele zake dawa ya aina yoyote ili ziwe ndefu. Alipenda kuchana nywele zake zikiwa zimesimama vizuri na akazipa jina Afro look yaani mwanekano wa Kiafrika, hapo ndipo neno ‘Afro” lilipozaliwa.

Miriam Makeba alikuwa mstari wa mbele kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini na hata Marekani. Makaburu walisi kwamba nyimbo zake zinalenga siasa zao lakini yeye mwenyewe alikana jambo hilo na kusema haimbi siasa bali anachokiimba ndio ukweli ulivyo nchini humo. Hapo nyimbo zake nyingi zikapigwa marufuku.

Yapo mengi aliyoyafanya na kuyapa kipaumbele katika harakati za maisha yake hasa katika harakati za kudai uhuru. Mzee Nelson Mandela alikuwa akimuita Miriam Makeba kwamba ni mama wa taifa la Afrika Kusini katika muziki. Miriam Makeba ni mmojawapo wa washawishi wa kuwepo kwa muziki pekee nchini Afrika Kusini maarufu kama Kwaito. Mpaka alipofariki, Miriam Makeba alikuwa na mtoto mmoja tu.


© Kizito Mpangala  (0692 555 874,  0743 369 108

No comments:

Post a Comment

Maoni yako