NA MWANDISHI WETU
MKOA wa Ruvuma unatarajia
kupata hifadhi ya wanyamapori ya pili ya asili inayoitwa Kilima Mbamba (Mbamba
Hill) ambayo ipo mjini Mbamba Bay makao makuu ya wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma.
Hifadhi pekee Tanzania ya
kwanza ya asili iliyopo mjini inaitwa Luhira iliyopo kilometa saba toka mjini
Songea mkoani Ruvuma iliyoanzishwa mwaka 1974. Mkoa wa Ruvuma unapata hifadhi
ya pili ya asili mjini.
Akizungumzia hifadhi hiyo Afisa
Maliasili na Utalii wa Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe anasema mchakato wa
kuendeleza Mbamba Hill unaendelea vizuri na kwamba ya tayari bajeti
imepitishwa.
“Tumeshapima eneo lote la
Hifadhi ya Mbamba Hill,lina ukubwa wa hekta 420,ndani ya hifadhi hiyo kuna
wanyama kama nyani, nyoka, pimbi,chui na ndege wa aina mbalimbali’’, anasema
Challe
Amesema bajeti ya kujenga uzio
kuzunguka Mbamba Bay Hill imepitishwa na kwamba ujenzi unatarajia kuanza wakati
wowote fedha zitakapoletwa na kwamba mara baada ya ujenzi wa uzio kukamilika
wanyamapori wa aina mbalimbali wanatarajia kuongezwa.
Anawataja wanyama ambao wanatarajia
kuongezwa katika hifadhi hiyo kuwa ni Swala, Fisimaji, mbuzi Mawe, Digidigi, Mbawala
na kwamba wanyama watakaongezwa ni wale ambao wanaweza kuishi katika mazingira
ya hifadhi hiyo ambayo imeungana na ziwa Nyasa.
©Albano Midelo, Ofisa habari wa
Manispaa ya Songea.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako