NA HONORIUS MPANGALA, BAHI
NILIPOKUWA mdogo niliamini maisha ni jambo ambalo
liko tofauti na la kuogofya sana katika jamii. Sababu kubwa ni pale nilipokuwa
nayasikia maneno kama “Usicheze na maisha”. Fikra zangu zilinipeleka kuwa
maisha ni jitu linalotisha sana katika jamii.
Baada ya makuzi nikapata misemo kama “Maisha
yenyewe ndiyo haya haya” nikaanza kutambua kumbe mwenendo wa kuanzia asubuhi
unaamka hadi usiku unaingia kulala hizi harakati zote ufanyazo ndiyo maisha
yenyewe.
Katika vipindi ambavyo wapiga kura na wananchi wa
kawaida toka vyama vya siasa wanajiona kama na wao ni wenyechama basi ni katika
kampeni za uchaguzi. Kipindi hiki kila mwanachama anajiita ni mwenyechama. Ni
kipindi ambacho watu hao hudiriki kunukuu maneno ya wagombea wao na kuiaminisha
hadhira aliyonayo kuwa chama chetu kitatekeleza mambo kadha wa kadha.
Licha ya elimu inayotuambia siasa ni sayansi wako
sahihi kwa yale wanayoyafanya katika mikakati ya kufanikiwa katika siasa.
Niliwahi kuambiwa na Mzee mmoja ambaye
alikuwa Mwenyekiti wa tawi wa chama fulani cha siasa kuwa hata uchawi ni
sayansi pia, ila uchawi wa kizungu ni wa faida zaidi kuliko huu wa kiafrika.
Hivyo hata mimi naweza kuamini siasa ni sayansi
kwa wenzetu wa mataifa yaliyoendelea lakini kwa nchi za kiafrika ambako
demokrasia tunaiga sioni kama siasa ni sayansi.
Vyama vya siasa vimekuwa na kawaida ya kuwatumia
wanachama au wapiga kura kwa ujumla kama Makarai kwa fundi muashi. Karai
hukumbukwa wakati wa kuwekewa “UdongoUlaya” na “UdongoAfrika” wakati wa ujenzi
na litahifadhika vyema sana hadi ujenzi uishe lakini mara baada ya kukamilika
ujenzi utalikuta karai halikusafishwa lilipomaliza kazi yake na limetelekezwa
katika maeneo ambayo siyo ya kuthaminika tena.
Wapiga kura na wanachama wa vyama vya siasa
wamekuwa na mitazamo tofauti sana wakati wa kampeni. Pia kumekuwa na mizuka
inayokuja bila kutarajiwa wakati huo ambao unaweza kuwakuta hata wafuasi
wakigombana kwasababu ya kutetea vyama vya huku wenyechama wakiwa katika Viti
vya kuzunguka na hawajui kwa namna gani mfuasi umepigwa au kuumizwa na juhudi
za kukitetea chama chako.
Vilemba, kofia, Fulana, kanga, vitenge na vidani
vya mkononi vimekuwa kama sehemu ya kuelezea mtu ni mfuasi wa chama gani. Licha
ya kukisemea sana chama unakuta maisha ya hao waliokuwa wananadi chama chao Kwa
kunukuu maneno matamu na yenye matumaini ya maisha wakiwa wamechoka na maisha
na kutaabika sana.
Kitu wanachosahau watu ni kwamba hawakujua kuwa
maisha yao ni yao hayana uhusiano wowote na kiongozi wa kisiasa ambaye alipata
kazi hiyo kuwekewa alama ya vema labda atakuwa msaada wa kuleta chumvi na sukari
kama ilivyofanyika usiku wa kuamkia siku ya uchaguzi.
Kauli za kusema vyuma vimekaza huwa najiuliza
kukaza huko anakaza kiongozi kiasi kwamba mtu akashindwa kwenda shambani kulima
na hatimaye akaja akauza mazao yake? Tatizo ni maisha ya utegemezi ambayo wote
tumeyazoea kuwa kila kitu kinaendana na utegemezi kutoka katika serikali. Sasa
inapokuja suala la kukutaka ujiendeshe mwenyewe kimaisha ndipo tunapolitupilia mbali
suala la ugumu wake kwa aliyechaguliwa kuwa kiongozi. Tatizo ni kuchukua na
kumeza maneno ya wakati wa kampeni na kufikiri kuwa ndiyo uhalisia wa maisha
utakuwa hivyo.
Nimesimamia chaguzi mbili yaani wa mwaka 2010 na
ule w mwaka 2015 nikiwa Mkoa wa Mbeya. Nazikumbuka kampeni zile lakini
niliporejea maeneo yale Julai mwaka 2017, nikakuta mazungumzo tofauti toka kwa
watu walioonekana ni wenyechama wakati wa kampeni za uchaguzi wakasahau kama
wao ni wanachama tu.
Kwavile fikra na mitazamo yao na mimi iko tofauti
katika suala la kuiona siasa ndiyo kila kitu nilibaki kukaa kimya huku
nikitasabamu wakati wenzangu wakiwa wanazungumza kwa kusikitikia hali iliyopo
ni ngumu kimaisha. Nilipoulizwa mbona kama unacheka jibu langu
lilikuwa nilikataa kuishi kwa kutegemea masuala ya kisiasa kuwa ndiyo muafaka
ya utatuzi wa maisha yangu. Palepale nikawaambia nendeni bustanini mkalime
nyanya au vitunguu bei iko vizuri sokoni.
Nikawaambia jinsi ufuta unavyotafutwa nyakati hizo.
Nikawaeleza juu ya faida kilimo cha biashara. Nilipowaambia mwanamuziki wa
Bongo Fleva, Seleman Msindi au maarufu kwa jina la Afande Sele wa Mkoani Morogoro
sasa hivi yuko shambani analima Pilipilihoho, Bamia,Matikiti,Karoti,Nyanya, Vitungu
na Mbogamboga (Horticulture) na anauza walishangaa.
Niliwapa mfano wa Afande Sele kwasababu alikuwa
ameingia katika siasa na kugombea ubunge kupitia ACT-Wazalendo jimbo la
Morogoro Mjini lakini baadaye alipogundua mitazamo yake inakinzana na uhalisia
wa siasa iliyopo akaamua kujiweka kando.
Laiti kama tungelijua kama wenyechama wanawaona
wanachama kama Makarai wakati wa ujenzi basi sidhani kama wangefikia hatua ya
kulalamikia mamlaka mbalimbali katika ugumu wa maisha wanayoyasema.
Mnufaika namba moja katika masuala ya siasa katika
uongozi anaweza kuwa mwanafamilia ya kiongozi. Lakini wengine wataishia
kukutana na lugha nzuri ambayo itawafanya waamini kukosea ni jambo ambalo lipo.
Ujanja wa kitumia maandiko ya kwenye vitabu vitakatifu na uhalisia wa wananchi
wanaojifanya kuzijua dini huingia miguu yote miwili na kuamini kuwa hata Mungu
alisema samehe saba mara sabini.
Si ajabu kuona wanasiasa wakijifanya kujihusisha
na masuala ya Mungu baada ya kuwa viongozi wakati hapo awali wakati wa kutafuta
walipishana kwa waganga wa kienyeji kama magari yanayopishana Ubungo mataa huko
Dar es salaam.
Utegemezi wa maisha ya kufikiri wanasiasa ndio
watakao kuletea sukari, sabuni na chumvi kama wanavyowahadaa siku kadhaa kabla
ya uchaguzi ndio kitu kinachowafanya wengi wafikiri kuwa maisha yapo hivyo
kupitia uongozi wa mgombea husika.
Aliyekuja na kauli ya ‘pambana na hali yako’
natamani nimjue walao nimwagizie zawadi kwa ubunifu. Maana uhalisia wa
alichokisema ndiyo unaotakiwa katika maisha kamwe usitegemee kuweka bango hata
katika milango ya maskani yenu itafanya ugumu ulionao wa maisha upungue kwa
kutazama picha.
Kuna kijana aliyebandika bango la mgombea fulani
katika mlango wake katika kibanda chake cha biashara mkoani Mbeya. Naye alijiona
ni mwenyechama kwa wakati ule kwani aliitwa na viongozi wa eneo lile na kupewa
posho ya kusambazia vijana wenzake.
Siku aliponieleza uzuri wa bango lile kukaa pale
nikamwambia watumie kwa akili hao jamaa zako kwani maisha baada ya uchaguzi
wenzako watakuwa wanaonyesha Pikipiki walizopewa halafu wewe utakuwa umebaki
kama ulivyo na bango lako. Na huo ndo uhalisia ulitokea maisha yamekuwa
yaleyale. Maeneo ni yaleyale kwa mtu yuleyule. Hii ndio siasa ya kiafrika ya
utegemezi wa fikra na mitazamo kwa kutoka kwa wanasiasa.
Kila mmoja aichunguze njia yake ya kutafuta maisha
lakini kuna wale wanaoingia kichwa kichwa bila kujua uhalisia wa kile wanachokihitaji
kama kitapatikana kwa njia zipi. Bibi zetu na babu zetu kule vijijini wanapokuwa
wanapokuwa na masimulizi ya hii nchi ilikotoka utaona wanakuambia shika jembe
ukalime ni kama wanatambua msingi wa maisha uko katika mikono na kichwa chako
na sio mwanasiasa.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako