January 17, 2018

KUPIGA MARUFUKU MAVAZI YA NUSU UCHI

NA PROFESA ANNA TIBAIJUKA (MB)
Profesa Tibaijuka.

 UKIONA watu wanahangaika na suala la mavazi hasa kukazania yale yanayoficha mwili wa mwanamke ujue wana matatizo yao wamelishwa kasumba ya wageni. Dhana ya kuficha mwili ni kweli haina Uafrika wowote ndani yake. Mwafrika katika asili yake haangaiki kuficha mwili wa mwanamke. Hauoni kama chombo cha kumfurahisha mwanaume bali kiungo muhimu kumruhusu mwanamke kutimiza wajibu wake.

Kwa mfano wakati mwanamke wa kizungu anahangaika kujificha kunyonyesha mtoto Mwafrika asili anatoa ziwa mtoto ananyonya hadharani. Hapa titi ni mali ya mtoto siyo ya mume.

Kwa hiyo kabla ya wakoloni kufika na wamisionari walioandamana nao wakiwa wamevaa nguo ndefu watoto walikuwa uchi wasichana walipewa ngozi kujisitiri sehemu za siri wakivunja ungo na wanawake nao yalikuwa hayo hayo. Kulikuwa hakuna ubakaji kwa sababu hiyo. 

Ni kweli utasema jamii ilikuwa haijaendelea na maskini. Unaweza pia kusema hali ya maendeleo ilikuwa duni.Nguo hakuna. Lakini hoja hapa ninayolenga kupangua ni ile kwamba wanawake wakijifunua kwa kuonyesha uso au mikono au matiti au miguu yao au mapaja wanawakwaza wanaume. Sio kweli. Mbona mababu zetu hawakukwazika hizo enzi nilizoelezea? Mbona hawakubaka watoto na wasichana kama ilivyo sasa?

Dhana kwamba mwili wa mwanamke ni chombo cha anasa kwa mwanaume zimepandikizwa katika jamii ya Kiafrika na ziko katika fikra. Kuwafunika wanawake kwa mavazi marefu na shungi hakuondoi tamaa na mawazo ya anasa juu yao kwa wenye nia hiyo. On the contrary kunachochea jambo hili. Wanaume wanabaki kufikiri huyu sasa huko ndani yukoje? Hii inaweza kuchochea mashambulizi ya ubakaji kuliko kusaidia kuyaepusha.

Angalia Ulaya ambapo hakuna anayehangaika na kuthibiti mavazi. Hata uvae mini skirt ya namna gani hakuna anayejali. RUKSA. Wasichana wanavaa kaptula no problem. Jamii imejikomboa kimawazo na kifikra. Wanajua jinsi mwili na maumbile ya mwanamke yalivyo.

Kwa hiyo kama hupendi kuwanyanyapaa wanawake huwezi kuwalazimisha au kuwapangia mavazi na muonekano. Wacha waamue wenyewe wanavyotaka kwa sababu zao. Wengine utamaduni na dini wengine siasa (kutafuta kukubalika) wengine sheria za kazi au shughuli yao na waliowengi kutaka kupendeza tu. Let the women be free in deciding for themselves what to wear. Trust their judgement.

Nawasilisha.
Prof.Anna Tijaijuka,
Mbunge - Muleba kusini.

MUHIMU: Profesa Tibaijuka ni Waziri wa zamani wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi ambaye pia amewahi kuwa mkurugenzi wa Shirika la Makazi la Umoja wa mataifa (UN-HABITAT).


No comments:

Post a Comment

Maoni yako