Markus Mpangala |
Ndugu zangu waungwana, kama kuna kitu tumejilemaza katika
nchi yetu hii ni ile hali ya kujitumbukiza katika janga la kufikiria matatizo
tu. Wapo watu wanafikiria kila kukicha na kusubiria tatizo litokee ndio
wanakuwa wa kwanza kupayuka. Kuna mchezo mbovu katika sasa zetu unaendelea hapa nchini.
mwanasiasa anahama chama kimoja kwenda kingine akiwa na lundo la TUHUMA.
Mathalani mwanasiasa anahama CHADEMA anakwenda CCM. Au anahama CUF anakwenda
ADC, au anahama CHADEMA anakwenda CUF.
Au anahama ADC na kwenda TLP. Kila siku utasikia eti
nilitumika kuwadanganya watanzania au wapigakura. Kwa wale wataalamu wa kusoma
tabia za watu wanabaki wanajiuliza, hii ni tabia mpya au udhiafu wa kutokomaa
kifikra? Sababu mwanasiasa anapohamia chama kingine kisha anakuwa na
kapu la TUHUMA ni moja ya udhaifu mkubwa wa ukomavu wake kisiasa. Ni udhiafu na
tumekuwa tukijipongeza kwa upuuzi huu kwamba ndio ugangwe wa kuonekana ni
wanasiasa weledi.
Haikatazwi kuhama chama, haikazwi kutoa TUHUMA. Lakini moja
ya udhaifu wa mwanasiasa au mkoamavu kifikra, na aliyejipika akajiivisha kisha
chama/siasa zikamfanya aive hawezi kutoa lundo la TUHUMA kwa chama anachohama. Ni utoto na siasa za kitoto kuanzia watoto hadi wakubwa.
Hayo ni dhahiri yanaonyesha namna gani tumeshindwa kutengeneza wanasiasa wenye
ushindani badala yake tumekuwa na idadi kubwa ya wanasiasa wapika majungu, wivu
wa kujinga na kadhalika.
Nakiri ni makosa makubwa sana katika siasa zetu. Nitatoa
mifano midgo tu, Tambwe Hizza alirudi CCM akitokea chama cha CUF. Wakati
anarudi CCM alisema kuwa kule CUF alitumika vibaya na alidanganya mengi,
ingawaje hakutaja alichotumiwa au alichodanganya.
Kwa mkondo ule wanasiasa wanaorudi CCM wanasema hilo hilo.
Akihama CHADEMA kwenda CCM, au akihama CCM kwenda CHADEMA anatamka ukakasi kuwa
wapo watu ambao wanasababisha matatizo ndani ya chama na wkamba wao wanaamua
kuhama. Utoto mkubwa umeenea na ni aibu sana kwa mwanasiasa kijana
kuigia siasa za kikoloni ambazo zimekuwa na ubainafsi na kushindwa kutengeneza
misngi. Angalia hii pia, Arcado Ntagazwa alipohamia CHADEMA alisema sababu ni
maovu ya CCM.
Ni kwamba kwa mkondo uleule wa Tambwe Hizza ambaye aliamua
kuondoka CUF kisha akakabidhiwa kitengo cha PROPAGANDA cha CCM, akidai
alitumika vibaya. Hii nchi yetu inachekesha mwanasiasa anahamia chama kingine
anakishutumu kile anachotoka. Kuna haja gani dada yangu mpendwa Juliana Shonza
kumwambia mwenyekiti wa CCM kuwa alipokuwa CHADEMA alitumika vibaya? Natambua
wapo wanasiasa shupavu, na Juliana Shonza anaelekea kuwa shupavu, lakini moja
ya dosari alizokumbana na kuangukia kwenye tope la mtindo wa lundo la TUHUMA.
Nasema hilo sababu huyu ni mwanasiasa kijana na anakuwa
msingi wa vijana kuchukua uamuzi wa kuhamia kwingine. Lakini ushauri wa msingi
haifai kabisa kuhamia chama kingine ukiwa na shutuma ambazo zinakuweka katika
darubini ya uangalizi huku watu makini ndani ya chama wanabaki wakitoa gego na
fizi kwa kujiuliza, tumfanyeje mtu huyu? Je kama mwanasiasa alitumika vibaya atokako, ataweza
kuaminika aendako? sichelei kusema hizi ni siasa dhaifu sana. Hakuna sababu ya
kujaza orodha ya maovu ndio umahiri wa kuhamia chama kingine, nadhani ni siasa
za kitoto.
Wazee wetu wamekuwa waasisi wa siasa za kitoto kama hizi,
maana rcado Ntagazwa angeliweza kutumia weledi kuhamia CHADEMA. Profesa
Abdallah Safari naye angetumia weledi kuueleza umma sababu za kuhamia CHADEMA.
Mabere Marando angetumia weledi kuhamia CHADEMA.Vivyo hivyo ilipaswa kuangaliwa kwa wanasiasa wengine ili
kuondokana na mtindo unaomea siku hizi eti ukihamia chama kipya unatakiwa
kuonekana u mtakatifu na kutubu 'madhambi' ya utokako, lakini wale wanaokupokea
kwanza wanapoteza imani juu yako.
Kisha wanachofanya kukukejeli na kukuona u mtumwa wa siasa
na umekosa misingi. Muhimu tutengeneze wanasiasa ambao wanajua nini maana ya
siasa, na nini ushindani wa kisiasa. Lau hata wakihamia vyama vingine wawe na
uhodari wa hoja sio kutegemea kuwatusi au kuwatuhumu wengine. Aibu, acheni
siasa za kitoto kwa wakubwa na watoto.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako