Na Albert Sanga, Iringa |
Leo nina neno na wafanyakazi
waliopo katika sekta mbalimbali; za umma na za binafsi. Nimeamua kuandika
waraka huu wa uchumi leo kwenda kwa wafanyakazi kutokana na sababu kuu tatu. Mosi,
uwepo wa mbinyo wa kuongezeka kwa gharama za maisha ikilinganisha na vipato
halisi vya wafanyakazi.
Pili, kuwepo kwa uwezekano wa
wafanyakazi kujikwamua kiuchumi kupitia ujasiriamali. Tatu, hata kama
wafanyakazi wasipoona umuhimu wala ulazima wa kuongeza vipato vyao; bado
wafanyakazi ni moja ya kundi linaloweza kuliokoa taifa hili kwa kutengeneza
maelfu ya ajira ikiwa wataamua kufanya hivyo.
Wafanyakazi wengi (japo yaweza
kuwa sio wote) watakubaliana na mimi ya kwamba mishahara na marupurupu
yanayotolewa ajirani hayatoshelezi mahitaji ya kimaisha. Gharama za maisha
zimekua juu, mfumuko wa bei unazidi kutikisa nchi na imefika mahali watu
hawaelewi waishi vipi.
Upandaji wa maisha hauendani na
ongezeko la mshahara, malengo ya kimaisha sio tu kwamba hayatimii; lakini
hayawezi kutimia kama mtu utaendelea kutegemea namna ile ile ya kipato-mshahara
na marupurupu.
Yapo mambo mawili ningependa kila
mfanyakazi afahamu. Cha kwanza ni kuwa; mabadiliko tunayoshuhudia nchini,
ikiwemo kupanda kwa gharama za maisha na mfumuko wa bei ni mabadiliko ambayo
yanaukumba ulimwengu mzima na sio Tanzania pekee.
Kwa maana hiyo, utatuzi wa suala
hili ni kuachana na kufikiria kienyeji (local thinking) badala yake watu
tufikirie kiupana (global thinking). Sambamba na hilo ni vema mtu mmoja mmoja
kuwa na mtazamo chanya kuhusu ramani ya maisha kwa ujumla.
Cha pili ni kuwa; siasa haziwezi
kuamua hatma yako isipokua umeziruhusu kufanya hivyo. Labda niiseme falsafa
yangu kuhusu siasa ndipo naweza kueleweka zaidi; “Politics has nothing to do with
my destiny”. Maana ya falsafa yangu hii ni kwamba siasa zinaweza kunizuia kwa
muda kufika ninakotaka, lakini haziwezi kunizuia milele.
Nikisema hivi simaanishi
ninaukana umuhimu wa siasa katika ustawi wa kiuchumi kwa wafanyakazi na mtu
mmoja mmoja. Isipokuwa ninachotaka turekebishe ni ile hali ya kudhani siasa
zitafanya kila kitu maishani mwetu.
Nimeyataja mambo hayo mawili ili
kusafisha njia ya kuelekea kwenye fikra pevu kuhusu uhuru wa kiuchumi kwa
wafanyakazi. Kila mfanyakazi ni vema akafahamu kuwa usalama wa maisha yake
hauwezi kuletwa na ongezeko la mshahara. Bila kulitambua na kulikubali hili
tunaweza kuwa shidani; kwa sababu mara nyingi mtaji wa wanasiasa kupatia kura
huwa ni ongezeko la mishahara!
Wanauchumi tunafahamu vizuri
mchezo unaotokea pindi serikali inapoongeza mishahara, pasipo kuongeza tija ya
uzalishaji. Iko hivi, unapoongeza mzunguko wa fedha, (unbalanced injection of
money into circulation) mfano kwa kuongeza mishahara kinyume na mizania ya
kiuchumi; ikiwa hakuna tija katika uzalishaji basi unakuwa ukiibua mfumuko wa
bei (inflation).
Kuanzia mataifa madogo mpaka
makubwa hadi nikiandika makala hii yanasumbuliwa na kusuasua kwa uchumi.
Wanapojaribu kushusha ‘inflation’ wanajikuta wametengeneza uhaba mkubwa wa
ajira, wanapojaribu kumimina ajira mitaani wanajikuta mfumuko wa bei unainua
pembe zake.
Hata hivyo nikiri kuwa
inawezekana kuleta msawazo wa ujazo wa fedha na mfumuko wa bei; lakini
kufanikiwa kwake kunategemea visababishi vingi mno (simulation factors) ambavyo
kutokana na utamaduni wa nchi yetu kiuchumi; sio rahisi kuvifanikisha vyote. Yote
katika yote; hizo ni lugha na misamiati ya wachumi; lakini ni nini maana yake
kwa mfanyakazi?
Hayo juu yanatupa kutambua kwamba
kumbe usalama wa maisha ya mfanyakazi utapatikana kwa kujifunza mbinu za
kuutumia mshahara kidogo anaoupata kuzalisha mifumo, bidhaa na huduma
zitakazomwongezea tija. Hili linaweza kufanikishwa kwa mfanyakazi kuanzisha
miradi midogo midogo nyumbani au mikubwa mahali pengine, kufungua biashara na
hata kutumia vipawa alivyonavyo nje ya ajira yake kuzalisha fedha.
Nianze sasa na yale mambo matatu
yaliyonisukuma kuwaandikia waraka huu, nikianza na lile la kwanza. Udogo wa
mishahara isiyoendana na gharama za maisha unazidi kuleta msiba katika nchi
yetu.
Hebu fikiria, mfanyakazi analipwa
mshahara mdogo ambao akishalipa kodi ya nyumba, akanunua chakula, akafanya
matumizi mengine ya msingi; kila mwisho wa mwezi anajikuta ana madeni. Tangu
Januari hadi Desemba mfanyakazi huyu anakua ni mtu sio tu wa madeni ila ni madeni
yanayoongezeka. Hana tumaini la kujikwamua kesho wala keshokutwa.
Kutokana na hali hii tumezalisha
wafanyakazi wengi ambao wajibu wao wameugeuza kama
hisani makazini, ndio hawa ambao hawawezi kukuhudumia mpaka umewapa chochote.
Wengine wameendelea ‘ku-survive’ kwa kuunga unga, wanaishi kwa mizinga kila
wakati na kila sehemu. Huwezi kuwalaumu; wanalazimishwa na mazingira
yanayowakabili.
Nchi sasa hivi imejipatia
‘mamilionea’ bandia ambao wamepata fedha zao kwa njia ya kughushi mikataba,
kupewa hongo, kupokea rushwa kubwa na ndogo pamoja na wizi wanaoufanya
makazini. Wakishapata fedha hizo ndipo wanajenga majengo makubwa makubwa,
wananunua magari ya kifahari na kuishi maisha ya kifalme. Wengi wetu tumeingia
katika mtego wa kuwasifu watu wa namna hii ya kwamba ni ‘wajanja’,
‘watafutaji’, ‘wenye akili’, ‘matajiri’ na majina mengine yenye sifa.
Kuna atahri mbili kubwa
mfanyakazi unaposhawishika kupata mafanikio kwa njia zisizo halali. Mosi ni
kwamba unaliangamiza taifa na
kuwadhulumu wengine. Pili, unaharibu utu wako wa ndani na kupoteza amani
ya rohoni. Iko hivi; kikawaida uovu humrudia muovu, wema humrudia mwema.
Ukijikusanyia mali ama fedha kwa
njia ya wizi, rushwa, hongo ama ujanja-ujanja; utajikuta unaishi maisha
yasiyokua na amani kunakopelekea kukosekana kwa furaha maishani mwako.
Kikawaida mtu unapaswa uwe na mafanikio yanayoleta utulivu katika roho na nafsi
yako; kinyume na hapo haina maana ya kuwa na mafanikio.
Najua wapo watu mnaowafahamu
ambao wametajirika kwa njia za mikato; nanyi mnaona kama wanaishi maisha mazuri
yenye furaha; ukweli wanaujua wenyewe kama ambavyo tunathibitishiwa na wataalamu wa ukuaji wa
kiroho, saikolojia na maumbile; ya kwamba uovu humrudia mwovu.
Unaweza kutumia rushwa kutajirika
lakini malipo ukayapata kupitia mgogoro wa ndoa na kudharaulika; ndio maana
huwa sishangai ninapoona watu wengi wakitafuta furaha kupitia ngono na ulevi;
wengi wao njia walizotumia kupata mafanikio waliyonayo zimewapa ‘garantii’ ya
kutokua na furaha maisha yao yote!
Kwa nini ninasema haya yote? Ni
kwa sababu ninataka tuangalie upande wa pili ya kwamba tupende ama tusipende ni
lazima wafanyakazi wote wafanikiwe ili kukabiliana na yanayowakabili maishani;
lakini mnafanikiwaje? Ndipo hapo ambapo ninataka tuyaone maisha katika mwanga
wa ujasiriamali
Kila mfanyakazi anastahili kuishi
maisha ya ushindi wa kiuchumi!
stepwiseexpert@gmail.com; 0719 127 901
Very nice write-up. I certainly love this website. Stick with it!
ReplyDeletemy web site - cartown