Markus Mpangala |
Na Markus Mpangala, Dar es Salaam
Tukio la waziri wa Mambo ya Ndani
Emmanuel Nchimbi kuwafukuza Makuruta 95 wa Chuo Cha Polisi (CCP) Moshi kwa kile
alichooita kugundulika kutumia rushwa kujipatia ajira, bado linaelea katika
vichwa vya watu juu ya msingi wa maadili yetu.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi,
Renatus Chalamila amehusishwa na rushwa katika kuajiri. Waziri Nchimbi
amechukua hatua zaidi baada ya kumsimamisha kazi Kamishna huyo. Alisema pia taarifa za uchunguzi za
Kamishna huyo, ambaye anashughulikia masuala ya ajira zimewasilishwa kwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete ambaye ana mamlaka ya kumfukuza kazi au
uamuzi mwingine wowote.
Japokuwa waziri Nchimbi ametaja pia
maofisa kadhaa wa Jeshi la Polisi ambao wamehusishwa na makosa mbalimbali
lakini binafsi nimeguswa na huku chini kabisa (Makuruta). Kwa maana nyingine harakati za vijana 95
ambao wamefukuzwa na waziri Nchimbi waliokuwa wakitarajiwa kuingia kwenye ajira
ya ndani ya Jeshi la Polisi, linatuletea swali la msingi juu ya maadili na
namna tunavyojenga usalama wetu nchini. Hii ina maana katika Makuruta hao 95
tulikuwa na watu wenye tabia tofauti, lakini baya zaidi wamekutana katika
msingi wa kutoa rushwa ili wapate ajira.
Namna nyingine tunajiuliza mfumo wetu wa
jira katika sekta za ulinzi na usalama ukoje na nani anawajibika kuutengeneza
pale unapokwenda kombo. Makuruta 95 ni wengi au hata wangelikuwa
watano tu, lakini ukweli tunabakia katika mwenendo mbovu wa jamii iliyochoka
kufuata kanuni hivyo kila kitu kinatakiwa kwenda ‘fasta fasta’. Ni tabia hii ya ‘fast tracking’
inatufikisha mahali pabaya kabisa na kushuhudia vijana wadogo wakijihusisha na
rushwa.
Naam kufukuzwa kwao ni ushahidi wa wazi
kabisa jamii yetu imeoza na hata wale viongozi kule juu akiwemo Kamishna Renatus
Chalamila, ni taswira iliyoko huku kondeni. Kama CCP leo hii imegubigwa na vikwazo
vya ajira mpaka vijana wetu watoe rushwa ina maana mfumo wetu wa kutumia
rasilimali watu umegubikwa na maadili duni. Wengi wanatoa ajira kwa misingi ya
jinsia, wajihi, rushwa, na kadhalika.
Kwa namna nyingine sio sifa nzuri kwa
Jeshi letu adhimu la Polisi. Mwanazuoni wa masuala ya kijeshi Sun Tzu kwenye
kitabu chake cha ‘The Art of War” anasema kama jeshi likiingia vitani kisha
likapoteza mwelekeo basi wakulaumiwa ni Jenerali wa jeshi husikal Sun Tzu
anasema iwapo jeshi likiwa kwenye gwaride linatii maagizo yote; kushoto geuka,
kulia geuka, au mbelee tembeaaaa!
Waziri Nchimbi |
Iweje jeshi hilo likapoteza umahiri huo
ndani ya uwanja wa vita. Bahati mbaya Sun Tzu alisahau kuwa katika uwanja wa
vita kuna matukio ambayo yanaweza kubadilisha mwelekeo au tabia za jeshi. Kama mwanajeshi hakuwa thabiti licha ya
mafunzo yake, basi haitashangaza kuona siku moja akishindwa kuingia uwanja vita
sababu tu ya kukosa misingi binafsi ya kulitumikia jeshi.
KWANINI JESHI LA POLISI LIWE NYENZO?
Moja makosa makubwa yanayofanyika katika
jamii yetu ni kushindwa kuelewa watoto wetu wanatakiwa kufanya kazi gani katika
maisha yao. Wapo wazazi ambao hawajui na watoto nao
hawajui wafanye kazi gani hata wanapofika kidato cha nne. Wengi wao wakishapata
matokeo ya mitihani yao ndipo huanza kujiuliza wafanye kazi gani.
Kwa Makuruta 95 waliokubali kutoa rushwa
ina maana kuwa walikuwa wanataka kulitumia Jeshi la Polisi kama nyenzo ya
kufanya kazi nyingine hapo baadaye. Mtu makini akichambua hili na kuangalia
mwenendo wetu kwa Jeshi la Polisi, wapo wanaojiunga sio sababu ya mapenzi yao
bali kwakuwa wanataka ‘kutoka’ kimaisha hivyo mwelekeo uliopo ni CCP Moshi. Sina shaka kabisa, Jeshi la Polisi
linaweza kufanya uchunguzi wa mambo mbalimbali ikiwemo hili. Ni rahisi
kukukotoa idadi ya wahitimu wa Jeshi la Polisi kila mwaka na wanakopelekwa na
muda wao kazini.
Kisha Jeshi la Polisi linaweza kuanza
kufuatilia wahitimu hao kama wameendelea na kazi ya Upolisi kwa muda gani na
wanafanya nini baada ya kujiondoa katika jeshi la Polisi. Ninasema hivi kwakuwa katika nyakazi zetu
Jeshi la Polisi kwa baadhi ya watu wanatafsiri kama sehemu ambayo wanakwenda
vijana walioshindwa maisha hivyo kwa muda fulani wanajua wataweza kupata nyenzo
ya kufanya kazi nyingine.
Ni wazi wengi waliowahi kujiunga Jeshi la
Polisi kwa uadilifu wamedumu na wanaendelea kuheshimu taalumu yao. Lakini wapo
wengine wanalitumia Jeshi la Polisi kama nyenzo ya kufanikisha mipango ya
maisha. Ni kweli wana haki, lakini hawa vijana
wetu baadhi yao wanaweza kabisa kuwa ndani ya jeshi la Polisi kisha baadaye
wakipata njia za kufanya shughuli nyingine (baada ya kuelimishwa na au
kulifanya jeshi kuwa mtaji).
Endapo Jeshi la Polisi limeweza kugundua
Makuruta 95 wameingia kwa rushwa safari hii ni vema likafanya uchuguzi mwingine
juu ya wahitimu wake na vituo vyao vya kazi.
HASARA
Hakuna hasara kubwa kama watu kutumia
idara za usalama kama nyenzo ya kufanikisha mipango yao. Tunahitaji askari
waadilifu na wenye kuipenda kazi yao. Tunahitaji watu ambao sio tu watakuwa
wakilalamikia mishahara midogo bali kutumia kidogo hicho kwa uadilifu na
kulinda maslahi ya nchi yetu.
Lakini hakuna hasara kubwa inayotokea
kama kitendo cha Makuruta 95 hao au wale waliowahi kupitia CCP Moshi na
kadhalika wanaoingia maisha ya kawaida ya mtaani. Katika mazingira haya, “hisia” za
ongezeko la Uhalifu haliwezi kukosekana kabisa. Na ili kukabiliana nalo ni vema
kutafuta njia mwafaka za mkunusuru Jeshi letu la Polisi ili lisiwe na
linakusanya tu kama kokoro na kujikuta limejaza askari wasiowaadilifu.
Ni mbaya, na hatutakuwa tumeokoa jamii
inayoamua kufikiria RUSHWA kwanza ndipo ipate ajira. Ni vyema katika tukio la
Makuruta waliofukuzwa wafuatiliwe na kuhojiwa zaidi, na iwapo wazazi wao
walihusika kuchochea (kama) basi nao wanatakiwa kupitiwa na mkono wa sheria.
Kuwafukuza Makuruta pekee hakutoshi mheshimiwa Waziri Nchimbi. Nimemaliza.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako