Showing posts with label mkimbizi. Show all posts
Showing posts with label mkimbizi. Show all posts

October 07, 2017

NIMEWASILI

Salama nimewasili, jirani kanipokea,
Mekaa kwenye kivuli, upepo unapepea,
Nimekuwa mdhalili, mengi yamenipotea,
Nimewasili salama, jirani kanipokea.

Nilikotoka najuta, watu wengi wamekufa,
Mazingira ya utata, yamejaa nyingi nyufa,
Maadui masalata, ni kama vile malofa,
Nimewasili salama, jirani kanipokea.

October 05, 2017

NINAONDOKA

Ndugu zangu sikieni, mimi hapa naondoka,
Ninahitaji amani, mirindimo nimechoka,
Ninakwenda kwa jirani, hata kama akifoka,
Ninaondoka jamani, amani naitafuta.

Mitaani kuna mambo, twakimbizana daima,
Yapo mengi machafuko, yananitisha daima,
Yatokea milipuko, inanipatia homa,
Ninaondoka jamani, amani naitafuta.

Risasi zinasambaa, mirindimo inazidi,
Naishia kutambaa, ninapigwa na baridi,
Ninawasha mishumaa, kufukuza ukaidi,
Ninaondoka jamani, amani naitafuta.