Na KIZITO MPANGALA
Mafundisho ni moja kati ya
elimu ambayo haina mpinzani katika maisha yetu ya kila siku. Mafundisho hayo
yapo kwa namna mbalimbali, kuna mafundisho ya jumla, kuna mfundisho ya kipekee
ambayo hugusia katika uga husika kama vile mafundisho ya dini, mafundisho ya
stadi za kazi, mafundisho ya maadili, mafundisho ya rika na kadhalika. Hayo yote
husaidia kujenga jamii na kuiweka katika mwenendo unaokunalika na wengi na
ambao una manufaa mazuri kawa jamii hiyo na pengine hata kuakisi kwa jamii
nyingine mahali popote duniani.
Mafundisho ya kijinsia yana
umuhimu mkubwa sana katika maisha yetu. Jinsia fulani ifundwe yale yanayopaswa
kufanyika nayo ili kuendeleza maadili au jeme lipatikanalo kutoka katika
mafundisho hayo. Ikiwa mtu wa jinsia tofauti ataifunda jinsia nyingine fundisho
fulani, kinachotakiwa ni kufikiri kilichosemwa ili kubaini kama kina manufaa ya
kurekebisha kitu fulani kwa jinsia iliyofundwa au kama kina maudhui mabaya
dhidi ya jinsia iliyofundwa kishapo hukumu itolewe, iwe hukumu chanya au hukumu
hasi.
Kitendo cha kutoa mafundisho
kinaweza kuwa cha namna mbili. Huenda mafundisho yakatolewa kinagaubaga au kwa
kutumia mifano ambayo inalenga kurekebisha jambo fulani katika jamii. Ikiwa hilo
linafanyika, si vema kulalamika ghafla bila kufikiri lengo au dhamira ya
mafundisho hayo. Na kwa sasa jinsi ilivyo rahisi kusambaza taarifa katika
mitandao basi ndani ya dakika kadhaa dunia yote huenda ikajua kinachojiri na
kisha kila aliyepata taarifa anatoa maelezo yake kadiri ya taarifa
ilivyomfikia. Watasifu, watalaani, watahamasisha watu kuwa watulivu,
watamshutumu mnenaji, watamtetea mnenaji na kadhalika.
Katika suala hili la kuishi
katika mafundisho yanayotolewa kwa mifano, inawezekana mfundaji anakuwa na nia
ya kuonya au kurekebisha jambo fulani lakini huenda akaeleweka tofauti na lengo
la fundisho lake. Hii inatokea mara nyingi na pengine husababisha maandamano
ambayo yanaweza kuzua madhara kwa waandamanaji wakiwa wanakemea fundisho
wasilolikubali au kama limefikirirwa kuwa ni la kejeli kawa kundi fulani katika
jamii.