NA KIZITO MPANGALA
STEPHEN HAWKING alizaliwa mwaka
1942 jijini
Oxford nchini Uingereza kwa wazazi Frank Hawking na Isobel Hawking. Japokuwa familia
yake ilikuwa na mtikisiko kifedha lakini wazazi wake walijitahidi kujiendeleza
kielimu katika chuo kikuu cha Oxford. Baba yake alisoma udakitari wa dawa na
mama yake alisoma Falsafa, Sayansi ya Siasa, na Uchumi katika chuo hicho.
Baba yake na mama yake
walikutana kwa mara ya kwanza muda mfupi tu bada ya kuanza kwa vita ya pili ya
dunia katika Taasisi ya Utafiti wa Dawa ambapo baba yake alikuwa mtafiti na mama yake alikuwa katibu wa taasisi hiyo. Ndipo
mapenzi yao yalipoanza na walibahatika kupata mtoto wa kiume ambaye ni Stephen
Hawking.
Familiya ya Hawking ilisifika
kwa kuwa na kiwango kizuri cha upeo wa akili tangu wazazi hadi watoto wao. Muda
mwingi walipokuwa nyumbani kulikuwa na ukimya ikidhaniwa kuwa wanasafiri mara
kwa mara lakini sivyo! Ukimya uliotawala ndani ya familia hiyo ulitokana na
wazazi kuwazoesha watoto kujisomea vitabu jambp ambalo walilipenda na ndipo
Stephen Hawking alipodhihirisha kiwango chake katika upeo wa akili. Walikuwa wakiishi
kwenye nyumba kuu kuu iliyokuwa na maktaba ya familia ndani.
Stephen Hawking alianza shule katika
shule ya Byron mtaa wa Highgate jijini London. Baadae alilalamikia shule hiyo
kutokana na mfumo wake uliokuwa ukitumika kufundishia, jambo ambalo lilinampa
ugumu katika kujifunza zaidi. Wazazi wake walipohamia katika mji wa Mt. Albans,
Stephen alijiunga na shule ya upili ya wasichana ya Mt. Albans mjini hapo kwa
muda mfupi na baadae akahamishiwa katika shule ya Radlett katika mji mdogo wa Hertfordshire.
Wazazi wake waliipa elimu
kipaumbele kwa kiasi kikubwa na kuwahimiza wajisomee vitabu vilivyokuwepo
katika maktaba ya familia ndani ya nyumba yao.
Baba yake alitamani Stephen akasome katika shule binafsi ya Westminster
lakini kwa bahati mbaya siku ya kufanya mtihani wa kujiunga na shule hiyo Stephen
alishikwa na homa kali lakini pia wazazi wake hawakuweza kulipa ada katika
shule hiyo iliyokuwa ikitoza kiasi kikubwa cha fedha wakati huo, hivyo Stephen
alibaki katika shule aliyokuwepo.
Stephen Hawking alijizolea
marafiki wengi katika shule aliyokuwepo kutokana na kiwango chake cha upeo wa
akili katika masomo, hivyo hata yeye mwenyewe alifurani kuwa na marafiki na
kucheza nao pamoja. Wakiwa shuleni walifundishwa stadi za kazi na mambo mengine
yahusuyo maisha kwa ujumla. Walijifunza kutengeneza maboti na vielelezo
mbalimbali vya ndege.
Mwaka 1958
wakisaidiana na mwalimu wao wa Hisabati bwana Dikran Tahta walitengeneza kompyuta
wakitumia vifaa vya saa kubwa ya
kielektroniki iliyokuwa mbovu, pia walitengeneza simu za mezani kwa kutumia
vifaa vya vyombo vibovu vya kielektroniki.
Stephen Hawking alipewa jina la
utani shuleni ambapo alikuwa akiitwa “Einstein”, pia alikuwa na udhaifu katika
maendeleo yake kitaaluma lakini alijitathmini kwa msaada wa mwalimu wake wa
Hisabati bwana Dikran Tahta na kuamua kujikita katika masomo ya sayansi, akawa
anaimarika kitaaluma. Aliweka bidii zaidi katika Hisabati na alipofika chuo
kikuu alisoma Hisabati zaidi.
Baba yake alimhimiza asome
udakitari wa dawa (Doctor of Medicine) akimuambia kuwa kuna ajira chache sana
ambazo zinahitaji wajuzi wa Hisabati, hivyo alimsihi aachane na Hisabati ili
asome udakitari wa dawa. Alimsihi pia ajiunge na chuo kikuu cha Oxford. Baada ya kujiunga ilitokea kwamba
ni ngumu kusoma hisabati wakati ule kutokana na uhaba wa walimu ndipo Stephen
akachagua kusoma Fizikia na Kemia. Mkuu wa chuo alimsihi Stephen avute subira
hadi mwaka wa masomo utakaofuata kwamba kutakuwa na walimu wa kutosha lakini Stephen
alifadhiliwa.
Alianza masomo mwezi wa kumi
mwaka 1959 katika
chuo kikuu cha Oxford akiwa na miaka 17. Miezi
18 tangu
aanze masomo katika chuo hicho alihisi kuchanganyikiwa kitaaluma kutokana na
hulka yake ya kujilinganisha na wengine kitaaluma hivyo alijiona yeye si kitu
na kwamba hafai lolote kusoma chuo kikuu, lakini mwalimu wake wa Fizikia katika
chuo hicho bwana Robert Berman alimtibu kisaikolojia kwa kumuambia “ninapofundisha
ninataka kukuonyesha kwamba kuna kitu fulani cha pekee inabidi kifanywe, na
usikifanye kwa kuangalia watu wengine walifanyaje au wanafanyaje”. Kutokana na
maneno hayo, Stephen alionyesha mabadiliko makubwa kitaaluma alipoanza mwaka wa
pili wa masomo na mpaka alipofika mwaka wa tatu. Kadiri ya mwalimu wake huyo
alisema kwamba Stephen likuwa kijana mwerevu kati ya waerevu.
Alipenda kujisomea hadithi za
kisayansi na kujihusisha na muziki. Pia alikuwa mmoja kati ya washiriki wa
masindano ya kuendesha maboti katika mashindano yaliyokuwa yakifanyika chuoni
hapo.
Stephen alisema kwamba katika
maisha yake ya kitaaluma chuoni Oxford miaka mitatu alitumia masaa 1000 tu
kujisomea katika jumla ya miaka hiyo mitatu, hivyo mtihani wa mwisho wa
kumaliza mafunzo ulimpa changamoto na akaamua kujibu maswali machache tu ya
kipengele kimoja cha Fizikia ya Nadharia (Theoretical Physics) akiwa na lengo
la kujiendeleza na masomo ya Cosmolojia katika chuo kikuu cha Cambridge ambapo
alihitajika kupata ufaulu wa daraja la kwanza. Kutokana na mfadhaiko, alilala
usingizi hafifu sana siku moja kabla ya kufanya mtihani wa mwisho, hivyo
akapata alama zilizopungua kidogo kupata daraja la kwanza na kulazimika kufanya
mtihani wa marudio uliojulikana kama “Viva” ili kusahihisha matokeo.
Stephen Hawking alijihisi ya
kwamba ni mwanafunzi mvivu na mgumu kuelewa masomo kwa ufasaha. Alipoulizwa kuhusu
matokeo yake ya awali alijibu hivi “mkinipa daraja la kwanza nitakwenda
Cambridge, mkinipa daraja la pili nitabaki hapa Oxford, natumaini mtanipa
daraja la kwanza”. Walimu wake walitambua kipawa chake cha upeo wa akili na
walikuwa wakimpa uangalizi mkubwa sana bila kumuambia yeye mwenyewe. Baadae akapewa
daraja la kwanza.
Alikwenda nchini Iran na rafiki
zake kwa ajili ya mapumziko baada ya kumaliza chuo huko Oxford, na aliporudi
Uingereza alianza kufanya kazi zilizohusu taaluma yake katika Ukumbi wa
Kisayansi wa Trinity mjini Cambridge mnamo mwaka 1962.
Alipoanza masomo ya shahada ya
uzamivu alihisi kwamba amekosea njia katika taaluma. Alipata changamoto
kubwa na hivyo kukata tamaa ya kuendelea
na masomo ya Cosmolojia. Pia alihisi hataweza kujiendeleza na hisabati tena
kutokana na changamoto alizopata. Lakini alihimili changamoto hizo hadi mwisho
wa masomo yake.
Muda mfupi baadae
alipata homa na hivyo kufanyiwa upasuaji na akabainika kuwa anasumbuliwa na
homa iliyoiangamiza “motor nuerone” na kumfanya apooze mwili. Dakitari alimshauri
aendelee na masomo japokuwa mwili wake ulikuwa ukiendelea kupooza taratibu,
hivyo hakuweza kutembea na akawa anatumia baiskeli mpaka hivi sasa, vilevile
alipata ugumu wa kupangilia matamshi yake kwa usahihi kutokana na kupooza
kuanzia shingoni na kuathiriwa katika matamshi wakati anapozungumza.
Alirudi masomoni katika
hali hiyo na kwa mshangao mkubwa aliboreka zaidi katika taaluma na pia aliweza
kuboresha matamshi yake kwa msaada wa kitabibu.
Alpoanza kuwa mkufunzi
alikuta mjadala mzito uliokuwa ukijadiliwa na wakufunzi wenzake wa Cosmolojia
kuhusu jinsi ulimwengu ulivyotokea. Alikuwa mkufunzi hodari licha ya kuwa
maisha yake kuwa katika baiskeli muda mwingi huku shingo ikiwa imekwenda upande
kama anavyonekana pichani kutokana na kupooza mwili. Mwka 1965 aliandika insha yake
mashuhuri kuhusu mjadala uliokuwa ukijadiliwa kuhusu jinsi ulimwengu
ulivyotokea. Aliandika akiwa bado kijana lakini akiketi kwenye baiskeli muda
mwingi.
Mwaka 1966 alitunukiwa shahada ya
uzamivu katika Hisabati Tumizi (Applied Mathematics) na Fizikia ya Nadharia
(Theoretical Physics) na alijikita zaidi katika Cosmolojia (Cosmology). Na baadae
kazi yake aliyoandika kutokana na utafiti alioufanya (licha ya kuwa na kilema
kama anavyoonekana pichani) ya “Singularities and the Geometry of Space – Time” iliheshimiwa na
hivyo akashinda tuzo ya Adams katika sayansi.
Mwaka 1970 aliteuliwa kuwa profesa
wa hisabati katika chuo kikuu cha Cambridge. Katika maisha yake kitaaluma
amejikita zaidi katika sayansi ya ulimwengu (The science of Universe). Kadiri muda
ulivyosonga alizidi kudhoofika na kulazimia kupata matibabu mara kwa mara akiwa
nyumbani kwake.
Mwaka 1982 alihudhuria mkutano huko
Vatican kuhusu ulimwengu ndipo alipotoa msimamo wake hadharani na kusema “hakuna
mwanzo, hakuna mwisho, na hakuna mipaka katika ulimwengu”, tukumbuke kuwa
ulimwengu una maana pan asana kisayansi, ulimwengu ni zaidi ya ukubwa wa dunia
hii au sayari yoyote kwa kuwa ulimwengu ni jumla ya sayari zote na vyote
vilivyomo katika anga. Stephen Hawking ansema kwamba nadharia ya Biblia
inayosema kwamba kulikuwa na mwanzo wa ulimwengu siyo ya kweli na haina
mashiko, hivyo hakuna mwanzo, mwisho, wala mipaka katika ulimwengu.
Pamoja na kuwa kilema na
kuwa na tatizo la kufanya mawasiliano kwa usahihi, Stephen Hawking ni
mwanafizikia aliyeweka kando ukilema wake na kujikita katika taaluma yake ya
Fizikia. Hali ya kuwa kilema ilimpelekea kuachana na mkewe licha ya kuwa na
watoto aliopata na mkewe huyo. Alitumia muda mwingi kufikiri masuala ya sayansi
na kuweza kuandika vitabu vingi kuhusu Cosmolojia ambavyo vinatumika katika
vyuo mbalimbali duniani.
Stephen Hawking
amesafiri kwenda sehemu mbalimbali duniani kwa shughuli binafsi na kikazi.
Stephen Hawking amekuwa gwiji wa
Cosmolojia na kusikika masikioni mwa watu wengi duniani kwa umahiri wake
katika fizikia na hisabati licha ya kuwa kilema kwa muda mrefu jambo ambalo
lilimpelekea kuwa na baiskeli maalumu iliyounganishwa na kompyuta ambayo
inamsaidia katika mazungumzo na mambo mengine katika maisha yake.
Stephen Hawking
amejitokeza mara nyingi katika mijadala mingi kuhusu Cosmolojia jambo ambalo
alisema ndilo la maisha yake yote. Amekuwa mtu wa kutumainiwa katika vyuo
mbalimbali duniani kwa taaluma ya Cosmolojia.
Hakika kilema si
ugonjwa! Leo Stephen Hawking ambaye bado anatumia pumzi ya bure aliyojaliwa na
Mungu ameshinda nishani zaidi ya 10 kwa muda wote wa maisha yake aliyoyaweka
katika sayansi. Hawking ansema kwamba kila mmoja anao uwezo wa kujifunza
anachokipenda.
Amekuwa na afya dhaifu
kwa muonekano wa kawaida mwilini lakini ana afya imara sana katika ubongo wake.
Muda mwingi wakati wa mapumziko hutumia kuzungumza na binti yake Lucy Hawking
na ambaye humuwakilisha katika upokeaji wa zawadi kwenye matamasha mbalimbali
anayoalikwa. Bega lake la kulia ndilo lililoathirika zaidi pamoja na miguu,
lakini kwa hakika Mungu ni mkubwa, ubongo wa Stephen Hawking una afya imara
sana ya maarifa na mambo mbalimbali maishani. Hivi sasa vyuo vingi vinafaidi
kazi zake kuhusu Cosmolojia ambapo hutumika katika mafunzo ya kupata shahada ya
uzamivu katika sayansi ya anga, na maisha yake muda mwingi ni juu ya baiskeli
yake maalumu kama anavyoonekana pichani. Yuko hai.
© Kizito Mpangala
0692 555 874, 0743 369 108.
0692 555 874, 0743 369 108.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako