21 October 2017

UTEUZI WA UBUNGE


TABASAMU NA KITABU


Huyu ni rafiki yangu. Anaitwa Ragin Mbaga, ila tuwapo farashani hupendelea kumwita "Mzee wa bustani ya usomaji". 

Kitu kimoja kwetu tunapenda kusoma vitabu. Tunapenda kuandika andika maarifa. Tunapenda kusambaza upendo kupitia usomaji wa vitabu. Tunajua jamii inaweza kupigana dhidi ya ujinga kwa kutumia silaha ya vitabu. Tunapenda kujifunza kwa waliotuzidi na hata tuliowazidi. Madhumuni yetu ni kuhamasisha usomaji wa vitabu kwa wote.  

Kitu kingine zaidi, tuna amani sana mioyoni. Mimi nasoma "Mbio za Jasusi" cha Frowin Kageuka na yeye anasoma "Ishinde tabia ya kughairisha mambo" cha Joel Nanauka. Katika maisha furahia na ukipende kile ufanyacho. Ni tiba maridhawa.

Markus Mpangala,
Morogoro,
Oktoba 10/2017.

UCHAMBUZI WA KITABU CHA UHAMASISHAJI

KITABU: ISHINDE TABIA YA KUGHAIRISHA MAMBO
MWANDISHI: JOEL NANAUKA
MCHAMBUZI: MARKUS MPANGALA


JOEL NANAUKA ni miongoni mwa waandishi wazuri katika vitabu vya uhamasishaji na utambuzi. Kitabu chake cha “Ishinde Tabia ya Kughairisha Mambo” kimechapishwa na kampuni ya Benison Communication &Printing iliyopo Dar es salaam na kupewa nambari za usajili ISBN 978-9987-761-99-9.

Msingi wa kitabu hiki unaanza kupatikana katika utangulizi wake ambapo mwandishi anaandika, “Unakumbuka wakati watu wametangaziwa kujisajili kwaajili ya kupiga kura? Unakumbuka watu walivyotangaziwa kuhusu usajili wa vitambulisho vya utaifa? Ni siku gani watu walijaa zaidi? Bila shaka, utakumbuka ni siku ya mwisho hata kama waliliona tangazo. Kuna watu kila siku wanatuma maombi ya kazi siku ya mwisho hata kama waliliona tangazo hilo miezi miwili kabla. Kuna watu kila wakati watatuma ripoti yao siku ya mwisho, kuna watu kila wakati kazi waliyopewa kufanya wataiwasilisha dakika za mwisho” (uk.2).

Sura ya kwanza ya kitabu hiki inaeleza tabia za baadhi ya watu kupanga mipango fulani na kushindwa kutekeleza. Mathalani mtu anapanga kutekeleza jambo fulani lakini kabla hajaanza au akifika nusu ya jambo lenyewe anaahirisha. Mwandishi anatumia utafiti wa Profesa Joseph Ferrari ambaye aligundua kuwa takribani asilimia 20 ya watu duniani ni waahirishaji wakubwa wa mambo yao. 

Kwa mfano, mtu anataka kununua saruji kwaajili ya kujiandaa kwa ujenzi wa nyumba, pengine inahitajika mifuko 150, lakini yeye ananunua 50, na kuahirisha ujenzi kisha anasema ataanza mwaka mwingine. 

Mwandishi amebainisha taswira halisi katika maeneo ya kazi. Anasema wapo wafanyakazi ambao hawapendi kutekeleza kazi zao kwa wakati badala yake wanasubiri hadi dakika za mwisho ndipo waanze kuhaha huko na huko. Kimsingi tabia hizi zinazozungumzwa zinawagusa watu kila kaliba. Haijalishi umri wala nasaba au jinsia.

“Unaweza ukachukua daftari lako kuandika, ama ripoti yako ama hata kusoma kitabu, ukaamua kuwa unafanya unachotaka kwa nusu saa bila kuyumbishwa na kitu chochote, ghafla baada ya dakika 10 unajikuta nunashika simu na unasema ngoja niangalie meseji, kuja kushtuka unajikuta umeshatumia takribani nusu saa kuperuzi mitandao na hamu ya kuendelea na kazi uliyokuwa unaifanya inapotea kabisa. Ama wakati mwingine unasema ngoja niangalie TV kidogo kisha nitalala ama nitasoma kidogo, kuja kugundua unakuwa umeshafika saa 7 usiku na umeshindwa kuondoka kwneye TV yako. Ni kitu gani kinasababisha uamue jambo moja na kisha ujikute umefanya kitu tofauti,”(uk.9).

Katika muktadha huo mwandishi anakumbusha kuwa wapo watu wanaoishi kwa kuahirisha. Wengine ambao hadi wakumbushwe ndipo hutekeleza jambo fulani. Wapo watu ambao hawezi kujikita kwenye eneo husika. 

Tunaweza kutumia dhana ya “kutanga tanga kimawazo”. Kwamba anayetanga tanga kimawazo anakuwa na vitu vinavyovuruga zaidi utaratibu wa utendaji wa kazi. Hali ya kutanga tanga kimawazo huchochea uvivu na uzembe. 

Mathalani unaweza kuona mtu anajishughulisha kupika jikoni, kwakuwa anajua itachukua dakika takribani 5 au zaidi, anakwenda sebuleni kutazama TV au kukaa mbali na jikoni ili afanye kitu kingine kisichohusika na mapishi. Katika hali kama hiyo unaweza kushuhudia mtu huyo akikurupuka alikokaa na kukimbilia jikoni kutazama anachokipika baada ya kugundua kuwa ameunguza. Mara nyingi vitu vinavyosababisha hayo ni vile tunavyodhani ni vinatupatia raha na kadhalika.

Ili kubaini hilo mwandishi ameeleza tabia za watu mbalimbali na namna wanavyoweza kuahirisha mambo. Wengi wao hukosa nidhamu ya muda, wana mambo mengi yasiyokwisha (sababu ya kutotekeleza kwa wakati na kulimbikiza majukumu), wanatatizo la kulipua mambo, na wanakosa vipaumbele.

Sura ya pili anazungumzia tabia zingine zinazochochea kuahirisha mambo ni kutenda jambo katika dakika za mwisho ambayo huchochea presha kubwa. Pia watu wenye tabia hizo hawafanikiwi kwasababu wanaendeshwa na maoni ya watu. 

Anasema wapo watu ambao wanaogopa kulipia gharama za uamuzi wao hivyo wana tabia ya kuahirisha mambo. Ili kufahamu zaidi yaliyomo katika sura za tatu, nne na tano ni vema msomaji akitafuta kitabu hiki na kujipatia elimu.

Nihitimishe kwa kumkumbusha mwandishi juu ya matumizi sahihi ya maneno ya Kiswahili. Usahihi ni “Kuahirisha” si “kughairisha. Mwandishi wa habari na nguli wa Kiswahili, Amabilis Batamula, anasema “Naomba nisahihishwe kipengele cha lugha kama nakosea, maana na mimi kwa kupenda kuhariri nimeshajishtukia. Hilo neno kughairisha linatumikaje hapo? Ninavyofahamu mimi kuahirisha ndio ‘Procrastination’, kusogeza sogeza, na kughairi ni kubadili mawazo na kuacha kufanya ulichokwisha amua kufanya. Nisahihishwe tafadhali.”.

MBUNGE WA CHEMBA AONDOA HOJA YA KUONGEZA MUDA WA UBUNGE

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

MBUNGE  wa Chemba Juma Nkamia (CCM)amesema ameondoa kwa muda kusudio lake la kutaka kuwasilisha muswada binafsi wa mabadiliko ya Katiba unaohusu kuongeza ukomo wa Bunge. 
JUMA NKAMIA
Nkamia ambaye aliwasilisha kusudio hilo  katikati ya mwezi uliopita mjini Dodoma kwa mujibu wa kanuni ya 81(2) ya kanuni za Bunge toleo la 2016,kupitia barua yake aliyoisaini Septemba 12  iliyokuwa ikipendekeza kuongeza muda wa bunge kutoka miaka mitano hadi saba na kupunguza wa uongozi wa vijiji kutoka miaka mitano hadi minne.

Kupitia ujumbe mfupi aliouandika katika mtandao wa kijamii wa WhatsApp,alisema ameamua kuondoa kusudio hilo  baada ya mashauriano  na maelekezo kutoka kwa viongozi wa juu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM).

“Ndugu viongozi wenzangu naomba kuwataarifu kuwa baada ya mashauriano na maelekezo  ya viongozi wa juu wa chama(CCM) na hali ya kisiasa  katika nchi kadhaa za Afrika  Mashariki  nimelazimika kuondoa kwa muda hoja yangu binafsi ya ukomo wa Bunge niliyokusudia kuiwasilisha katika bunge lijalo,”aliandika Nkamia.

Mbali na andiko hilo gazeti hili pia lilimtafuta Nkamia kupitia simu yake ya kiganjani ili kumuuliza kama  na sababu nyingine zaidi ya alizozitaja kupitia ujumbe  huo mfupi na lini atakuwa teyari kuwasilisha tena muswada huo alisema.

“Naomba ibaki hivyo hivyo kama ilivyo kwenye meseji  sina cha kuongeza,kuhusu ni lini nitapeleka tena nayo subiri kwa sababu nimesema nimesitisha kwa muda maana yake nitawasilisha tena nitakapokuwa teyari,”alisema Nkamia.

Hoja ya  Nkamia ambayo ilianzia  katika Bunge lililopita ilikuw aikipingwa na wanazuoni pamoja na wanasiasa wakongwe akiwemo Spika Mstaafu wa Bunge Pius Msekwa.

Msekwa ambaye alikuwa akiongea na televisheni ya Azam  mwishoni wa wiki hii alisema  chama cha CCM hakiwezi kukubaliana na maoni au mpango wa kuongeza muda wa kiongozi yeyote kutoka kipindi cha miaka mitano kilichopo kikatiba kwa sasa.

Msekwa alisema kwa uzoefu wake bungeni tayari anaona kuna tafakari nyingi zilizofanywa kabla ya Taifa kuamua kipindi cha utawala kuwa miaka mitano na si vinginevyo.

Alisema hoja hiyo inabidi iangaliwe kwa umakini mkubwa kutokana na ukweli kuwa, iwapo kiongozi atakuwa mbaya, maisha yanaweza kuwa ya mateso kupitia kiongozi huyo na kuongeza kuwa hilo hata Hayati Baba wa Taifa, Julius Nyerere aliliona hilo.

“Ni kwamba miaka kumi tu inatosha, ili kama mtu ni mbaya tuvumilie kwa hiyo miaka kumi, na siyo kwamba haikufikiriwa. .na sidhani kama CCM itakuwa na nafasi ya kujadili hilo kwa sasa” alisema Msekwa. Mbali na Msekwa wasomi wakiwemo Dk.Benson Bana nao walimpinga huku akisema kuwa lengo lake lilikuwa ni kujipendekeza kwa Rais Dk. John Magufuli ili ampe uwaziri.

FUAMBAI SIA AHMADU: MWANAMKE ANAYETETEA UKEKETAJI AFRIKA.

Na KIZITO MPANGALA

FUNAMBAI SIA AHMADU alizaliwa mwaka 1969 nchini Sierra Leone katika jamii ya kabila la Kono kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Alifanya kazi na UNICEF nchini Gambia. Fuambai Sia Ahmadu alipata shahada ya uzamili katika chuo cha masuala ya Uchumi jijini London Uingereza akiwa kama mataalamu wa Anthropojia. Baadae aliendelea na masomo zaidi katika chuo kikuu cha Chicago na kupata shahada ya uazmivu.

Anafahamika zaidi kwa utetezi wake wa ukeketaji hasa akifikiria zaidi kutoka katika jamii ya kabila la Kono ambapo yeye mwenyewe amekeketwa na anafurahia jambo hilo. Anasema masuala mengi kuhusu ukeketaji hayajaeleweka kwa ufasaha miongoni mwa watu wengi duniani.   

Katika kitabu cha “AFRICAN STUDIES” chenye masuala mbalimbali kuhusu jamii mbalimbali za Afrika lipo swali linalouliza hivi ‘je, ukeketaji ukubaliwe na kuendelezwa kama jambo bora la kimila? Watu kadhaa walitoa majibu kuhusu swali hilo kulingana na mtazamo wao wanavyoona. Fuambai Ahmadu alikubali katika insha yake maarufu ya “Rites And Wrongs” kwa mujibu wa kitabu cha “FEMALE CIRCUMCISION AFRICA: CULTURE, CONTROVERSY AND CHANGE” kilichoandikwa na Lynne Rainer, 2001. 

Kabla ya jibu la Fuambai Ahmadu, mwanadada Liz Creel Et Al alipinga suala la ukeketaji. Jibu la mwanadada huyu ni kwa mujibu wa ripoti ya “ABANDONING FEMALE GENITAL CUTTING: PREVALENCE, ATTITUDES AND EFFORTS TO END THE PRACITCE” iliyoandikwa na taasisi ya Population Reference Bureau, Agosti 2001 Marekani ambapo Liz anasema serikali za Afrika zipitishe sheria kali inayobana wakeketaji.

Bi Fuambai Ahmadu anatetea ukeketaji na kukosoa baadhi ya waandishi hasa wasio wa Afrika na wa Afrika pia wanaohimiza ukeketaji ukomeshwe na kuwataka wanawake na wasichana wa Afrika wawe na muonekano wa Kimagharibi.

Bi Fuanmbai Ahmadu anasema na anaamini kwamba ukeketaji haupaswi kuzuiliwa kwa kuwa unaambatana na mila zingine kulingana na jamii husika inayotekeleza zoezi la ukeketaji ambazo zinampa mkeketwaji kuwa mwanamke anayekubalika zaidi na jamii yake katika mapokeo ya kihistoria ya jamii hiyo. Yeye ni mmojawapo kati ya waliokeketwa katika jamii ya kabila la Kono nchini Sierra Leone. 

Bi Fuambai Ahmadu anasema anachukizwa na wale wanaohubiri ubaya wa ukeketaji kwamba hawajaona na hawajui jema lililomo kwenye shughuli hiyo na hivyo hulinganisha na maeneo wanayoishi wao ambayo ukeketaji haufanyiki. 

Katika makala yake ndefu ya “RITES AND WRONGS: EXCSION AND POWER AMONG KONO WOMEN OF SIERRA LEONE” amezungumza mengi kuhusu ukeketaji. Katika makala hayo, anazishauri serikali za Afrika siruhusu ukeketaji ufanyike na ziborshe mazingira ya kufanyia ukeketaji yawe ya kitabibu zaidi yaani ukeketaji ufanyike hospitalini badala ya kienyeji. Ansema “the issue of female initiation and circumcision is of significant intellectual and personal interest to me” yaani “suala la uhamasishaji na ukeketaji kwa wanawake ni jambo la muhimu la kiakili na matakwa binafsi kwangu”

Bi Fuambai Ahmadu anasema yeye kama mtaalamu wa Anthropolojia kama walivyo Wanaanthroplojia wengine anavutiwa sana na masuala ya kijamii, kidini, kiitikadi, na kimila katika jamii nyingi na zaidi ni katika maeneo anayoyajua zaidi. Andai zaidi kwamba suala ukeketaji liboreshwe mazingira yake na hivyo liwe la kitabibu zaidi ili kuondokana na athari ndogondogo.
Ni Fuambai anasema utafiti mwingi kuhusu ukeketaji unafanywa na wale wasioishi Afrika na pengine hawana asili ya Afrika au wale wanaoishi Afrika na wenye asili ya Afrika lakini hawaishi katika jamii ambazo zinafanya ukeketaji. Ansema wanawake wengi wanaoandika habari kuhusu madhara ua ukeketaji hwajaishi katika jamii zinazoheshimu ukeketaji. Anaongeza kusema kwamba ukeketaji hauna madhara, kinachotakiwa sasa ni kuboresha mazingira ya kufanyia shughuli hiyo.

Bi Fuambai ansema kuwa wanaopinga ukeketaji wameathiriwa na hoja za kizungu na hisia hasi dhidi ya ukeketaji. Anasema wengi wanaokosoa ukeketaji wanajitetea kwa hoja za kimagharibi dhidi ya miili ya wanawake kwa kigezo cha hoja kwamba sehemu inayoondolewa katika shughuli ya ukeketaji ndiyo msingi mkuu msisimko wa hisia za mwanamke katika  tendo la ndoa. Yeye anapinga vigezo hivyo vyote na kusema kwamba hata sehemu hiyo ikiondolewa mwanamke atabaki na msisimko wake kama kawaida. Na vile vile inasaidia kumfanya mwanamke awe mwaminifu zaidi katika ndoa yake na kuepukana na tama ya kunuia kufuata wanaume wengine.

Bi Fuambai Sia Ahmadu kwa sasa ana uraia wa Marekani. Anatoa msisitizo kwamba kutokana na madhara ya muda mfupi baada ya kukeketwa ni vema jambo hilo lifanyike hospitalini ili kuepuka madhara hayo kuwa makubwa.
Msomaji wa makala haya, umepata nyongeza ya maarifa kuhusu ukeketaji na jinsi Bi Fuambai anavyotetea suala hilo kwa nguvu. Huo ndio masimamo wake. Maoni yako ni muhimu sana kuhusiana na suala hili la ukeketaji hasa katika dunia ya leo ya sayansi na teknolojia kama ilivyoasisiwa rasmi mwezi Januari mwka 2000.

0692 555 874, 0743 369 108

19 October 2017

STEPHEN HAWKING: MWANAFIZIKIA MGONJWA WA MUDA MREFU.

NA KIZITO MPANGALA

STEPHEN HAWKING alizaliwa mwaka 1942 jijini Oxford nchini Uingereza kwa wazazi Frank Hawking na Isobel Hawking. Japokuwa familia yake ilikuwa na mtikisiko kifedha lakini wazazi wake walijitahidi kujiendeleza kielimu katika chuo kikuu cha Oxford. Baba yake alisoma udakitari wa dawa na mama yake alisoma Falsafa, Sayansi ya Siasa, na Uchumi katika chuo hicho.

Baba yake na mama yake walikutana kwa mara ya kwanza muda mfupi tu bada ya kuanza kwa vita ya pili ya dunia katika Taasisi ya Utafiti wa Dawa ambapo baba yake alikuwa mtafiti  na mama yake alikuwa katibu wa taasisi hiyo. Ndipo mapenzi yao yalipoanza na walibahatika kupata mtoto wa kiume ambaye ni Stephen Hawking.

Familiya ya Hawking ilisifika kwa kuwa na kiwango kizuri cha upeo wa akili tangu wazazi hadi watoto wao. Muda mwingi walipokuwa nyumbani kulikuwa na ukimya ikidhaniwa kuwa wanasafiri mara kwa mara lakini sivyo! Ukimya uliotawala ndani ya familia hiyo ulitokana na wazazi kuwazoesha watoto kujisomea vitabu jambp ambalo walilipenda na ndipo Stephen Hawking alipodhihirisha kiwango chake katika upeo wa akili. Walikuwa wakiishi kwenye nyumba kuu kuu iliyokuwa na maktaba ya familia ndani.

Stephen Hawking alianza shule katika shule ya Byron mtaa wa Highgate jijini London. Baadae alilalamikia shule hiyo kutokana na mfumo wake uliokuwa ukitumika kufundishia, jambo ambalo lilinampa ugumu katika kujifunza zaidi. Wazazi wake walipohamia katika mji wa Mt. Albans, Stephen alijiunga na shule ya upili ya wasichana ya Mt. Albans mjini hapo kwa muda mfupi na baadae akahamishiwa katika shule ya Radlett katika mji mdogo wa Hertfordshire.

Wazazi wake waliipa elimu kipaumbele kwa kiasi kikubwa na kuwahimiza wajisomee vitabu vilivyokuwepo katika maktaba ya familia ndani ya nyumba yao.  Baba yake alitamani Stephen akasome katika shule binafsi ya Westminster lakini kwa bahati mbaya siku ya kufanya mtihani wa kujiunga na shule hiyo Stephen alishikwa na homa kali lakini pia wazazi wake hawakuweza kulipa ada katika shule hiyo iliyokuwa ikitoza kiasi kikubwa cha fedha wakati huo, hivyo Stephen alibaki katika shule aliyokuwepo.


Stephen Hawking alijizolea marafiki wengi katika shule aliyokuwepo kutokana na kiwango chake cha upeo wa akili katika masomo, hivyo hata yeye mwenyewe alifurani kuwa na marafiki na kucheza nao pamoja. Wakiwa shuleni walifundishwa stadi za kazi na mambo mengine yahusuyo maisha kwa ujumla. Walijifunza kutengeneza maboti na vielelezo mbalimbali vya ndege.

Mwaka 1958 wakisaidiana na mwalimu wao wa Hisabati bwana Dikran Tahta walitengeneza kompyuta  wakitumia vifaa vya saa kubwa ya kielektroniki iliyokuwa mbovu, pia walitengeneza simu za mezani kwa kutumia vifaa vya vyombo vibovu vya kielektroniki.

Stephen Hawking alipewa jina la utani shuleni ambapo alikuwa akiitwa “Einstein”, pia alikuwa na udhaifu katika maendeleo yake kitaaluma lakini alijitathmini kwa msaada wa mwalimu wake wa Hisabati bwana Dikran Tahta na kuamua kujikita katika masomo ya sayansi, akawa anaimarika kitaaluma. Aliweka bidii zaidi katika Hisabati na alipofika chuo kikuu alisoma Hisabati zaidi.

Baba yake alimhimiza asome udakitari wa dawa (Doctor of Medicine) akimuambia kuwa kuna ajira chache sana ambazo zinahitaji wajuzi wa Hisabati, hivyo alimsihi aachane na Hisabati ili asome udakitari wa dawa. Alimsihi pia ajiunge na chuo kikuu  cha Oxford. Baada ya kujiunga ilitokea kwamba ni ngumu kusoma hisabati wakati ule kutokana na uhaba wa walimu ndipo Stephen akachagua kusoma Fizikia na Kemia. Mkuu wa chuo alimsihi Stephen avute subira hadi mwaka wa masomo utakaofuata kwamba kutakuwa na walimu wa kutosha lakini Stephen alifadhiliwa.

Alianza masomo mwezi wa kumi mwaka 1959 katika chuo kikuu cha Oxford akiwa na miaka 17. Miezi 18 tangu aanze masomo katika chuo hicho alihisi kuchanganyikiwa kitaaluma kutokana na hulka yake ya kujilinganisha na wengine kitaaluma hivyo alijiona yeye si kitu na kwamba hafai lolote kusoma chuo kikuu, lakini mwalimu wake wa Fizikia katika chuo hicho bwana Robert Berman alimtibu kisaikolojia kwa kumuambia “ninapofundisha ninataka kukuonyesha kwamba kuna kitu fulani cha pekee inabidi kifanywe, na usikifanye kwa kuangalia watu wengine walifanyaje au wanafanyaje”. Kutokana na maneno hayo, Stephen alionyesha mabadiliko makubwa kitaaluma alipoanza mwaka wa pili wa masomo na mpaka alipofika mwaka wa tatu. Kadiri ya mwalimu wake huyo alisema kwamba Stephen likuwa kijana mwerevu kati ya waerevu.

Alipenda kujisomea hadithi za kisayansi na kujihusisha na muziki. Pia alikuwa mmoja kati ya washiriki wa masindano ya kuendesha maboti katika mashindano yaliyokuwa yakifanyika chuoni hapo.

Stephen alisema kwamba katika maisha yake ya kitaaluma chuoni Oxford miaka mitatu alitumia masaa 1000 tu kujisomea katika jumla ya miaka hiyo mitatu, hivyo mtihani wa mwisho wa kumaliza mafunzo ulimpa changamoto na akaamua kujibu maswali machache tu ya kipengele kimoja cha Fizikia ya Nadharia (Theoretical Physics) akiwa na lengo la kujiendeleza na masomo ya Cosmolojia katika chuo kikuu cha Cambridge ambapo alihitajika kupata ufaulu wa daraja la kwanza. Kutokana na mfadhaiko, alilala usingizi hafifu sana siku moja kabla ya kufanya mtihani wa mwisho, hivyo akapata alama zilizopungua kidogo kupata daraja la kwanza na kulazimika kufanya mtihani wa marudio uliojulikana kama “Viva” ili kusahihisha matokeo.

Stephen Hawking alijihisi ya kwamba ni mwanafunzi mvivu na mgumu kuelewa masomo kwa ufasaha. Alipoulizwa kuhusu matokeo yake ya awali alijibu hivi “mkinipa daraja la kwanza nitakwenda Cambridge, mkinipa daraja la pili nitabaki hapa Oxford, natumaini mtanipa daraja la kwanza”. Walimu wake walitambua kipawa chake cha upeo wa akili na walikuwa wakimpa uangalizi mkubwa sana bila kumuambia yeye mwenyewe. Baadae akapewa daraja la kwanza.

Alikwenda nchini Iran na rafiki zake kwa ajili ya mapumziko baada ya kumaliza chuo huko Oxford, na aliporudi Uingereza alianza kufanya kazi zilizohusu taaluma yake katika Ukumbi wa Kisayansi wa Trinity mjini Cambridge mnamo mwaka 1962.

Alipoanza masomo ya shahada ya uzamivu alihisi kwamba amekosea njia katika taaluma. Alipata changamoto kubwa  na hivyo kukata tamaa ya kuendelea na masomo ya Cosmolojia. Pia alihisi hataweza kujiendeleza na hisabati tena kutokana na changamoto alizopata. Lakini alihimili changamoto hizo hadi mwisho wa masomo yake.

Muda mfupi baadae alipata homa na hivyo kufanyiwa upasuaji na akabainika kuwa anasumbuliwa na homa iliyoiangamiza “motor nuerone” na kumfanya apooze mwili. Dakitari alimshauri aendelee na masomo japokuwa mwili wake ulikuwa ukiendelea kupooza taratibu, hivyo hakuweza kutembea na akawa anatumia baiskeli mpaka hivi sasa, vilevile alipata ugumu wa kupangilia matamshi yake kwa usahihi kutokana na kupooza kuanzia shingoni na kuathiriwa katika matamshi wakati anapozungumza.

Alirudi masomoni katika hali hiyo na kwa mshangao mkubwa aliboreka zaidi katika taaluma na pia aliweza kuboresha matamshi yake kwa msaada wa kitabibu.

Alpoanza kuwa mkufunzi alikuta mjadala mzito uliokuwa ukijadiliwa na wakufunzi wenzake wa Cosmolojia kuhusu jinsi ulimwengu ulivyotokea. Alikuwa mkufunzi hodari licha ya kuwa maisha yake kuwa katika baiskeli muda mwingi huku shingo ikiwa imekwenda upande kama anavyonekana pichani kutokana na kupooza mwili. Mwka 1965 aliandika insha yake mashuhuri kuhusu mjadala uliokuwa ukijadiliwa kuhusu jinsi ulimwengu ulivyotokea. Aliandika akiwa bado kijana lakini akiketi kwenye baiskeli muda mwingi.

Mwaka 1966 alitunukiwa shahada ya uzamivu katika Hisabati Tumizi (Applied Mathematics) na Fizikia ya Nadharia (Theoretical Physics) na alijikita zaidi katika Cosmolojia (Cosmology). Na baadae kazi yake aliyoandika kutokana na utafiti alioufanya (licha ya kuwa na kilema kama anavyoonekana pichani) ya “Singularities and the Geometry of Space – Time” iliheshimiwa na hivyo akashinda tuzo ya Adams katika sayansi.

Mwaka 1970 aliteuliwa kuwa profesa wa hisabati katika chuo kikuu cha Cambridge. Katika maisha yake kitaaluma amejikita zaidi katika sayansi ya ulimwengu (The science of Universe). Kadiri muda ulivyosonga alizidi kudhoofika na kulazimia kupata matibabu mara kwa mara akiwa nyumbani kwake.

Mwaka 1982 alihudhuria mkutano huko Vatican kuhusu ulimwengu ndipo alipotoa msimamo wake hadharani na kusema “hakuna mwanzo, hakuna mwisho, na hakuna mipaka katika ulimwengu”, tukumbuke kuwa ulimwengu una maana pan asana kisayansi, ulimwengu ni zaidi ya ukubwa wa dunia hii au sayari yoyote kwa kuwa ulimwengu ni jumla ya sayari zote na vyote vilivyomo katika anga. Stephen Hawking ansema kwamba nadharia ya Biblia inayosema kwamba kulikuwa na mwanzo wa ulimwengu siyo ya kweli na haina mashiko, hivyo hakuna mwanzo, mwisho, wala mipaka katika ulimwengu.

Pamoja na kuwa kilema na kuwa na tatizo la kufanya mawasiliano kwa usahihi, Stephen Hawking ni mwanafizikia aliyeweka kando ukilema wake na kujikita katika taaluma yake ya Fizikia. Hali ya kuwa kilema ilimpelekea kuachana na mkewe licha ya kuwa na watoto aliopata na mkewe huyo. Alitumia muda mwingi kufikiri masuala ya sayansi na kuweza kuandika vitabu vingi kuhusu Cosmolojia ambavyo vinatumika katika vyuo mbalimbali duniani.

Stephen Hawking amesafiri kwenda sehemu mbalimbali duniani kwa shughuli binafsi na kikazi. Stephen Hawking amekuwa gwiji wa  Cosmolojia na kusikika masikioni mwa watu wengi duniani kwa umahiri wake katika fizikia na hisabati licha ya kuwa kilema kwa muda mrefu jambo ambalo lilimpelekea kuwa na baiskeli maalumu iliyounganishwa na kompyuta ambayo inamsaidia katika mazungumzo na mambo mengine katika maisha yake.

Stephen Hawking amejitokeza mara nyingi katika mijadala mingi kuhusu Cosmolojia jambo ambalo alisema ndilo la maisha yake yote. Amekuwa mtu wa kutumainiwa katika vyuo mbalimbali duniani kwa taaluma ya Cosmolojia.
Hakika kilema si ugonjwa! Leo Stephen Hawking ambaye bado anatumia pumzi ya bure aliyojaliwa na Mungu ameshinda nishani zaidi ya 10 kwa muda wote wa maisha yake aliyoyaweka katika sayansi. Hawking ansema kwamba kila mmoja anao uwezo wa kujifunza anachokipenda.

Amekuwa na afya dhaifu kwa muonekano wa kawaida mwilini lakini ana afya imara sana katika ubongo wake. Muda mwingi wakati wa mapumziko hutumia kuzungumza na binti yake Lucy Hawking na ambaye humuwakilisha katika upokeaji wa zawadi kwenye matamasha mbalimbali anayoalikwa. Bega lake la kulia ndilo lililoathirika zaidi pamoja na miguu, lakini kwa hakika Mungu ni mkubwa, ubongo wa Stephen Hawking una afya imara sana ya maarifa na mambo mbalimbali maishani. Hivi sasa vyuo vingi vinafaidi kazi zake kuhusu Cosmolojia ambapo hutumika katika mafunzo ya kupata shahada ya uzamivu katika sayansi ya anga, na maisha yake muda mwingi ni juu ya baiskeli yake maalumu kama anavyoonekana pichani. Yuko hai.

© Kizito Mpangala 
0692 555 874,   0743 369 108.  

18 October 2017

SABUNI ZA MAWESE MWANGA, KIGOMA

Wachuuzi wa sabuni maarufu Kigoma ambazo hutengenezwa kwa malighafi ya Mawese. Sabuni zina wateja sana. Mfano maeneo ya Dar es salaam kama mtu atabahatika kuwa na mtaji halafu akasambaza hata kwa wale wenye maduka ya jumla atapata fedha. Hii bidhaa nzuri sana.
 

RIWAYA YA WANG LIPING

KITABU: DOUDOU NA MAMA WAKWE ZAKE
MWANDISHI: WANG LIPING
MCHAMBUZI: KIZITO MPANGALA
Doudou Na Mama Wakwe Zake ni hadithi iliyoandikwa kwa lugha ya Kichina na mwandishi Wang Liping na kutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili na wakalimani Chen Lianying na Han Mei. Kitabu hiki kina jumla ya kurasa 261 na kimegawanyika katika sehemu 24 za masimulizi yenye mtiririko mzuri ambapo sehemu inayofuata inategemea mhimili kutoka sehemu iliyopita. Kimechachapishwa na Zhenjiang Literature and Art Publishing House kikiwa katika lugha ya kichina na baada ya kutafsiriwa kwa Kiswahili kimechapishwa na Mkuki Na Nyota jijini Dar es Salaam Tanzania na kupewa namba za usajili (ISBN) 978 – 9987 – 08 – 284 – 1. Shukrani kubwa ziende kwa wakalimani  Chen Lianying na Han Mei kwa kutangaza lugha ya Kiswahili.

Ni hadithi inayofahamisha maisha ya kawaida ya Wachina lakini mafundisho yake yanafaa kwa kila mmoja wetu duniani. Hadithi hii kwa mara ya kwanza iliingia nchini Tanzania ikiwa kama mlolongo wa tamthiliya ambapo ilikuwa imefanyiwa marekebisho ambayo yalifanya mazungumzo ya wahusika yasikike kwa Kiswahili. Ilikuwa ikionyeshwa na shirika la habari la taifa (TBC) mwaka 2011.

Msichana Mao Doudou alikumbwa na mkasa wa kuachwa na mpenzi wake ambaye alikuwa mpenda pesa kuliko upendo kwa mwenzi wake. Katika hali kama hii maishani ni wazi kuwa ndoa ya aina hii haiwezi kusonga mbele endapo itatanguliza pesa mbele kuliko upendo unaostahili miongoni mwao. Miaka ya sasa ndoa nyingi zinakumbwa na tatizo hili ambalo huanza mwanzoni tu mwa mahusiano. Na mtu anayejitutumua kujionyesha ana pesa sana mbele ya mpenzi wake hakika huyo ni masikini wa fikra!

Tafuta mpenzi anayekufaa lakini usitume watu wakutafutie kisha wewe ukubaliane naye bila hata kuelewana kwa kina. Jambo hili ndilo liliomgharimu kijana Mao Feng na kupelekea kuachana na mpenzi huyo siku mbili tu baada ya harusi kufanyika. Mchakato wa kutafuta mchumba nchini China unafanywa na makampuni rasmi ambayo hukutafutia mchumba kwa kuilipa kampuni hiyo na kisha kujaza fomu maalumu. hiyo ni biashara ya kipekee sana ambayo huifaidisha serikali kwa kodi. Hivyo basi, mchumba tafuta mwenyewe, usijiiunize kwenye matatizo yasiyo ya lazima. 

Katika jamii zetu tumeona au tumefikwa na hali ya kuishi na mzazi wa kambo, hii ni kutokana na sababu mbalimbali ambazo zinakuwa nje ya uwezo wetu kuzitatua. Mao Doudou baadae anapata mume ambaye ni Yu Wei na kuishi pamoja kwa misukosuko kutoka kwa mama wakwe zake. Lakini je, kwa nini MAMA WAKWE NA SIYO MAMA MKWE? Imezoeleka kuwa mama mkwe ni mmoja tu. Lakini hilo ni mtihani mkubwa sana endapo baba na mama wakaachana na kisha kuoa au kuolewa tena, kwa hali hii itakuwa ni MAMA WAKWE na siyo MAMA MKWE tena, vile vile ni BABA WAKWE na siyo BABA MKWE tena!

Katika hao mama wakwe, yupo mama mzazi wa kijana wa kiume ambaye anaishi na baba wa kambo pia yupo mama wa kambo wa kijana wa kiumbe ambaye anaishi na baba yako mzazi, hapo ndipo ugomvi unajitokeza kila mmoja anadai umpelekee mkwe. Ugomvi wa ndoa wa wazazi hakika mtoto usiuingilie, kwani Wahenga wa Kiswahili husema “wagombanao ndio wapatanao”. Ni vitendo vya aibu kugombana ovyo katika familia ambayo imekuwa na msingi thabiti tangu awali. Lakini kwa uvumilivu na busara kama alizozionyesha msichana Mao Doudou ushindi unapatikana kwa kishindo! Msichana Mao Doudou ni mfano wa kuigwa katika hadithi ya kitabu hiki.

Mapenzi ni matamu sana ikiwa huna ujeuri kwa mwenzako na yeye hana ujeuri kwako wewe! Kwa mahabuba yenye raha na amani mmoja wenu anaweza akakuambia ametembea duaniani kote kutafuta mpenzi lakini hajaona mpenzi mzuri kama wewe hapo mlipo! Safi kabisa. Hapa tumkumbuke nguli wa fasihi ya Kimombo bwana William Shakespeare katika mashairi yake aliposema kuwa kwenye mapenzi kunahitajika aina fualni ya uwongo ili umuweke mpenzi wako kwenye mstari ulionyoka na asitoke! Vitendo vya kudanganyana kiholela katika mapenzi ni ujinga. Hilo lilimkumba Mao Feng ambaye ni mtaalamu wa kuwabwaga wasichana hao akishakamilisha dhamira yake. Lakini wakati ulipofika wa kuachwa yeye aliona dunia ipo kichwani mwake ameibeba! Kwa hiyo, tujifunze na tuwe wa kweli. Hapa namkumbuka afande Issa Mnyongo alipotuasa kwa kusema “vijana kuweni wa kweli”

Umaarufu ni jambo la kujivunia kwa wapenda umaarufu na kujihisi kuwa ulimwengu mzima unawatazama. Mtu yeyote aliye maarufu kwa jambo lolote, tafadhali chunga sana umaarufu wako kwa kuwa kuna wakati umaarufu huo unaweza kuwa UMMA-HARUFU. Kijana Mao Feng kwa umaarufu wake aliweza kuwahadaa wanawake na kuwa mlevi kupindikia jambo liliomfanya aingie kwenye ndoa na mtu aliyemzidi umri kwa kiasi kikubwa na ndoa ikayeyuka siku mbili tu baada ya harusi. Makinika na fundisho linalotoka hapa.

Yeyote anayeitwa mama mkwe basi azingatie kwa nini anaitwa mama mkwe. Mama mkwe ni kiongozi, ni mzazi, ni mlezi, ni mshauri, ni mwalimu na kadhalika. Mama mkwe anayefikiri kwamba fedha ndio msingi wa upendo kwa watoto wake kuingia kwenye ndoa basi huyo hana sifa hizi zilizotajwa isipokuwa tu yeye takuwa ni mlanguzi, tapeli, mfitini, mchonganishi, mchochezi, mjanja, mwongo, mwenye chuki na kadhalika. Mao Doudou ni binti anayempinga mama yake hadharani kwamba fedha siyo msingi wa upendo kwa mume wake, Mao Doudou anasema (akiwa amekasirika); “mama sipendi useme hivyo! Ni kwa nini kina mama wengi wako hivyo, wao wanachoangalia ni pesa tu” Uk. 36. Makinika na fundisho linalopatikana hapa.

Mama mkwe mwenye nia njema na watoto wake walioingia katika maisha ya ndoa ni mfariji, ni mwalimu, ni kiongozi, ni mlezi, ni mzazi, ni mshauri, ni mwenye amani ya nafsi na kadhalika. Pongezi hizi apate mama yake mzazi Mao Doudou baada ya kukosolewa na binti yake huyo kuhusu mawazo yake katika fedha. Mama anabadili msimamo na kumfariji binti yake kwa moyo wenye faraja kwamba wanaweza kuishi kwa kuvumiliana bila hata fedha ingawa kuna wakati watahityaji fedha kwa matumizi mbalimbali. Mama anasema; “Haya, kama unaweza kuvumilia maisha ya kawaida yasiyo na fedha nyingi mimi siwezi kupinga”. Hapa mama amejitambua kwa kiasi kikubwa sana, anapaswa kumfariji mtoto na siyo kumjaza falsafa za maisha ya ndoa bila fedha hayaendi, hii si kweli.

Kila mmoja anapenda kupendwa na mtu wa jinsia tofauti kwa namna ya pekee yenye ukaribu wa pekee na kwa hali pekee. Hilo ni juio la kila binadamu ingawa wapo binadamu wenye umri mdogo ambao wanakua na baadae watatambua hilo. Hata mimi nahitaji kupendwa na mtu wa jinsia tofauti kwa namna ya pekee! Ndio ubinadamu huo. Tuwape pole wale wote waliopoteza wenzi wao kwa namna mbalimbali. Hali hii inaweza kukufanya uchanganyikiwe kwa wakati fulani. Dada Yu Hao katika kitabu hiki alipoteza mume wake katika ajali ya gari siku mbili tu baada ya harusi, hali hii imemsababishia aishi kwa mfadhaiko kwa muda mrefu na hivyo kupata matatizo ya akili. Poleni nyote mliokumbwa na matatizo kama hayo. Jamani mapenzi matamu!

Kijana wa kiume, kwa kuwa name ni wa kiume kama wewe wa kiume usomaye hapa, basi makinika na funzo hili alilolionyesha kijana Yu Wei kwa kujitambua kwa umakini mkubwa. Yu Wei alijiweka wazi kwa mpenzi wake Mao Doudou aliyempenda maishani. Hakumuahidi magari, fedha, majumba na kadhalika. Hii ilimfanya akubalike zaidi na familia ya Mao Doudou kwa uwazi wake. Hivyo basi, kijana mwenzangu wa kiume makinika na fundisho hili. Kuwa muwazi. Tabia ya kudanganya kwamba una magari, fedha nyingi, maduka makubwa, majumba makubwa na kadhalika itatupeleka pabaya katika maisha yetu. Uchunguzi ukifanyika utaona kwamba anayeahidi au kutamba hivyo hata mkokoteni wa kuvuta na punda hana! Kama kweli unavyo vitu hivyo, basi usivipe kipaumbele kwa mpenzi wako!

Kusema kweli kuishi pamoja na mama mkwe mtukutu ni taabu zaidi kuliko kufanya kazi nyingine, mbali na kuwa mtiifu na mvumilivu wakati wa kukosolewa na mama mkwe wa aina hii, ni lazima kuwa na uwezo mwingine wa kukabiliana naye! Mama mkwe wa namna hii ni hatari zaidi kwa wanawe. Mama mkwe sikiliza kwa makini, hata kama mkweo amekosea jambo au kama humpendi jitahidi kuwa naye karibu kwa amani na ujitathmini kwa nini humpendi. Katika kitabu hiki tunaona jinsi Cao Xinmei anavyomchukia Mao Doudou lakini Mao Doudou anajitahidi kumvumilia. Kwa hiyo, fundisho lake ni kwamba mama mkwe unapaswa kuwa mstahimilivu na mwenye busara unapokuwa na mkweo. Mkweo ni binadamu kama wewe na ukumbuke kuwa na wewe ulikuwa mkwe kwa wazazi wa mume wako. Kama ulitendewa jambo baya huko basi jitahidi sana usihamishie kisasi chake kwa mkwe uliyenaye hapo!

Wakati wa dhiki udhati ndio huonekana kwa kiasi kikubwa sana. Kumpenda ndugu, jamaa, au rafiki yako kwa dhati kusionekane wakati wa dhiki tu bali ni wakati wote. Ikiwa kama mwadhani ya kwamba kumpenda ndugu, jamaa, na rafiki zenu kunahitaji fedha za kigeni basi jueni ya kwamba mnakosea. Msijivike mavazi yanayosimulia fedha ili kuonyesha upendo kwa ndugu, jamaa, au rafiki zenu. Upendo siyo fedha na fedha siyo upendo! Makinika na falsafa hii ndogo yenye manufaa makubwa.

Wifi ni mtu mzuri sana katika familia na anao umuhimu wake kwa mkeo wewe kijana wa kiume. Wifi anaweza kumchombeza mke wako ili amakinike zaidi kwa mahabuba mazito kwako, anaweza kumchombeza mkeo ili ajihisi kuwa bila wewe mambo yake yote yanaharibika, anaweza kumchombeza ili ajisikie kuwa yupo kwenye ghala salama lisilo na wadudu wanaoharibu nafaka, anaweza kumchombeza ili ajihisi kuwa wewe ni jemedari wa majukumu yanayokupasa kwake bila kuchenga na ajihisi kuwa hakuja kwako kula na kunywa bali alifuata mapenzi ili kulainisha moyo wake! Haya ni matunda ya wifi bora. Lakini endapo wifi anakuwa kinyume na chombezo kama hizo basi kila kukicha anamsimanga mkeo, anamkejeli, anamtukana, anampa kila neno la kumkatihsa tama. Kwa hakika wifi kama huyu ni bomu kubwa sana. Hivyo basi, ninyi mawifi kaeni na mawifi zenu vizuri ili muishi kwa amani na furaha.

Pan Meili ni msichana anayetambua thamani ya kuonekana kwa asili na siyo kujiweka nakshi mbalimbali za urembo mpaka kujiondolea asili yake. Hivyo basi kina dada mnapaswa kujali asili ya mionekano yenu ili mjiepushe na magonjwa ya ngozi yanayotokana na matumizi yasiyo ya lazima ya vipodozi vikali au vilivyokwisha muda wake wa kutumiwa.

Mafunzo yanayopatikana katika kitabu hiki yanafaa sana katika maisha yetu. Akina dada igeni mfano wa dada Mao Doudou katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha ya ndoa. Msidanganyike kusema kuwa  maisha ya ndoa bila fedha nyingi hayaendi. Nanyi mama wakwe popote mlipo msiwatendee wakwe zenu vibaya, kama ni kuwaonya basi muwaonye kwa nidhamu na heshima ili muishi kwa amani na furaha daima.

Ushauri wangu kwa waandaaji wa tamthiliya ya SIRI ZA FAMILIA ambayo hurushwa na Clouds Media, ni kwamba wanaweza kuiweka tamthiliya hiyo katika kitabu itakapomalizika ili kutunza kumbukumbu kwa miaka ijayo kama mwandishi Wang Liping alivyofanikisha hilo katika maonyesho ya MAO DOUDOU NA MAMA WAKWE ZAKE.

© Kizito Mpangala

     0692 555 874, 0743 369 108

17 October 2017

MAONI YA MHARIRI: KWA WILAYA YA NYASA DUNIA HAIJABADILIKA?

Majuzi nimeona picha ya mwanadada mashuhuri katika mtandao wa Instagram, Mange Kimambi akionyesha majengo ya hospitali ya Lumeme wilayani Nyasa ikiwa na mazingira mabaya ya kufanyia kazi na ukosefu wa huduma muhumu. Pamoja na jengo lenyewe kutokamilika, lakini limekuwa likitumika hivyo hivyo.

Kwangu mimi ile ilikuwa habari kubwa sana kwa wilaya yetu ya Nyasa. Kama mwanahabari naamini kuripotiwa matukio au masuala yasiyofaa  ndani ya jamii ambayo haitoi habari za kutosha ni njia mojawapo kubwa ya kubadili mwenendo.

HAPA CHINI kuna Blogu ya JIMBO LA NYASA. Lakini habari za Jimbo husika ziliwekwa mara ya mwisho Januari mwaka huu. Nimejiuliza wasaidizi wa Mbunge wanafanya nini kama hawawezi kutoa taarifa za ofisi ya mbunge? Najiuliza hivi hatuoni umuhimu wa habari zetu zikiwa hadharani bila kujali mbaya au nzuri?

Je waanzilishi wa blogu ya JIMBO walikusudia tamasha au nini? BONYEZA HAPA KUTAZAMA.  Kimsingi habari za Jimbo la Nyasa ni lazima zitolewe wala kwa wananchi. Pili inadhihirisha "kuamini" kuwa NYASA ni ileile ambayo inaishi pasipo kuwa na habari zozote. Mtazamo huo si sahihi ndio maana wahusika wanaona "bora liende tu" huku wakisahau na kushindwa "KUMUUZA" mbunge. 

Nimejiuliza hadi leo hata kutengeneza ukurasa wa habari za mbunge kwenye mitandao hatuwezi kweli?  Hivi mahusiano ya mbunge na wapigakura wake yana maana gani? Naandika hapa kwasababu naamini wapo wahusika wanaofikisha ujumbe. Ningependa kuwakumbusheni kuwa "kutomuuza mbunge" katika ulimwengu wa kidigitali ni uzembe. Labda tunaweza kutembelea wananchi kila kona ya jimbo, lakini tunapawa kuelewa kuwa taarifa za huko ziwekwe sehemu maalumu kutunza kumbukumbu sio mambo ya "MASJALA" tena (hizo ni zama za kale mawe).

Kwa heshima nawakumbusha wasaidizi wa mbunge, kutoitendea haki blogu, kutozungumzia hata utalii ambao ni chachu ya kukuza mzunguko wa fedha wilayani kwetu ni UDHAIFU unaopaswa kurekebishwa.
Ninawatakieni majukumu mema. 
HABARI NI BIASHARA. HABARI NI UCHUMI.

MARKUS MPANGALA,
Oktoba 17/ 2017
Dar es salaam

TAKWIMU MUHIMU ZA WILAYA YA NYASA HADI OKTOBA 2017


1. Total Number of Hamlets in the District = 425

2. Total Number of Households for Nyasa dc = 31,146

3. Total Female Population for Nyasa dc = 74,768.


4.Total Male Population for Nyasa dc = 71,392.

5. Total Population for Nyasa dc = 146,160.

6. Total Number of Secondary school = 14

7. Total Number of Primary School = 106
Total Number of Villages = 84


8. Total Number of Ward = 20

9. Total Number of Division = 3

CHANZO: Nyasa dc statistics

UTAMU WA WIMBO WA TAIFA UKO KOMBE LA DUNIA.

NA. HONORIUS MPANGALA
 
ILIKUWA miaka Sita ya Ubabe wa soka barani Afrika kuanzia mwaka 2006 hadi 2012. Kila mpenzi wa soka alimfahamu Hassan Shehata,kila mpenzi wa soka alimfahamu Waile Gomaa. Ilikuwa nyakati za Misri kunyanyasa mataifa mengine ndani ya bara la Afrika. Ilimchukua Kameruni miaka tisa kulipiza manyanyaso aliyopata toka kwa Misri ya kiumeni mwaka 2008 pale Ghana.
Ni Misri ambayo iliipa hasara CAF kuunda kombe lingine la Afcon baada ya kulibeba lile awali Mara nne Mfululizo. Mwaka 2006 fainali zilizoandaliwa na Misri wakikutana na Ivory coast ya Didier Drogba.
KIKOSI CHA MISRI

Fainali ile iliisha kwa matuta na wenyeji kutwa taji. Licha ya kuwa na kikosi ambacho kilikuwa na vijana taklibani Saba wakitoka kikosi cha Al Ahly ambayo ilikuwa moto wa kuotea mbali. Hapa nawazungumzia Mohammed Barakat,Saeed Moward,Essam El Hadary,Ahmed Hassan,Hossam Hassan,Mohammad Mido,Mohammed Aboutrika na wengineo. Ilikuwa ni kikosi kilichojaa vipaji kikiwa na hamasa kubwa kutoka kwa kocha mzawa Hassan Shehata kiliwafanya wapinzani wafikirie Mara mbili zaidi.

Ukuta ulioongozwa na Waile Gomaa ilikuwa kama unakutana na Rio Ferdinand wa nyakati za Vodafone na Manchester Utd yake. Beki mmoja chuma halafu bedui anacheza kibabe kiasi kwamba hupati nafasi ya hata kumiliki mpira kama mshambuliaji. Kwa lugha za sasa za mtaani unaweza kusema 'ana kuvugaa' kama ulivyo.

Si mnakumbuka Zengwe la Hassan Shehata na Mido katika Nusu fainali ya afcon iliyowalutanisha Misri na Senegal 2006. Ilikuwa Senegal ya vipaji haswa. Kuna nyakati unaweza kukaa na kutoa majibu kuwa soka la kipaji limeondoka miguuni mwa wachezaji tunao watazama sasa. 

Lile zengwe ilikuwa baada ya Kufanyika mabadiliko yaliyomuingiza uwanjani Amri Zaki na kumtoa Mido. Mwarabu yule hakufurahishwa aligombana kwa maneno na kocha wake. Ajabu ya mwenyezi Mungu Zaki akafunga bao lililowapeleka fainali na kumwacha Mido akishindwa kushangilia huku Shehata akimwonyeshea kidole katika kichwa chake akimaanisha akili.

Licha matukio matamu yenye kusisimua kwa nyakati za zote za Ubabe wa Misri jambo pakee ilikuwa kizazi hicho hakikufanikiwa kufuzau kombe la dunia. Asikudanganye mtu hakuna raha kama kuimbiwa wimbo wa Taifa katika mashindano ya kombe la dunia.Misri walijaribu kuitafuta raha hiyo lakini wakaishia kuipata wanapocheza Afcon.

Mara ya mwisho kwa Misri kushiriki ko be la dunia ilikuwa mwaka 1990. Katika fainali zilizofanyika nchini Italia ikawa mwisho wao hadi sasa ambapo Mohammed Sarah anawapeleka Urusi mwakani. Ilikuwa nyakati za utawala wa Hosney Mubarak ndipo waMisri walipoimba kwa pamoja na wachezaji wao wimbo wa taifa pale Italia.

MOHAMMED SALAH

Wakiwa na nahodha na golikipa mkongwe Essam El Hadary Misri wanafuzu huku akiwa na wadogo zake ambao wametengeneza kikosi kilichoandika historia ya Misri tena. Matumaini ya kurudi katika Ubabe wa soka la Afrika yalianza kuonyesha matumaini katika michuano ya Afcon ya mwaka huu pale Gabon. Ukikitazama kikosi chao kina majina maarufu mawili yaani Mohammed Sarah na Mohammed Elneny katika dimba huku kaka yao El Hadary akihakikisha hakuna mpira unaompita na kutinga wavuni.
Juni 8 ilikuwa ya kihistoria kwao baada ya kufanikiwa kutinga faninali za kombe la dunia la mwakani. Magoli ya mawili ya Salah dhidi ya moja la Congo Brazzaville yaliwapaisha na kuwafikisha Urusi. 

Jambo pekee katika Mchezo huo ni goli la dakika ya 90+3 lililofungwa kwa mkwaju wa penati na Salah ndilo lililofanya Misri yote ilindime kwa Shangwe vifijo na ndelemo. Ilikuwa zaidi ya sherehe kila mmoja alijikuta akifurahia matokeo ya Timu ya taifa licha ya tofauti za kisiasa zinazolitafuna taifa hilo kwa maandamano na mapigano ya wanajeshi wa serikali na Waasi.

Ukitaka kujua raha ya kuimbiwa wimbo wa taifa kombe la dunia muulize Serey Die nahodha wa sasa Ivory Coast. Alitoa mchozi wakati wimbo wa taifa unaendelea pale Brazil katika Mechi iliyowakitanisha Ivory Coast dhidi ya Japan. Mchezo ambao wapenzi wengi wa soka ilibidi wasubili hadi kumi za usiku kwa masaa ya Afrika mashariki kumwona Die akiangua kilio.
WAEL GOMAA
Nawaona wamisri wakiangua kilio zaidi ya kile walichoangua pale Misri baada yachezo dhidi ya Congo Brazzaville. Ilikuwa kama ndoto kwa mkongwe El Hadary kutimiza ndoto za kuisaidia Misri kufuzu kombe la dunia. Vilio vya uchungu walivyolia Wamisri pale Sudan mwaka 2009 vimegeuka vilio vya furaha kwa mwaka 2017. Kuna wakati mnaweza kupitia mitihani mikubwa lakini kumbe Mungu anakuwa na maksudi nanyi. 

Ubabe wa Afcon kwa wamisri haukuwapeleka kombe la dunia lakini unyonge wao wa wakati huu unawafanya watimize ndoto na kwenda kuimba wimbo wao wa 'My country' katika ardhi ya Urusi. Utamu wa wimbo wa taifa mchezaji auimbe akiwa kombe la dunia.

Hakuna hoja yoyote ambayo inaweza kumfanya mtanzania akaona kama ni ya kujifunza Kwa kufuzu Kwa misri. Kama kufuzu Kwa Serengeti watanzania walichangiani je kwa Taifa Stars? Unajisikiaje Rais wa Misri kamwaga pesa Kwa vijana wake au unasikia Rais wa Panama kaamua siku moja kufanyika mpumziko ili kuwapongeza vijana wake. 

Misri mmepata mlichokitafuta kwa miaka takribani ishirini na sita. Nendeni Urusi mkawakilishe Wafrika ambao watakuwa wanawachukulia kama timua yao.

0628994409