Showing posts with label Iringa. Show all posts
Showing posts with label Iringa. Show all posts

September 10, 2013

WATANZANIA TUKAZANE KUWEKEZA KWENYE ARDHI



Na, Albert Sanga, Iringa
 
Leo ni mwaka mmoja kamili umepita tangu nilipoandika makala hapa safuni iliyokuwa na kichwa, “Njooni shambani mtajirike”. Ilikuwa ni makala iliyotoa shime kwa watanzania kuchangamkia fursa ya uwekezaji kwenye kilimo cha miti.

Katika makala ile niliwaeleza watanzania upana wa faida ya kuwekeza katika miti aina mbalimbali huku nikijikita katika miti ya mbao, karatasi na nguzo.  Nilichambua kwa kina sana gharama za upandaji wa miti hiyo, muda wa kuvuna, soko lake lilivyo na matarajio ya biashara hiyo kwa miaka ya baadae.

Leo ninaandika tena makala hii huku nikiwa na furaha tele moyoni mwangu kwa sababu makumi ya watanzania waliuitikia mwito wangu na wakachangamkia fursa hii. Kama ambavyo nilitamani iwe, ndivyo ilivyokuwa kwani wengi wamenijulisha kuwa hawakulazia damu, walichangamka na kuanza kuwekeza.
Ingawa mimi ni mmoja ya watanzania ambao wanajishughulisha na uwekezaji katika mashamba ya miti mkoani Iringa, kiu yangu ilikuwa ni kuona watu wakichangamkia fursa hii mahali kokote inakopatikana. Mikoa ya Tanga, Njombe, Mtwara, Tabora, Mbeya, Bukoba na kwingine kwingi kunastawi miti ya aina mbalimbali.

Kwa hakika wengi wameendelea kufanya hivyo kwani wamekuwa wakinijulisha. Wapo makumi waliosafiri hadi hapa Iringa kujifunza na kujionea fursa hii inavyowanufaisha na kuwatajirisha watu; kati yao wapo walioamua kuanza kuwekeza na wapo ambao walirudi makwao ili kujipanga kwa ajili ya kuwekeza wakati ujao. 

Furaha yangu ilikuwa kubwa zaidi pale ambapo wapo waliofika kujifunza hapa Iringa kasha wakaenda katika maeneo yao na kuanza kuwekeza. Wapo mamia ambao walizungumza nami kwa simu kutoka maeneo mbalimbali wakiwa wamevutiwa na habari zile.  

Nami kwa moyo mkunjufu nilishirikishana nao uzoefu wangu na kuwahamasisha waanze hata kama ni kidogo kidogo mahali popote wanapoona inafaa. Ni jambo la kujivunia na la fahari kutamka kwamba makala ile imekuwa na ‘impact’ kubwa mno kwa mamia ya watanzania ambao walihamasika kuanza kuwekeza katika miti kule Tanga, Tabora, Mbeya, Mtwara, Morogoro na wengine wengi hapa Iringa.

Kama ambavyo nimekuwa nikisema mara kwa mara katika makala zangu; ni kwamba muda wa kulalamika lalamika umekwisha. Mazoea na utamaduni wa watanzania wengi kudhani kwamba tunaonewa wakati wote haujatusaidia mpaka hapa kwa jinsi hii hakuna sababu ya kuendelea nao. 

Mtindo wa kuishi maisha ya kutaka kuhurumiwa yanatupotezea muda wenye thamani. Tumekuwa tukilalamika kuwa wageni (wanaokuja kwa jina la wawekezaji) wanatupora ardhi; lakini tusichokitafakari ni hiki, “Mimi kama mtanzania kwa nafsi yangu na kwa uwezo wangu nimefanya nini cha maana katika ardhi ninayoweza kuipata hapa nchini ama ninayomiliki?”.

Bahati nzuri ni kwamba idadi kubwa ya watanzania tunafahamu kuwa ardhi ni utajiri; lakini hatufanyi juhudi za makusudi kuuvumbua na kuutumia utajiri huo. Tunayo mamilioni ya hekta za ardhi zenye rutuba na zinazofaa kwa kilimo cha aina mbalimbali lakini bidii zetu hazijatosha hata tufike mahali tuseme ardhi haitutoshi.

Itakumbukwa kuwa wakati nikiandika makala ile mwaka jana pia nilizindua kampeni ya kimazingira niliyoibatiza jina la “Green The World And Become Rich”.  Kimsingi kampeni hii nililenga kuwahamasisha watanzania washiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira na wakati huo huo wakitengeneza utajiri. 

Unapochukua fedha yako na kuwekeza kwenye shamba la miti moja kwa moja unakuwa umetunza mazingira kupitia miti uliyopanda lakini pia usiku na mchana kadiri miti inavyoendelea kukua unakuwa ukitengeneza mamilioni. 

Na hii ni namna moja nzuri ambayo watanzania tunaweza kuwekeza kwenye ardhi. Leo unapanda miti inakaa miaka saba ama kumi unavuna halafu baada ya hapo ardhi yako unaitafutia matumizi mengine. Si hivyo tu, lakini katika hiki hiki kilimo cha miti; ndani ya shamba lako unaweza kufuga nyuki, ukawa unavuna asali hukuku ukisubiri kuvuna miti yako.
Msukumo wa kuanzisha kampeni hii ya “Green The World And Become Rich” niliupata baada ya kutafakari nafasi walizonazo watu wengi wenye nia ya kuwekeza katika kilimo cha miti na katika ardhi kwa ujumla. Nilifahamu kuwa sio rahisi sana kwa mtu kutumia fedha zake na kupanda miti kwa faida moja tu ya kutunza mazingira. 

Nilijaribu kufikiri namna ya kuongeza thamani; hivyo ilinibidi nifanye kazi ya kuwaelimisha watu mbalimbali mambo mengi kuhusu miti, biashara yake na namna inavyolipa. Ninafahamu kuwa mamia ya wanaoendelea kuwekeza kwenye miti sehemu mbalimbali Tanzania, kufuatia kampeni yangu; wanawezekeza kwa mtazamo wa kupata faida kifedha huko mbeleni. 

Hilo ni jema sana lakini wakati huo huo mimi na wadau wengine wa mazingira tunashangilia kwa sababu mazingira yanaimarika huku watu wakitajirika. Vile vile Nilitambua kuwa wengi wanaweza wasiwe na taarifa sahihi kuhusu kilimo hiki, kwa maana ya maeneo kinakostawi, taratibu za upataji maeneo, lakini kubwa kuliko yote ni namna ya usimamiaji pindi wakiwa mbali. 

Nilifahamu mtu angeweza kujiuliza maswali mengi yakiwemo; “Nitawezaje kumiliki shamba Tabora wakati mimi kikazi nipo DaresSalaam?”, “Nitawezaje kufahamu biashara ya mbao, magogo, pindi ukifika muda wa kuvuna?”, “ Mbali na faida nitajuaje gharama za uendeshaji na je nitazimudu?”.  

Katika kampeni hii kulikuwa na majibu yote ambao kwa wale waliovutiwa kuwekeza Iringa katika maeneo inakowekeza kampuni yangu, nilijitolea kuwapa usaidizi wa kuwatunzia na kuyahudumia mashamba yao. Fursa bado zipo nyingi, watanzania wenzangu tusilale.
Ninapoandika makala haya leo ninatumia wasaa huu kuwakumbusha wale jamaa zangu wa kule Tanga, Tabora, Mbeya na kwingine ambao waliniahidi kuwa wataanza kuwekeza katika maeneo yao mwakani (yaani mwaka huu). 

Msimu ndio umeanza, kuandaa mashamba, kuaandaa miche na maandalizi mengine. Hapo hapo mlipo fanyeni kitu katika ardhi zenu, wekezeni kwa manufaa yenu na ya watoto wenu, isaidieni dunia kwa kuboresha mazingira yake.

Wale waliofika Iringa wengi wao nilikuwa ninawapa zawadi ya nakala ya sheria ya ardhi ya mwaka 1999. Na wengine waliokuwa wakiwasiliana nami nilikuwa ninawapa semina fupi kuhusu sheria ya ardhi. Kiujumla sheria hii inatupendelea mno wazawa tofauti na malalamiko mengi ambayo huwa ninayasikia.

Pengine Watanzania tuna tatizo katika ubunifu na inapotokea wengine wamebuni tunakuwa wepesi wa kudhani wametuibia. Mathalani, tunaishi na ardhi tusiyoifanyia kazi miaka nenda rudi, akitokea mwekezaji akabuni mradi Fulani katika ardhi hiyo; tunaanza kuja juu! Hatujiulizi tulikuwa wapi na kwa nini hatukuchangamkia?

Kingine kinachotumaliza Watanzania wengi ni ile dhana ya kudhani kuwa kilimo ni utumwa, shamba tunaona ni kwa ajili ya waganga njaa na waliokosa nafasi ya kupata ajira nzuri. Hii ni dhana mbaya na inachangia sana watanzania kutokuwa na mikakati ya kuitumia ardhi kikamilifu. 

Hata hivyo nikiri kuwa wapo watanzania ambao wanatambua thamani ya ardhi na wanaitumia ardhi vizuri kwa uzalishaji na uwekezaji wenye tija. Lakini idadi hiyo haitoshi ukilinganisha na idadi ya wasiotambua nguvu na utajiri wa ardhi ambao wanaendelea kulalamika ugumu wa maisha na waliopoteza tumaini.

Jambo jingine linalotumaliza watanzania ni kutokuwa na maono ya muda mrefu. Wengi wetu tunataka mambo ya papo kwa papo, hatupendi kuangalia mambo ya vipindi virefu mbele. Mfano mzuri ni katika hili la uwekezaji katika ardhi. 

Mtu anaona ni kupoteza fedha kununua shamba leo ambalo pengine linaweza kuja kutumika miaka ishirini huko baadae. Mtu anaona ni kama kupoteza fedha kupanda miti leo ambayo atakuja kuivuna miaka saba ama miaka kumi ijayo. 

Wasichokumbuka wengi ni kuwa unachopuuza kufanya leo kwa gharama ndogo miaka ishirini ama kumi ijayo hutakuwa na uwezo wa kukifanya hata kama ukitamani. Mzee wangu mmoja hapa Iringa alinisimulia namna alivyopuuza kununua kiwanja kimoja hapa mjini Iringa mtaa wa Miyomboni mwaka 1994. 

Wakati huo anasema kiwanja hicho kilikuwa kikiuzwa kwa shilingi laki nne; lakini mwaka jana, 2012 kimeuzwa kwa milioni 320! Mzee wangu huyu anasema mwaka huo 1994 laki nne kwake zilikuwa ni hela ndogo sana lakini akapuuza. Leo hii miaka 20 baadae kiwanja kile kile kimeuzwa mara mia nane ya bei aliyoipuuza ilhali yeye (mzee wangu huyu) leo hana hata ujanja wa kupata milioni kumi! 

Kwa maneno yake anasema, “Ningekuwa na mipango ya muda mrefu katika kuwekeza kwenye viwanja, ardhi na mashamba, leo mimi ningekuwa milionea hapa mjini” Anachofanya mzee wangu huyu ni utekelezaji wa ule msemo, “Majuto ni mjukuu”!
Watanzania tusilale, ushindi wetu kiuchumi umo ardhini!
stepwiseexpert@gmail.com +255 719 127 901

March 26, 2013

BIASHARA NA UCHUMI: TAIFA LINAWAHITAJI "WAJASIRIAKAZI"

Albert Sanga, Iringa

Nimekua nikiandika makala za hamasa kuhusu ujasiriamali ikiwa ni hatua ya kukabiliana na mabadiliko ya kiuchumi ambapo kuna upungufu mkubwa wa ajira, lakini pia kuna mfumuko wa gharama za maisha kiasi kwamba hata walioajiriwa wanapata wakati mgumu kumudu vema maisha ya kila siku.

Moja ya swali ambalo nimekuwa nikiulizwa mara kwa mara ni hili, “Sanga unataka kila mtu awe mjasiriamali?” Jibu langu katika swali hilo limekuwa ni hili siku zote: “Ndio, natamani kila mtanzania awe mjasiriamali”.

Nafikiri ipo haja tuangalie kinagaubaga dhana hii ya ujasiriamali kwa mtazamo mpana. Ujasiriamali umegawanyika katika makundi mawili. Mosi ni ujasiriamali wa kibiashara (entrepreneurship) na pili ni ujasiriamali wa kikazi (intrepreneurship). Kundi la kwa linahusisha wajasiriamali waliojiajiri na kundi la pili linahusisha wajasiriamali walioajiriwa. Wajasiriamali walioajiriwa wanaitwa “Wajasiriakazi” na wajasiriamali waliojiajiri walipaswa kuitwa “Wajasiriabiashara”.

Wataalamu wa Kiswahili itabidi waliweke sawa hili kwa sababu neno “Ujasiriamali” linatumika kiupendeleo kwa kuwalenga wale tu waliojiajiri wakati linatakiwa kuyafaa makundi yote mawili. Nadhani sasa utaelewa ni kwa nini ninasema natamani kila mtanzania awe mjasiriamali. Leo katika makala haya nitajikita kueleza dhana ya ujasiriamali kazini. Hivyo basi kila ninapohamasisha watu kuwa wajasiriamali, haimaanishi huwa ninawananga wale walioajiriwa, la hasha! Mtu yeyote aliye mweledi wa uchumi na kiimani anafahamu umuhimu wa kila mtu kusimama katika nafasi yake kutimiza kusudi la taifa na kusudi la Mungu. Hakuna aliye bora zaidi ya mwenzake; aliyeajiriwa ama aliyejiajiri, mfanyakazi ama mwajiri, wote wana umuhimu sawa.

Kwa sababu hakuna ujasiriamali kama hakutakua na watendakazi. Kwa hiyo waajiri (wajasiriamali wa kibiashara) wanahitajika kwa wingi na wafanyakazi (wajasiriamali wa kikazi) wanahitajika pia. Kwa maana hii taifa linahitaji kuwapata wafanyakazi ambao watawiana na ndoto za taifa na wajasiriamali katika kujenga uchumi na kuleta maisha bora. Miaka ya karibuni dhana ya ujasiriakazi imekuwa ikipata umaarufu mkubwa, ingawa ni watu wachache ambao wanaielewa vema dhana hii. Watafiti wengi wanakubaliana kuwa dhana ya ujasiriakazi ni jamii ya dhana ya ujasiriamali(entrepreneurship) lakini hii ikiwa inafanyika ndani ya taasisi, makampuni, na serikalini ikihusisha “usimamizi wa rasilimali kiubunifu”.

Dhana ya ujasiriakazi inaonesha kuwa ilijitokeza na kushika kasi duniani miaka takribani thelathini iliyopita. Ujasiriakazi unahusisha uundaji, uendelezaji na utekelezaji wa mawazo na tabia mpya katika maeneo ya kazi. Ubunifu unaweza kuhusisha kubuni bidhaa mpya ama huduma, kubuni mfumo mpya wa utawala ama mpango mpya ama mikakati inayohusiana na wafanyakazi katika eneo husika. Wajasiriakazi ni watu ambao si lazima wawe wagunduzi wa bidhaa ama huduma mpya isipokuwa ni watu ambao wanabadilisha mawazo ama fikra kwenda kwenye uhalisia wenye faida. Ni watu ambao ukiona huduma ama bidhaa basi ujue kuwa wapo nyuma yake.

Ni watu ambao huunda timu za kiutendaji ili kuhakikisha kuwa wanafanya juhudi kushughulikia mawazo yao kuwa katika uhalisia. Wajasiriakazi si lazima wawe watu wenye uwezo wa juu sana kiakili (geniuses), lakini ni watu wa upeo wa kawaida kiakili. Kwa mtazamo huu tunaona kuwa dhana ya ujasiriakazi inajikita zaidi katika kutoa msukumo mpya na kuwezesha maeneo ya kazi kuwa na ubunifu na njia mbadala za kutekeleza majukumu yake. Muunganiko wa wafanyakazi katika maeneo husika yanapelekea kutengenezwa kwa sura mpya ya taasisi, ama kampuni ama kitengo cha serikali.

Wafanyakazi wajasiriakazi ni wale wanaohitaji uhuru na urahisi wa kutumia rasilimali za maeneo yao ya kazi, wenye hamasa kutoka ndani (self motivated) na wanaoguswa kwa mafanikio chanya ya maeneo yao ya kazi. Mara nyingi hawa huwa wana ujuzi na maarifa mazuri ya kurasimisha madaraka, wanajiamini, wanafanya utafiti wa kimasoko na kihuduma, hawaogopi kufukuzwa makazini na wanajikita katika kuthamini uwepo wa wateja ama watu wanaowahudumia. 

Kiujumla mahitaji ya dhana ya ujasiriakazi yanajikita katika kuibuka kwa mambo yafuatayo. Uwepo wa makampuni mengi ya kibiashara yanayoshindana kwa mbinu za kisasa pamoja na watu kupoteza imani na mifumo iliyozoeleka na kikiritimba ya kiutawala na kiuongozi katika taasisi mbalimbali (binafsi na serikalini). Vile vile ujasiriakazi unapata mashiko kutokana na kuibuka kwa watu wenye akili na uwezo mkubwa ambao wanaanzisha makampuni kwa kutumia mbinu zilizoibwa kutoka makampuni makongwe. Lakini kubwa kuliko yote ni kiu ya watu kuona kuwa kila eneo la biashara ama huduma linakuwa na ufanisi.

Mfumo wa dunia wa sasa unalazimisha kutekelezwa kwa vitendo dhana ya ujasiriakazi katika maeneo mbalimbali kutokana na sababu mbalimbali. Kwa upande wa makampuni ya kibiashara, inaonekana kuwa ushindani wa kibiashara kwa sasa umekuwa ni mkubwa na uliotete mno kiasi ambacho kila mfanyakazi anahitajika kuwa mbunifu kwa ajili ya kuyasaidia makampuni husika. 

Viongozi wa kisiasa nao wanajikuta katika mbinyo wa kutimiliza dhana hii ya ujasiriakazi katika mifumo wanayoiongoza, kutokana na matakwa ya wapiga kura wao. Wananchi katika miaka ya sasa ambayo inaongozwa na mageuzi ya utandawazi wamekuwa makini mno katika kubaini mahitaji yao halisi. Wapo makini sana na ahadi wanazopewa na viongozi wao, wapo makini na muda, na wapo makini sana na mienendo ya kiutekelezaji wa ahadi mbalimbali zinazotolewa.

Miaka ya sasa wananchi wamechoshwa na ukiritimba uliokuwa kama utamaduni katika ofisi mbalimbali za serikali. Mtindo wa mtu kufuatilia faili mwezi mzima kisa anashinikizwa kutoa rushwa “kiaina” umewachosha sana wananchi. Wengi wa wananchi wamebahatika kupata elimu, wanawasiliana na dunia, wanajifunza huko kwingine mambo yanaendaje, wanahoji, wanataka kujua kwa nini huku kwetu mambo yawe hivi?

Ni jambo lililo dhahiri kabisa kuwa kutekelezwa kwa dhana hii ya ujasiriakazi katika maeneo mengi (hasa ya serikali) kunaweza kuleta shida na kuchukua muda mrefu sana kukamilika. Hata hivyo wadau wa maeneo ya kazi ni vema wakaungana na mtaalamu katika masuala ya ubunifu wa kijasiriakazi, James Brian Quinn, ambaye alibaini vigezo vifuatavyo katika kuwawezesha wafanyakazi kuwa wabunifu katika maeneo ya kazi.

Anataja vigezo hivyo kuwa ni mazingira mazuri ya kufanyia kazi na maono, mtazamo katika masoko yanayohudumiwa na mwisho ni muundo wa taasisi husika. Quinn anasema kuwa makampuni na taasisi zilizofanikiwa zimekuwa na maono kamili na yanayotekelezeka kwa huduma na bidhaa wanazozalisha, wanatengeneza na kutoa huduma kwa kuzingatia mahitaji kamili ya mteja. Kigezo kingine ni kuwa na mibadala mingi katika kushughulikia mambo yahusianayo na majukumu yao. Kwa mfano, kitengo cha elimu katika wilaya ama mkoa kinaweza kuwa na mkakati wa kutatua tatizo la upungufu wa walimu na uhaba wa madarasa.

Ikiwa afisa elimu wa ngazi husika atakuwa ni mjasiriakazi atahakikisha kuwa anakuwa na njia zaidi ya moja kuhakikisha kuwa changamoto hizo zinatatulika kwa ukubwa. Mbali na pengine kusubiri kuletewa tu fungu kutoka serikalini atakuwa na plan B na C ya ama kuitisha harambee ama kutafuta ufadhili. Huyu ndio mjasiriakazi kazini. 

Yapo mambo ya msingi ambayo yanapaswa kufanywa katika maeneo ya kazi ili kufanikisha kusimika ujasiriakazi. Mambo hayo ni kujiwekea malengo ambayo ni lazima yajadiliwe na kukubalika na wafanyakzi wote pamoja na viongozi wao. Kuwepo na mfumo unaoelekeza na kushughulikia mirejesho ili wajasiriakazi wajisikie kutambulika na kuthaminiwa.

Jambo jingine ni kwa viongozi wa maeneo ya kazi kuhakikisha wanasisitiza kuwepo kwa majukumu ya mtu mmoja mmoja. Mara nyingi kutoa majukumu kiujumla huwa kunapunguza uwajibikaji kwa sababu kila mmoja anahisi hahusiki moja kwa moja. Ili kuinua ari na hamasa ya wajasiriakazi kufanya kazi kwa bidii ni lazima kutoa zawadi na tuzo kulingana na ufanisi wa kazi.
0719 127 901,
stepwiseexpert@gmail.com

March 13, 2013

UCHUMI NA BIASHARA: "UCHUMI" NDIO LUGHA YA AFRIKA MASHARIKI

Albert Sanga, Iringa

Wiki mbili zilizopita nimekuwa nikiandika waraka wa kiuchumi kwa wafanyakazi. Kwa ujumla wake waraka huo utakuwa ni mrefu hadi sehemu ya kumi. Kutokana na urefu huo nimejipangia kutouleta kwa mfululizo wa wiki zinazofuatana. Badala yake nitakuwa nikiuleta kwa wiki tofauti tofauti mpaka uishapo mwaka huu.

Leo ninapenda tuperuzi nafasi ya uelewa wetu sisi watanzania linapokuja suala la uchumi katika jumuiya ya Afrika Mashariki. Unapotaja Afrika Mashariki ni kwamba kuna mambo ya msingi ambayo yanaushikilia uhusiano huu. Pamoja na mambo mengine nguzo kuu ya uwepo wa jumuiya hii ni suala la uchumi. Ndio maana tunaongelea soko la pamoja, kuunganisha sarafu zetu, kusafiri kwa mitaji pamoja na rasilimali watu.

Mambo mengine yanayojadiliwa na kushughulikiwa katika ushirikiano huu yanasaidia tu kuboresha lengo kuu la msingi; ambalo ni kuboresha uchumi wa ukanda huu. Kwa tafsiri ya mkato ni kuwa lugha ya Afrika Mashariki ni uchumi. Ili kunufaika na jumuiya hii ni lazima kuijua lugha hii, ni lazima kuyajua matendo ya kiuchumi, ni lazima kuelewa mwenendo wa kiuchumi na ni lazima kutambua nafasi ya mtu mmoja mmoja katika uchumi.

Wakinga tuna msemo mmoja usemao, “Kama wewe sio mchawi, hakikisha unamfahamu mganga mzuri”. Si lazima uwe mjuzi ama mtaalamu wa mambo ya uchumi na lugha za uchumi wa darasani ili kuijua lugha ya Afrika Mashariki; bali unaweza kujifunza na kujizoesha kutoka kwa ‘waganga’(wataalamu) na baadae nawe ukawa ‘mchawi’ (mtumiaji).

Je, watanzania tunaijua kwa kiasi gani lugha inayotumika Afrika Mashariki? Je, tunaelewa maana na matendo ya kufanya tunaposikia viashiria vya masoko ya hisa, masoko ya mitaji, sarafu ya pamoja, ushirikiano wa kodi na ushuru au tunapoambiwa mtiririko wa rasilimali watu? Kwa bahati mbaya sana ni kuwa kutojua lugha hizi hazitoi msamaha wa kuhurumiwa linapokuja suala la utekaji wa fursa zilizopo kwenye jumuiya hii.

Hebu tuangalie baadhi ya mifano michache ya lugha ya Afrika Mashariki. Unaposikia masoko ya mitaji na hisa kichwani kwako ni lazima kuje maneno kama DSE (Dar es Salaam Stock Exchange) , USE (Uganda Stock Exchange) na NSE (Nairobi Securities Exchange). Haya ni masoko ambayo kunatokea ununuzi wa hisa na ubadilishanaji wa mitaji pale.

Hapo kuna makampuni ambayo yanapeleka sehemu yake kuwa miliki ya umma hivyo unaweza kununua ama kuuza sehemu za makampuni hayo. Kujua kuhusu DSE, NSE, na USE hakuhitaji mpaka uwe unamiliki hisa ama mtaji pale isipokua mwenendo wake unaathiri sana uchumi wa eneo hili na hivyo kuathiri ustawi wako binafsi kiuchumi.

Nikisema habari za hisa na mitaji mtu anaweza kudhani ninaongelea masuala ya kitaalamu sana. Kumbuka kua ninaongelea lugha ya Afrika Mashariki. Namna makampuni yanavyojiandikisha na kuuza mitaji kwenye masoko ya hisa na mitaji kunaonesha mtiririko na mwelekeo wa mitaji katika ukanda mzima.

Nasi tunajua kua ulipo mzoga ndipo wakutanikapo tai. Tai wanajuaje kua sehemu Fulani kuna mzoga? Jibu ni rahisi, wanatumia harufu kutambua. Je, unajuaje kua Uganda ama Rwanda kuna fursa za kuwekeza?

Ni kwa kuangalia mwenendo wa mitaji na hisa kama moja ya kiashiria kati ya vingi vilivyopo. Ubaya ni kwamba hata kama wewe usipoisikiliza harufu ya “mzoga wa uwekezaji” wenzako kutoka nchi zingine za Jumuiya wataisikiliza harufu iliyopo hapa Tanzania nao watakusanyika.

Ninapoongelea habari za DSE, USE na NSE naelewa kuwa si rahisi sana kwa wengi kuelewa fursa zilizopo ndani yake pengine kutokana na historia ya uchumi na mazoea yetu. Wenzetu Kenye NSE ilianza (japo sio rasmi) mwaka 1954 wakati sisi DSE ilianza mwaka 1996.

Wanzetu wana uzoefu mkubwa na lugha hii wameizoea kwa kiasi kikubwa. Pale NSE makampuni yaliyojiandikisha ni zaidi ya 50 wakati hapa kwetu DSE kuna makampuni pungufu ya 20 tena mengine yakiwa ni yale yale ya kule Kenya (Cross listing).

Kwa upande wa Uganda hawana tofauti na sisi kwa maana ya kuanza, kwa ni USE ilianza 1997 lakini spidi yao ya kuijua lugha hii ni kubwa mno. Mwaka 2010 USE ilikua ni kinara wa masoko yote ya hisa Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa kutumia kipimo cha ALSI (All Shares Index) ikiwa na mrejesho wa faida ya asilimia 74% kwa hisa zinazonunuliwa na kuuzwa.

Sina lengo la kukupitisha porini katika takwimu za kitaalamu lakini kuna kitu nataka tujifunze; Kenya walitangulia miaka mingi, Uganda ni wapya kama sisi lakini wanajifunza kwa kasi ya jabu. Wenzetu walishatangulia na wengine wanakimbia lakini sisi tunazinduka polepole mno.

Nikiri wazi kuwa mambo kama haya ya hisa na mitaji kiasili yaliibuka kutokana na ubepari, lakini kwa kua tumeamua “kuchanganyika” hatuna ujanja zaidi ya kuungana nao. Kumbuka kua, “Kama wewe sio mchawi hakikisha unawajua waganga wazuri”, hatuna ujanja inatakiwa tujifunze na kuizoelea lugha hii ili tuweze kuelewana na wenzetu wa hapa ‘Jumuiyani’

Katika robo ya mwaka jana makampuni mengi ya umma na binafsi katika nchi zote tano za Afrika Mashariki yameendelea kutoa ripoti zao za kifedha na kiutendaji kwa mwaka ulioishia Desemba, 2012. Hapa napo tunaweza kuitathmini hali yetu tuliyonayo katika lugha ya Afrika Mashariki kwa kuangalia namna tunavyozipokea ripoti hizo.

Nianze na namna jirani zetu Kenya wanavyozipokea ripoti hizo. Wakati makampuni 20 makubwa (yaliyopo kwenye 20 Shares Index) yakiachia ripoti zao nchini Kenya; kulikua na  gumzo mitaani kila mmoja akihaha kuzifuatilia, kuzisoma na kuzitafsiri. Wanahisa na wasio wanahisa wanataka kujua kampuni gani imefanya vipi, ipi imeizidi ipi, ipi ina fursa na gawio zuri kwa kuwekeza, ipi ina mikakati gani ya muda ujao na mengine mengi.

Gazeti moja la nchini Kenye lilipiga picha inayoonesha watoto wa sekondari katika mji wa Naivasha wakisoma ripoti ya mojawapo ya benki za biashara nchini Kenya. Walipoulizwa watoto hao mmoja wao alijibu hivi, “Mama ana hisa kwenye benki hii nataka nijue mwenendo wake”. Hapo ni Kenya!hadi watoto wa shule za sekondari wanaongea lugha ya Afrika Mashariki!

Hali ni tete kwa Tanzania kwa sababu ripoti za makampuni ya ndani ama ya wawekezaji huwa hazipokelewi kwa hamasa yeyote. Kwanza ni wachache ambao wanafuatilia ripoti hizo na achilia mbali uwezo wa kutafsiri maana na athari za ripoti hizo kwa Afrika Mashariki na watu wake.

Kule Rwanda na Burundi wenzetu ndio kwanza wanajenga upya nchi zao; hivyo sio rahisi sana kutoa hitimisho la moja kwa moja kuhusu hisia zao katika lugha ya Afrika Mashariki kiuchumi; lakini kiu yao ya kuinuka kiuchumi na kijamii inaonesha namna ambavyo wanaweza kutupita.

Unaposoma ripoti za makampuni haya (Financial Statements) kuna ishara zinatoa ikiwemo, “Nenda katafute ajira sehemu fulani”, “Nenda kawekeze kitu fulani mahali fulani”, “Ondoka mahali fulani kwa sababu pameharibika”. nakadhalika. Kwa kutozijua lugha hizi tunabaki tumeduwaa tusijue cha kufanya wala kwa kuelekea. Kwa kua wenzetu wanaelewa lugha na matendo ya Ki-Afrika Mashariki ni rahisi na itaendelea kuwawea rahisi kunufaika na lugha hii.

Tatizo letu watanzania wengi tunatumia malalamishi kama silaha ya kujiokoa na hatari za Afrika Mashariki. Juhudi zetu katika kuteka fursa za jumuiya hii zimeota matege na tumekua na mtazamo mdogo mno kuhusu mambo tunayotakiwa kufanya.

Kwa mfano; kitendo cha kukazana kujifunza Kiingereza ama kukazana kununua ardhi kwa ajili ya fursa za Afrika Mashariki sio kibaya lakini ni mtazamo mdogo sana. Tukiijua lugha ya Afrika Mashariki kiuchumi; tutaona na kuoneshwa mambo mengi sana yatupasayo ndani ya Jumuiya hii.

Kwa leo nikomee hapa, lakini natarajia kuendelea na chambuzi mbalimbali kuhusu biashara, ujasiriamali na uchumi katika mtazamo wa ki-Afrika Mashariki huko mbeleni.

Watanzania tunahitaji ushindi wa kiuchumi Afrika Mashariki!



February 12, 2013

BIASHARA NA UCHUMI: UNAHITAJI 'GIA' YA UVUMILIVU KUMUDU BIASHARA



Albert Sanga, Iringa
Makala haya ninayaandika leo ikiwa ni baada ya kumtembelea Bw. Frank Mwaisumbe nyumbani kwake; jumapili mbili zilizopita na kubadilishana nae mawazo. Bw. Mwaisumbe ni mfanyabiashara aliyepo mjini Iringa anaemiliki kampuni inayohusika na uwakala wa safari za Anga, iitwayo Getterland Company Limited na pia ni mmoja ya waasisi wa shirika la Mindset Empowerment linaloendesha mashindano ya mbio za Ruaha Marathon.

Nilimfahamu Bw. Mwaisumbe zamani kidogo na kuna kitu cha kusisimua hapa; kwa sababu ni mwalimu aliyenifundisha kozi ya masoko nikiwa chuo kikuu Tumaini Iringa. Wiki iliyopita mtakumbuka nilieleza namna wasomi wetu (wahadhiri, maprofesa na madaktari wa biashara) wanavyokwama kuzalisha wafanyabiashara halisi; kwa sababu wanafundisha mambo ambayo wenyewe “hawayajui kwa vitendo”.

Huyu Bw. Mwaisumbe ni mmoja ya wahadhiri ambao walinipa hamasa kubwa sana kibiashara nikiwa chuo kikuu; kwa sababu alikuwa akifundisha “biashara” halisi kwa sababu ni mfanyabiashara aliyefanya biashara nyingi sana tangu kitambo. Vyuo vyetu nchini vinawahitaji watu wa jamii ya Bw. Mwaisumbe katika kuwasaidia wahitimu wetu kujiajiri badala ya kulilia ajira ambazo “hazipo”

Ninashirikiana kwa ukaribu sana na Bw. Mwaisumbe zaidi sana katika shirika lake la Mindset Empowerment; ambapo mimi ni Mratibu (Coordinator) wa shirika hili. Katika kushirikiana huku kuna mambo mengi sana kuhusu uzoefu kibiashara ambayo nimekuwa najifunza kutoka kwake.
Jumapili hiyo niliyomtembelea tulitumia muda mwingi kujadili mipenyo, staili, mbinu na mambo yanayosababisha wafanyabiashara mbalimbali duniani kufanikiwa. Nilijifunza mengi sana katika mazungumzo yetu haya na nikakumbuka visa vingi vilivyowahi kunipata katika harakati zangu kibiashara.
Katika kujadili tulibaini kuwa hakuna mfanyabiashara yeyote duniani anaesimama mara moja kirahisi. Kila mfanyabiashara aliyefanikiwa ukimfuatilia historia yake atakueleza namna alivyoanguka-anguka na kusimama, namna alivyojaribu mambo mengi lakini akafanikiwa katika machache ama katika moja bila kusahau namna alivyopokea upinzani mkali katika kufanikisha hilo unaloliona limefanikiwa.

Binafsi ninakumbuka mtaji wangu wa kwanza niliupata (kwa jasho langu mwenyewe bila kupewa na mtu) nikiwa na miaka 19 kwa kuchuuza vitunguu kutoka pale Mang’ula Karatu na kuvipeleka Arusha mjini. Ilikuwa ni biashara niliyoipatia kweli kweli kiasi kwamba nikaweka malengo ya kuanzisha chuo cha mafunzo ya kompyuta na biashara.

Ndani ya mwaka mmoja nilifanikisha lengo langu hilo kwa kufungua chuo hicho kule wilayani Mufindi.  Nakumbuka thamani ya kile chuo ilikuwa takribani milioni ishirini. Nilijiona niliyefanikiwa na kila nilikokuwa ninapita nilikuwa ninapokea heshima na pongezi za mafanikio hayo hasa ikizingatiwa kuwa nilikuwa nimezikamata “milioni” nikingali mdogo wa miaka 20 tu tena nikiwa ndio kwanza nimehitimu kidato cha sita.

Ukweli ni kwamba saa niliyodhani kuwa “nime-win” kumbe ndio saa ambayo nilikuwa naelekea kuanguka. Ile biashara ilianguka yote; ndani ya miezi miwili tu nikawa sina kitu! Kufilisika kwangu kulitokana na mambo mawili. Mosi; wafanyakazi niliowaajiri kuendesha chuo walijigeuza miungu watu, wakaanza kuwanyanyasa wanafunzi na kuzembea kufundisha. Nilikuja kupewa taarifa mwishoni mambo yakiwa yameharibika kabisa kuambiwa kuwa kati ya wanafunzi 104 waliokuwa chuoni wamebaki wanafunzi nane tu!

Nilichanganyikawa na nikaenda haraka sana kuwatimua kazi, lakini nilishakuwa nimechelewa na mambo yalikuwa yameshaharibika. Pili; kulitokea shoti ya umeme (kwa uzembe wao) na ukaunguza sehemu kubwa ya vifaa vya chuo kile zikiwemo kompyuta na vifaa vingine. Sikuwa na ujanja zaidi ya kukifunga kile chuo na kukubali matokeo ya kufilisika.

Leo hii ninapojikumbusha kuhusu biashara ile namtafakari mwandishi aitwaye Mchungaji Daktari Robert Schuller aliyeandika kitabu kiitwacho, “Success is Never Final Failure is Never Ending”. (Kufanikiwa sio kikomo na kushindwa sio mwisho). Anachomaanisha mwandishi huyu ni kuwa ukifanikiwa usijisahau na ukianguka usikate tama.

Ukweli ni kwamba kwenye biashara kuna mapito mengi sana kiasi ambacho mfanyabiashara unahitaji uvumilivu mkubwa mno kuendelea. Biashara sio lelemama! Unaweza kutumia miaka mingi sana katika kujenga biashara zako na kukusanya mali; lakini ukaja kupoteza kila kitu ndani ya dakika chache. Huhitaji kukata tamaa, unahitaji uvumilivu na kuanza upya. Huo ndio ujasiriamali na sifa ya mjasiriamali ni kutokukata tamaa.
Unadhani mchezo umeishia hapo? La hasha! Sikukata tamaa, nilisimama na kuanza kujikongoja tena; safari hii nikaamua kufanya biashara ya kukusanya na kuuza alizeti kule wilayani Njombe katika maeneo ya Irembula. Kama kawaida; si rahisi kufanya biashara peke yako; ni lazima uwe na watu. Hata huko kwenye alizeti nilikuwa na watu niliowaamini kunikusanyia na kunitunzia.

Mwanzoni nilienda vizuri; nikajisemea moyoni; loo! Biashara si ndio hii? Kumbe nilikuwa nimepotea kwani mkasa mwingine ukanitokea. Nikiwa nimekopa fedha kutoka kwa watu na kukusanya alizeti kwa wingi huku nikijua saa ya kuuza nakuwa milionea; nikadhulumiwa mchana kweupe! Yule nilipotunza alizeti akaauza alizeti magunia yote kisha akakimbia na fedha zote na hadi leo ninapoandika makala hii ikiwa imepita miaka kadhaa sifahamu alipo.

Huu ukawa ni msiba mwingine kibiashara kwangu. Tena ni bora angekuwa alikimbia na mtaji wangu pekee; lakini aliondoka na hela hata nilizokopa; hii ina maana nilipoteza mtaji wote na nikabakiwa na madeni. Hii ndio biashara, sikukata tamaa ndio maana hadi leo “nimekomaa” na biashara. Kimsingi sina miaka mingi kiumri na wala sina miaka mingi sana katika biashara, lakini kuna visa vingi mno vya kushindwa na kufanikiwa vilivyonitokea hadi sasa; kiasi kwamba nikisema nivilete vyote gazeti zima halitatosha kwa juma moja.

Hata hivyo; katika mikasa yangu miwili niliyoileta hapo juu kuna mambo machache napenda uyajue ambayo Bw. Mwaisumbe amenisaidia sana kuyajua. Mosi unapokuwa katika biashara unatakiwa uwe na imani isiyoteteleka ya kuwa kuna siku utafanikiwa. Inawezekana ukawa unafanya biashara lakini haujui “utatoka” lini.

 Inawezekana umeshapata hasara nyingi mno katika biashara zako; lakini kama ukibaki na imani hii hakika ipo siku utafanikiwa tu. Bw. Mwaisumbe huwa anapenda kusema hivi “Mtu aliyeanguka-anguka sana katika ujasiriamali, siku akiinuka, hataanguka tena. Na mtu anaeanguka na kusimama hahofii kuanguka kesho kwa sababu anajua ataamka tu”

Pili; asilimia kubwa ya sisi wajasiriamali tunaangushwa sana na watu wengine, ediha tunaowaamini ama tunaowaajili ama tunaoamua kupanda nao tunapopanda kibiashara. Pamoja na uweli huu; haimaanishi kuwa usiwaamini watu; la hasha! Jambo la kufanya ni kuhakikisha unajitahidi kadiri uwezavyo kutafuta, kushirikiana na kuajiri watu sahihi katika ujasiriamali wako. Itakumbukwa kuwa nimewahi kuandika kupitia gazeti makala yenye kichwa; “Mjasiriamali na Sayansi ya kuajiri wafanyakazi”

Tatu; unapofanya ujasiriamali ama kama unatamani kuingia katika ujasiriamali hutakiwi kuogopa kupoteza mtaji ama hatua uliyonayo. Kitu cha thamani katika ujasiriamali sio mali ama fedha unazofanikiwa kuzipata; bali ni “akili ya fedha (financial IQ), kujiamini na uzoefu unaoupata kila unapofanya biashara. Ni vema mjasiriamali kujenga ujasiri na kujiamini (spirit) kiasi kwamba ujisemee kuwa “hata kama nikipoteza kila kitu nilichonacho leo, ninaweza kurudisha na zaidi ya nilivyokuwa navyo”.

Niandikie: stepwiseexpert@gmail.com;  0719 127 901

December 19, 2012

HALI YA WAVUVI NA UVUVI KATIKA ZIWA NYASA WILAYANI NYASA

Mvuvi akiwa na zana zake za kazi. 
PICHA: kwa hisani ya kaka Francis Godwin

UHABA wa samaki ziwa Nyasa upande wa Tanzania unaochangiwa na vifaa duni vya uvuvi umepelekea baadhi ya wanaume wa tarafa ya Mwambao wilaya ya Ludewa mkoani Iringa kutelekeza familia na kwenda nchini Malawi kufanya shughuli za uvuvi kama njia ya kukwepa changamoto za uchumi zinazoendelea kuwa kikwazo katika wilaya hiyo.
Uchumi wa wananchi wa tarafa yaMwambao ambao ulikuwa ukitokana na ajira ya uvuvi kwenye ziwa Nyasa nao umezidi kuporomoka kwa kasi kubwa na kupelekea hata biashara za wananchi wa maeneo hayo ambazo zilianzishwa kutokana na wingi wa wageni waliokuwa wakifika kujumua samaki kwenye ziwa hilo pia kuathirika kwa kiasi kikubwa.
Kama inavyofahamika kuwa uvuvi wa samaki kwa wananchi wa tarafa ya Mwambao wilayani Ludewa ndio shughuli kubwa ya kiuchumi ambayo imekuwa ikitegemewa na karibu robo tatu ya wakazi wa tarafa hii ya Mwambao na ndio shughuli iliyopelekea tarafa hiyo kuwa na mzunguko mkubwa wa fedha hasa kipindi cha nyuma japo kwa sasa imeanza kubaki historia pekee. 
Bonyeza kiungo;    SOMA ZAIDI HAPA

December 18, 2012

SASA UNA HAKI YA KUMILIKI GARI!




Je, unahitaji kununua gari la kutembelea, gari la abiria ama la mizigo? Nyaluke Motors, biashara tanzu ya Anesa Co.,Ltd; tunakupa jibu zuri la hitaji lako. Sasa tunaagiza na kuuza magari aina mbalimbali (used cars) kutoka Japan. Tuna utaratibu na mfumo ambao haujawahi kuwepo Tanzania. Unachohitaji kufanya ni kuchagua gari ulipendalo ama kutuarifu; kisha sisi tutaliagiza na kukuletea mahali popote ulipo Tanzania.
Gharama zote utatulipa baada ya kukabidhiwa gari lako. Kwa kununua gari kupitia Nyaluke Motors utaweza kupata unafuu wa hadi milioni 5 ukilinganisha na bei zilizopo katika showrooms zote nchini. Chagua gari lolote; Nissan Serena, Nadia, Xtrail, Prado, Scania, Fuso, n.k: kisha sisi tutatimiza ndoto yako kwa bei nafuu sana na utaratibu rahisi.
Pia kwa kupitia mpango rafiki ambapo mteja anaweza kulipia gari kwa awamu; akiwa anaendesha gari lake. Tunapatikana: Iringa-Mjini na Kilombero-Morogoro.
Wasiliana nasi kupitia: stepwiseexpert@gmail.com. Haijawahi kutokea Tanzania; ununuzi wa magari kurahisishwa namna hii. Changamka sasa ununue na kumiliki gari lako mapema. Nyaluke Motors: tunaamini kuwa; "KUMILIKI GARI NI DEMOKRASIA YA KILA MTANZANIA".