February 12, 2013

BIASHARA NA UCHUMI: UNAHITAJI 'GIA' YA UVUMILIVU KUMUDU BIASHARA



Albert Sanga, Iringa
Makala haya ninayaandika leo ikiwa ni baada ya kumtembelea Bw. Frank Mwaisumbe nyumbani kwake; jumapili mbili zilizopita na kubadilishana nae mawazo. Bw. Mwaisumbe ni mfanyabiashara aliyepo mjini Iringa anaemiliki kampuni inayohusika na uwakala wa safari za Anga, iitwayo Getterland Company Limited na pia ni mmoja ya waasisi wa shirika la Mindset Empowerment linaloendesha mashindano ya mbio za Ruaha Marathon.

Nilimfahamu Bw. Mwaisumbe zamani kidogo na kuna kitu cha kusisimua hapa; kwa sababu ni mwalimu aliyenifundisha kozi ya masoko nikiwa chuo kikuu Tumaini Iringa. Wiki iliyopita mtakumbuka nilieleza namna wasomi wetu (wahadhiri, maprofesa na madaktari wa biashara) wanavyokwama kuzalisha wafanyabiashara halisi; kwa sababu wanafundisha mambo ambayo wenyewe “hawayajui kwa vitendo”.

Huyu Bw. Mwaisumbe ni mmoja ya wahadhiri ambao walinipa hamasa kubwa sana kibiashara nikiwa chuo kikuu; kwa sababu alikuwa akifundisha “biashara” halisi kwa sababu ni mfanyabiashara aliyefanya biashara nyingi sana tangu kitambo. Vyuo vyetu nchini vinawahitaji watu wa jamii ya Bw. Mwaisumbe katika kuwasaidia wahitimu wetu kujiajiri badala ya kulilia ajira ambazo “hazipo”

Ninashirikiana kwa ukaribu sana na Bw. Mwaisumbe zaidi sana katika shirika lake la Mindset Empowerment; ambapo mimi ni Mratibu (Coordinator) wa shirika hili. Katika kushirikiana huku kuna mambo mengi sana kuhusu uzoefu kibiashara ambayo nimekuwa najifunza kutoka kwake.
Jumapili hiyo niliyomtembelea tulitumia muda mwingi kujadili mipenyo, staili, mbinu na mambo yanayosababisha wafanyabiashara mbalimbali duniani kufanikiwa. Nilijifunza mengi sana katika mazungumzo yetu haya na nikakumbuka visa vingi vilivyowahi kunipata katika harakati zangu kibiashara.
Katika kujadili tulibaini kuwa hakuna mfanyabiashara yeyote duniani anaesimama mara moja kirahisi. Kila mfanyabiashara aliyefanikiwa ukimfuatilia historia yake atakueleza namna alivyoanguka-anguka na kusimama, namna alivyojaribu mambo mengi lakini akafanikiwa katika machache ama katika moja bila kusahau namna alivyopokea upinzani mkali katika kufanikisha hilo unaloliona limefanikiwa.

Binafsi ninakumbuka mtaji wangu wa kwanza niliupata (kwa jasho langu mwenyewe bila kupewa na mtu) nikiwa na miaka 19 kwa kuchuuza vitunguu kutoka pale Mang’ula Karatu na kuvipeleka Arusha mjini. Ilikuwa ni biashara niliyoipatia kweli kweli kiasi kwamba nikaweka malengo ya kuanzisha chuo cha mafunzo ya kompyuta na biashara.

Ndani ya mwaka mmoja nilifanikisha lengo langu hilo kwa kufungua chuo hicho kule wilayani Mufindi.  Nakumbuka thamani ya kile chuo ilikuwa takribani milioni ishirini. Nilijiona niliyefanikiwa na kila nilikokuwa ninapita nilikuwa ninapokea heshima na pongezi za mafanikio hayo hasa ikizingatiwa kuwa nilikuwa nimezikamata “milioni” nikingali mdogo wa miaka 20 tu tena nikiwa ndio kwanza nimehitimu kidato cha sita.

Ukweli ni kwamba saa niliyodhani kuwa “nime-win” kumbe ndio saa ambayo nilikuwa naelekea kuanguka. Ile biashara ilianguka yote; ndani ya miezi miwili tu nikawa sina kitu! Kufilisika kwangu kulitokana na mambo mawili. Mosi; wafanyakazi niliowaajiri kuendesha chuo walijigeuza miungu watu, wakaanza kuwanyanyasa wanafunzi na kuzembea kufundisha. Nilikuja kupewa taarifa mwishoni mambo yakiwa yameharibika kabisa kuambiwa kuwa kati ya wanafunzi 104 waliokuwa chuoni wamebaki wanafunzi nane tu!

Nilichanganyikawa na nikaenda haraka sana kuwatimua kazi, lakini nilishakuwa nimechelewa na mambo yalikuwa yameshaharibika. Pili; kulitokea shoti ya umeme (kwa uzembe wao) na ukaunguza sehemu kubwa ya vifaa vya chuo kile zikiwemo kompyuta na vifaa vingine. Sikuwa na ujanja zaidi ya kukifunga kile chuo na kukubali matokeo ya kufilisika.

Leo hii ninapojikumbusha kuhusu biashara ile namtafakari mwandishi aitwaye Mchungaji Daktari Robert Schuller aliyeandika kitabu kiitwacho, “Success is Never Final Failure is Never Ending”. (Kufanikiwa sio kikomo na kushindwa sio mwisho). Anachomaanisha mwandishi huyu ni kuwa ukifanikiwa usijisahau na ukianguka usikate tama.

Ukweli ni kwamba kwenye biashara kuna mapito mengi sana kiasi ambacho mfanyabiashara unahitaji uvumilivu mkubwa mno kuendelea. Biashara sio lelemama! Unaweza kutumia miaka mingi sana katika kujenga biashara zako na kukusanya mali; lakini ukaja kupoteza kila kitu ndani ya dakika chache. Huhitaji kukata tamaa, unahitaji uvumilivu na kuanza upya. Huo ndio ujasiriamali na sifa ya mjasiriamali ni kutokukata tamaa.
Unadhani mchezo umeishia hapo? La hasha! Sikukata tamaa, nilisimama na kuanza kujikongoja tena; safari hii nikaamua kufanya biashara ya kukusanya na kuuza alizeti kule wilayani Njombe katika maeneo ya Irembula. Kama kawaida; si rahisi kufanya biashara peke yako; ni lazima uwe na watu. Hata huko kwenye alizeti nilikuwa na watu niliowaamini kunikusanyia na kunitunzia.

Mwanzoni nilienda vizuri; nikajisemea moyoni; loo! Biashara si ndio hii? Kumbe nilikuwa nimepotea kwani mkasa mwingine ukanitokea. Nikiwa nimekopa fedha kutoka kwa watu na kukusanya alizeti kwa wingi huku nikijua saa ya kuuza nakuwa milionea; nikadhulumiwa mchana kweupe! Yule nilipotunza alizeti akaauza alizeti magunia yote kisha akakimbia na fedha zote na hadi leo ninapoandika makala hii ikiwa imepita miaka kadhaa sifahamu alipo.

Huu ukawa ni msiba mwingine kibiashara kwangu. Tena ni bora angekuwa alikimbia na mtaji wangu pekee; lakini aliondoka na hela hata nilizokopa; hii ina maana nilipoteza mtaji wote na nikabakiwa na madeni. Hii ndio biashara, sikukata tamaa ndio maana hadi leo “nimekomaa” na biashara. Kimsingi sina miaka mingi kiumri na wala sina miaka mingi sana katika biashara, lakini kuna visa vingi mno vya kushindwa na kufanikiwa vilivyonitokea hadi sasa; kiasi kwamba nikisema nivilete vyote gazeti zima halitatosha kwa juma moja.

Hata hivyo; katika mikasa yangu miwili niliyoileta hapo juu kuna mambo machache napenda uyajue ambayo Bw. Mwaisumbe amenisaidia sana kuyajua. Mosi unapokuwa katika biashara unatakiwa uwe na imani isiyoteteleka ya kuwa kuna siku utafanikiwa. Inawezekana ukawa unafanya biashara lakini haujui “utatoka” lini.

 Inawezekana umeshapata hasara nyingi mno katika biashara zako; lakini kama ukibaki na imani hii hakika ipo siku utafanikiwa tu. Bw. Mwaisumbe huwa anapenda kusema hivi “Mtu aliyeanguka-anguka sana katika ujasiriamali, siku akiinuka, hataanguka tena. Na mtu anaeanguka na kusimama hahofii kuanguka kesho kwa sababu anajua ataamka tu”

Pili; asilimia kubwa ya sisi wajasiriamali tunaangushwa sana na watu wengine, ediha tunaowaamini ama tunaowaajili ama tunaoamua kupanda nao tunapopanda kibiashara. Pamoja na uweli huu; haimaanishi kuwa usiwaamini watu; la hasha! Jambo la kufanya ni kuhakikisha unajitahidi kadiri uwezavyo kutafuta, kushirikiana na kuajiri watu sahihi katika ujasiriamali wako. Itakumbukwa kuwa nimewahi kuandika kupitia gazeti makala yenye kichwa; “Mjasiriamali na Sayansi ya kuajiri wafanyakazi”

Tatu; unapofanya ujasiriamali ama kama unatamani kuingia katika ujasiriamali hutakiwi kuogopa kupoteza mtaji ama hatua uliyonayo. Kitu cha thamani katika ujasiriamali sio mali ama fedha unazofanikiwa kuzipata; bali ni “akili ya fedha (financial IQ), kujiamini na uzoefu unaoupata kila unapofanya biashara. Ni vema mjasiriamali kujenga ujasiri na kujiamini (spirit) kiasi kwamba ujisemee kuwa “hata kama nikipoteza kila kitu nilichonacho leo, ninaweza kurudisha na zaidi ya nilivyokuwa navyo”.

Niandikie: stepwiseexpert@gmail.com;  0719 127 901

No comments:

Post a Comment

Maoni yako