February 11, 2013

CHOMBEZO: KILA MTU, MTU, MTU NA HAKUNA MTU



Markus Mpangala
Hii ni hadithi  kuhusu watu wanne waitwao Kila Mtu,Mtu, Mtu na Hakuna Mtu. Kulikuwa na kazi muhimu kufanywa, na Kila Mtu alikuwa na uhakika kila mtu angefanya kazi hiyo, lakini Hakuna Mtu aliyefanya hivyo. Mtu alipata hasira kuhusu hili, kwasababu ilikuwa ni kazi ya  Mtu. Kila Mtu aliwaza kuwa kila Mtu anaweza kufanya hivyo lakini Hakuna Mtu aliyetambua kwamba kila mtu asingefanya hivyo. Na mwisho iliishia Kila Mtu kumlaumu Mtu wakati Hakuna Mtu aliyefanya  chochote ambacho Kila Mtu angeweza kufanya. Mwisho wa hadithi……
Haya sasa tafakari. Je wewe unatumia pesa zako vizuri? Je una madeni mengi? Je wewe huachishwa kazi mara kwa mara? Nini sababu zako za kuachishwa kazi? Au ni kwasababu ya kazi yenyewe au yule aliyekupa kazi? Au ni kwasababu mazoea au tabia fulani ambayo unapaswa kurekebisha?
Ikiwa hutumii vizuri pesa zako mwenyewe, je utaweza kutumia pesa za familia? Je unatazama mambo yote kwa mtazamo mbaya? Tafakari mara nyingine. Jipe nafasi ya kufanya hivyo huku ukijua kuwa kazi inahitaji uelewa, umakini na bidii.  Sote tunajua kazi ni za kila mtu hapa duniani. Hakuna mtu ambaye anatarajia kazi ya mtu itafanywa na mtu mwingine. Kila mtu anajua anahitajika kufanya kazi kwa bidii ili asimtegee mtu au kumtegemea mtu.
Na kila mtu anahitaji kazi ili aishi vema, hakuna mtu asiyehitaji familia bora. Kwahiyo ili kutimiza haya ni lazima ujifahamu. Lakini ujue wajibu wako katika kazi yako. Na ufahamu mipaka ya kazi yako. Fahamu matumizi yako ya kila siku ili usimlaumu mtu kwakuwa hakuna mtu atakayekusaidia. Fahamu bajeti yako kwa siku,juma,mwezi, na mwaka. Lazima ujifahamu kila hatua unayokwenda mbele maishani. Tambua kila mtu anafanikiwa endapo atafuata kanuni za msingi za maisha.
Hakuna mtu anayependa kuona mtu anashindwa kufanya kazi yake bila sababu, kwakuwa tu mtu anategemea kufanya hivyo. Na asipofanya hivyo inakuwa shida na inamfanya mtu awe na hasira dhidi ya kila mtu. Pesa, kazi na maisha ni lazima viwe tofauti ili kuongoza familia yako. Usitegemee mtu ataongoza familia yako. Hakuna mtu atakayewaambia wanao wasome kwa bidii.  
Ukihitaji kazi, basi hakikisha unayo hoja za kusema kwa mtu. Je umekabiliana vipi na waombaji wapya wa kazi? Wangapi wanatimiza wajibu wao katika kazi, maana kila mtu anataka kuona mtu anafanya kazi yake ipasavyo. Je unalisaidiaje taifa kutokana na kazi yako? Unafahamu kuwa kutoangalia mambo kijuu juu inakusaidia kujifahamu na kuongoza vema ofisi yako au kupata kazi mpya?
Unatambua kuwa ndani ya ofisi yako kila mtu anahitaji cheo ulichonacho? Hakika nakuambia hakuna mtu ambaye hataki kuona mtu anaishi vizuri. Kila mtu anajua ni lazima afanye kazi na apendwe na kila mtu. Mtu huona fahari pale anaposifiwa na kila mtu kutokana na kuwajibika katika kazi yake. Kazi ya kila mtu ni mtu kuifanya kazi yake kwa bidii na hakuna mtu ambaye anapenda kuharibu kazi yake.
Kwa hakika ndugu zangu mnatakiwa kuwa waelewe  wa mambo na kila mtu ajue kuwa unaelewa. Mtu mwenye bidii ya kazi na kujifunza mambo hachoki kuwatumikia watu, na kila mtu hupenda kufanyiwa kazi zake vema. Usiwe mtu unayependezwa na mambo yaleyale au kukubaliana kila jambo kwa mtindo na sababu zilezile. Uwe mtu ambaye kila mtu anafahamu kuwa akihitaji ushauri basi atakuwa wa kwanza kuwajibika mbele ya hadhira.
Jipe muda wa kujisomea, fanya tafakari kila unachojisomea. Natambua kila mtu anachoka atokapo kazini, lakini hakuna mtu ambaye anapenda kukaa tu ofisini kwake bila kufanya kazi yoyote. Timiza malengo yako kwa kuwatumia watu. Uwe mtumishi wa kila mtu kulingana na cheo chako au nafasi yako kwa jamii. Kila mtu anahitaji msaada wako wa nasaha na mengineyo, kwani duniani tupo kwaajili yaw engine.
Wengine hawa ni kila mtu ambaye anajua umuhimu wa kuwatumikia. Na hakuna mtu ambaye hajui umuhimu wa hili. Je unadhani kazi ya mtu ni ipi? Na hadithi hii ya kila mtu inakupa funzo lolote? Na inawezekana ndugu yangu umekata tama ya maisha. Lakini tambua kila mtu amepitia kwenye milima na mabonde. Hakuna mtu aliyefika kileleni bila kuanguka.
Kila mtu anayepanda mlima Kilimanjaro kuna mahali aliteleza au kuanguka. Hakuna mtu ambaye amefanikiwa bila kuchoka, lakini unahitaji nidhamu zaidi ya kuchoka kuliko kuendelea kudhani kila mtu anaweza tu kufanikiwa akikaa sebuleni na kuota amefanikiwa.
Unachotakiwa kufanya ni kusema katika kazi za mtu basi wewe ni kila mtu na hakuna mtu anayeweza kuifanya kazi hiyo zaidi yako. Waingereza wanaomsemo wao,  simama uhesabiwe vinginevyo kaa chini usahauliwe. Kwa maneno hayo inamaana hakuna mtu muhimu katika maisha yako zaidi ya wewe. Hebu rudi juu usome falsafa ya leo ya Kila Mtu, Mtu, Mtu na Hakuna Mtu. Halafu jifahamu wewe ni nani kati ya hao wanne.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako