Showing posts with label afrika. Show all posts
Showing posts with label afrika. Show all posts

February 28, 2018

SERIKALI IMESIKIA KILIO CHA WENGI

NA GABRIEL MWANG’ONDA
HATIMAYE serikali imesikia kilio chetu kuhusu Single Customs Territory (SCT), wakati mfumo huu ukianzishwa na kutumika hapa kwetu Tanzania, binafsi nilipinga sana japo yalikuwa ni maazimio ya jumuiya za uchumi za Afrika Mashariki na SDC countries walikuwa ndio wanaanza kuipigia chapuo.
Mfumo huu unahusisha maafisa wa Forodha kutoka nchi jirani kuja kuweka kambi katika bandari yetu ili mtu akisema anaingiza bidhaa na zinaelekea DRC kisha aende kwenye deski la DRC lililopo hapahapa bandarini kwetu na kulipa kodi zote pale Bandari ya Dar es salaam. Kifupi ni kwamba sisi tulikuwa tunasaidia nchi jirani kudhibiti ukusanyaji kodi.
Mfumo huu ulilenga pamoja na mambo mengine kudhubiti wizi mkubwa wa bidhaa zinazokuwa zinanasinishwa kwamba ziko in transit wakati si kweli kwamba ni transit, mara nyingi huishia mikoa ya karibu na Dar es salaam na kurudi sokoni hapa nchini. 

December 02, 2017

FURAHA YA MAZEMBE ILIYOPORWA UWANJA WA NDEGE NA KABILA

NA. HONORIUS MPANGALA 
Rais Joseph Kabila ni mmoja ya marais wa Afrika ambao ni wamashabiki wakubwa wa mchezo Wa soka. Amekuwa akisapoti sana mchezo Wa soka Kwa timu yao ya taifa inayoitwa chui. Wadau wengi wa soka wanakumbukumbu ambayo aliiweka kwa kuwapa zawadi ya magari kila mchezaji na viongozi wote walioshiriki katika michuano ya CHAN iliyofanyika mwaka Jana 2016 nchini Rwanda. 

 Kabila ameonekana mara nyingi sana katika viwanja vya michezo akihudhuria mechi mbalimbali.Hata katika video ya ule wimbo maarufu 'Leopards fimbu na fimbu' ulioimbwa na Felix Wazekwa umemwonyesha rais akikabidhiwa kombe la Chan mwaka 2009 na Nahodha Wa wakati huo Tresor Mputu,ambalo Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo walilichukua baada ya kuwafunga Ghana katika uwanja wa Felix Houpout-Boigny pale Abidjan Nchini Ivory Coast.

November 13, 2017

HEKIMA ZA AFRIKA KATIKA MISEMO.

Kwenye mabano ni sehemu ambayo misemo husemwa.

1. Usiku una masikio. (Masaai)
2. Adui mwenye ufahamu ni bora zaidi kuliko rafiki asiye na ufahamu. (Senegal)
3. Sufuria bora haitoi chakula. (Nigeria)
4. Hata simba, mfalme wa nyika, anajilinda dhidi ya inzi. (Ghana)
5. Kama kitendea kazi chako ni nyundo pekee, kila tatizo kwako ni msumari. (Gambia)

November 04, 2017

TANZANIA YATAJWA KUONGOZA KWA MARADHI YA KIPINDUPINDU


NA MWANDISHI WETU

SHIRIKA la Afya Duniani imeitaja Tanzania kuwa  miongoni mwa nchi kumi kinara kwa watu wake kuugua ugonjwa wa kipindupindu. Mataifa  mengine yaliyotajwa ni pamoja na India ambayo ndio inayoongoza. Nyingine ni Haiti, Jamhuri  ya  Kidemokrasi  ya  Congo, Tanzania, Bangladesh, Uganda,  Msumbiji na Kenya, ambayo ilikumbwa na mlipuko mkubwa wa maradhi hayo kwa nyakati tofauti mwaka huu.

November 03, 2017

UCHAMBUZI WA KITABU: IT CAN'T BE TRUE



KITABU: IT CAN’T BE TRUE
MWANDISHI: JOHN MWAKYUSA
MCHAMBUZI: MARKUS MPANGALA

HII ni mara yangu ya kwanza kusoma riwaya ya mwandishi John R.P. Mwakyusa, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam. Riwaya inaitwa “It Can’t Be True: A Story from Uganda-the Pearl of Africa”, na kuchapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2017 na kampuni ya Partridge Publishing ya India.

November 02, 2017

FURSA: SEMINA YA WANAZUONI CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM


October 17, 2017

UTAMU WA WIMBO WA TAIFA UKO KOMBE LA DUNIA.

NA. HONORIUS MPANGALA
 
ILIKUWA miaka Sita ya Ubabe wa soka barani Afrika kuanzia mwaka 2006 hadi 2012. Kila mpenzi wa soka alimfahamu Hassan Shehata,kila mpenzi wa soka alimfahamu Waile Gomaa. Ilikuwa nyakati za Misri kunyanyasa mataifa mengine ndani ya bara la Afrika. Ilimchukua Kameruni miaka tisa kulipiza manyanyaso aliyopata toka kwa Misri ya kiumeni mwaka 2008 pale Ghana.
Ni Misri ambayo iliipa hasara CAF kuunda kombe lingine la Afcon baada ya kulibeba lile awali Mara nne Mfululizo. Mwaka 2006 fainali zilizoandaliwa na Misri wakikutana na Ivory coast ya Didier Drogba.
KIKOSI CHA MISRI

Fainali ile iliisha kwa matuta na wenyeji kutwa taji. Licha ya kuwa na kikosi ambacho kilikuwa na vijana taklibani Saba wakitoka kikosi cha Al Ahly ambayo ilikuwa moto wa kuotea mbali. Hapa nawazungumzia Mohammed Barakat,Saeed Moward,Essam El Hadary,Ahmed Hassan,Hossam Hassan,Mohammad Mido,Mohammed Aboutrika na wengineo. Ilikuwa ni kikosi kilichojaa vipaji kikiwa na hamasa kubwa kutoka kwa kocha mzawa Hassan Shehata kiliwafanya wapinzani wafikirie Mara mbili zaidi.

October 12, 2014

KWANINI AFRIKA HATUNA AFRICOPHONE AU BANTUPHONE?



Na Markus Mpangala, Dar es salaam

KUNA wakati unaweza kujiuliza utamaduni wa viongozi wetu kuzithamini jumuiya za nje ya Afrika unetokana na nini. Tunaweza kujitetea kwa namna nyingi ikiwemo uchumi duni unaosababisha tukose nguvu ya kitaifa.

Unaweza pia kuorodhesha sababu nyingi mno ambazo zinaweza kutunyima uwezo wa kuwa na jumuiya zinazotambulisha uwezo wa kiafrika kwenye siasa, uchumi, utamaduni na jamii.


Yapo maeneo tumeweza kuyalinda na kuonesha sisi ni waafrika halisi na tunalinda uafrika wetu. Bahati mbaya pia yapo maeneo yanayojenga nguvu na ubora wa Afrika hayajapewa kipaumbele.



Moja ya kazi za Cheik Anta Diop,

Mwanazuoni Cheikh Anta Diop alihubiri sayansi, siasa na utamaduni wa Afrika. Diop alihubiri uafrika kama Marcus Garvey, Malcolm X, na wengineo. Diop alihubiri ubora na nyakati zilizovurugwa katika historia ya mwafrika.

Kwamba Afrika kuna utamaduni, lugha, mazingira, staha na mambo yanayoweza kulibatumbulisha bara hilo kwa Uafrika wao.


Katika bara la Afrika ambalo linatajwa kugunduliwa kwa binadamu wa kwanza kuishi, lina sifa nyingine mbaya zaidi kwamba baadhi ya wakazi wake hawazipendi nchi zao.
Kwamba hawapendi utambulisho wao.

Hawapendi utamaduni wao na ndio maana hujishughulisha kubadilisha wajihi (kujichubua) na mengine yasiyowatambulisha kama waafrika.

Madai haya yamekuwa yakitolewa na wataalamu pamoja na wanahistoria wengi wa Ulaya pamoja na Amerika.
Sababu kubwa inajulikana kuwa waafrika wamejikuta kwenye utegemezi mkubwa wa kiuchumi, kisiasa na kijamii.


Jambo zuri zipo jamii ambazo zinalinda tamaduni zao na zinajali zaidi. Hata hivyo katika Bara la Afrika kuna vituko vingi na kuonesha dhahiiri kutegemea mawazo na fikra za kigeni.
Katika Afrika kuna nchi zipo kwenye Jumuiya ya Madola. Kwamba ni nchi zinazofurahia kutawaliwa na ukoloni wa Uingereza.


Katika Jumuiya ya Madola kuna wanachama wanaokutanishwa kila mara kwenye mikutano yao. Nchi hizo ambazo ni makoloni ya zamani ya Uingereza kwa upande wa siasa.


Upande wa pili kuna Michezo ya Jumuiya ya Madola ambao huwakutanisha mataifa yote yaliyotaliwa na Uingereza. Kwamba mataifa hayo licha ya kupata uhuru wa bendera bado yamekubali kuwa chini ya himaya ya wakoloni.


Safari hii wakoloni wakiwa wanatawala kutoka nchini mwao. Katika maeneo hayo mawili kutoka sehemu moja; waziri mkuu wa Uingereza huendesha vikao na mikutano pamoja na marais wa Afrika hususani nchi zilizotaliwa na Uingereza.


Rais Julius Nyerere na Fidel Castro wa Cuba.

Kwenye michuano ya Jumuiya ya Madola Malkia Elizabeth II wa Uingereza kuwahutubia wanamichezo na wanaoshiriki michezo hiyo wakiwakilisha kutoka mataifa yaliyokuwa chini ya himaya ya ukoloni.


Michuano ya mwaka huu ilifanyika mjini Glasgow nchini Scotland. Malkia anatawala nchi hizo kwa namna nyingine katika michezo ya madola na katika uchumi na siasa kwenye jumuiya hiyo.


Hayo ni mataifa yaliyotawaliwa na Uingereza, kwamba tunajinasibu kupinga ukoloni na kufundisha wanetu kuwa akina Kibanga waliwachapa makonde wakoloni hata wakatokomea.
Kwenye chaguzi mbalimbali ndani ya Umoja wa Afrika, mataifa yaliyotawaliwa na Uingereza yanaweza kujipanga na kutamba kuteteana ikiwemo kupeana nafasi za vyeo na kupigiana upatu kwa wagombea wao.


Mataifa haya ndiyo yanajigamba ni wazungumzaji wa lugha ya kiingereza na yanaitwa kwa kifupi Anglophone.
Tukigeukia upande wa pili tunakutana na mataifa yaliyotaliwa na Ufaransa. Mataifa haya yanajigamba kuwa ni wazungumzaji wa lugha ya Kifaransa, na huitwa Francophone.


Aghalabu kwenye kinyang’anyiro cha uongozi ndani ya Umoja wa Afrika (AU) tunashuhudia mnyukano mkubwa baina ya pande mbili; Anglophone dhidi ya Francophone.


Kwamba wale wenye kundi la Francophone walipiga kampeni kubwa kwa ajili ya Jean Ping ambaye ni mgombea kutoka kambi yao wakati wa kinyang’anyiro cha Ukuu wa Tume ya Umoja wa Afrika.


Mgombea wa Anglophone, Dk. Dlamini Nkosozana-Zuma alimshinda Jean Ping wa kambi ya Francophone, hivyo kuwa mkuu mpya wa Tume ya Umoja wa Afrika.


Kwenye nchi za Francophone, ulimwengu ulishuhudia wakiundiwa jukwaa jingine la Francafrique ambalo lilikuwa mahususi kuziweka pamoja na kujenga uhusiano baina ya nchi za Kiafrika zilizotaliwa na Ufaransa.


Francafrique ni sawa na ilivyokuwa ajenda ya Francophone. Ufaransa haikuishi hapo, iliwahi kumpa mwaliko aliyekuwa Rais wa Tanzania, Benjamin Mkapa kuhudhuria mkutano mkubwa wa kundi la Paris Club.


Kundi hilo linahusisha wachumi wenye nguvu zaidi na wanaotoa misaada ushauri wa kiuchumi na madeni kwa mataifa mbalimbali.


Ureno nao hawajabaki nyuma. Mwaka 1996 nchi zote zilizotawaliwa na Ureno zilijumuishwa kwenye jukwaa lao, Lusophone Africa.


Nchi zinazounda Lusophone Africa ni Angola, Cape Verde, Guinea-Bissau, Msumbiji, na Sao Tome and Principe. Awali nchi hizo ziliunda umoja wao wa ushirikiano unaojulikana kama PALOP (African Countries of Portuguese Official Language).


Hilo lilikuwa kujibinafsisha kwenye himaya ya Ureno sambamba na mkondo wa Anglophone na Francophone.
Katika dhana hii kulikoni bara la Afrika hatuna Bantuphone wala Africophone? Kwamba imekuwaje rais kwa viongozi na wananchi wa Afrika kujitambulisha kwenye Jumuiya za wakoloni wao Anglophone (Uingereza), Francophone (Ufaransa), Lusophone Africa (Ureno)?


Kwa mantiki hiyo lazima tujiulize maswali, inawezekanaje waafrika wakakubali kuwa jumuiya za Bantuphone na Africophone hazifai kwao, badala yake kuzing’ang’ania zile za wakoloni?


Ni kitu gani kinakwamisha kuundwa jumuiya za kiafrika kama Bantuphone na Africophone kuliko kuwekeza akili zetu kwa jumuiya za kikoloni?


Swali hilo linaweza kujibiwa kirahisi mno, kwamba huenda waafrika wanajisikia fahari zaidi kuongozwa na wakoloni licha ya kudai walipambana ili kuwafukuza kwenye ardhi zao.
Wakoloni wanatumia mbinu za jumuiya hizo kama nyenzo ya kuendeleza ukoloni wao kwa mataifa. Sielewi ndugu zangu.


Baruapepe; mawazoni15@gmail.com

© Andunje wa Fikra, 2014

June 24, 2013

RASIMU YA KATIBA MPYA, KUNA MASWALI YANATAKIWA KIJIBIWA


TANZANIA: 
Tumeelekeza nguvu na akili zetu kwenye uchaguzi mkuu 2015. 
Mpaka sasa hatuna mwafaka wa uchaguzi huo kwamba tutumie Katiba ipi, ya zamani ama hii iliyoko kwenye hatua ya Rasimu itakapokamilika. 

Tukumbuke wanachama wa shirikisho la Muungano; Zanzibar na Tanganyika watahitaji kutunga Katiba zao. Zanzibar wanayo Katiba yao, je watakubali kutunga katiba mpya? 

Je, mwanachama mwingine Tanganyika atakubali kuwa yeye ni Tanzania Bara halafu kwa wakati huo huo akiwa mwanachama wa shirikisho akatumia Katiba ya Tanganyika? 

Ni Tanganyika ama Tanzania Bara? Kama wewe unasoma RASIMU YA KATIBA, hakika kuna mengi unapaswa kuyatafakari kwa maslahi ya nchi. 

Nadhani tuitishe uchaguzi mkuu mwaka 2017, tujipange kwa kuwekeza kwenye MUDA kukamilisha zoezi hili, sio jepesi hili, halihitaji 'fasta fasta'.

May 12, 2013

KAMARA KUSUPA: MWAFRIKA ALIKUWA WA KWANZA KUWASILI MAREKANI KABLA YA CHRISTOPHER COLUMBUS

Na Markus Mpangala, Dar es Salaam
HIVI karibuni nilipata fursa ya kumhoji mwandishi wa kitabu cha ‘Kumrudisha Mwafrika kwenye Asili yake: Mradi mgumu kuliko yote,’ Mwinjilisti Kamara Kusupa.
Haya ndiyo mazungumzo yetu ambayo bila shaka yatawanufaisha Watanzania kufahamu nini maana na asili ya Afrika kwa ujumla wake na maisha halisi ya bara letu.
SWALI: Niliwahi kusoma vitabu vyako viwili, “Maisha yangu Gerezani”, baadaye kile cha “Hii ndiyo Tanzania tunayoitaka”. Kuna tofauti gani kati ya vitabu hivyo na hiki cha sasa?
KUSUPA: Tofauti ipo, sababu kile cha kwanza niliongelea maisha ya gerezani na namna vijana wanyonge wanavyoteseka. Wengine wanakosa utetezi na wengine hawana msaada wa kisheria na wapo wanaogandamizwa.
Nikiwa na Mzee Kusupa
Halafu kuna wale wanaosota miaka mingi bila kesi zao kutatuliwa. Kitabu changu cha pili kimeongelea suala la nchi yetu ya Tanzania, kwamba tunataka iweje na iongozwe vipi katika kutafuta katiba mpya. Naizungumzia Tanzania ya wakoloni, baada ya ukoloni, kipindi cha Nyerere na baada ya Nyerere. Halafu nimeongelea hili suala la vyama vingi vya siasa. Lakini kitabu hiki kipya namtazama Mwafrika na matatizo yake yanayomsonga kila kukicha bila ufumbuzi huku akiwa tegemezi. Mwafrika ambaye hajachukua nafasi kuyachukua mazuri ya mababu wa asili yake.
SWALI: Lakini maandiko ya namna hii yako mengi hapa nchini na kote Afrika kwa ujumla kuhusiana na Mwafrika. Wapo Watanzania ambao wameandika vitabu kuelezea matatizo ya Afrika, mfano Dk. Malima Bundara aliandika, “Waafrika ndivyo Tulivyo”. Je, wewe unazungumzia nini kwenye hiki kitabu kipya?
KUSUPA: Nakiri yapo maandiko mengi kuhusiana na Waafrika. Yapo maandishi kama ya akina Cheikh Anta Diop (Senegal), Dk. Elly Kamugisha (Tanzania), Franz Fanon (Algeria), Julius Nyerere, Leopold Senghor (Senegal), Ali Mazrui, Marcus Garvey, Nelson Mandela na wengineo.
Lakini jambo kubwa lililokuwa likijadiliwa ni nani hasa huyu Mwafrika. Lakini wakasahau kuwa Mwafrika huyu ana asili zake, hizo ndizo ninazoongelea kwenye kitabu hicho kipya.
SWALI: Unakubaliana na mahitimisho mengi ya wasomi wa Afrika kuhusu Mwafrika ni nani na anaweza kurudi kwenye asili yake kwa njia gani?
KUSUPA: Wengi wanakubaliana kwamba Mwafrika ni mtu mweusi, hivyo kuwatenga Waarabu, Wahindi, Wazungu na Waberiberi ambao kimsingi nao wamejikuta wakiwa wamezaliwa katika bara ya Afrika hivyo hawawezi kutengwa.
Kwa mfano; msomi Dk. Harrith Ghassany alipata kuandika nini asili ya Afrika. Kwa utafiti wake akaelezea kuwa asili ya Afrika ni kutoka kule Tunisia.
Dk. Harrith alisema hayo kwenye kitabu chake cha “Kwaheri Uhuru, Kwaheri Ukoloni: Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia.” Yote haya yanatuletea swali la msingi Mwafrika huyu ni nani?
Hata hivyo dunia imebadilika na kila kona inatusaidia kujua nini hasa kinachopaswa kusemwa kwa dhati na moyo safi kwa nyakati za sasa na baadaye. Kuna Wazungu wamezaliwa Afrika Kusini, Tanzania na wengine nchi nyingine za Afrika.
Je, hawa watakwenda wapi ikiwa hawajui asili zao au mahali walikoanzia zaidi ya kujikuta wakiwa katika nchi wanazoishi. Ni kama ambavyo Waafrika walioko Ulaya, Amerika na Asia wanavyojiuliza ni namna gani wataweza kurudi Afrika ambako hawajui waanzie wapi.
Ni vigumu leo kumwelezea Jesse Jackson, Mohamed Ali warudi Afrika kutoka Marekani. Ni vigumu vile vile kumweleza Lennox Lewis wa Uingereza arudi barani Afrika.
Ni vigumu kumwambia Danny Jordan wa Afrika Kusini kwamba uchotara wake sio kitu arudi kwenye asili ya makaburu Uholanzi na kwingineko. Au ni vigumu kumwambia Hellen Zille, mwenyekiti wa chama cha upinzani cha Democratic Alliance (D.A) pale Afrika Kusini na gavana wa jimbo la Cape Town, kwamba arudi kwa wazungu wenzake.
SWALI: Unadhani hilo linatokana na uhusiano wa Waafrika na wageni, ndio kiini cha Mwafrika kurudi kwenye asili yake?
KUSUPA: Kwanza niseme hii ni moja ya mabadiliko makubwa ya mipaka ya nchi ambayo imeshindwa kuzuia uhusiano wa wanadamu kutoka nchi moja hadi nyingine au kutoka jamii ya nchi moja kwenda jamii ya nchi nyingine.
Leo Mwafrika anaweza kuzaa na Mchina au Mkorea hivyo ni vigumu mtoto atakayezaliwa kutotambuliwa kuwa Mwafrika, na kuangalia asili. Lakini wapo watu wanaojaribu kujiuliza ni namna gani wanaweza kuwakumbusha Waafrika wenzeo kuwa Mwafrika alikuwa na asili yake.
Hata kwenye dini, Waafrika wanazo. Ukisema Waafrika hawana dini nitakuambia soma maandiko ya Mchungaji Blacid Temple kwenye kitabu chake cha “Bantu Philosophy”, kwa hiyo ushahidi wa asili zetu upo kidini, kisiasa na kiuchumi.
Propaganda iliyohubiriwa kwa nguvu na pia kufundishwa na elimu ya kikoloni ni kwamba Mwafrika ameanza kuwa na dini baada ya ujio wa Waarabu na Wazungu barani Afrika.
Baada ya kazi ni gumzo
Kwa mfano; katika Afrika ya Mashariki, Uislamu uliingizwa katika karne ya nane na wafanyabiashara kutoka Ghuba ya Uajemi (leo tunaita Iran), hao wafanyabiashara wa kiajemi ndio walioitia jina la Dar es Salaam mji maarufu wa Tanzania lenye maana ya mbingu ya amani.
SWALI: Je, ni kweli kwamba kabla ya ujio wa wafanyabiashara wa kiajemi, Waafrika wa eneo hili hawakuwa wakimwabudu Mungu?
JIBU: Narudi kama nilivyoeleza mwanzoni, Waafrika walimjua Mungu wa kweli, walimwabudu na kuishi kulingana na miongozo yake. Ushahidi wa kuonyesha Mwafrika aliabudu Mungu kabla ya ujio wa Uislamu na Ukristo ni uwepo wa majina yanayoendana na masuala ya kiroho na ibada.
Lakini tunapokuja kwenye eneo linalohusu mambo ya kiroho, maneno kama ibada, Nnungu, Mungu, Mulungu, Ngai, Nkoyi, Kyala, Malaika na Banzelu neno kutoka lugha ya Kilingala lenye maana ya viumbe weupe wanaong’ara  ni udhihirisho wa kwamba Mwafrika  alimjua Mungu na alikuwa na mawasiliano naye.
Katika somo hili tunajadili kwa ufupi juu ya Uislamu, Ukristo, Ubuntu na dini ya asili iitwayo Alabba ndani ya kitabu nimeeleza sana hili.
SWALI: Mwafrika haonekani kutajwa kwamba mmoja wa watu waliowahi kuishi au kufika Marekani kabla ya ukoloni. Labda tuseme Latini Amerika yote kusini na kaskazini. Lakini tunashuhudia Waafrika wengi wakiwa huko na baadhi ya mila na desturi zao zinalingana na Waafrika wa bara la Afrika. Kwa nini?
KUSUPA: Kwanza niseme wanaoeneza kuwa Mwafrika hakuishi Marekani kabla ya biashara ya utumwa hawako sahihi, au kule Latini Amerika. Kuna sababu nyingi, lakini kubwa ilianzia kwa Columbus.
Mwafrika alikuwa wa kwanza kuwasili Marekani kabla ya Christopher Columbus, hata ukisoma maandiko yenye ushahidi yaliandikwa na Profesa Ivan Sertima kwenye kitabu chake "THEY CAME BEFORE COLUMBUS". Hizo  'voyage' mbalimbali za Christopher Columbus zimejaa mengi ya kushangaza na kwa nini yanachukuliwa kuwa kama yalivyo au ukweli wenyewe? Waafrika wanayo mengi hayakuandikwa vizuri.
SWALI: Kwa hiyo una maana kwamba ndani ya Kumrudisha Mwafrika kwenye Asili yake: Mradi mgumu kuliko yote umeelezea nyongeza yake na hali halisi ya Mwafrika na asili zake, ukizingatia dhana ya uhai pia?
KUSUPA: Kwanza tunaangalia sisi Waafrika ni nani na asili yetu ikoje, hicho ndio kiini. Dhana ya uhai inakuwa kubwa na inachukua mkondo mkubwa pia, hivyo basi kitabu cha KUMRUDISHA MWAFRIKA KWENYE ASILI YAKE; MRADI MGUMU KULIKO YOTE nimeleta baadhi ya majibu ya maswali ambayo kila mara watu wanajiuliza.
Nimeelezea kuanzia kwenye dini, siasa, utamaduni, na mengine mengi kuhusu Afrika, nimeelezea mengi kwamba kuna makosa kadhaa yanafanyika ni vigumu kuizungumzia Afrika kama wanazuoni Ali Mazrui wanaoitazama Afrika kichotara.
SWALI: Unazungumzia Afrika ya kichotara, una maana gani hasa?
KUSUPA: Hakuna wakati wowote katika historia ya dunia na maisha ya mwanadamu kiujumla, ambapo Afrika imeacha kuhusiana na watu kutoka nje ya bara hili, hivyo nazungumzia Afrika na Wageni kutoka Ulaya, Amerika na Asia. Tangu awali na baada ya Kristo watu kutoka nje wamekuwa wakiingia Afrika kwa sababu moja au nyingine.
Katika mada hii ya Afrika na wageni, tunazungumzia wageni wa aina tatu kutoka nje ya bara la Afrika. Tunajadili juu ya Afrika na wafanyabiashara kutoka mabara mengine ya Asia, Ulaya na Arabuni, Afrika na waeneza dini kutoka nchi za ulaya magharibi na Afrika na Wazungu wa  magharibi waliojifanya wavumbuzi yaani wale wachoraji wa  ramani za kuonyesha mito mikubwa, milima mirefu na maziwa.
Tunajadili juu ya Afrika na tamaduni za kigeni, Afrika na dini za kigeni na mwisho tunajadili juu ya Afrika na tawala za kigeni ikiwa ni pamoja na mifumo inayoendelea kutumika hadi sasa kuongoza maisha ya Waafrika.
Kila jamii imekuwa kwenye asili yake na inakuwa vigumu kurudi kwenye asili yake. Tujiulize je, dini za Waafrika ni zipi? Mfumo wa utawala wa Waafrika ni upi?
Msingi wao na dhana ya uhai vikoje? Uhusiano wao na jamii za nje ukoje? Je, Mwafrika ataepuka dhahama ya mabadiliko ya kijamii duniani? Je, Mwafrika ataweza kurudi katika asili yake?
Nadhani ni moja ya mambo ya kusisimua na hakika yatakuwa na hamasa kwa wasomi mbalimbali na wananchi wengine. Kikubwa tuseme kama kweli tutaweza kurudi kwenye asili yetu au ni mradi mgumu?
SWALI: Katika kitabu chako umegusia suala la muungano wa bara Afrika?
KUSUPA: Hilo nimezungumzia kwa kina. Nimeanza toka kwenye utumwa, ukafuatia ukoloni na baadaye utawala wa chama kimoja au udikteta wa chama kimoja.
Hatimaye Afrika imeletewa utandawazi unaoyafanya mataifa yenye nguvu yawe dikteta wa kudumu wa kuzilazimisha nchi za Afrika kujiendesha sawa na watakavyo wao.
Afrika iligawanywa vipande vipande na kuitwa majina mapya na wakoloni, lakini pia wakoloni hao wakati wanachora na kuweka mipaka yao ya kufikirika, ndipo waafrika tulipogawanywa na kutenganishwa na kupewa utambulisho mpya wa kuitwa Watanganyika, Wakenya, Waganda, Wakongo, Wanyarwanda, Warundi, Warhodesia, Wamozambiki, Wanigeria, Wakameruni, Waghana, Wasenegali, Wamali, Waliberia, Wasealeoni, Wanamibia, Waangola, Wasudan, Wasomalia, Waethiopia n.k.
Wakati wakoloni wanaigawa Afrika na kuweka mipaka yao mipya tofauti na ile mipaka ya asili iliyokuwa inatambuliwa na wenyeji, pia waafrika walitenganishwa na kuumbiwa hisia mpya. Mpaka wa kutenganisha nchi na nchi nyingine uliweza kupita katikati ya eneo moja na kuwafanya watu wa kabila moja au ukoo mmoja kuwa na uraia wa nchi mbili tofauti. Hivyo Afrika lazima iungane.
SWALI: Nashukuru kwa kushirikiana katika fursa hii. Naamini Watanzania watanufaika kutoka katika maandiko yako mazuri ya kitabu chako.
KUSUPA: Karibu wakati mwingine, ninyi vijana mnatakiwa kujua zoezi jipya la Afrika kuwa na mipaka mipya lilimpa Mwafrika hisia mpya na utambulisho mpya. Nitafanya mhadhara UDOM kuelezea hilo Mungu atujalie. Kwa hiyo lazima tujirudishe kwenye asili zetu.
Baruapepe; mwanazuoni27@gmail.com