November 03, 2017

UCHAMBUZI WA KITABU: IT CAN'T BE TRUE



KITABU: IT CAN’T BE TRUE
MWANDISHI: JOHN MWAKYUSA
MCHAMBUZI: MARKUS MPANGALA

HII ni mara yangu ya kwanza kusoma riwaya ya mwandishi John R.P. Mwakyusa, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam. Riwaya inaitwa “It Can’t Be True: A Story from Uganda-the Pearl of Africa”, na kuchapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2017 na kampuni ya Partridge Publishing ya India.


Kitabu hiki kimepewa nambari za usajili 978-1-54-37-0041-1, ambapo kimegawanywa katika sura 13 zilizobeba matukio tofauti yanyomsaidia msomaji kupata picha kamili.

Mandhari ya kitabu hiki ni Tanzania na Uganda. Mwandishi anasimulia mkasa wa Albert Mukasa ambaye akiwa na miaka 10 na mwanafunzi wa shule ya msingi Kyashemeire iliyopo Mbarara nchini Uganga anashuhudia wazazi wake wakiteswa na baadaye kuuawa na askari wa serikali iliyokuwa madarakani.


Huzuni aliyokuwa nayo Albert haielezeki. Maisha yalikuwa shuruba kwake. Akajiunga na kikosi cha waasi akiwa kinda. Alipania kulipa kisasi juu ya watu waliohusika na mauaji ya wazazi. 

Mwandishi anaanza kwa kutusimulia namna Albert Mukasa alivyoshuhudia askari hao baada ya mauaji wakilaumiana kwanini walimuua mama yake Albert.  Mwandishi anasimulia kuwa ghadhabu ya Albert ilichochea kukatisha shule na kujiunge na kikosi cha waasi cha NRA, na baada ya kuchukua madaraka, Albert na askari wengine ambao hawakumaliza shule walipelekwa tena shuleni. 

Mwandishi anaonyesha mabadiliko ya uongozi kati ya awali na ulioingia kwa njia ya mtutu wa bunduki. Kwamba waasi wa NRM walikuja na mipango mizuri ya uongozi na kuituliza Uganda.

Katika sura ya pili Mwandishi anasimulia wasifu na shughuli za Alvani Kasalirwe. Alvin alikuwa wakili mashuhuri akifanya kazi na taasisi mbalimbali akiwemo mwekezaji raia wa Denmark, Karina Kirsten. Hata hivyo likatokea tukio la kushangaza baada ya wakili Alvin kuuawa kwa bomu lililotegwa garini. Ni nani ameshiriki kutega bomu lililomuua Wakili Alvin? Hapo ndipo kazi ya Albert inaanza kuchukua nafasi kwakuwa alikuwa ofisa usalama mwenye jukumu la kupeleleza mkasa huo. 

Katika hekaheka za kupeleleza mkasa kifo cha Alvin anajikuta akiangukia mikononi mwa wanawake wawili wenye sifa tofauti; Sharon Erepu na Esther Atukunda. 

Mwandishi anaonyesha matukio matatu tofauti yanayowahusisha wanawake hawa. Esther alikuwa mhudumu wa Baa, wakati Sharon binti mrembo alikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu. Tukio la kwanza ni lile la Albert kukutana na Esther aktika Baa akiwa njiani kuelekea kwenye maziko ya wakili Alvin Kasalirwe kama sehemu ya upelelezi wa mauaji yake. 

Mazungumzo ya Esther na Albert yanajenga taswira ya kipekee ambayo msomaji anavutiwa namna wamandishi alivyopangilia mkasa wenyewe. Baadaye tunadokezwa kuwa Esther Atukunda alikuwa shushushu anayejihusisha kukusanya taarifa za matukio mbalimbali mitaani. Hivyo kukutana na ‘mpelelezi’ Albert Mukasa. 

Tukio la pili ni lile la Sharon Erepu kukutana na mpelekezi Albert kupitia kaka yake Lawrence Okanya ambaye alisoma naye alipokwua chuoni (King’s College, Budo). Sharon alikuwa mchumba wa wakili Alvin, kwahiyo Lawrence alikuwa shemeji ya Alvin. 

Mwandishi anatuonyesha ‘lifti’ aliyotoa Albert wka Lawrence na Sharon inampa mwangaza mpya kumfahamu muuaji wa wakili Alvin. Tukio la tatu linamhusu Sharon Erepu ambaye alipanga kumtambulisha mchumba wake, Paul Emmanuel Komba, mtoto wa askari wa zamani wa JWTZ aliyepigana vita vya Uganda na baadaye kutoa maunzo kwa askari wapya walioachwa madrakani nchini humo. 

Inagundulika kuwa Paul Komba ni binamu wa Sharon. Paul ni mtoto wa sajenti mstaafu Emmanuel Komba aliyezaa na mwanamke wa Uganda, Ajaro ambaye ni shangazi wa Sharon. Upelelezi unaendelea hadi kubainika kuwa muuaji wa Alvin ni Lawrence Okanya. Lawrence alitumiwa na mwekezaji raia wa Denmark,Karina Kirsten. Wasifu wa Karina Kirsten umechorwa kama mchungaji ambaye alikuja kueneza neno la Mungu na rafiki yake Mchungaji Sebina. 

Nyuma ya pazia wawili hawa walipanga mauaji ya wakili Alvin kwakuwa alikuwa mwanaharakati wa mazingira kwa upande mmoja na mwingine kama wakili wao. Alvin alipinga ajira za watpto migodini.

Dhamira kuu zinazopatikana katika kitabu hiki; madhara ya utawala mbovu katika nchi,utumikishaji wa watoto vitani,umasikini,tama ya kupata mali ya Lawrence hadi kuua, nafasi ya watoto kuchagua wachumba kwasababu Ajaro alikataliwa na wazazi wa Emmanuel Komba kwakuwa walishamchagualia mchumba, uthubutu, kutokata tamaa,thamani ya kufanya kazi,maadili, na ulevi kwa kutaja chache.

Mwandishi amedumisha baadhi ya mila na desturi muhimu kwa wakazi wa Afrika masharika. Pili, amedumisha matumizi ya misemo ya lugha asili na Kiswahili. Uhondo wa kitabu hiki ni kukisoma mwenyewe zaidi.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako