Showing posts with label mengineyo. Show all posts
Showing posts with label mengineyo. Show all posts

December 27, 2012

MIKONO NA MOYO WA NATHAN MPANGALA KUWAFANYA WATOTO WENYE SARATANI KUTABASAMU

Nathan Mpangala akiwa anawafundisha watoto kuchora michoro mbalimbali. 
Nathan Mpangala ni miongoni mwa watanzania wanaogusa mioyo ya watu kutokana na kazi zao za sanaa. Wengi wanakumbuka michoro ya katuni za Kijastibikozi na mingine mingi sana. 
Yeye ndiye mwasisi wa michoro ya katuni za Daladala ambazo huchapishw ana gazeti la MAJIRA hapa nchini. Tasnia ya uchoraji imemfikisha katika nchi mbalimbali kuhudhuria mihadhara ya kuelimisha jamii akiwa miongoni mwa waandishi wa habari wanaotumia vipaji vyao kufikisha ujumbe kwa njia ya sanaa za michoro. Moja ya kazi zake kubwa zinazoonekana kote nchini kupitia Televisheni ya ITV ni kibonzo cha MTU KWAO. 
Kibonzo hivyo hubeba ujumbe mbalimbali wenye nia ya kuelimisha na kuburudisha jamii. Kutokana na kipaji chake, Nathan Mpangala anarudisha faida anayopata kwa kazi hiyo kwenda kwa jamii. 
Amekuwa akifanya hivyo kupitia programu ya WAFANYE WATABASAMU akiwa na lengo la kuwaliwaza watoto wote wanaougua saratani nchini. Juhudi hizo ni kutokana na mapenzi yake kwa jamii na nchi kwa ujumla. Kama anavyoonekana pichani akiwa na watoto hao, pamoja na mchoro mwingine upande wa kulia unavyoonyesha watu wasiofikiria jamii yao. 
Hakika Mikono na moyo wa NATHAN MPANGALA umekuwa faraja kwa wazazi wa watoto na watoto hao kwa ujumla. Nawe waweza kuchangia juhudi zake kwa kuungana naye katika WAFANYE WATABASAMU.


Anaelezea zaidi safari yake .............
UCHORAJI UMEPAMBA MOTO. Baadhi ya watoto wanaendelea na matibabu ya saratani katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam, wakijimwayamwaya wakati wakichora. Kupitia Program ya Wafanye Watabasamu, nilitembelea watoto hao kuwapa zawadi kisha kuchora nao. 
Katika ziara hiyo niliyoambatana na baadhi ya wachoraji katuni na marafiki wa Wafanye Watabasamu tuliwazawadia watoto zawadi kisha kuchora nao. Kwa niaba ya watoto, nawashukuru ndugu na marafiki wa Programu ya Wafanye Watabasabu kwa zawadi mbalimbali walizochangia ambazo zimefanya ziara hiyo kuwa ya mafanikio. Pia nawashukuru sana marafiki na wachoraji wote waliojitokeza na kuungana nami Muhimbili. Picha na michoro mbalimbali iliyochorwa na watoto hayo iko njiani.

October 27, 2012

ELIMU: SEKONDARI ZA WILAYA YA NYASA ZAENDELEA KUBORESHWA

Wengi wanafahamu kuwa Wilaya ya Nyasa ni miongoni mwa Wilaya zilizoundwa na kuzinduliwa mwaka huu. Kila wilaya inapoundwa basi masuala mengi yanahitaji kufanyiwa kazi. Moja ya masuala hayo ni elimu. Wilaya Nyasa kwa sasa kuna mengi yanafanyika yenye lengo la kuongeza maendeleo na kuboresha zaidi. Shule zinajengwa au kuboreshwa ili kuweka mazingira mazuri ya kusomea. Kufuatia suala hilo, Nyasa inaelekea kuhimiza ujenzi wa shule mpya na zile za zamani kurekebishwa kwa manufaa wa wananchi wote. Hapa ni baadhi ya shule ambazo zinafanyiwa marekebisho na zilizokamilika. Elimu ni Uhai, kama Misitu ni Uhai.
Picha ya juu inaonyesha sehemu ya majengo la shule ya Sekondari ya Mkwaya baada ya kukamilika kwa ujenzi wake na kuboresha mazingira ya shule hiyo.
Picha ya pili inaonyesha nyumba ya Mwalimu katika shule ya Sekondari ya Mkwaya. Hii ni moja ya mikakati ya kuweka mazingira mazuri kwa walimu wa sekondari katika wilaya ya Nyasa.

Picha inaonyesha majengo mawili ya madarasa katika Sekondari ya Kipololo. Ujenzi wa Sekondari hiyo unatokana na fedha za mradi wa serikali kuboresha Elimu ya Sekondari(MMES) kwa kushirikiana na LGCDG kwa mwaka wa fedha 2006/2007 
Picha ya mwisho inaonyesha jengo la shule ya Sekondari ya Ruanda. Jengo hilo ni miongoni mwa majengo yanayotakiwa kukarabatiwa ili kuboresha hali yake na kuweka mazingira mazuri ya kusomea.

PICHA ZOTE na Hoops Kamanga, Nyasa

October 18, 2012

AJALI YA LORI BARABARA YA MBINGA-SONGEA


Ajali ya lori la ujenzi la kampuni ya Wachina inayojenga barabara ya Mbinga-Songea ambayo imetokea leo asubuhi saa tatu. Ajali hiyo imetokea katika kijiji cha Lipumba ambacho kipo kilometa chache tu kutoka Mbinga mjini.

Hata hivyo hakuna mtu aliyeruhiwa katika ajali hii. Soma zaidi Hapa

January 11, 2009

CO.MMENTS + BLOGLINES= mambo mapya

Jana niliandika kuhusu huduma ya Aggregators/Bloglines kisha nikasema unaweza kurahisisha mambo kwa huduma hizo. Lakini nikatoa anuani ya kusoma zaidi mambo hayo ya www.mwongozo.wordpress.com Sasa leno niseme hii CO.MMENTS na BLOGLINES pia. Huduma ya CO.MMENTS ni tamu sana, nayo inakuletea habari mpya kuhusu maoni uliyoyaacha mahali/katika blogu uliyoacha MAONI.
Huduma hii inachofanya ni kukupa taarifa mpya toka sehemu ulizoacha maoni, mfano umetembelea blogu ya Koero kisha ukaacha maoni wakati huohuo unataka kujua wasomaji au wanablogu wengine watasema nini juu ya maoni uliyotoa, kawaida unachofanya ni kurudi pale ulipoacha maoni ya wengine kuendeleza mjadala.
CO.MMENTS inakusanya maoni yote mapya toka mijadala unayoshiriki na kukuletea katika akaunti yako. Kwetu TZ tunajua baadhi yetu tunategemea huduma za kulipia kwahiyo suala la MUDA ni muhimu sana, kwani unaweza kutembelea blogu 25 halafu hazina mambo mapya.
Huduma ya CO.MMENTS na BLOGLINES zinakusaidia kukusanya habari mpya na MAONI mapya toka kwenye idadi yoyote unayotaka hata 100 na kukuletea katika ukurasa mmoja.
Sasa hii huduma ya CO.MMENTS inakupatia fursa ya kujua blogu zote ulizopitia na kuacha MAONI wapo wasomaji au wanablogu wamechangia, kwahiyo maoni yao yanakuwa yanakusubiri uyasome ili kuendeleza mjadala.
Binafsi nimejaribu hiyo, na napata taarifa za maoni katika akaunti yangu kila ninapoacha maoni mapya katika blogu yoyote, na nimeanzia kwa dada Koero na mengine nitayapata. NB: ili kujiunga na huduma hii unajiunga na BLOGLINES kwa urahisi hapa www.mwongozo.wordpress.com nyingi sana kuhusu huduma hizo.

January 08, 2009

Maisha! maisha! maisha

Duhh! jamani wakati fulani pale mji wa Mzuzu-Malawi, nilijiuliza mambo kadhaa kuhusu maisha yetu. Samahani usiwaambie uhamiaji kama situmii pasipoti wala mayai visa, maana wale ni ndugu zetu bwana tunalonga kinyanja na kuingia kwa mitumbwi poa. Haya maisha ya Bongo na kule naweza kusema aheri kwetu japo kwa sumuni. Jamani nakumbuka baadhi ya vijiji au mitaani tu wapo wanaoamini Wabongo maisha tunapeta, lakini sote tunajua kinachoendelea. Sasa kwa kawaida huwa najiuliza sana maisha yetu hapa kijijini Lundu na haya ya ndugu zangu wa damu kule Mzuzu na maeneo mengine! Jamani maisha! maisha! maisha! maisha! maisha! maisha!

November 26, 2008

ndizi ndizi KAPOLOTA karibu sana

wale walaji wa ndizi KAPOLOTA karibuni. Dada Yasinta huko ughaibuni unazikumbuka hizi

November 17, 2008

kuvua dagaa usiku


dagaa wa ziwa nyasa ni watamu sana, wananoga mno, ukila unajiumauma tu hamu na kuzidi kunogea. SASA ukitazama picha hii utaona KARABAI zimefungwa mtumbwini, hapo ndipo kazi inafanyika kwani ukisha funga hivyo kazi inaanza kwenda kilindini na anyavu ya kuvulia kusaka kitoweo kunoga na utamu kuliko chochote..... ebu taja kitu kingine kitamu kuliko dagaa? najua utataja nanii....... nini ile ...... sijui ebu inaitwaje!!!! aahaa tuache, hayo. haya ndiyo mambo ya nyasa na zana zao

November 11, 2008

Je ni mapenzi yangu kuwa hali hii??


sijui jawabu, labda nimekosa thawabu
Hakika sina aibu, maisha ni yangu
Ni maisha yangu, ndiyo thawabu yangu
kamwe hiana si kwangu, nangoja adabu

Naishi kivyangu, siishi waishivyo
Moyoni furaha yangu, imani ilivyo
Furaha imedumu, haina kasoro
kuishi kudurusu, thawabu yangu

Salamu wenye heri, mola awarehemu
mioyo iwe buheri, nafsi zidumu
Moyoni sina huzuni,jirani usiniudhi
yangu yakuudhi, yako yanipa riziki?

Aghalabu sipigi kite, kwani mola ajua
mababu wasisikitike, moyoni natunza
imani isipotee, liwalo leo na kesho
faraja inikuze, upendo udumu hata mtondogoo

Wanipata ewe mwanadamu, sikio walitega?
akilize zidumu,ubongo wako umejaa
wanielewa ewe chakaramu, kesho unaogopa
sifazo ewe mwanadamu, itakupa malapa

ooh kwaheri ewe mnumanuma, ewe mpenda lukuma
alamsiki nakwambia, buheri na afya njema
sina hiana nakuga kwa pendo, iwe siku njema
siku ya upendo siyo mitego,iwe daima pamoja

October 29, 2008

natabasamu jamani RAHA za hapa nyasa

tazama tabasamu hilo linavyoukita. tabasamu linakuita bila kinyongo. kaja huyu je wewe uliye jirani? karibu nyasa

October 22, 2008

hawa nao,wanatukatishia utamu au?

ONE LOVE yaleyale UKIMWI, eeeh mimisijui kama ukimwi nini, lakini unajua utamu ukikolea unaliza sana .......... la asali. eeeh jamani kama huji kufa tazam makaburi... lakini utamu nao...........

October 08, 2008

maswali magumu

Mwanablogu Yasinta Ngonyani aliandika kuhusu yeye katika blogu yake. Ilikuwa Agosti 23, 2008 kwamba udadisi kwake ni sehemu ya maisha, akaongeza kwamba katika hali hiyo amejikuta amepoteza baadhi ya marafiki hasa wale wasiopenda maswali yake yaani walikuwa wakikerwa na maswali yake. Mimi sijui walikerwa kwasababu gani, wao wanajua. Sasa mimi namfahamu kiasi dadangu Yasinta, jamani hapo ni kiboko ya maswali yaani jamaa anauliza maswali mpaka unaona hee huyu vipi? Ukweli mmoja ya waathirika ya maswali yake ni Mnyasa hapa lakini kawaida ya Mnyasa ni uvumilivu na utulivu ndiyo uliobaini kwamba uulizwaji kwake maswali ni njia yake ya uwasilishwaji wa urafiki tofauti na wengine walivyokuwa wakidhani. Jamani dadangu anamaswali mpaka unaweza kuungua utadhaniumeunguzwa na moto. Sasa huwa najiuliza vipi mjomba wangu Erik na Camilla watakuwaje? nikajikuta nimegota,nimeishiwa maneno ya kuwatabilia. Lakini maswali yake yanakufanya muda wote uwe unafanya kazi ya kujibu na usipojibu heee umemkimbia au la. Jamani mimi nilivumilia na nimekubali kwamba kama alivyoandika ni kawaida yake kwahiyo naona poa tu. Habari ndiyo hiyo, kublogu/kuandika unachopenda

September 21, 2008

haswaaaa na mchana kama huu njaa

hapa kazi hakuna kuremba

August 17, 2008

yaleyale ya kuvua kusaka kitoweo

mnyasa kwa kuwasaka samaki humuwezi yaani anajua majira ya kila aina kwa samaki mbalimbali.Karibuni nyasa,si unaona hapo walivyobize na kazi yao

July 08, 2008

Siyo Ukali Bali Anafurahia Nyasa

Kuna swali dadangu Ruhuwiko bloguni aliniuliza kuhusu huyu mnyama,nilikwepa kulijibu shauri nilikuwa natafuta kwanza picha yake na sasa nimeibamba.Ilikuwa adhuhuri fulani watu wakakusanyika kushangaa huyu mnyama wengine wakajiuliza ni Mamba gani huyu asiyejificha?Lakini ukweli ni kwamba dadangu alikuja nyasa toka ughaibuni lakini akaogopa kuogelea kisa mamba.Kimsingi huyu ni mnyama ambaye anaogopwa sana na Binadamu.Pale Liuli mzungu mmoja aliitwa Rainer alishikwa kwenye jicho na mamba mpaka kifo kikamkuta ikadaiwa ni sayansi ya kiafrika.Mimi sijui ila kwa hakika mambo wapo lakini kusema ndiyo hatari katika ziwa letu ni hapana,hawa ni wanyama ambao kila mmoja anatamani kuwaona,niambie kama unaogopa nikupe mbinu za kupuuza na kukupa nyakati za kuibuka kwa mamba ziwa nyasa.Kwa faida ya wasomaji ni kwamba nyakati za masika ni rahisi sana,hususani mwezi desemba na machi.Pia kiangazi hasa mwezi oktoba jua kali na joto kali,mamba hutokea sana vipindi hivi lakini siyo kuhatarisha maisha....hivi nimejitahidi kujibu au sijaweza?.....

July 02, 2008

Mnyasa Nimetua Mbinga Leo Unasemaje.......

Angalia picha hii kwa umakini halafu niambie inakupa fikra kidogo?Mmhh hapa ni barabara kuu ya Mbinga mjini pale,ukingalia kwa mbali kidogo kuna jengo au mnara fulani-hapo ni jimboni au makao makuu ya jimbo la mbinga.Sasa itazame barabara hii halafu jiulize ni mara ngapi unapenda hali hiyo,ni namna gani unaweza kuwa na ustadi wa mazingira bora au maisha bora kwa kila raia.Lakini sitaki ulaumu ila nimependa sana hii picha nilipoipiga kwa mara ya kwanza kwani inaonyesha njia kuu ya mjini na maduka pembeni.Ukiwa upande wa juu pale karibu na hoteli ya Madina njia panda ya benki ya NMB na barabara ya kwenda kiwanda cha kahawa ndipo barabara hii ilipo.Ni barabara kuu katikati ya mji.Habari ndiyo hiyooo wabunge wa jimbo la Mbinga magharibi na mashariki.

June 04, 2008

Wamo,Siyo Samaki pekee

kama unafikiri wanyasa wanachokiweza ni kuvua samaki na kujua majiraya kutega nyavy zao basi hujakosea ila hujui nini kinachoendelea hapo.Tazama wanaume wakiwa mzigoni wamekaza viuno,meno,miguu mpaka ngozi hakuna masihara hapo utaumia.kwanza inabidi uwe umeshiba sahani kama tano za ugali wa muhogo ikiwa wewe ni mgeni,lakini wenyewe ni nguvu za asili wale hawajui kwendaklabu za mazoezi kama huko mijini kwenu wanaogopa kansa shauri ya kutu za vyuma.

April 06, 2008

LINDA Yuko Hoi ,Ligambusa Limemchosha

Ama kweli huu ni urithi kwa Wanyasa.Hivi unakumbuka kisa cha JANETI kutua nyasa na salamu yake "inyahi"?,umesoma au hujasoma?{kitafute humu}.Basi Janeti ana nduguye huyu dada LINDA yaani watoto wa kinyasa hawapotei.Ikawa harusi Jumamosi hii,ngoma za wanaysa zikaporomoshwa hapo,madogoli yakakolea nyuzi bin nyuzi,watu wanakatika viuno kwa maraha ya harusi.Lakini LINDA mtoto wa wanyasa anaishi mjini kakumbana na ngoma za wanyasa "Ligambusa" kaanza kubinua viuno,kafunga kanga kiunoni,viatu kaweka kando,kacheza sambamba na wanyasa,kadhihirisha unyasa licha kuwapo mjini yaani ilikuwa burudani, acha nicheke niringe nina mwanya?.Basi dada kaona ngoja acheze kwa bidii huku mpigaji akivuta nyuzi bin nyuzi Ligambusa linakubali bila ubishi watu wanaselebuka,dada huyu naye kaanza kuonyesha madoido yake ya hapa na pale akamudu kwenda sambamba na watoto wa kinyasa.Kwa hakika ngoma ya Ligambusa kwa wanyasa linachezwa zaidi na vijana kuliko watu wazima kwani inahitaji ukakamavu,mitindo yake ya kasi,inahitaji pumzi.Sasa nashuhudia harusi ya kinyasa hapa nilipo na wanyasa wanasuuza nyoyo za wasio wanyasa, wanaduwaa.Mwishowe ananijia na kuniambia "unalijua Ligambusa mtoto wa nyasa wewe?".kuona hivyo nikamwambia subiri uchovu baada ya kucheza.Mmmh leo jumapili kaamka analamika "Nipo hoi,nguvu sina, mwili umechoka",nikamkumbusha nilivyosema,akabaki kucheka akidai wanyasa ni watu safi sana,yaani licha ya uchovu lakini Ligambusa limenikuna sana natamani kucheza kila siku nyuzi bin nyuzi,kasahau uchovu.Heeeh sijui nimejieleza vizuri kuhusu Linda,hivi inaeleweka?.karibuni nyasa jamani utamu wa Ligambusa mwaujuaaa??

March 13, 2008

Samaki anaujanja Mezani?

Moja ya mitaala ya maisha ya Wanyasa ni uvuvi.Huu ni ukurasa mkuu wa kijana wa kinyasa kujifunza au kuusoma vyema uvuvi atake asitake.Mtaala huu huvutia sana ikiwa unazingatia kanuni zake.Wanyasa wengi wanawafundisha watoto wao namna ya kuoposha samaki au kutega nyavu na mambo mengine yahusuyo uvuvi.Kwa kijana wa kinyasa kuvua samaki ni fahari na ni utamaduni murua kwa maisha yake ya kila siku.Huu unamaana kwamba huwezi ukamweka samaki mezani halafu akaleta ujanja kwani ujanja wake ni kabla ya kufika hapo vinginevyo ameliwa.Kuzaliwa kijana wa kinyasa halafu akakwepa angalao kujifunza namna ya kuvua samaki ni kukiuka tamaduni na utaratibu wa Wanyasa.Ndiyo maana nilianza kublogu kuhusu nyasa yaani kuwapa watu kitu tofauti na mambo ya wanasiasa.Kwa mnyasa na mtoto wake maisha hayo wala siyo mateso bali ni fahari na nuru ya kutumikia utamaduni wake wa kila siku.Kijana anajifunza mbinu za kuvua samaki katika vipindi tofauti toka kipindi cha kiangazi na aina ya samaki wake,masika aina ya samaki wake na vipindi vingine ambavyo kwa wanyasa hufahamu mbinu na uelekeo wa samaki n.kMitaala nina maanisha kwamba utaratibu kamili wa kila siku kwa wavuvi wa samaki,hivyo ili mtoto wa kinyasa afuate kanuni au asifuate basi asizaliwe nyasa.Kutozaliwa nyasa labda unaweza kuleta ujanja mezani,lakini kwa mtoto wa kinyasa hana ujanja kwani tayari amezaliwa eneo lenye ubora wa kutukuza tamaduni zake.Ukiwaona wanyasa lazima utagundua kwani hawapendi ujanja wa mezani bali wao hushindana na mawimbi ya ziwa lenye mawimbi kuliko yote duniani la Nyasa,je wewe uliyezaliwa nyasa unaweza kuleta ujanja?Je samaki anaujanja mezani? kilichobaki ni kuliwa tu,na kijana wa kinyasa lazima uvua samaki tu hata kama atapa shahada za uzamili za mbinguni lakini aliwahi kuvua au siyo wanyasa wenzangu.msikasirike haya mawazo tu..!!!!!

December 26, 2007

NYASA;krisimasi,furaha,burudani na uhai wa wanyasa

Naam nilikuwa katika kijiji lundu kujionea burudani na furaha ya kusherehekea krisimasi ambayo bila shaka ni ni wakati wa wazazi,watoto,ndugu,jamaa na marafiki kujumuika katika simu hii ambayo hupatika mara moja kwa mwaka pale wakristo wanapokumbuka siku ya kuzaliwa Yesu krsito.Ni kawaida yangu kutulia katika siku za aina hii lakini nilishindwa kutulia ilibidi nijiulize nitaandika nini nikifika Mbinga asubuhi hii maana wenzenu mambo ya mtandao haya mapaka tusafiri kidogo ndipo tuandika katika blogu namna hii.Naam nimekuwa katika mzunguko mkali wa siku hiyo ya krisimasi ili kujionea burudani,furaha na uhai wa wanyasa katika maisha yao lakini nikaona sisi bina damu tuna kawaida ya kusahau matatizo siku kama hizi maana nikaona hata wale maadui wanakumbatiana kwa wema kuikumbuka siku ya mwokozi wao.Asubuhi hii ikawa balaa maana kuna jamaa alikwenda kuvua samaki hivyo nimemwahidi kwenda kupata japo kitoweo kumbe mwenzie naondoka zangu kusafisha macho mjini Mbinga angalu nione wamjini wanaburudika vipi hata siku kama ya leo.Nimekuta watu wamelewa,wanatapika hovyo,mara mafumanizi na uchafu kibao na nikaambiwa na mwenyeji wangu kuwa kuna mwanamke mmoja kafumaniwa na kijana wa kinyasa mtaa wa Flastoo.Hapo nikaguna huyu mnyasa yuko hai kweli? nikambiwa wanyasa wana mbio katika hatari maana jamaa kachia mbio kuokoa uhai wake....si unajua fumanizi za wenyemali.Sasa badala ya furaha,burudani na uhai wa wanyasa jamaa kasafiri hadi hapa mjini halafu anajiona wa leoleo na vihela mbuzi vyake akakoswakoswa na wenye uchu wa kutanya uhai wa wenzie na bahati yake kwa wanyasa kuwa mbio kali ni sifa moja ya uhai wako nyakati za hatari.Ndiyo wanyasa wa mbio za ajabu mithiri ya swali mbugani.Lakini baada ya kuandika hapa mjini katika blogu hii natarajia niende zangu kijiji maana jamaa akija nadhani ataghadhibika kwani nimeahidi kununua samaki wake ili apate pesa za kuburudika na furaha ya familia maana jana kalewa mipombe halafu kasahau familia lakini kaahidi leo ni burudani ya familia yote sasa watoto wako juu kwelikweli maana wanataka kuonyesha uwezo wao wa kuburudika. mapumziko mema,watu wote wa ughaibuni maana najiuliza hivi Ndesanjo anasoma habari za wanyasa kweli?vipi kaka Jeff,DaMija,Michuzi na kitoto pale London?sijui lakini polepole,KARIBUNI NYASA!