December 27, 2012

MIKONO NA MOYO WA NATHAN MPANGALA KUWAFANYA WATOTO WENYE SARATANI KUTABASAMU

Nathan Mpangala akiwa anawafundisha watoto kuchora michoro mbalimbali. 
Nathan Mpangala ni miongoni mwa watanzania wanaogusa mioyo ya watu kutokana na kazi zao za sanaa. Wengi wanakumbuka michoro ya katuni za Kijastibikozi na mingine mingi sana. 
Yeye ndiye mwasisi wa michoro ya katuni za Daladala ambazo huchapishw ana gazeti la MAJIRA hapa nchini. Tasnia ya uchoraji imemfikisha katika nchi mbalimbali kuhudhuria mihadhara ya kuelimisha jamii akiwa miongoni mwa waandishi wa habari wanaotumia vipaji vyao kufikisha ujumbe kwa njia ya sanaa za michoro. Moja ya kazi zake kubwa zinazoonekana kote nchini kupitia Televisheni ya ITV ni kibonzo cha MTU KWAO. 
Kibonzo hivyo hubeba ujumbe mbalimbali wenye nia ya kuelimisha na kuburudisha jamii. Kutokana na kipaji chake, Nathan Mpangala anarudisha faida anayopata kwa kazi hiyo kwenda kwa jamii. 
Amekuwa akifanya hivyo kupitia programu ya WAFANYE WATABASAMU akiwa na lengo la kuwaliwaza watoto wote wanaougua saratani nchini. Juhudi hizo ni kutokana na mapenzi yake kwa jamii na nchi kwa ujumla. Kama anavyoonekana pichani akiwa na watoto hao, pamoja na mchoro mwingine upande wa kulia unavyoonyesha watu wasiofikiria jamii yao. 
Hakika Mikono na moyo wa NATHAN MPANGALA umekuwa faraja kwa wazazi wa watoto na watoto hao kwa ujumla. Nawe waweza kuchangia juhudi zake kwa kuungana naye katika WAFANYE WATABASAMU.


Anaelezea zaidi safari yake .............
UCHORAJI UMEPAMBA MOTO. Baadhi ya watoto wanaendelea na matibabu ya saratani katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam, wakijimwayamwaya wakati wakichora. Kupitia Program ya Wafanye Watabasamu, nilitembelea watoto hao kuwapa zawadi kisha kuchora nao. 
Katika ziara hiyo niliyoambatana na baadhi ya wachoraji katuni na marafiki wa Wafanye Watabasamu tuliwazawadia watoto zawadi kisha kuchora nao. Kwa niaba ya watoto, nawashukuru ndugu na marafiki wa Programu ya Wafanye Watabasabu kwa zawadi mbalimbali walizochangia ambazo zimefanya ziara hiyo kuwa ya mafanikio. Pia nawashukuru sana marafiki na wachoraji wote waliojitokeza na kuungana nami Muhimbili. Picha na michoro mbalimbali iliyochorwa na watoto hayo iko njiani.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako