Showing posts with label Vitabu. Show all posts
Showing posts with label Vitabu. Show all posts

February 26, 2018

ZAWADI YA VITABU KWA MARA NYINGINE

JUMAMOSI Februari 24 mwaka huu nilipatiwa zawadi ya vita viwili kutoka kwa Bwana Ragin Mmbaga, kama vinavyoonekana pichani. Vitabu hivyo vimeandikwa na Bwana Johne Wisse. Kuna kitabu cha TONE LA DAMU cha lugha ya kiswahili na THE BROKEN CAMPUS RULE cha lugha ya Kiingereza. 
Ninawashukuru kwa kujali kuwa visima vya maarifa. Hakika mwaka huu nimeanza kwa furaha kubwa kwani huyu anakuwa mtu wa tatu kuniletea vitabu kibaruani kwangu. 

Usomaji wa vitabu ndicho kitu ninachokipenda zaidi. Ndicho kilevi au kitu ambacho kinachukua muda wangu wote kuhakikisha nafurahi. Zaidi ya hapo navutiwa na mchezo wa soka. Vitabu ni kitu muhimu sana. Namshukuru Ragin Mmbaga kwa niaba ya John Wisse. ASANTENI SANA

-MARKUS MPANGALA

February 10, 2018

OFA YA VITABU TPH BOOKSHOP, SAMORA AVENUE, DAR ES SALAAM.

 
PUNGUZO 20% kwa sikukuu ya Valentine. Mpe umpendaye zawadi ya kudumu. Vitabu vyote vya mahusiano, mapenzi, ndoa na urafiki Bei ni 20% Karibu sana dukani kwetu. #KitabuNiZawadi

January 26, 2018

UCHAMBUZI WA KITABU: SAFARI YA YERUSALEM KUTAFUTA AMANI

NA MARKUS MPANGALA
BOUTROS Boutros Ghali aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kati ya mwaka 1992 hadi 1996 amefariki dunia Februari 16 mwaka 2016 akiwa na miaka 93.

Leo tunachambua kitabu chake cha “Egypt's Road to Jerusalem:: A Diplomat's Story of the Struggle for Peace in the Middle East” kilichozindualiwa rasmi Mei 20, 1997. Kitabu hicho kina jumla ya kurasa 366, kimechapishwa na Random House(1997) na kikiwa katika lugha ya kiingereza. Boutrous amekipatia namba ISBN-10: 0679452451.

Boutros Ghali anatuelezea miaka minne ya uzoefu wake katika utawala wa aliyekuwa Rais wa Misri, Anwar as-Sadat. Anatuonyesha namna alivyochaguliwa kwenye uwaziri wa mambo ya nje mwaka 1977 na kifo cha rais Sadaat mwaka 1981. 

Katika kitabu hiki Boutros Ghala anadhihirisha umahiri alioonyesha katika masuala ya diplomasia wakati wa kusaka amani ya mashariki ya kati. Ikumbukwe eneo la mashariki ya kati limekuwa kwenye migogoro ya muda mrefu kiasi kwamba ufumbuzi umekuwa mgumu. 

Ni eneo ambalo mwandishi wa kitabu hicho anatukumbusha hatua kwa hatua walizokuwa wakichukua katika kuhakikisha amani inarejea mashariki ya kati. Anatuonyesha namna ambavyo Misri na Israel zilivyokuwa zikifanya juhudi za kumaliza uhasama wao. 

January 04, 2018

ZAWADI YA MWAKA MPYA 2018! KITABU

Adella
ADELLA ABELL ni mtani wangu. Jirani yangu nyumbani. Sahibu wangu. Dada yangu. Ni msomaji mzuri wa vitabu. Katika kuanza mwaka mpya amenipatia zawadi ya kitabu hiki chenye masimulizi ya visa, mikasa, kesi,upelelezi na hukumu mbalimbali zilizowahi kutolewa na mahakama ndani na nje.
Mojawapo ya mkasa uliomo kitabu ni ule wa familia ya George Liundi, mkewe Doris Liundi na watoto wao (Nadhani wengine wamewahi kusikia masimulizi ya maisha ya Taji Liundi).

December 30, 2017

VITABU 50 NILIVYOSOMA MWAKA 2017

NAWASILISHA orodha ya vitabu nilivyosoma mwaka 2017. Ukitazama orodha zangu za usomaji vitabu utabaini kuwa ya mwaka imeongezeka. Nimesoma vitabu 50 na kuna mabaki kadhaa hayaguswa kabisa.
Mwaka 2017 nimejikuta nikiwa nimeongeza uwezo wa kusaka maarifa zaidi kutokana na ongezeko la vitabu ingawa sina desturi ya kupanga idadi yake.

Kwa mwaka 2018 ninatarajia kuongeza maarifa zaidi katika vitabu vya biashara na uchumi, lakini haina maana nitasoma vingi kuzidi ‘ala za roho” (riwaya). Pamoja na changamoto za majukumu na mengineyo, suala la vitabu limebaki kuwa nyeti maishani mwangu. 

December 01, 2017

MACHO VITABUNI


NAAM! Mara kadhaa ninapotembelea jiji la Dar es salaam wengi hutuita  wageni kama “watu wa mikoani”. Lakini ninachokiona wakati mwingine ni kuzikali fursa ikiwemo ya kutembelea maduka ya vitabu.

Wahenga wanasema ni heri ukatekwa nyara, kushikiliwa mateka kwa muda fulani katika duka la vitabu kwani unakuwa umehiari mwenyewe. Pia wanasisitiza kitabu ni silaha. 

November 25, 2017

UCHU WA MADARAKA DHIDI YA UZALENDO

KITABU: ZIMBABWE: STRUGGLES-WITHIN-THE-STRUGGLE (1957-1980)”
MWANDISHI: PROFESA MASIPULA SITHOLE
MCHAMBUZI: MARKUS MPANGALA
JESHI la Zimbabwe limetangaza wiki iliyopita kuchukua madaraka nchini humo na kumwondoa Rais Robert Mugabe ambaye ametawala nchi hiyo kwa kipindi cha miaka 38 hadi sasa. Kutokana na hali hiyo tunalaizmika kukumbuka namna mwanazuoni Profesa Masipula Sithole alivyobainisha matatizo ya Zimbabwe kupitia kitabu chake cha “Zimbabwe: Struggles-within-the-struggle (1957-1980)”

November 15, 2017

ULINZI WA FAMILIA UPO MIKONONI MWETU

KATIKA kitabu hiki….. mhusika Ttiisa anafungua albamu. Ina picha nzuri kila anapofunua. Moja kwa moja anatupia jicho picha ya Suuna.Ni Suuna kipenzi chake. Aliyeingia nae penzini kwa miaka miwili (sasa), bila kujali namna Suuna alivyoleta ugonjwa wa Ukimwi ktk penzi lao (mechi za ugenini?).
 
Katika albamu hiyo hiyo Ttiisa anatazama pia picha ya Ggenza, mtoto wake aliyekuwa na umri wa miezi minne tu lakini alifariki dunia. Kulikoni? Riwaya inakupa jawabu
**************
Ttiisa ana ukimwi. Amekutana na Dona ambaye hana kazi (hana ajira wala hajajiajiri). Makutano yao yanaleta matatizo makubwa ambayo ni somo kwa maisha ya Kampala ya leo (Uganda). Maisha yao hayaeleweki. Sasa walifanyaje hadi kueleweka? ...
Ndo utamu wa nakala ngumu(hard copy) unafunua ukurasa mmoja hadi mwingine kisha unapambia mate kwa mbaaaaali....
#ThanksMolio.B.#

November 10, 2017

ZAWADI YA VITABU

Zawadi ya vitabu niliyopewa na Molio Baldwin. Asante sana rafiki
Mimi na Molio Baldwin ni marafiki Facebook. Tumetimiza miaka mitano ya urafiki wetu kwa kufanya kitu tofauti. Sote ni wapenzi wa kusoma vitabu. Badala ya maneno ya pongezi tuliamua kununuliana vitabu vitano kadiri ya umri wa urafiki wetu. Leo nimepokea zawadi yangu ya vitabu (pichani). 

October 21, 2017

TABASAMU NA KITABU


Ragin Mmbanga (kushoto) na Markus Mpangala (Kulia)
Huyu ni rafiki yangu. Anaitwa Ragin Mbaga, ila tuwapo farashani hupendelea kumwita "Mzee wa bustani ya usomaji". 

October 16, 2017

CHUO CHAANZISHA SHAHADA YA WADUDU

NAIROBI, KENYA

KITUO cha Elimu na Utafiti kinachofadhiliwa na Benki ya Dunia kimeasisiwa katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Jaramogo Oginga Odinga na kinasubiri ruhusa ya kuanzishwa kwa programu za Uzamifu na Uzamili kuhusu wadudu wanaoweza kuliwa.

Taasisi hiyo inapania kubuni njia za kuzalisha wadudu hao kwa wingi bila ya kuharibu mazingira ili kukidhi utashi mara baada ya wazo hilo likifanywa kuwa biashara.Wadudu wanaoliwa sana maeneo ya Magharibi mwa Kenya, ambao wana wingi wa madini ya protini na Zinki watafanywa kuwa biashara ili kuimarisha uwepo wa chakula cha kutosha, na kuondoa dhana mbaya katika kula wadudu. 

October 11, 2017

SOMO LA LEO

“Mheshimiwa Kakunda (Joseph –Naibu Waziri Tamisemi) nakuagiza kuanzia leo maana wewe ndiyo nimekukabidhi jukumu la elimu, nataka mtihani wa 2019 shule za vipaji zote 22 ziongoze mtihani wa Taifa na shule binafsi ziwe nyuma, lakini tuongoze kwa halali si ubabaishaji hapo ndipo shule binafsi za makanjanja zitajifuta zenyewe,”

-Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Selemani Jafo.

October 09, 2017

"BIASHARA NI KAMA VITA" –(1)

NA MARKUS MPANGALA
 
NOVEMBA 8 mwaka huu Bunge la Jamhuri ya Muungano lilikataa kusaini mkataba wa Ushiriakiano na Jumuiya ya Ulaya (EPA) ambao mchakato wake ulianza mwaka 2001. Mwanazuoni Yash Tandon ni ameeleza kwa kina ubaya na hatari ya mkataba wa EPA kupitia kitabu chake cha “Trade Is War; The West’s War Against the World,’ chenye jumla ya kurasa 196. Kitabu hichi kimechapwa mwaka 2016 na Kampuni ya Mkuki na Nyota na kikapewa nambari 978-9987-75-342.
 Tandon anasema Afrika inatakiwa kuwa makini kwenye mikataba ya aina hiyo. Anaelezea jinsi Marekani, Ulaya na Japana zinavyolitumia Shirika la kibiashara duniani (WTO) kwa madhumuni ya kuchota rasilimali za mataifa madogo. EPA (European Partnership Agreement) ni mojawapo ya silaha kubwa iliyopangwa kuchota rasilimali na kuua soko Afrika mashariki. EPA inataka asilimia 80 ya masoko ya ndani yaachwe wazi na kuruhusu kuingizwa bidhaa za Ulaya.

October 05, 2017

TUZO YA NOBEL: NGUGI WA THIONG’O HOI TENA!!!!

Kazuo Ishiguro (pichani) raia wa Uingereza ameshinda tuzo ya Nobel katika fasihi kwa mwaka 2017. Amepata ushindi huo baada ya kuwabwaga washindani wake Margaret Atwood, Ngugi Wa Thiong’o na Haruki Murakami.Vitabu vyake ni kama ifuatavyo:-

September 16, 2017

WATU NA VITAVU

Ni raia wa Afrika Kusini akiwa katika sehemu ya viunga vya jiji la Johannesburg. Huwa anasoma vitabu na kuueleza umma maudhui na mafundisho yaliyomo kitabuni, wapitao na kusikiliza humchangia fedha kadiri ya ridhaa ya mchangiaji. 

Ukimuadhima kitabu anasema ni bora akuuzie kwani yeye ameshasoma hivyo anapenda ununue na ukakisome kwa uhuru zaidi kuliko kuwa na mashaka ya muda wa kurudisha. Hivyo ndivyo apatavyo ridhiki.


September 15, 2017

KITABU NI SILAHA


KITABU: AYA ZA SHETANI


"Aya zilizopo katika msahafu wa Shetani ni kutafuta walio wasafi na kuwaingiza kwenye uchafu. Haziangalii hulka au usomi wa mtu. Kumbuka, Vivi naye ni mke wa mtu! Kama ameshindwa kuziona dhambi zake, hawezi akaziona anazomfanyia mwingine," alisema Lucas na kusisitiza Judith amekuwa msagaji kama Mama Jenifer na Vivi. (uk.182).

MAHABUSU
Mahabusu yote ilinuka harufu nzito yenye jasho la watu wasiooga, mikojo na hata vinyesi. Kwa hali halisi Mahabusu yote ilinuka Kutuzi, alisema George (uk.199).

Kiburi cha Judith kinaendana na simulizi nyingine ya "DHIHAKA" iliyoandikwa Beka Mfaume.
WATU.

Katika maisha kuna watu wanaweza kukulaghai, kukuyumbisha, na kulinda maslahi yao kwa staili ya "ACACIA". Najua nakuibia ila ni sheria zako (akili zako) sio Mimi. Mtu anajua anakuharibu lakini hajali juu ya hatima yako. Subira ni jambo muhimu sana kuwajua wadanganyifu. JILINDE.

©Markus Mpangala,

MWANDIKO WAKO NI UPI?



Kila mwandishi wa kitabu anatakiwa kuwa mwandiko wake rasmi. Mwandiko huo humtambulisha mwandishi kila kazi yake inapochapishwa na kuingizwa sokoni. Hiyo inatusaidia sisi wasomaji kutambua mwandiko wa mwandishi husika.

Na mwandiko huo upo kwenye “Font Style”. Uchaguzi mzuri wa mwandiko unamfanya mwandishi kuuza kazi zake kwa mwandiko rasmi.

FIKIRIA UMRI WAKE


MIMI ni miongoni mwa watu ninaopenda kujisomea vitabu. Nimefunzwa hilo tangu nikiwa kijijini kwetu Lundu. Mafunzo hayto ni kutokana na wazazi nilivyowaona wakiwa bize na vitabu wakijisomea au kufanya shughuli zao.

katika umri wangu siwezi kusema sina mdua kwakuwa nimeshazoea hilo. Kwahiyo ninakukumbusha msomaji tafakari mwonekano wake wa huyo bibi pichani. Mtazame namna alivyojikita ili asikose uhondo. Mwangalie kwa mara nyingine.

Hivi husomi vitabu kwasababu huna muda?




May 12, 2013

KAMARA KUSUPA: MWAFRIKA ALIKUWA WA KWANZA KUWASILI MAREKANI KABLA YA CHRISTOPHER COLUMBUS

Na Markus Mpangala, Dar es Salaam
HIVI karibuni nilipata fursa ya kumhoji mwandishi wa kitabu cha ‘Kumrudisha Mwafrika kwenye Asili yake: Mradi mgumu kuliko yote,’ Mwinjilisti Kamara Kusupa.
Haya ndiyo mazungumzo yetu ambayo bila shaka yatawanufaisha Watanzania kufahamu nini maana na asili ya Afrika kwa ujumla wake na maisha halisi ya bara letu.
SWALI: Niliwahi kusoma vitabu vyako viwili, “Maisha yangu Gerezani”, baadaye kile cha “Hii ndiyo Tanzania tunayoitaka”. Kuna tofauti gani kati ya vitabu hivyo na hiki cha sasa?
KUSUPA: Tofauti ipo, sababu kile cha kwanza niliongelea maisha ya gerezani na namna vijana wanyonge wanavyoteseka. Wengine wanakosa utetezi na wengine hawana msaada wa kisheria na wapo wanaogandamizwa.
Nikiwa na Mzee Kusupa
Halafu kuna wale wanaosota miaka mingi bila kesi zao kutatuliwa. Kitabu changu cha pili kimeongelea suala la nchi yetu ya Tanzania, kwamba tunataka iweje na iongozwe vipi katika kutafuta katiba mpya. Naizungumzia Tanzania ya wakoloni, baada ya ukoloni, kipindi cha Nyerere na baada ya Nyerere. Halafu nimeongelea hili suala la vyama vingi vya siasa. Lakini kitabu hiki kipya namtazama Mwafrika na matatizo yake yanayomsonga kila kukicha bila ufumbuzi huku akiwa tegemezi. Mwafrika ambaye hajachukua nafasi kuyachukua mazuri ya mababu wa asili yake.
SWALI: Lakini maandiko ya namna hii yako mengi hapa nchini na kote Afrika kwa ujumla kuhusiana na Mwafrika. Wapo Watanzania ambao wameandika vitabu kuelezea matatizo ya Afrika, mfano Dk. Malima Bundara aliandika, “Waafrika ndivyo Tulivyo”. Je, wewe unazungumzia nini kwenye hiki kitabu kipya?
KUSUPA: Nakiri yapo maandiko mengi kuhusiana na Waafrika. Yapo maandishi kama ya akina Cheikh Anta Diop (Senegal), Dk. Elly Kamugisha (Tanzania), Franz Fanon (Algeria), Julius Nyerere, Leopold Senghor (Senegal), Ali Mazrui, Marcus Garvey, Nelson Mandela na wengineo.
Lakini jambo kubwa lililokuwa likijadiliwa ni nani hasa huyu Mwafrika. Lakini wakasahau kuwa Mwafrika huyu ana asili zake, hizo ndizo ninazoongelea kwenye kitabu hicho kipya.
SWALI: Unakubaliana na mahitimisho mengi ya wasomi wa Afrika kuhusu Mwafrika ni nani na anaweza kurudi kwenye asili yake kwa njia gani?
KUSUPA: Wengi wanakubaliana kwamba Mwafrika ni mtu mweusi, hivyo kuwatenga Waarabu, Wahindi, Wazungu na Waberiberi ambao kimsingi nao wamejikuta wakiwa wamezaliwa katika bara ya Afrika hivyo hawawezi kutengwa.
Kwa mfano; msomi Dk. Harrith Ghassany alipata kuandika nini asili ya Afrika. Kwa utafiti wake akaelezea kuwa asili ya Afrika ni kutoka kule Tunisia.
Dk. Harrith alisema hayo kwenye kitabu chake cha “Kwaheri Uhuru, Kwaheri Ukoloni: Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia.” Yote haya yanatuletea swali la msingi Mwafrika huyu ni nani?
Hata hivyo dunia imebadilika na kila kona inatusaidia kujua nini hasa kinachopaswa kusemwa kwa dhati na moyo safi kwa nyakati za sasa na baadaye. Kuna Wazungu wamezaliwa Afrika Kusini, Tanzania na wengine nchi nyingine za Afrika.
Je, hawa watakwenda wapi ikiwa hawajui asili zao au mahali walikoanzia zaidi ya kujikuta wakiwa katika nchi wanazoishi. Ni kama ambavyo Waafrika walioko Ulaya, Amerika na Asia wanavyojiuliza ni namna gani wataweza kurudi Afrika ambako hawajui waanzie wapi.
Ni vigumu leo kumwelezea Jesse Jackson, Mohamed Ali warudi Afrika kutoka Marekani. Ni vigumu vile vile kumweleza Lennox Lewis wa Uingereza arudi barani Afrika.
Ni vigumu kumwambia Danny Jordan wa Afrika Kusini kwamba uchotara wake sio kitu arudi kwenye asili ya makaburu Uholanzi na kwingineko. Au ni vigumu kumwambia Hellen Zille, mwenyekiti wa chama cha upinzani cha Democratic Alliance (D.A) pale Afrika Kusini na gavana wa jimbo la Cape Town, kwamba arudi kwa wazungu wenzake.
SWALI: Unadhani hilo linatokana na uhusiano wa Waafrika na wageni, ndio kiini cha Mwafrika kurudi kwenye asili yake?
KUSUPA: Kwanza niseme hii ni moja ya mabadiliko makubwa ya mipaka ya nchi ambayo imeshindwa kuzuia uhusiano wa wanadamu kutoka nchi moja hadi nyingine au kutoka jamii ya nchi moja kwenda jamii ya nchi nyingine.
Leo Mwafrika anaweza kuzaa na Mchina au Mkorea hivyo ni vigumu mtoto atakayezaliwa kutotambuliwa kuwa Mwafrika, na kuangalia asili. Lakini wapo watu wanaojaribu kujiuliza ni namna gani wanaweza kuwakumbusha Waafrika wenzeo kuwa Mwafrika alikuwa na asili yake.
Hata kwenye dini, Waafrika wanazo. Ukisema Waafrika hawana dini nitakuambia soma maandiko ya Mchungaji Blacid Temple kwenye kitabu chake cha “Bantu Philosophy”, kwa hiyo ushahidi wa asili zetu upo kidini, kisiasa na kiuchumi.
Propaganda iliyohubiriwa kwa nguvu na pia kufundishwa na elimu ya kikoloni ni kwamba Mwafrika ameanza kuwa na dini baada ya ujio wa Waarabu na Wazungu barani Afrika.
Baada ya kazi ni gumzo
Kwa mfano; katika Afrika ya Mashariki, Uislamu uliingizwa katika karne ya nane na wafanyabiashara kutoka Ghuba ya Uajemi (leo tunaita Iran), hao wafanyabiashara wa kiajemi ndio walioitia jina la Dar es Salaam mji maarufu wa Tanzania lenye maana ya mbingu ya amani.
SWALI: Je, ni kweli kwamba kabla ya ujio wa wafanyabiashara wa kiajemi, Waafrika wa eneo hili hawakuwa wakimwabudu Mungu?
JIBU: Narudi kama nilivyoeleza mwanzoni, Waafrika walimjua Mungu wa kweli, walimwabudu na kuishi kulingana na miongozo yake. Ushahidi wa kuonyesha Mwafrika aliabudu Mungu kabla ya ujio wa Uislamu na Ukristo ni uwepo wa majina yanayoendana na masuala ya kiroho na ibada.
Lakini tunapokuja kwenye eneo linalohusu mambo ya kiroho, maneno kama ibada, Nnungu, Mungu, Mulungu, Ngai, Nkoyi, Kyala, Malaika na Banzelu neno kutoka lugha ya Kilingala lenye maana ya viumbe weupe wanaong’ara  ni udhihirisho wa kwamba Mwafrika  alimjua Mungu na alikuwa na mawasiliano naye.
Katika somo hili tunajadili kwa ufupi juu ya Uislamu, Ukristo, Ubuntu na dini ya asili iitwayo Alabba ndani ya kitabu nimeeleza sana hili.
SWALI: Mwafrika haonekani kutajwa kwamba mmoja wa watu waliowahi kuishi au kufika Marekani kabla ya ukoloni. Labda tuseme Latini Amerika yote kusini na kaskazini. Lakini tunashuhudia Waafrika wengi wakiwa huko na baadhi ya mila na desturi zao zinalingana na Waafrika wa bara la Afrika. Kwa nini?
KUSUPA: Kwanza niseme wanaoeneza kuwa Mwafrika hakuishi Marekani kabla ya biashara ya utumwa hawako sahihi, au kule Latini Amerika. Kuna sababu nyingi, lakini kubwa ilianzia kwa Columbus.
Mwafrika alikuwa wa kwanza kuwasili Marekani kabla ya Christopher Columbus, hata ukisoma maandiko yenye ushahidi yaliandikwa na Profesa Ivan Sertima kwenye kitabu chake "THEY CAME BEFORE COLUMBUS". Hizo  'voyage' mbalimbali za Christopher Columbus zimejaa mengi ya kushangaza na kwa nini yanachukuliwa kuwa kama yalivyo au ukweli wenyewe? Waafrika wanayo mengi hayakuandikwa vizuri.
SWALI: Kwa hiyo una maana kwamba ndani ya Kumrudisha Mwafrika kwenye Asili yake: Mradi mgumu kuliko yote umeelezea nyongeza yake na hali halisi ya Mwafrika na asili zake, ukizingatia dhana ya uhai pia?
KUSUPA: Kwanza tunaangalia sisi Waafrika ni nani na asili yetu ikoje, hicho ndio kiini. Dhana ya uhai inakuwa kubwa na inachukua mkondo mkubwa pia, hivyo basi kitabu cha KUMRUDISHA MWAFRIKA KWENYE ASILI YAKE; MRADI MGUMU KULIKO YOTE nimeleta baadhi ya majibu ya maswali ambayo kila mara watu wanajiuliza.
Nimeelezea kuanzia kwenye dini, siasa, utamaduni, na mengine mengi kuhusu Afrika, nimeelezea mengi kwamba kuna makosa kadhaa yanafanyika ni vigumu kuizungumzia Afrika kama wanazuoni Ali Mazrui wanaoitazama Afrika kichotara.
SWALI: Unazungumzia Afrika ya kichotara, una maana gani hasa?
KUSUPA: Hakuna wakati wowote katika historia ya dunia na maisha ya mwanadamu kiujumla, ambapo Afrika imeacha kuhusiana na watu kutoka nje ya bara hili, hivyo nazungumzia Afrika na Wageni kutoka Ulaya, Amerika na Asia. Tangu awali na baada ya Kristo watu kutoka nje wamekuwa wakiingia Afrika kwa sababu moja au nyingine.
Katika mada hii ya Afrika na wageni, tunazungumzia wageni wa aina tatu kutoka nje ya bara la Afrika. Tunajadili juu ya Afrika na wafanyabiashara kutoka mabara mengine ya Asia, Ulaya na Arabuni, Afrika na waeneza dini kutoka nchi za ulaya magharibi na Afrika na Wazungu wa  magharibi waliojifanya wavumbuzi yaani wale wachoraji wa  ramani za kuonyesha mito mikubwa, milima mirefu na maziwa.
Tunajadili juu ya Afrika na tamaduni za kigeni, Afrika na dini za kigeni na mwisho tunajadili juu ya Afrika na tawala za kigeni ikiwa ni pamoja na mifumo inayoendelea kutumika hadi sasa kuongoza maisha ya Waafrika.
Kila jamii imekuwa kwenye asili yake na inakuwa vigumu kurudi kwenye asili yake. Tujiulize je, dini za Waafrika ni zipi? Mfumo wa utawala wa Waafrika ni upi?
Msingi wao na dhana ya uhai vikoje? Uhusiano wao na jamii za nje ukoje? Je, Mwafrika ataepuka dhahama ya mabadiliko ya kijamii duniani? Je, Mwafrika ataweza kurudi katika asili yake?
Nadhani ni moja ya mambo ya kusisimua na hakika yatakuwa na hamasa kwa wasomi mbalimbali na wananchi wengine. Kikubwa tuseme kama kweli tutaweza kurudi kwenye asili yetu au ni mradi mgumu?
SWALI: Katika kitabu chako umegusia suala la muungano wa bara Afrika?
KUSUPA: Hilo nimezungumzia kwa kina. Nimeanza toka kwenye utumwa, ukafuatia ukoloni na baadaye utawala wa chama kimoja au udikteta wa chama kimoja.
Hatimaye Afrika imeletewa utandawazi unaoyafanya mataifa yenye nguvu yawe dikteta wa kudumu wa kuzilazimisha nchi za Afrika kujiendesha sawa na watakavyo wao.
Afrika iligawanywa vipande vipande na kuitwa majina mapya na wakoloni, lakini pia wakoloni hao wakati wanachora na kuweka mipaka yao ya kufikirika, ndipo waafrika tulipogawanywa na kutenganishwa na kupewa utambulisho mpya wa kuitwa Watanganyika, Wakenya, Waganda, Wakongo, Wanyarwanda, Warundi, Warhodesia, Wamozambiki, Wanigeria, Wakameruni, Waghana, Wasenegali, Wamali, Waliberia, Wasealeoni, Wanamibia, Waangola, Wasudan, Wasomalia, Waethiopia n.k.
Wakati wakoloni wanaigawa Afrika na kuweka mipaka yao mipya tofauti na ile mipaka ya asili iliyokuwa inatambuliwa na wenyeji, pia waafrika walitenganishwa na kuumbiwa hisia mpya. Mpaka wa kutenganisha nchi na nchi nyingine uliweza kupita katikati ya eneo moja na kuwafanya watu wa kabila moja au ukoo mmoja kuwa na uraia wa nchi mbili tofauti. Hivyo Afrika lazima iungane.
SWALI: Nashukuru kwa kushirikiana katika fursa hii. Naamini Watanzania watanufaika kutoka katika maandiko yako mazuri ya kitabu chako.
KUSUPA: Karibu wakati mwingine, ninyi vijana mnatakiwa kujua zoezi jipya la Afrika kuwa na mipaka mipya lilimpa Mwafrika hisia mpya na utambulisho mpya. Nitafanya mhadhara UDOM kuelezea hilo Mungu atujalie. Kwa hiyo lazima tujirudishe kwenye asili zetu.
Baruapepe; mwanazuoni27@gmail.com