October 09, 2017

"BIASHARA NI KAMA VITA" –(1)

NA MARKUS MPANGALA
 
NOVEMBA 8 mwaka huu Bunge la Jamhuri ya Muungano lilikataa kusaini mkataba wa Ushiriakiano na Jumuiya ya Ulaya (EPA) ambao mchakato wake ulianza mwaka 2001. Mwanazuoni Yash Tandon ni ameeleza kwa kina ubaya na hatari ya mkataba wa EPA kupitia kitabu chake cha “Trade Is War; The West’s War Against the World,’ chenye jumla ya kurasa 196. Kitabu hichi kimechapwa mwaka 2016 na Kampuni ya Mkuki na Nyota na kikapewa nambari 978-9987-75-342.
 Tandon anasema Afrika inatakiwa kuwa makini kwenye mikataba ya aina hiyo. Anaelezea jinsi Marekani, Ulaya na Japana zinavyolitumia Shirika la kibiashara duniani (WTO) kwa madhumuni ya kuchota rasilimali za mataifa madogo. EPA (European Partnership Agreement) ni mojawapo ya silaha kubwa iliyopangwa kuchota rasilimali na kuua soko Afrika mashariki. EPA inataka asilimia 80 ya masoko ya ndani yaachwe wazi na kuruhusu kuingizwa bidhaa za Ulaya.


Anasema mabadiliko ya kiuchumi yamezua vichekesho kwa uchumi wa kimataifa na maendeleo ya kiuchumi kwa ujumla, ingawa China imeleta taswira mpya. Mataifa hayo yamevumbua mbinu mpya ya kibiashara na kuunda kundi la G20 lililolazimika kuziingiza nchi hizo kuleta uwiano. Kuanzishwa BRICS (Brazil, Russia, india, China na South Africa) kumechochea mabadiliko ya kibiashara na uchumi.

China ilianzisha Benki ya Miundombinu (Chinese Infrastructure Bank) ambayo ilikuwa mahususi kushughulikia miradi ya ujenzi wa miundombuni na mikopo kwa kampuni za uhandisi ili kuchochea mapinduzi ya sekta hiyo. Mwaka 1995 nchi zinazoendelea kiuchumi zilisafirisha bidhaa kwa asilimia 42. Mwaka 2103 nchi hizo zimesafirisha bidhaa kwa asilimia 57, ambapo nusu yake zilikwenda China. Asilimia 60 ya biashara za nchi hizo zilikwenda India na Brazil. Kuanzia mwaka 2001-2011 biashara kati ya Mataifa ya Afrika na BRICS ilikuwa kutoka dola bilioni 22.9 hadi dola bilioni 267.9.

Licha ya umuhimu wa ushirikiano kati ya Afrika, Ulaya, Marekani kwa pamoja na Brazil, India na China, bado hakuna usawa wa biashara baina ya mataifa makubwa na madogo. China ndiyo mdau mkuu wa biashara na Afrika kwa dola bilioni 198.5 wakati Marekani na Afrika ni dola bilioni 99.8 kwa mwaka 2013. Uwekezaji wa China barani Afrika hadi mwaka 2014 ulikuwa dola bilioni 40. India imepenya soko la Afrika kupitia kampuni za Bharti, Essar na Tata.

Tandon anafichua mikataba inayosababisha kikwazo cha maendeleo ya kiuchumi katika nchi za Afrika, ACP (Africa Caribbean na Pacific), makoloni ya zamani kubanwa na mikataba ya Lome Convention I,II&III na Cotonou.
Vibano walivyovipata kwenye mikataba hiyo ni vidogo kuliko vile vya mkataba wa EPA kama ungesainiwa. Anaeleza mpambano mkali wa vikao uliokuwapo jijini Dar es salaam kati ya timu ya ushawishi wa mikataba ya EU dhidi ya Jumuiya ya Afrika mashariki (EAC).

Kwamba Shirika la biashara duniani (WTO) linafanya kampeni kuzifukarisha nchi ndogo kupitia taratibu na sheria zake.

BIASHARA NI VITA
Tandon anakuja kufafanua kwanini kitabu hiki amesema biashara ni vita. Toka zamani biashara ni silaha kubwa katika vita vya maslahi kati ya mataifa tajiri na masikini. Matokeo yake vita hivyo ni wimbi la watu wanaoitwa wahamiaji kukimbia umasikini na ufukara katika mataifa machanga na kwenda mataifa tajiri.
Vita vya kibiashara vilisababisha kesi ya wakulima wadogo wa Kenya (Kenya Small Scale Farmers) dhidi ya serikali iliyokuwa ikishinikizwa isisaini mkataba wa EPA. Anasema biashata ilichangia ukoloni na ukoloni mambo leo huko India, kuanguka kwa ufalme wa Ottoman, umasikini wa Mexico na mataifa mengine ya Amerika kusini.

Anaonyesha namna mataifa ya Afrika yanavyoweza kufanya vizuri kwa kuimarisha ushirikiano wa ndani; COMESA, SADC, na EAC. Anatolea mfano hoja za waziri wa biashara wa Rwanda Monique Nsanzabaganwa alivyoweza kuwashawishi mawaziri wa biashara katika mkutano wao uliofanyika Kigali (Uk.17-18). 

Anaeleza kuwa mbali ya mikataba hiyo mara nyingi hutumiwa MFN yaani kwa kimombo ‘Most Favoured Nation’ ili kuingia kirahisi soko la ndani kwa manufaa yao. Vikwazzo vya kibiashara hutumika kama nyenzo ya kuhakikisha ufukara na dhiki vinaielemea nchi husika, hivyo kuilazimu kupiga magoti kwa WTO (Uk.21-23).

Changamoto kwa mataifa ya Afrika kubaini utapeli wa kibiashara unaokuja kwa lugha tamu tamu. Anasema hakuna usawa katika shirika la biashara duniani. Anatoa mfano mikataba ya Singapore, Doha, Seattle na Canncun ambayo inasisitiza ‘Fair Trade For Africa’ kwamba ni ulaghai kwani imesababisha ajira za mamilioni ya watu kupotea pamoja na ufukara kuongezeka (Uk.24-26)

Itaendelea

KUPATA KITABU HIKI, PIGA SIMU NAMBA 0718144517/0685115758.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako