Showing posts with label elimu. Show all posts
Showing posts with label elimu. Show all posts

March 07, 2018

KITABU KIPYA KUTOKA KWA MWANDISHI BEKA MFAUME

March 02, 2018

KUTOKA CHINA HADI CHUO CHA TEKNOLOJIA DAR ES SALAAM (DIT)

NA KIZITO MPANGALA
DUNIANI kuna ubunifu wa namna mbalimbali unafanyika katika teknolojia ili kurahisisha shughuli mbalimbali katika maisha yetu ya kila siku. Ubunifu wa kiteknolojia umekuwa ni lulu mojawapo katika ulimwengu huu wa Sayansi na Teknolojia hasa katika umeme na elektroniksi, ingawa upo ubunifu mwimgine nje ya uga huu wa umeme.
Kiti cha magurudumu manne ni kifaa cha muhimu sana kwa wagonjwa katika hospitali mbalimbali duniani. Na ubunifu mbalimbali hufanyika ili kuboresha utendaji wa kiti hiki. Kiti hiki kwa sasa kina magurudumu manne ambapo makubwa mawili na madogo mawili na hutegemea nguvu za mgonjwa kama anaweza kukisukuma yeye mwenyewe na kama hawezi basi anasukumwa na mtu mwingine.
Tofauti na baiskeli ya magurudumu matatu, kiti hiki kina ukubwa ambao unatosha kwa mtu mmoja tu kuketi na anayesukuma hulazimika kuembea. Vilevile hakichukui nafasi kubwa. Hakiwezi kutumika kama njia mojawapo ya usafiri barabarani kama ilivyo baiskeli ya magurudumu matatu inayotumiwa na walemavu wengi duniani kote.
Kiti hiki kilianza kubuniwa nchini China mnamo karne ya tano na baadae nchini Ugiriki mnamo karne ya sita ambapo kilibuniwa kwa ajili ya kubebea watoto na wazee wasioweza kutembea na kisha kuwasukuma ili kuwafikisha sehemu waliyokusidia. Nchini China awali walikuwa wakitumia matoroli kwa ajili ya kuwabeba wazee wasioweza kutembea na pia vilema na vilevile kubebea mizigo mizito. Michoro ya kiti cha magurudumu mawili iliyochorwa nchini China ilionekana mwaka 525 B.K huko Ulaya.

March 01, 2018

USHAURI KWA RAIS: NAKUOMBA KUBALI TUENDELEE KUCHANGISHANA

NA.HONORIUS MPANGALA
KWANZA kabisa nianze na kukusalimia shikamoo mheshimiwa Rais wangu, Dk. John Pombe Magufuli. Najua hii kazi ni ngumu kama usemavyo wewe mwenyewe lakini sina budi kukuombea uione nyepesi ili uweze kupata nguvu ya kututumikia vyema kama yalivyokuwa malengo yako siku unaenda kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo.

Mheshimiwa nikiwa safarini kuelekea makao makuu ya nchi yetu Dodoma, katika gari nilipata tafakuri  ambayo ilinifanya nitoe kitabu changu cha kuandika kumbukumbu na kuhifadhi mawazo yangu ambayo nimeona nikuandikie. 

Hoja yangu kubwa ambayo ilikuwa ikizunguka katika kichwa changu ni ile niliyokumbuka kauli yako ya kupiga marufuku wananchi kuchangishwa mchango wowote katika shule za serikali.

February 26, 2018

ZAWADI YA VITABU KWA MARA NYINGINE

JUMAMOSI Februari 24 mwaka huu nilipatiwa zawadi ya vita viwili kutoka kwa Bwana Ragin Mmbaga, kama vinavyoonekana pichani. Vitabu hivyo vimeandikwa na Bwana Johne Wisse. Kuna kitabu cha TONE LA DAMU cha lugha ya kiswahili na THE BROKEN CAMPUS RULE cha lugha ya Kiingereza. 
Ninawashukuru kwa kujali kuwa visima vya maarifa. Hakika mwaka huu nimeanza kwa furaha kubwa kwani huyu anakuwa mtu wa tatu kuniletea vitabu kibaruani kwangu. 

Usomaji wa vitabu ndicho kitu ninachokipenda zaidi. Ndicho kilevi au kitu ambacho kinachukua muda wangu wote kuhakikisha nafurahi. Zaidi ya hapo navutiwa na mchezo wa soka. Vitabu ni kitu muhimu sana. Namshukuru Ragin Mmbaga kwa niaba ya John Wisse. ASANTENI SANA

-MARKUS MPANGALA

February 12, 2018

LEVARDIS ROBERT MARTYN BURTON JR: MSEMINARI ALIYEUVAA UAFRIKA KWENYE FILAMU YA “ROOTS” KWA JIN LA KUNTA KINTE.

Na Kizito Mpangala

Ukimtazama hata kwa picha utasema ni mzaliwa halali wa Gambia kutokana na mwonekano wake katika filamu iliyomlazimu kuwa Mgambia.
Alizaliwa mwaka 1957 nchini Ujerumani Magharibi (sasa Ujerumani) kwa wazazi Levardis Robert Martyn Burton Sr na Erma Gene. Baba yake alikuwa ni mpiga picha wa jeshi la Marekani katika kituo cha afya cha Landstuhl cha jeshi la Marekani nchini Ujerumani. Mama yake alikuwa mwelimishaji wa jamii.

Burton Jr na dada zake wawili walilelewa na mama yao katika mji wa Sacramento jijini Calofonia nchini Marekani huku baba yao akibaki Ujerumani kikazi.
Burton Jr alivutiwa na kujiunga na Seminari na hivyo akakubaliwa kuanza masomo katika Seminari ya Mtakatifu Pius X katika kitongoji cha Calt jijini Califonia kwa lengo la kuwa padre.
Alipokuwa Seminarini, alipenda kusoma vitabu vya falsafa na kufanikiwa kuwasoma wanafalsfa kadhaa Seminarini hapo. Katika falsafa hizo, alivutiwa na kuwasoma kazi za wanafalsafa Lao Tzu, Nietzsche na Kierkegaard ambazo zilimfanya awahoji walimu wake kama Ukatoliki ndiyo dhehebu pekee kweli.
Alipofikia umri wa miaka 17 alihitimu katika Seminari hiyo na kuamua kujiunga na chuo kikuu cha Califonia Kusini kwa masomo ya sanaa. Alitunumiwa shahada ya kwanza ya sanaa huku akijikita katika uigizaji.

ANA KWA ANA NA MBUNGE WA VITI MAALUMU CHADEMA, NDUGU UPENDO PENEZA


Sisi katika blogu yetu tunakutana na wanasiasa mbalimbali bila kujali itikadi zao. Au pia viongozi wa kila kada tunazungumza nao bila kujali fani zao. 
Madhali wengi wao ni marafiki zetu maana ni watanzania wenzetu basi huwa tunazungumza nao mambo yahusuyo  ustawi wa jamii yetu kwa ujumla wake. Tunazungumzia maendeleo ya elimu, uchumi, siasa, utamaduni, afya na kadhalika.
Madhumuni yetu ni kuendelea kuzungumzia maendeleo ya wananchi pamoja na furaha ya jamii. Tunajikita katika maslahi ya taifa letu. Tanzania ni nchi yetu na hatuna kwingine. Tutailinda na kuikosoa ikibidi.
Pichani; kutoka kushoto ni Gabriel Mushi (mwandishi wa gazeti la RAI), mhariri wa Blogu hii Markus Mpangala (katikati) na Mbunge wa Viti maalumu ndugu Upendo Peneza.

JOSEPHINA MARGARET BAKHITA: MTAKATIFU MWAFRIKA ALIYEPONEA MIKONONI MWA MAHAKAMA YA ITALIA.

NA KIZITO MPANGALA

JOSEPHINA Margaret Bakhita alizaliwa mwaka 1869 mjini Darfur kitongoji cha Olgassa nchini Sudan katika jamii ya kabila la Daju. Baba yake aliheshimiwa sana kwa kuwa alikuwa ni kaka ya Chifu wa kabila hilo. Bakhita aliishi kwa furaha akiwa hajui mateso ya kitumwa yanakuwaje.
Alipofikia umri wa miaka minane, alitekwa na Waarabu wafanyabiashara ya utumwa ambao tayari walikwishamteka dada yake miaka miwili kabla ya kumteka Bakhita mwenyewe. Alilazimishwa kutembea mwendo wa kilometa 960 peku kutoka Darfur hadi El Obeid. Kabla ya kufika El Obeid alikuwa ameuzwa mara mbili njiani.

Bakhita alipofikia umri wa miaka 12 alikuwa ameuzwa tena mara tatu na kisha kusafirishwa mpaka Uturuki. Huko alikumbwa na mateso mengi na uchungu hali iliyompelekea kusahau jina lake la asili na hivyo alilazimika kutumia jina alilopewa na Waarabu, Bakhita likimaanisha mtu mwenye bahati. Kisha akasilimishwa.

Bakhita alinunuliwa na tajiri wa biashara ya watumwa ambaye alikwa Mwarabu na kumtumikisha kama mfanyakazi wa kuwahudumia binti zake wawili ambao waliishi nae vizuri. Alipokorofishana na mtoto wa kiume wa Mwarabu huyo alipigwa na kufikia hatua ya kushindwa kutembea kwa muda wa mwezi mmoja. 

February 03, 2018

JOHN LANGALIBALELE DUBE: MWANAFUNZI ALIYEAMINIKA KUWA NA TABIA CHAFU CHUONI MWASISI WA CHAMA CHA ANC, AFRIKA KUSINI.

Na Kizito Mpangala

John Langalibalele Dube alizaliwa mwaka 1871 kwa wazazi James Dube na Elizabeti Dube katika kitongoji cha Inanda,kwa sasa ni mkoa wa KwaZulu Natal. Jina lake la katikati yaani Langalibalele alipewa na wazazi wake likimaanisha “mwanga wa jua”. Baba yake alikuwa mchungaji katika kanisa la misheni ya Waamerika walioishi katika jamii ya Wazulu.
John Langalibalele Dube

Baba yake alikuwa kiongozi wa kabila la watu wa Qadi katika jamii ya Wazulu na jina lake lilikuwa Ngcobo Dube. Baada ya ujio wa Wamisionri alimua kujiunga na Ukristo na kisha akabatizwa kwa jina la JAMES DUBE. Huo ndio ulikuwa mwisho wa kuliongoza kabila hilo. John Langalibalele Dube alikuwa Mwalimu, Mhariri, Mpigachapa, Mshairi, Mwanafalsafa, Mwandishi wa Insha, na mwanasiasa nchini Afrika Kusini. 
 
John Langalibalele Dube alianza masomo katika kitongoji cha Inanda, na baadae akajiunga na chuo cha Adams (Adams College) kitongoji cha Amazimtoti kusini mwa mji wa Durban nchini Afrika Kusini. Akiwa chuoni hapo, walimu walipeleka lalamiko kwa wazazi wa John kwamba kijana wao ana tabia chafu chuoni hapo ambayo haiendani na sheria za chuo. Ndipo Mchungaji William Cullen Wilcox alipoteuliwa kuzungumza na kumkanya John Langalibalele Dube kwa tabia zake chafu (haikuwewa wazi ni tabia zipi hasa alizokuwa akizifanya). John alifuata nasaha alizopewa na kisha akabadili tabia.

Wamisionari wa Amerika walioondoka katika kitongoji cha Inanda, John aliambatana nao na kujiunga na chuo cha Oberline nchini Marekani. Aliambatana nao kwenda Marekani baada ya kupata ruhusa kutoka kwa baba yake Mzee James Dube ambaye alikuwa mchungaji na kiongozi katika chuo cha Adams. Wamisionari hao walikubali kwa sharti kwamba hawatamhudumia chochote kifedha, hivyo Mzee James Dube alipaswa kuingia mwnyewe mifukoni mwake.

GARETT AGUSTUS MORGAN: MJASIRIAMALI ALIYEVUMBUA TAA ZA KUONGOZEA MAGARI BARABARANI.

Na Kizito Mpangala

Garett Morgan alizaliwa mwaka 1877 katika kitongoji cha Claysville mjini Kentucky nchini Marekani akiwa na asili ya Afrika yaani. Baba yake alikuwa mtumwa aliezaliwa katika kitongoji cha Huntsville mjini Alabama. Baba yake alikuwa mtumwa kwa kurithishwa na wazazi wake waliokuwa watumwa. Miaka kadhaa baadae baba yake, John Morgan akawa Luteni Kanali wa jeshi la Marekani, Brigedia Jenerali katika jeshi la Kentucky kwa lazima. Mama yake Garett Morgan pia alikuwa mtumwa kama mume wake.

Garett Morgan alipofikia darasa la sita katika shule ya Brach Elementary mjini Claysville akiwa na umri wa miaka 16 alikwenda katika kitongoji cha Cincinnati mjini Ohio kutafuta kazi itakayompa ujira ili kupata mahitaji yake. Aliajiriwa mashambani.

Kama ilivyokuwa kawaida ya watoto wengi nchini Marekani wakati huo, Garett Morgan alilazimika kuacha shule akiwa darasa la sita na kuamua kufanya kazi katika mashamba kutwa nzima. Kutokana na bidii yake katika kazi, aliletewa mwalimu awe anamfundisha hapohapo shambani ambako ndiko yalikokuwa makazi huku akiendelea na kazi za shambani huko. 

Alifundishwa ufundi na baadae akawa fundi mahiri wa kutengeneza mashine za kushonea nguo yaani cherehani. Uzefu huo wa kutengeneza cherehani aliuheshimu na kujifunza zaidi jinsi mashine zinavyofanya kazi. Kazi yake ya kwanza kuvumbua ilikuwa ni cherehani inayotumia mkanda kama cherehani za sasa. Alivumbua cherehani hiyo tofauti na za mwanzo zilizokuwa zikizungushwa kwa mikono.

GEORGE CRUM: MPISHI MASHUHURI ALIYEVUMBUA CHIPSI YA VIAZI

NA KIZITO MPANGALA

Alizaliwa mwaka 1824 katika mji wa Saratoga, sasa ndilo jiji la New York nchini Marekani. Alijishughulisha na uwindaji na upishi katika migahawa ilikuwa katika milima ya Adirondack. Alifanya shughuli hizo kwa bidii lakini baadae alielekeza nguvu zake zaidi katika upishi. Jina lake lilikuwa ni George Speck. Kutokana na jina la uchepe kushamiri zaidi ambalo ni Crum, aliamua kujiita George Crum.

Baba yake aliitwa Abe Speck ambaye alikuwa mhamiaji kutoka Kentucky kwenda Saratoga. Akiwa Saratoga alimuoa mwanamke mwenye asili ya India ambapo baadae George alizaliwa. 

Bidii yake ilipoonekana zaidi, alichukuliwa na tajiri mmoja katika mgahawa ulioitwa Moon’s Lake House, karibu na maporomoko ya maji ya Saratoga. Mgahawa huo uliaminika kuwa ndio wenye gharama za juu za chalula. Hapo ndipo ujuzi wake wa upishi ulipofahamika na watu wengi zaidi. Licha ya kuwa na gharama za juu katika mgahawa huo watu walipenda kufika kwa wingi kutokana na umahiri wa George Crum katika upishi wake.

Bada ya kufanya kazi kwa muda mrefu katika mgahawa huo, George aliamua kumchukua dada yake ili wafanye kazi pamoja kutokana na ukata ulioikumba familia yao. Walikuwa ni wenye rangi mchanganyiko.

February 02, 2018

MFUMO WA UFUNDISHAJI NCHINI UNATAKIWA KUBADILISHWA

NA KIZITO MPANGALA
KILA mara inapofanyika mitihani kidato cha pili, nne na sita matokeo yanapokuwa mabaya wanaolaumiwa ni walimu. Matokeo yakiwa mazuri wanapongezwa walimu. 

Tunakumbuka matokeo ya kidato cha nne yamewahi kubatilishwa wakati wa uongozi wa serikali ya awamu ya nne. Ilibidi NECTA wafanye usahihishaji upya ili kuja na matokeo mazuri kutokana na awali kuwa mabaya kwa nchi nzima.
Mwenendo mzima wa sekta ya elimu mara nyingi Walimu wamebebe lawama nyingi. Lakini ipo haja ya watendaji wakuu (yaani serikali yetu) kubadilisha mfumo wa ufundishaji unaotumiwa hapa nchini. 

Nasema hivi baada ya kufanya utafiti na kubaini kuwa ili mtu awe amebobea kwenye ufundishaji lazima awe na uwezo mkubwa katika somo fulani. Kwahiyo naongelea namna ya kuwabadilisha watu ili kuleta manufaa ya elimu, uwezo wao na kuwasaidia wanafunzi.

Ingefaa kila mwalimu hapa nchini awe anafundisha somo moja tu na kwa madarasa mawili tu kwa siku nzima. Somo hilo moja ndilo liwe hilo tu hadi atakapostaafu. Mbinu hii itasaidia ubobezi mzuri wa somo husika kwa walimu wetu.

Isiwe mwalimu wa Historia alazimike kufundisha tena somo la Uraia. Mwalimu wa Biolojia alazimike tena kufundisha somo la Kemia. Mwalimu wa Hisabati alazimike tena kufundisha somo la Fizikia. Mwalimu wa Kiswahili alazimike tena kufundisha somo la Kiingereza kwa kuwa tu eti anajua sana kuidadavua fasihi. Mwalimu wa biashara(Commerce) n alazimike tena kufundisha uhasibu (Accounts) ingawaje masomo haya yanashabihiana kwa namna fulani.

January 31, 2018

UCHAMBUZI WA KITABU: "AMEZIDI"

MWANDISHI: SAID AHMED MOHAMED

MCHAMBUZI: KIZITO MPANGALA

AMEZIDI ni tamthiliya iliyopgwa chapa na East African Educational Publishers (Nairobi, Kampala, na Dar es Salaam) ambapo chapa ya kwanza ilitolewa mwaka 1995. Kitabu hiki kimesajiliwa kwa namba za usajili ISBN 9966-46-752-1.

Tamthiliya hii imegawanyika katika maonyesho kumi ya jukwaani ambapo kila onyesho lina ujumbe ambao unailenga jamii ya Afrika kwa ujumla hasa katika suala la maendeleo ya liuchumi, kielimu kijamii na kadhalika. Wahusika wakuu wa tamthiliya hii ni Ame na Zidi. Maonyesho haya yote na tamthilya yenyewe kwa ujumla ni cmhezo wa mawazoni tu!
Ame na Zidi wanajikuta katika umasikini mkubwa katika bahari iliyojaa mali. Katika hali hii ya uhitaji wanatambua kuwa hawana lingine la kufanya ila kuomba misaada ili wayatosheleze mahitaji yao. Msaada unapokuja unaleta madhara mengi zaidi.

Onyesho la kwanza linaonyesha Zidi akiwa anamwamsha nduguye Ame aliyekuwa amelala kukiwa kumeshakuchwa. Zidi anamwonyesha Ame mihogo miwili aliyotoka kuitafuta ili wapate kuila.

Onyesho la pili linaonyesha Ame na Zidi wakiwa katika kasri lao wanalisifia kasri hilo lililojaa samani nyingi kutoka Paris (Ufaransa) na vito mbalimbali pamoja na mazuria kutoka Iran.

January 26, 2018

TUNAPOKOSEA NI PALE TUNAPOCHANGANYA ELIMU,SIASA

NA HONORIUS MPANGALA
HISIA zangu zimenifanya niwe mtu tofauti kabisa kuhusiana na matumizi ya baadhi ya maneno hapa nchini. Mengi hutumiwa na viongozi wa ngazi za juu kuwaona wale waliopo chini au wasio na vyeo kama wao kuwa  wenye kiwango fulani cha dhiki kinachostahili kuitwa cha chini. Ni hapo ndipo nakuwa na hisia tofauti sana juu ya kutumia maneno fulani dhidi ya kundi jingine hasa lile ninaloongoza au viongozi wanaloliongoza. 
Makala hii imechapishwa katika gazeti la MTANZANIA toleo la leo
Japokuwa nimekuwa mtu nisiyependezwa na na hili neno “Wananchi wa hali ya chini”' lakini najiuliza hao wa hali ya juu ni akina nani, wanafanya nini kutokuwa na hali ya chini na njia zao zikoje ili tuwaambie wa hali ya chini wajifunze kwenda huko juu? 
Suala elimu katika nchi yoyote ni muhimu na linatakiwa kupewa kipaumbele sana. Kiuhalisia mazingira ya wanafunzi kwa shule nyingi zinazomilikiwa na serikali zimekuwa na changamoto kubwa na kupelekea hata matokeo mabaya kwa shule hizo.

Lakini unakuta baada ya kutazama wapi walipojikwaa wao wanakawaida ya kulaumu mwendo Wa aliyedondoka kuwa hatazami vyema au hatembei vyema.

Tangu iliposemwa elimu bure maisha ya wanafunzi yamekuwa na changamoto zake na wazazi waliipokea katika mitazamo yao hii hoja. Kutokana na kuzoea kupewa pewa tangu zama za wakaloni, waafrika wengi wamekuwa wavivu wa kujitafutia wao na kutatua changamoto wao huku wakitegemea tusaidiwa kama ilivyokuwa katika maisha ya ukoloni au kwa wale waliokuwa wanaishi karibu na Taasisi za kidini zilivyokuwa zikitoa misaada.

UCHAMBUZI WA KITABU: SAFARI YA YERUSALEM KUTAFUTA AMANI

NA MARKUS MPANGALA
BOUTROS Boutros Ghali aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kati ya mwaka 1992 hadi 1996 amefariki dunia Februari 16 mwaka 2016 akiwa na miaka 93.

Leo tunachambua kitabu chake cha “Egypt's Road to Jerusalem:: A Diplomat's Story of the Struggle for Peace in the Middle East” kilichozindualiwa rasmi Mei 20, 1997. Kitabu hicho kina jumla ya kurasa 366, kimechapishwa na Random House(1997) na kikiwa katika lugha ya kiingereza. Boutrous amekipatia namba ISBN-10: 0679452451.

Boutros Ghali anatuelezea miaka minne ya uzoefu wake katika utawala wa aliyekuwa Rais wa Misri, Anwar as-Sadat. Anatuonyesha namna alivyochaguliwa kwenye uwaziri wa mambo ya nje mwaka 1977 na kifo cha rais Sadaat mwaka 1981. 

Katika kitabu hiki Boutros Ghala anadhihirisha umahiri alioonyesha katika masuala ya diplomasia wakati wa kusaka amani ya mashariki ya kati. Ikumbukwe eneo la mashariki ya kati limekuwa kwenye migogoro ya muda mrefu kiasi kwamba ufumbuzi umekuwa mgumu. 

Ni eneo ambalo mwandishi wa kitabu hicho anatukumbusha hatua kwa hatua walizokuwa wakichukua katika kuhakikisha amani inarejea mashariki ya kati. Anatuonyesha namna ambavyo Misri na Israel zilivyokuwa zikifanya juhudi za kumaliza uhasama wao. 

January 23, 2018

ZOLILE HECTOR PIETERSEN: MTOTO ALIYELAZIMU KUANZISHWA KWA KUMBUKUMBU YA MAUAJI YA KIMBARI AFRIKA KUSINI, TAREHE 16 JUNI KILA MWAKA.

Na Kizito Mpangala

Zolile Hector Pietersen akiwa amebebwa na
Mbuyisa Makhubo baada ya kupgwa risasi.
kushoto ni Antoinete Sithole, dada yake
Zolile Hector Pietersen akilia.
Zolile Hector Pietersen alizaliwa tarehe 19/08/1963 mjini Soweto nchini Afrika Kusini wakati falsafa ya ubaguzi wa rangi ikiwa imepamba moto. Falsafa ya ubaguzi wa rangi ilikuwa ikijulikana kama Apartheid, ambayo ilikuwa ikiendeshwa na makaburu waliokuwa wakitawala nchi ya Afrika Kusini.

Jina halisi la ukoo wake ambalo lilikuwa likitumika na familia yake ni Pitso, lakini fdamilia hiyo ililazimika kubadili na kuwa Pietersen ili kuendana na falsafa ya Apartheid, na kujihisi kama wao ni makaburu ilhali wakiwa ni weusi. Familia hiyo iliamaua kufanya hivyo ili kukwepa dhuruma za makaburu. Hata jina la Zolile lilifutwa kwa muda ili apate nafasi ya kusoma. 

January 22, 2018

UCHAMBUZI WA VITABU KILA IJUAMAA


Kwa mwezi safu hii inachambua vitabu vinne (4). Kwa mwaka inachambua vitabu 48. Ni safu maalumu kwa uchambuzi wa vitabu pekee. Ni safu iliyodumu kwa miaka minne sasa ndani ya gazeti hili. Ni safu inayopendwa na kampuni za uchapishaji wa vitabu, waandishi na wasomaji pia. Ni safu inayotanua masimulizi au maarifa yaliyomo. 
Una kitabu chako wataka kichambuliwe? Wenzako wanakuja, kwanini wewe usubiri u! Ongea nasi, uwafikie wadau wengi…..

January 21, 2018

ERATOSTHENES WA KIRENE: MWANAHISABATI ALIYEISHI AFRIKA NA KUKADIRIA MZINGO WA DUNIA KWA KIVULI CHA MWANZI.

Na Kizito Mpangala

Eratosthenes alizaliwa mwaka 276 KK (Kabla ya kuazaliwa Yesu Kristo) mjini Kirene, Libya ya sasa. Kirene ni mji mashuhuri ulioundwa na Wagiriki wa kale walioishi Afrika ya Kaskazini hasa Libya ambako ndiko ulikokuwa mji wa Kirene maeneo ya Tripolitania ( sasa ni Tripoli), na Misri maeneo ya Alexandria ilikokuwa maktaba mashuhuri iliyotumiwa na wataalamu wengi wa Ugiriki ya kale. 

Alikuwa akifanya mazoezi mbalimbali ya viungo kila siku asubuhi na jioni. Alijifunza kusoma, kuandika, na kuhesabu. Ni kama vile falsafa ya elimu ya msingi inayotumiwa nchini Tanzania yaani KKK (Kusoma, Kuandika na Kuhesabu). Pia, alijifunza uandishi wa mashairi na vilevile masuala ya muziki.

January 19, 2018

TAITU BETUL: MALKIA JASIRI ALIYEASISI MJI MKUU WA ETHIOPIA, ADDIS ABABA.

Na Kizito Mpangala

Taitu Betul alizaliwa mwaka 1851 nchini Ethiopia ambayo wakati huo ilikuwa ni Milki ya Ethiopia kabla ya kuwa Jamhuri. Neno Taitu kwao lilimaanisha “mng’ao wa jua au jua”, hilo ndilo lilikuwa jina lake la asili.
Baada ya kubatizwa katika kanisa la dhehebu la Orthodox aliitwa Walatta Mikael, lakini baadae alilirudia jina lake la asili yaani Taitu Betul. Baba yake alikuwa aliitwa Betul Haile Maryam ambaye alikuwa na uhusiano na ukoo wa Mfalme Sulemani. Lakini baba yake huyo hakufahamika sana kama alivyofahamika mjomba wake  aliyeitwa Dejazmach Wube Haile Maryam, ambaye alikuwa mtawala wa Ethiopia Kaskazini miaka ya 1840.
Familia ya baba yake Taitu ilikuwa imeweka makazi yake katika mkoa wa Semien ambao ulikuwa ukitawaliwa na Mfalme Susenyos I. Baba yake alikuwa ni mjukuu wa Ras Gugsa ambaye alikuwa mshirika wa familia iliyotawala eneo la Yejju iliyokuwa na asili ya kabila la Oromo. Baba yake huyo alikuwa Muislamu na baadae akabadili dhehebu akajiunga na Ukristo.

Taitu Betul alikuwa na nafasi kubwa ya kuwepo katika ngazi za juu katika maeneo hayo kutokana na ndugu zake wengi kuwa katika nafasi za milki mbalimbali hasa katika ngazi za mikoa. 

Taitu Betul aliolewa mara nne na kuachwa kabla ya kukutana na Mfalme Menelik wa Shewa kama mke wa tatu. Muda mfupi baadae, baada ya kuolewa na Mfalme Menelik wa Shewa, Mfalme huyo akatawazwa kuwa Mfalme wa Milki ya Ethiopia (Ethiopian Empire). Taitu Betul akiwa kama Malkia pamoja na mumewe Mfalme Menelik II walikuwa wanamiliki watumwa elfu sabini (70,000).

January 15, 2018

ELIMU BURE INAVYOTESA WATOTO WA WANANCHI WA HALI YA CHINI

NA HONORIUS MPANGALA
KITAALUMA na hisia zangu zimenifanya niwe mtu tofauti kabisa kuhusiana na matumizi ya baadhi ya maneno hapa nchini. Mengi hutumiwa na viongozi wa ngazi za juu kuwaona wale waliopo chini au wasio na vyeo kama wao kuwa  wenye kiwango fulani cha dhiki kinachostahili kuitwa cha chini. Ni hapo ndipo nakuwa na hisia tofauti sana juu ya kutumia maneno fulani dhidi ya kundi jingine hasa lile ninaloongoza au viongozi wanaloliongoza. 
Japokuwa nimekuwa mtu nisiyependezwa na na hili neno “Wananchi wa hali ya chini”' lakini najiuliza hao wa hali ya juu ni akina nani, wanafanya nini kutokuwa na hali ya chini na njia zao zikoje ili tuwaambie wa hali ya chini wajifunze kwenda huko juu? 

December 30, 2017

VITABU 50 NILIVYOSOMA MWAKA 2017

NAWASILISHA orodha ya vitabu nilivyosoma mwaka 2017. Ukitazama orodha zangu za usomaji vitabu utabaini kuwa ya mwaka imeongezeka. Nimesoma vitabu 50 na kuna mabaki kadhaa hayaguswa kabisa.
Mwaka 2017 nimejikuta nikiwa nimeongeza uwezo wa kusaka maarifa zaidi kutokana na ongezeko la vitabu ingawa sina desturi ya kupanga idadi yake.

Kwa mwaka 2018 ninatarajia kuongeza maarifa zaidi katika vitabu vya biashara na uchumi, lakini haina maana nitasoma vingi kuzidi ‘ala za roho” (riwaya). Pamoja na changamoto za majukumu na mengineyo, suala la vitabu limebaki kuwa nyeti maishani mwangu.